![]()
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Baada ya msiba Kinape alibakia kwenye kaburi na mpenzi wake ambaye usiku wa jana yake alikuwa naye kabla ya kuagana kuonana alfajiri ya siku ile kwa ajili ya safari ya kijijini. Alibakia ameliinamia kaburi huku msiba kwake ukianza upya.
Deus na ndugu na jamaa walimbembeleza sana mpaka alipokubali kuondoka makaburini. Moyoni aliapa lazima atamshikisha adabu aliyehusika na kifo cha Happ. Mwanzo alikuwa na wasiwasi na Kilole, lakini kilio alicholia kumlilia mchumba wake aliamini kabisa hausiki kabisa.
SASA ENDELEA...
****
Usiku wakiwa nyumbani Deus katika kutafuta vitu kwenye kabati alishtuka kuona kiwambo cha bastola yake kipo kwenye nguo. Alishtuka kwani siku zote hukiweka mbali kutokana na kutotumia sana kutokana na matukio ya kijibizana kwa risasi na wauza madawa ya kulevya kupungua.
Alikichukua na kukinusa kilionesha kimetumika, alijiuliza mbona kinanuka baruti kama kimetumika. Wazo la haraka lilikuwa kuikagua bastola, alipofungua droo alishtuka kuona haipo kama alivyoiweka.
Aliitoa na kuifungua upande wa risasi, alizidi kushangaa baada ya kuzikuta pungufu ya risasi sita. Alijiuliza bila kupata jibu kuwa risasi zile zimekwenda wapi, alinusa mdomo wa mtutu wa bastora na kukuta umetumika.
Alijikuta akipata wasiwasi na kumwita mkewe aliyekuwa sebuleni akizungumza na Kinape ili amulize. Kilole aliingia chumbani bila kujua anaitiwa nini.
Alishtuka baada ya kumuona mumewe ameshikilia bastora na kiwambo chake. Mshtuko wake ulikuwa dhahili ambao ulionekana wazi kwa mumewe.
Mshtuko ule aliuona na kujua kuna kitu anachokijua mkewe kuhusiana na matumizi ya bastola ile. “U..unasemaje mume wangu?” alisita kidogo.
“Nani katumia hii bastola?” alimuuliza kwa sauti ya kiaskari.
Kilole aliamini kabisa akibabaika lazima atakuwa swali la kujibu, alitulia kwa muda akipanga la kujibu mume wake ambaye alionekana amekunja uso alilirudia swali lake la mwanzo.
“Nakuuliza mbona hunijibu nani katumia siraha yangu?”
“Si..si..jui.”
“Hujui ina maana mimi ndiye niliyetumia?”
“Kama hujatumi wewea nani mwingine anaweza kuitumia hiyo bastora, mimi niitumie kwa kazi gani?”
“Hujanijibu nani katumia hii bastola na kiwambo chake pia risasi zangu sita hazipo?”
“Sijui.”
“Mke wangu sitaki utani nieleze ukweli la sivyo leo utanitambua mimi nani, unaweza kuikodisha kwa watu wafanye uharifu ili mimi niingie matatizoni.”
“Mume wangu hiyo imeanza lini, niikodishe ili iweje, nina shida gani mimi?”
“Kama huna shida nani kaitumia, kumbuka vitu vyote vinakaa sehemu ya siri tunayojua mimi na wewe.”
“Kama unataka kufanya lolote juu yangu fanya lakini mimi sijui lolote.”
Kauli ile ilimuudhi sana Deus na kuamini kabisa mke wake anajua kila kitu juu ya matumizi ya bastola ile kutokana na kushtuka alipoingia ndani na kumuona ameshika ile silaha.
Alimsogelea mkewe kumpa kipigo ili aseme ukweli juu ya matumizi ya silaha ile kwa kuamini kabisa kama silaha ile ikikamatwa inatumika vibaya basi lazima yeye ndiye atakaye julikana anafanya mchezo ule na kufia gerezani. Wakati anamsogelea amzabe makofi, simu yake iliita, aliipokea na kuzungumza
“Haloo,” alizungumza huku akitoka nje kutokana na simu kuwa ya kikazi.
Taarifa iliyomfikia alitakiwa uwanja wa ndege mara moja kuna ndege iliyosemekana kuna mtu ana madawa ya kulevya hivyo ilitakiwa akamatwe. Taarifa ile ilikuwa inatoka kwa mkuu wake, alibadili nguo harakaharaka na kupitia vifaa vya kazi na kuelekea mlangoni, kabla ya kutoka alisema:
“Nakwenda nikirudi nikute jibu la sivyo leo humu ndani patachimbika.”
Deus alitoka kutokana na kuchanganywa na matukio ya ndani, alijikuta akimsahau hata Kinape aliyekuwa amejilaza kwenye kochi, alipofika mlangoni alikumbuka hajamuaga rafiki yake aligeuka na kumsemesha Kinape aliyekuwa kwenye dimwi la mawazo mikono kichwani.
“Besti...Besti,” alimwita zaidi ya mara mbili ndipo aliposhtuka. “E..ee.eeh,” Kinape alikuwa kama umeamshwa usingizini. “Unaonekana upo mbali sana?”
“Wee acha tu, hata sielewi kama nitaweza kuidhibiti hali hii mpaka napata mawazo ya kijinga.” “Mawazo gani tena rafiki yangu.”
“Eti nami nijiue nimfuate mpenzi wangu.”
“Wewee! Mawazo gani hayo rafiki yangu, baada ya Happy kuna maisha mengine na farijiko lingine.”
“Ni kweli, siamini kama nitampata kama Happy, Deus yule mwanamke alinipenda mapenzi ya dhati toka moyoni mwake. Nina imani hata kifo chake kinatokana na kulilinda penzi letu.”
“Besti hebu tuache sheria ichukue mkondo wake.”
”Watamkamataje mtu ambaye hajulikani?”
“Mkono wa sheria ni mrefu atashikwa tu amini hilo best.”
Kauli ile ilimtisha Kilole aliyekuwa kwenye mlango wa chumbani akifuatilia mazungumzo. Wasiwasi kumjaa na kuamini kabisa mumewe kutokana na kazi yake ya kijeshi anajua siri nyingi, pengine hata tukio lile anajua yeye ndiye aliyefanya.
Alijikuta akitetemea na kujiona atafia gerezani au kinyongwa, lakini aliendelea kusikiliza kwa kuijificha. Alimuona mume akitoka nje na baada ya muda alisikia gari lake likiondoka.
Alirudi chumbani na kukaa kwenye kitanda kutafuta majibu ya maneno ya mume wake. Aliamini ile ni vita alitakiwa kumuwahi mumewe kabla hajafanya jambo lolote baya, wazo la haraka lilikuwa kwenda kwa wakuu wake hasa yule alimweleza hailewani naye baada ya kuzurumiana fedha za rushwa ya madawa ya kulevya.
Aliamini kupitia yule bwana atafanikisha mpango wake, kwa vile mumewe alisema akirudi akute jibu na yeye aliamini kabisa hakuwa na jibu la kumjibu hasa akizingatia siraha ile anayejua ni yeye na mumewe tu. Aliona kujiepusha na maswali yasiyo na majibu na mwisho wake kujulikana yeye ndiye muuaji ni kutoroka.
Aliamua kutoroka na kwenda kulala nyumba ya wageni ile kesho amtafute yule mkuu wa mumewe na kumweleza kuwa mumewe anajihusisha na dawa za kulevya.
Alijua yule bwana atataka kumkomoa na kuja kufanya upekuzi kwa vile atakuwa amwelekeza lazima atatiwa hatiani. Alichukua baadhi ya nguo za kuvaa kesho na kuziweka kwenye mkoba alimuaga mfanyakazi kwa kumwambia siri ile asimwambie mtu. “Marry hakikisha mtoto amekula vizuri.”
“Hakuna tatizo dada.”
“Na hizi utanunua chochote,” alimpa elfu ishirini.
“Asante dada.” Alitoka hadi sebuleni kumuaga Kinape.
“Shemu nakuja mara moja.” “Hakuna tatizo, wacha na mimi nikalale,” Kinape alijibu huku akielekea chumbani bila kuuliza safari ile ya wapi.
***
Siku ya pili Kilole alifika makao makuu ya kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, alimuulizia yule mzee ambaye jina lake alikuwa analijua moja. Baada ya kuingia getini alikwenda mapokezi na kuulizia. “Samahani dada mzee Shamo yupo?”
“Wewe nani yake?”
“Mtu wake wa karibu.”
“Ameingia sasa hivi.”
“Naomba nimuone.” “Subiri,” yule dada alisema huku akinyanyua simu, baada ya kuzungumza alisema:
“ Nenda chumba namba sita.”
Kwa vile hakuwa mgeni sehemu ile alikwenda moja kwa moja chumba namba sita na kugonga mlango.
“Ingia,” sauti nzito toka ndani ilisema. Alizungusha kitasa na kuingia ndani, mbele ya meza kubwa kulikuwa na mzee mmoja aliyekuwa na mvi nyingi kichwani zilizompendeza.
“Karibu mrembo.”
“Asante, shikamoo.”
“Asante, nikusaidie nini?” Kilole alitengeneza uongo huku akiusema hata ugomvi wao, baada ya kumsiliza alimuuliza:
“Una uhakika na usemacho?”
“Mimi si ndiye mkewe sasa unataka uhakika gani zaidi ya huu?”
“Okay, muda si mrefu tunakuja kwako.”
“Asante mzee wangu.”
Kilole aliondoka moyo wake ukiwa mweupe kama seluji, moyoni alijisemea akuanzae mmalize.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda kama alivyopanga alirudi aliamua kurudi nyumbani kwake akiamini muda ule mumewe atakuwa kazini mpaka arudi jioni angekuwa amekwisha wekwa chini ya ulinzi.
Alipofika nyumbani alishangaa kumkuta mumewe nyumbani kumbe naye hakurudi jana alipoondoka na kurudi asubuhi ile. Japo alipatwa na mshtuko uliofanya haja ndogo imtoke kidogo alijitahidi kuuficha.
“Karibu mke wangu,” Kilole alishangazwa na hali ya mumewe ambaye hakuonesha hasira. Kilole hakujibu alikimbilia chumbani na kuangua kilio kitu kilicho mfanya mumewe amfuate na kumbembeleza.
“Mke wangu bado una yaleyale ya jana?” Deus alimuuliza mkewe kwa sauti ya upole. “Siku hizi hunipendi, nimekuwa mke mwema na muaminifu siku zote za ndoa yetu, lakini bado umekuwa huoneshi nina umuhimu kwako,” Kilole alisema kwa sauti ya kilio cha uongo.
“Mke wangu, kama kimetokea kitu cha tofauti ndani nimuulize nani kama si wewe mke wangu?”
“Ni kweli, lakini kama sijui mimi nitajibu nini, tena ulitaka kunipiga.”
“Ni hasira za mpito lakini baada ya kujua kosa langu niliamua kuliacha, lakini muhimu kuwa na uangalizi mzuri wa vitu vyetu usipovitunza wewe nani avitunze...Halafu lile gari lako linaingia mwisho wa wiki.”
“Usiniambie! Asante mpenzi wangu.”
Kilole alinyanyuka na kumkumbatia mumewe huku akiamini bado ni mshindi na muda si mrefu Deus ataionja joto ya jiwe. Wakati wao wanabembeleza kikosi maalumu cha kupambana na dawa za kulevya kilikuwa nje ya nyumba ya Deus na kugonga hodi. Deus alitoka nje kuwakaribisha alishtuka kumuona mkuu wake mzee Shamo:
“Ooh! Mzee karibu naona leo mmenitembelea.”
Waliingia wote ndani na kuketi kwenye kochi wakati huo Deus alimwita mkewe awahudumie wageni.
“Mke wangu kuna wageni hebu njoo uwasikilize wanatumia nini.” “Tunashukuru, hatuna muda tumekuja kufanya kazi moja hapa kwako.”
“Kazi moja! Ipi hiyo?” Deus alishtuka.
“Nina imani unaelewa vizuri kazi yetu ni nini?”
“Naijua, ndiyo maana hata mimi nimerudi alfajiri kufuatilia mtu mmoja aliyeingiza dawa za kulevya.” “Ni kweli, lakini huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Una maana gani?”
“Kuna msamalia mwema mmoja amesema kuwa wewe unajishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya.” “Mimi?” Deus alishtuka kusikia vile.
“Unashtuka nini, sasa hivi upo chini ya ulinzi na kutuachia kufanya upekuzi.”
“Fanyeni tu, hizi ni njama za kuchafuana lakini kila kitu kitafahamika.”
Deus aliwekwa chini ya ulinzi na upekuzi ulianza mara moja, Kilole alijifanya kushtuka na kuuliza:
“Jamani kuna nini tena?”
“Siyo kazi yako,” Mzee Shamo alijibu kwa sauti kali.
“Jamani mume wangu kafanya nini?” Kilole aliendeleza usanii. “Wee waache, naona kila siku wananichokonoa lakini ukweli utajulikana,” Deus alisema bila kujua bomu lipo ndani litalipuka muda wowote.
“Hebu njoo hapa,” mzee Shamo alimwita Kilole kwa sauti ya ukali. Kilole alimfuata nakumwacha mumewe amekalishwa chini ya ulinzi, alipofika karibu alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Kuna mabadiliko?”
“Hakuna kila kitu kipo vilevile.”
“Ipo sehemu gani?”
“Ndani ya kabati.” “Okay,” baada ya kusema vile alisema kwa sauti kali kupoteza lengo.
“Haya na wewe rudi kwa mwendawazimu mwenzako.
” Kilole alishikwa na askari mmoja na kwenda kukalishwa pembeni ya mumewe, upekuzi uliendelea huku Deus akisema kwa hasira: “Yaani mkikosa hicho mnachokitafuta walahi nitazaa na mtu.” “Mume wangu mbona wanakufuatafuata?” Kilole aliendelea kulalamika kiuongo.
“Wee waache, mwaka huu nitakufa mimi au mtu, nimechoka kuchezewa kama mpira,” Deus aliendelea kulalamika kwa hasira.
“Wee piga kelele utanyamaza muda si mrefu,” mzee Shamo alisema huku akiendelea kufanya upekezi wa uongo kabla hawajafanya kilichowapeleka pale.
Baada kutafuta sehemu nyingine mwisho waliingia chumbani na kufungua kila sehemu na mwisho walichukua briefcase iliyokuwa ndani ya kabati na kuifungua. Ndani ya briefcase kulikuwa na dawa za kulevya zilizokuwa ndani ya mifuko, mzee Shamo alisema kwa furaha:
“Amekwisha, hapa hata ateremke masihi kumtetea hatoki.”
Waliibeba na kutoka nayo hadi sebuleni na kuifungua mbele ya Deus.
“Nilikueleza mapema kuwa huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Hiyo nini?” Deus alitaka kunyanyuka kwa hasira lakini alitulizwa na siraha zilizokuwa zimemtazama. “Deus umekwisha, nilikueleza toka zamani kuwa wewe mtoto mdogo huwezi kushindani na mimi, kwa hili utafia gerezani.” “Muongo mkubwa huwezi kuja kuniwekea madawa ili kunitia hatiani, lakini nikitoka nitakuua nakuapia,” Deus alipagawa kuona ndani briefcase yake kuna madawa ya kulevya.
Itaendelea