Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.comILIPOISHIA: Alichukua chupa tupu ya bia akaipasua na kusaga vipandevipande ili avinywe. Aliona ni vema akanywea maji, akafuata maji kwenye glasi.
***
Akili ilimruka Eg, kwamba Lina atakuwa ameshika uelekeo gani, akahisi nyumbani kwake, yeye akakodi bodaboda…
“Please anko nikimbize Kijitonyama haraka sana,” Eg alimwambia suka.
SASA JISUKUME NAYO…
Bajaj iliendeshwa kwa mwendo wa kasi kidogo hadi Kijitonyama nje ya nyumba ya Lina, Eg akashuka bila kulipa nauli na kukimbilia ndani ili kumuwahi Lina kabla hajajimaliza kama alivyoahidi mwenyewe kwamba anakwenda kujiua.
“Lina...Lina…” aliita Eg kwa sauti ya juu akikimbilia chumbani, alisukuma mlango na kumkuta Lina anaweka vipande vya chupa kwenye kikombe ili avinywe.
“Wee…weeee, acha hivyo Lina…Lina,” Eg alimrukia Lina wakaenda wote sakafuni…
“Lina noo! Usifanye hivyo tafadhali,” alisema Eg akimpokonya glasi Lina.
Cha ajabu Lina akaanza kulia kwa sauti ya juu kama vile amesikia habari za msiba wa mama yake mzazi.
Kusikia mayowe hayo, yule dereva wa Bajaj nje akawasha Bajaj yake na kutimua mbio. Haikujulikana mara moja kisa cha kukimbia vile wakati yeye alipeleka abiria pale.
Baadhi ya majirani walifika kutaka kujua kulikoni Lina akaangua kilio vile. Wengi walijua amepatwa msiba mzito, kama si baba, mama. Lakini ndani ya moyo wake, Lina ndiyo alianza kuingiwa na hisia za kitendo alichokifanya ndiyo maana akalia sana. Alipata hisia kali na kujilaumu kwa kumfanyia mumewe, Semi kitendo kibaya kama kile.
“Hodi wenyewe,” majirani walibisha hodi.
Eg akatoka akiwa ameshika glasi iliyokuwa na vipande vya chupa ndani ambapo Lina alitaka kuvinywa…
“Karibuni.”
“Jamani mbona tunasikia kilio, vipi tena?”
“Ah! Amepata taarifa si nzuri sana.”
“Kafiwa.”
“Ndiyo.”
“Na nani?”
“Shangazi yake kijijini. Ndiye aliyemlea.”
“Oh! Mpe pole, shangazi akishakulea huyo ni mama mzazi kabisa,” alisema mama mmoja jirani. Kwa ubinadamu, majirani hao walitoa michango mbalimbali. Wengine walifungua vitenge wakatoa elfu kumi, wengine elfu ishirini. Jumla zilipatikana laki moja, Eg akasema moyoni…
“Ama kweli kufa kufaana lakini huku si kufa kufaana bali wajinga ndiyo waliwao.”
Walipoondoka, Eg alimwaga zile chupa kwenye taka, akarudisha glasi mahali pake na kurudi chumbani. Hakuwahi kuingia chumbani kwa Lina ndiyo mara ya kwanza siku hiyo.
Kwa haraka sana Eg aliamua kutumia ufahamu wake kumpigia simu Semi ambaye muda huo alikuwa gesti amejipumzisha baada ya kumalizana na wazazi wa Lina. Baba wa Lina alikuwa akimtafuta kwa simu binti yake bila mafanikio baada ya kuzima simu.
“Shem…” aliita Eg…
“Ndiyo shem, mzima?”
“Mzima wapi bwana, kuna matatizo huku!”
“Matatizo gani?” alihoji Semi bila kuonesha dalili ya mshtuko.
“Mkeo ametaka kunywa vipande vya chupa.”
“Kisa?”
“Nadhani kwa yaliyotokea shem.”
“Sasa shem akinywa yeye ndiyo nimekunywa mimi? Na nikinywa mimi ndiyo amekunywa yeye sidhani kama ni shida.”
“Ni shida! Unajua tuko ndani ya nyumba yako?”
“Ndani ya nyumba yangu, mmeingiaje?”
“Sijui, mi nimemkuta ndani akiwa ameshika glasi ina vipande vya chupa tayari kwa kuvibugia.”
Kuna sauti ilipita kwenye kichwa cha Semi ikisema…
“Umefanya mangapi katika maisha yako ambayo ni machukizo kwa Mungu mbona umesamehewa? Jaribu kusamehe na wewe. Mbona Zanzibar una mwanamke. Morogoro una mwanamke. Tanga ulikwenda ukaishi kwa mwanaume siku saba nzima tena ukiwa na huyuhuyu Lina, samehe bwana.”
“Sikia shem. We si upo hapo?”
“Ndiyo.”
“Kwanza hebu niambie ukweli, Lina alilala kwako jana?”
“Hapana, nimekuja baada ya kumkosa kwenye simu ndiyo nikajua labda anaumwa, nikaja na kumkuta na glasi…
“Nilipomuulizia akanisimulia matatizo makubwa sana…”
“Ina maana ulikuwa huyajui shem?”
“Nilikuwa siyajui hata moja, nimeshangaa sana sana, tena sana.”
Kwa mbali, Semi alianza kumwamini Eg japo awali alijua ni mulemule tu. Aliamini zaidi baada na yeye kukumbuka kwamba akiwa na wazazi wa Lina, Korogwe alikata simu akazima.
Pia alianza kuamini alipobaini kwamba Lina hakuwa kwa Eg lakini akaingiwa na wasiwasi kwamba kama hakuwa kwa Eg alikuwa wapi!
“Sasa sikia shem?”
“Ndiyo shem…ndiyo shem…nimekuelewa shem…sawa shem….eee, sawa shem….oke shem…”
Muda wote, Lina alikuwa akisikiliza baada ya kugundua kuwa, Eg alikuwa akiongea na mumewe lakini hakujua walikuwa wakiongea nini ila kwake yeye ilikuwa ni hatua kama kweli Semi amepoteza muda wake kumsikiliza Eg ambaye ni rafiki yake kipenzi.
Eg alipomaliza kukata simu tu, Lina akamuwahi hata kabla hajapumua…
“Naamini ni Semi huyo?” aliuliza kwa haraka Lina.
“Ndiyo mwenyewe.”
“Amesemaje? Niambie tafadhali…”
“Anasema mimi nisiondoke hapa nikuangalie mpaka yeye aje kesho,” alisema Eg na kumfanya Lina kuwa na matumaini kidogo kwamba huenda msamaha ukatembea kama si kupita.
“Anaweza kunisamehe kweli kwa jinsi ulivyoongea naye?”
“Anaweza. Tena uwezekano ni mkubwa kuliko unavyofikiria.”
“Mh! Ikiwa hivyo kweli Mungu ni mwema kwangu,” alisema Lina.
“Lakini Lina,” aliita Eg…
“Niambie.”
“Mimi nina wazo…”
“Lipi hilo Eg?”
“Kwa nini tusiende kwa yule padri aliyekufungisha ndoa ukatubu yote kisha yeye akamwita Semi kumpa maelekezo ya msamaha kwako?”
Lina aliangalia juu kama anayejiuliza jambo fulani. Alionesha kukubaliana na maneno ya Eg. Alimkumbuka padri huyo ambaye siku si nyingi zilizopita alikutana naye mjini akamuuliza…
“Ndoa yako inasemaje? Bado iko imara?”
“Iko imara Faza Denis.”
“Mungu awabariki sana.”
“Amina Faza Denis.”
“Eg ni kweli Eg. Mimi pia nakubaliana na wewe,” alisema Lina baada ya kuwaza kwa muda mfupi.
***
Ilikuwa jioni ya saa kumi na moja, walikwenda kanisani kuonana na Faza Denis ambaye aliwapokea kwa mikono miwili huku akimpongeza Lina kwamba amenawiri, mumewe anamtunza vizuri.
“Enhe, Lina nikusaidieni nini? Mwenzio anataka kufunga ndoa kama wewe?” aliuliza Faza Denis…
“Hapana Faza Denis. Nina matatizo makubwa sana sana sana tena sana…”
“Ndani ya ndoa? Maana sitarajii umeniletea matatizo ya kiofisi.”
“Ndani ya ndoa Faza Denis.”
“Mumeo Semi yuko wapi?”
“Yuko ukweni kwake, Korogwe.”
“Una maanisha kwa wazazi wako?”
“Ndiyo.”
“Haya, nakusikiliza,” alisema Faza Denis huku akikaa sawasawa kwenye kiti, kiganja cha mkono wa kulia akakitumia kushikilia kidevu…
“Huyu ni rafiki yangu mkubwa, anaitwa Agnes. Mimi nimezoea kumwita Eg, wengine wanamwita hivyo. Kanisindikiza hapa…
“Faza, kuna tukio nimelifanya ndani ya ndoa limeniletea hali mbaya sana pengine hata ndoa yangu kutaka kuvunjika…”
“Ni lipi hilo Lina? Unanitisha hata mimi kiongozi wako wa kiroho.”
Lina alianza kusimuliza kisa kizima cha James kwake mpaka kufunga naye ndoa nyingine.
Wakati anasimulia, kuna muda Faza Denis alitingisha kichwa kusikitika, wakati mwingine alitumbua macho. Pia kuna wakati alitumia kiganja cha mkono wa kulia kujifuta uso kama vile alikuwa na jasho.
Ilifika mahali Faza Denis alilaza mikono yake yote kwenye meza kama aliyekuwa akitaka kumsikiliza kwa karibu Lina. Kuna kipindi Lina alisema maneno yaliyomfanya padri huyo kumwangalia Eg kama anayemuuliza ‘eti ni kweli?’ Eg naye akawa anasema ni kweli kwa kutingisha kichwa juu, chini.
“…hayo ndiyo yaliyotokea Faza Denis mpaka leo hii. Kama si huyu Eg ningekuwa mfu saa hizi. Nakuomba sana tena sana, natubu ni kosa lakini niombee kwa Mungu anisamehe na mume wangu pia anisemehe, nimekosa mnisamehe wote,” alimaliza Lina kisha padri akahema kwa nguvu…
“Lina!” aliita Faza Denis.
“Abee faza.”
“Pole sana. Najua mapito yako yote yalikuwa yamesimamiwa na shetani. Hukuwa na uwezo wa kumshinda kwa sababu ana nguvu sana kwako.
Wewe ukilala huombi, ukiamka huombi wala kumshukuru Mungu. Mara ya mwisho kukuona kanisani siku ile ulipokuwa umemsindikiza yule binti wa mzee Mchemsho aliyetaka cheti chake cha ubatizo hapa, sijakuona tena…
“Sasa kwa sababu umetubu ina maana umelijua kosa lako na Mungu anasema siku zote kwamba, kila mwenye kuomba msamaha asamewehe hata saba mara sabini kwa saa ishirini na nne.
“Nitampigia simu Semi ili akifika tu aje kuniona tuyaongee haya mambo.
Nitamwambia ulikuja kutubu kwangu. Ila kabla hamjaondoka niwaombee kidogo,” alisema Faza Denis huku akiweka mikono sawa kwa maombi. Alimshika kichwani Lina, akamwombea kwa dakika kama tatu kisha akampa mkono wa baraka aondoke.
***
Semi alikuwa amekaa kwenye kiti jirani kabisa na Faza Denis, Lina alikuwa pembeni, Eg naye pembeni lakini jirani na Lina, James hakuachwa nyuma maana aliitwa na faza huyo japokuwa walikuwa hawajuani lakini James aliitikia wito…
“Nadhani bwana James utakuwa unajua kisa cha kukuitia?” aliuliza padri huyo.
“Sikuambiwa, ila nilipokuta haya mazingira nimejua,” alijibu James…
“Asante sana kwa uelewa. Napenda vijana wenye uelewa kama wako…Semi unajua?”
“Na mimi kama huyu bwana James…”
“Nashukuru, lakini Lina na Eg mnajua kila kitu?”
“Ee tunajua kila kitu faza,” walijibu kwa pamoja wawili hao.
“Mimi sina maneno marefu, kesi iliyopo hapa ni ya ndoa mbili. Kesi hii imeletwa na Lina mwenyewe ambaye ndiye mhusika.
“James ni kweli mnamo mwezi mmoja uliopita ulifunga ndoa na Lina?”
“Ni kweli faza, tena ilikuwa ndoa halali kabisa kwa wakati ule.”
“Unaposema ilikuwa ndoa halali kabisa kwa wakati ule una maana gani?”
Je, unajua nini kilitokea hapo? Usikose kusoma siku ya kesho.