MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.comDominick akaingiza mkono mfukoni na kisha kuitoa simu yake. Akaiwasha na moja kwa moja kwenda katika sehemu ambayo ilikuwa na kumbukumbu juu ya simu zote zilizoingia.
“Kuna namba hii nataka uende ukaiulizie” Dominick alimwambia Edmund huku akimpa simu.
“Namba ya nani hii?”
“Ya mwanamke yule aliyenipigia siku ile”
“Sasa nitamjua vipi?”
“Nenda katika kampuni hii ya simu, ukifika waambie uongo wowote hadi wakwambie namba hii ni ya nani na anakaa wapi. Tukimpata huyu mwanamke, kila kitu kitakuwa rahisi” Dominick alimwambia Edmund.
“Sawa”
**********
Pius akakifuata kitanda kile na kulifunua shuka. Kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amejifunika kitandani pale. Pius akalifunua shuka, ni mito tu ndio ambayo ilikuwa kitandani pale, ilikuwa imepangwa vizuri.
SONGA NAYOOO
Kila mmoja alionekana kukasirika, hawakuamini kama Dominick angeweza kuwafanyia ujanja ule ambao kwao ulionekana kuwa wa kitoto sana. Walichokifanya baada a hapo ni kuanza kumtafuta katika kila kona ya chumba hicho.
Walifungua kabati na kutoa nguo zote lakini wala Dominick hakuonekana. Hawakuonekana kuridhika hali iliyowapelekea kutoa kila kitu uvunguni mwa kitanda lakini napo Dominick hakuonekana kabisa.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, kumkosa Dominick ndani ya chumba kile ilionekena kuwashangaza kupita kiasi. Kitu walichokifanya mahali pale ni wote kujitawanya na kuanza kumtafuta Dominick. Amri moja tu ndio ambao ilitolewa mahali hapo, kumuua popote pale watakapomuona.
*******
Siku iliyofuata, Edmund akaanza safari ya kuelekea katika jengo la kampuni ya simu za mkononi ya Etisalat lililokuwa Posta mpya. Tayari Edmund alikwishajua ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea mara tu atakapofika ndani ya jengo lile.
Mara baada ya kufika katika sehemu ya maulizo, akaulizia sehemu ambayo ilikuwa ikipatikana huduma ile ambayo alikuwa akiihitaji kwa wakati ule. Alipoelekezwa, moja kwa moja akaanza kuelekea kule kulipokuwa na chumba maalum.
“Nikusaidie nini?” Sauti nyembamba ya msichana ilimuuliza mara baada ya salamu.
“Kuna namba ya mtu ambaye ananitisha kila siku, ni namba ngeni kwangu, sifahamu anataka nini” Edmund alimwabia dada yule ambaye alikaa kimya kumsikiliza.
“Nafikiri ametumwa, kila siku sina amani moyoni. Natamani kumfahamu mtu huyu ili nijue ni kwa jinsi gani nitaweza kujilinda” Edmund alimwambia dada yule.
“Unafikiri anaishi hapa hapa Dar es Salaam?”
“Sifahamu. Kwa kweli sifahamu”
“Unafanya kazi wapi?”
“Mimi ni mfanyabiashara, mara kwa mara huwa ninasafiri kwenda nchi mbalimbali” Edmund alidanganya.
“Namba yenyewe iko wapi ya huyo mtu?”
Hapo hapo Edmund akaichukua simu yake na kuiangalia namba ile ambapo baada ya kuipata, akamgawia msichana yule. Kazi ya kuanza kuitafuta katika kompyuta yake iliyokuwa mezani ikaanza. Dakika mbili zikakatika, mtumiaji wa namba ile akapatikana.
“Mwenye namba hiyo anaitwa Saida Hamisi. Anaishi Sinza Makaburini” Msichana yule alimwambia Edmund.
“Kumbe Saida! Ni rafiki yangu ambaye mara kwa mara huwa tunataniana sana. Nafikiri amebadilisha namba. Nikitoka hapa, nitanunua laini nyingine na mimi nianze kumzingua” Edmund alimwambia dada yule huku akijifanya kumfahamu Saida.
“Kumbe unamfahamu?”
“Sanaaa. Nimesoma nae kuanzia msingi mpaka chuoni”
“Chuo gani?”
“I.F.M” Edmund alijibu na kisha kuondoka.
Tayari kazi ambayo alipewa alikuwa amekwishaimaliza. Ujanja alioufanya wa kujifanya kumfahamu Saida ulionekana kuwa ujanja ambao haukushtukiwa na msichana yule. Akaingia ndani ya gari lake na safari ya kuelekea nyumbani kuanza huku moyoni akiwa na shauku ya kumpa Dominick taarifa.
“Vipi?” Dominick aliuliza mara baada ya Edmund kuingia ndani.
“Poa. Nimefanikiwa”
“Kweli?”
“Ndio”
“Ni nani?”
“Msichana mmoja anakaa Sinza Makaburini, anaitwa Saida Hamisi” Edmund alimwambia Dominick.
“Safi sana. Huyu ndiye atakuwa mwanzo wa safari yangu ya kuwagundua wabaya wangu” Dominick alimwambia Edmund.
Kazi ya kumtafuta Saida ikaanza. Wakaanza kujiandaa tayari kwa safari ya kuelekea Sinza. Dakika kumi baadae walikuwa ndani ya gari wakielekea Sinza Makaburini. Ndani ya dakika kumi na tano, gari lao likasimama katika eneo lililo karibu na makaburi ya hapo Sinza.
“Samahani” Edmund alimwambia mwanaume mmoja ambaye alikuwa amekaa nje ya saluni moja.
“Bila samahni”
“Kuna dada yangu namtafuta, anaitwa Saida Hamisi”
“Umeelekezwa anakaa wapi?”
“Hapa Sinza Makaburini. Unamfahamu?”
“Mhhhh! Jina lake si geni masikioni mwangu”
“Ulikwishawahi kulisikia wapi?”
“Hapa hapa. Hebu subiri” Mwanaume yule alimwambia na kisha kuingia ndani ya saluni, alipotoka, alitoka na mwanaume mwingine.
“Kuna Saida Hamisi mmoja tu ndiye ninamfahamu”
“Yupi?”
“Anakaa hapo mbele, nyumba yenye rangi nyeupe isiyokuwa na geti” Mwanaume yule alimwambia Edmund.
Edmund akaridhika na kwa jinsi alivyoelekezwa, akarudi garini na kisha kumfahamisha Dominick kile ambacho kiliendelea mahali pale. Gari likawashwa na kisha safari ya kuelekea katika nyumba ile kuanza.
Huku wakiwa wamebakiza umbali mdogo kuifikia nyumba ile, wakashangaa watu wawili kutoka katika gari jingine lililopaki katika eneo la nyumba ile wakiteremka na kuanza kuingia ndani ya nyumba ile kifujofujo.
Tayari Dominick na Edmund walikwishaanza kuhisi kitu, wakatulia garini na kusubiria kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea mahali hapo. Wala hazikupita dakika nyingi, wanaume wale waliokuwa wameingia ndani ya nyumba ile wakaanza kutoka huku wakiwa na Saida ambaye alionekana kuwa chini ya ulinzi wao.
“Mh! Kuna usalama kweli hapa?”
“Wala hakuna, kuna kitu nafikiri kinaendelea”
Gari lile likaendeshwa mpaka barabarani na kisha safari ya kuelekea kusipojulikana kuanza. Dominick na Edmund hawakutaka kubaki mahali pale, tayari waliona kuna kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali pale, wakaanza kulifuatilia gari lile.
“Hapa kuna kitu, tuendelee kufuatilia hivi hivi” Dominick alimwambia Edmund huku wakiendelea kulifuatilia gari lile ambalo likaanza kuingia katika barabara ya Nyerere kuelekea Bagamoyo.
********
Kila kitu kilionekana kwenda tofauti na mipango waliyokuwa wameipanga kabla. Kutokufanikiwa kuuawa kwa Dominick kulionekana kuwachanganya kupita kiasi. Kila siku walikuwa wakikutana na kufanya vikao vya dharura, hawakujua ni wapi walitakiwa kuanzia.
Hawakuelewa ni kwa nini vijana ambao walikuwa wakiwatuma walishindwa kabisa kufanya kazi ile ambayo walitaka ifanyike. Dominick alionekana kuwazidi ujanja vijana wao. Walipewa taarifa juu ya uwepo wa Dominick ndani ya nyumba moja iliyokuwa Mbezi, waliwatuma vijana wao kwenda kumuulia huko huko ndani ya nyumba hiyo, lakini cha ajabu, walishindwa kumuua.
Kila kitu kilionekana kwenda shaghalabaghala. Walijiona kuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha Dominick anauawa ndani ya miezi hiyo miwili. Mipango ilikuwa ikiendelea kama kawaida lakini walijiona kutakiwa kufanya kitu ambacho kingewafanya kutokujulikana na mtu yeyote juu ya uovu ambao waliufanya.
“Yule msichana” Mzee mmoja aliwaambia wenzake.
“Msichana gani?”
“Tuliyemwambia ampigie simu Dominick amuite pale New Africa Hotel”
“Amefanya nini sasa? Au anahusika na nini kwa sasa?”
“Anaweza akatoa siri ya kila kitu kinachoendelea, si unajua wasichana walivyo”
“Hiyo kweli. Kwa hiyo mnataka tufanye nini ili kujilinda”
“Tumuueni tu, hiyo ndio salama yetu ya kutokujulikana”
Hayo ndio maamuzi ambayo yaliafikiwa katika chumba ambacho walikuwa wamefanya mkutano wa siri. Benard, mvulana ambaye aliwaunganisha wazee hao watatu na Saida akaitwa na kuelezwa kwamba Saida alikuwa akihitajika kwa kazi nyingine mahali hapo.
Benard akaanza kuwaelekeza mahali msichana huyo alipokuwa anakaa. Hakukuwa na muda wa kupoteza tena, kila kitu kilitakiwa kufanyika kwa haraka haraka. Simu ikapigwa na baada ya dakika kumi na tano, vijana watatu wakaingia ndani ya nyumba hiyo.
“Kuna kazi moja mnatakiwa kufanya”
“Kazi gani bosi?”
“Kuna msichana tunataka apotee haraka iwezekanavyo”
“Msichana gani”
“Saida”
“Yule ambaye mlimshirikisha kipindi cha nyuma?”
“Ndiye huyo huyo” Mzee huyo aliyeonekana kiongozi kati ya wazee wale aliwaambia.
Akaanza kuwapa maelekezo juu ya mahali ambapo Saida alipokuwa akiishi kwa wakati huo. Maelekezo yalichukua dakika tano, vijana wote wakaonekana kuelewa mahali ambapo Saida alipokuwa akikaa.
“Kwa hiyo tumuue humo humo ndani?”
“Hapana, mchukueni na mumpeleke sahemu yoyote ile. Mtakapomuua, tuwasiliane basi”
“Sawa bosi”
Vijana wale wakaanza safari ya kuelekea Sinza huku akili yao ikiwa na lengo moja tu la kufanya mauaji. Wakaziangalia bunduki zao ambazo zilikuwa na risasi za kutosha. Walichukua dakika kumi na tano mpaka kufika Sinza Makaburini ambapo wakateremka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba ile iliyokuwa imepakwa rangi nyeupe. Hawakupiga hodi, wakaingia ndani.
Saida alikuwa amekaa kochini huku akiangalia filamu ya Kitanzania iliyoigizwa na msanii Steven Kanumba. Ghafla akashtuka kuona watu watatu waliokuwa na bunduki wakiingia ndani. Hata kabla hajafanya kitu chochote kile, akashtuka akivamiwa na kuwekwa chini ya ulinzi.
“Ukipiga kelele, ukionyesha mgomo wowote au ukiuliza swali, roho yako itakuwa halali yetu” Pius alimwambia Saida ambaye alikuwa akitetemeka tu.
Wote wakaanza kuelekea nje huku Saida akiendelea kuwa chini ya ulinzi wao. Walipotoka nje, wakaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Bagamoyo kuanza. Saida hakuongea ktu chochote kile, alitamani kuulza juu ya kile kilichokuwa kinaendelea mahali hapo lakini kila alipokuwa akikumbuka maneno ambayo aliambiwa, alishindwa kuuliza.
“Mungu nisaidie... Mungu niokoe...” Saida alijikuta akiomba moyoni.
************
Dominick na Edmund bado walikuwa wakilifuatilia gari lile ambalo lilikuwa likeonyesha kwamba lilikuwa safarini kuelekea Bagamoyo. Hawakutaka kuliacha zadi ya mita ishirini, walikuwa wakiliangalia katika kila kona.
Bado walikuwa wakimhitaji Saida kuliko mtu yeyote katika kipindi hicho. Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika katika sehemu ambayo kulikuwa na pori la Mapinga. Gari likakata kona, likaacha barabara ya lami na kuingia katika barabara ya vumbi.
Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika katika sehemu ambayo haikuwa na dalili ya uwepo wa nyumba yoyote ile. Pius na wenzake wote wakateremka huku wakiwa na Saida na kisha kuanza kuelekea ndani ya msitu huo.
Dominick na Edmund wakalipita gari lile na kwenda kulisimamisha gari lao mbali na sehemu gari lile lilipokuwa. Wote wakateremka na kuanza kuelekea kule gari la Puis na wenzake liliposimama, walipofika karibu na eneo lile, nao wakaingia ndani ya pori lile kwa mwendo wa kunyata.
Sauti ya Sauda ilikuwa ikisikika ikipiga kelele, Dominick na Edmund wakajificha na kuanza kuchungulia kule kelele zilipokuwa zikisikika. Saida alikuwa amekaa chini huku akilia, Pius na wenzake walikuwa wameshika bunduki, walionekana kujiandaa kummiminia risasi Saida.
“Sali sala yako ya mwisho” Pius alimwambia Saida.
“Nitasali...nitasali ila kuna siri nataka kuwaambia” Saida aliwaambia.
“Unasemaje? Siri? Siri gani?” Pius alimuuliza Saida.
“Mtakaponiua mimi, na ninyi lazima mtauawa” Saida aliwaambia maneno ambayo yalionekana kuwashtua.
“Tutauawa? Kivipi?”
“Wanaona kwamba kama wakiniacha mimi nitatoa siri, lakini kwa upande mwingine, wamepanga kuwamaliza hadi ninyi, kwani watapowaacha siri itavuja juu ya uovu waliomfanyia Dominick. Kwa hiyo na ninyi lazima mtauawa” Saida aliwaambia.
Pius akashusha bunduki yake. Maneno aliyoyaongea Saida yalionekana kuwa na ukweli kabisa. Kila kitu ambacho walikuwa wakikifanya wazee wale kilikuwa siri kubwa ambayo hawakutaka ijulikane na mtu yeyote yule, hiyo ndio sababu ambayo iliwapelekea kuwatuma wao kumuua Saida.
Hawakujua ni nani angeuawa baada ya Saida. Hawakuwa na uhakika kama wazee wale wangewaacha hai kama wangekamilisha kila kitu, walijiona nao wao kuuawa kama alivyosema Saida.
“Ila kweli. Na sisi tunaweza kuuawa” Pius aliwaambia wenzake.
“Kwa hiyo tufanye nini sasa?”
“Tuondokeni”
“Tuondoke pasipo kumuua?”
“Ndio. Hauoni kama ameyaokoa maisha yetu!”
“Na wazee wakituuliza tuseme nini?”
“Kwamba tumeishafanya kazi waliyotutuma”
“Poa”
Pius na wanzake hawaktaka kuendelea kukaa mahali pale, walichokifanya ni kuanza kuondoka kurudi Dar es Salaam. Hawakutaka kuondoka na Saida, walitaka kuondoka peke yao.
“Wewe utarudi Dar peke yako” Pius aliwmwambia Saida na kisha wao kuondoka.
Saida akaanza kusali sala ya shukrani, hakuamini kama alikuwa amenusurika kuuawa katika tukio lile. Mara baada ya kumaliza kusali, akainuka kwa lengo la kuondoka, lakini hata kabala hajaondka, akashtukia akiwekwa chini ya ulinzi.
“Dominick.....!” Saida aliita kwa mshangao.
“Ndio mimi Saida. Sali sala yako ya mwisho. Ni lazima nikuue na ndio niende kuwaua watu waliokutuma” Dominick alimwambia Saida huku akionekana kukasirika.
“Naomba unisamehe Dominick. Naomba usiniue” Saida alimwambia Dominick huku akianza kulia.
“Ni lazima nikuue. Wewe si ulifanya mipango ya mimi kuuawa! Kuna sababu gani ya kukucha hai?” Dominick alimwambia Saida huku akiikoki bunduki yake.
“Naomba unisamehe” Saida alimwambia Dominick huku akipiga magoti mbele yake.
Dominick hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya akimwangalia Saida ambaye alikuwa akilia kama mtoto. Kila akikumbuka shida ambazo alizipata porini pamoja na mambo mengi yaliyotokea maishani mwake, alijiona kuwa na sababu ya kumuua Saida.
“Nisamehe Dominick....naomba unisamehe” Saida aliendelea kuomba msamaha.
“Kama utataka nikusamehe, nijibu juu ya kila swali nitakalokuuliza” Dominick alimwambia Saida huku akitetemeka kwa hasira.
“Nitakwambia. Niulize nitakwambia.....”
“Ni nani yuko nyuma ya haya yote? Ni nani ambaye aliiangamiza familia yangu? Ni nani ambaye anataka kuniua? Niambie maana ya maneno BoT kama kirefu chake si Bank Of Tanzania. Ninaitaka maana yake iliyomaanishwa na wauaji hawa” Dominick aliuliza maswali matatu mfululizo.
“Nitakwambia…nitakwambia Dominick” Saida alimwambia Dominick na kuendelea
“BoT ni kifupi cha majina matatu ya watu watatu wanayoyafaya haya” Saida alimwambia Dominick huku akiwa amepiga magoti karibu na miguu ya Dominick.
“Watu gani hao? Niambie ni watu gani hao” Dominick aliuliza kwa kukalipia huku akionekana kuwa na hasira.
“Mawaziri, mawaziri. Waziri Bonifasi wa Mali asili na Utalii, waziri Ombeni wa Miundombinu na waziri Tumaini wa Mambo ya Ndani” Saida alimwambia Dominick.
Dominick akaonekana kuchoka, hakuamini kile ambacho alikisikia masikioni mwake. Watu ambao walitajwa mahali hapo aliandika wizi wao wa mamilioni miaka miwili iliyopita, hakujua kama watu hao bado walikuwa na kisasi juu ya maisha yake.
“Yaani bado walikuwa na kisasi na maisha yangu mpaka wakaiangamiza familia yangu?” Dominick aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Edmund...Edmund...yaani watu hawa ndio waliiangaliza familia yangu? Ni lazima niwaue, ni lazima niangamize familia zao pia kama walivyoiangamiza yangu. Tena nitaziangamiza kwa kuzichoma moto na kisha kuwaua wao wenyewe. Ni lazima Edmund. NI LAZIMA……!!!” Dominick alimwambia Edmind huku akilia kama mtoto. Mwili wake ukabaki ukitetemeka kwa hasira, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kutetemeka kwa hasira.
“NI LAZIMA NIWAUE….” Dominick alisema kwa hasira huku akiondoka mahali hapo kwa mwendo wa kasi kuelekea kule walipolipaki gari.