Vijana wengine ambao nao nyuso zao zilikuwa zimefunikwa na vinywago wakaingia ndani. Christina akawekwa kochini na kuamriwa kutokupiga kelele zozote zile. Akabaki akitetemeka kama mtu ambaye alikuwa akisikia baridi kali.
Muda wote Christina alikuwa akilia, hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo. Kijana mmoja akamfuata Ibrahim ambaye alikuwa amewekwa katika kochi la pembeni, alipomfikia, akambeba na kumpelekea Christina.
“Jamani kuna nini tena? Mbona mnanitisha?” Christina aliuliza huku akionekana kutokuelewa chochote.
“Mumeo anafahamu kila kitu. Yaani hakuna hata kigeni asichokifahamu” Mwanaume mmoja alisema kwa sauti nzito iliyojaa mikwaruzo.
“Kitu gani? Mume wangu anafahamu kitu gani?” Christina aliuliza huku akiendelea kutetemeka.
“Anawachafua wazee wetu, anategemea tutamuacha hivi hivi?” Mwanaume mmoja alimuuliza Christina na kuendelea.
“Leo tutataka kumuonyesha ni kwa jinsi gani wazee wetu wamekasirika” Mwanaume yule alimwambia Christina.
Christina akafuatwa na mwanaume mmoja kutoka pale alipokuwa amekaa na kupelekwa jikoni. Huko akafungwa kamba mikononi na miguuni huku mdomo wake ukifungwa na kitambaa. Christina alijitahidi kupiga kelele lakini sauti yake wala haikuweza kusikika popote pale.
“Tuwaue kwa aina gani ya kifo” Mwanaume mmoja aliwauliza wenzake.
“Chochote tu. Ili mladi watu wasijue kama wameuawa”
“Sawa. Hapo nimekuelewa. Nenda kalete petroli garini” mwanaume yule aliagiza na mmoja wao kutoka nje na kuanza kuelekea nje ambako baada ya muda fulani akarudi akiwa na dumu la lita ishirini lililokuwa na mafuta ya petroli.
Wala hawakutaka kupoteza muda wowote ule, wakaanza kummwagia Christina pamoja na mtoto wake, Ibrahim ambaye alikuwa amemkumbatia na kisha kuendelea kumwaga na sehemu nyingine za nyumba ile. Baada ya kuona kila kitu kilikuwa tayari ndani ya mpango wao, mwanaume mmoja akachukua kiberiti na kuwasha.
“Mmmmmhhh.... mmhhhh..” Christina alisikika ndani.
Nyumba ikaanza kuteketea kwa moto hali iliyowafanya baadhi ya majirani kutoka nje ya nyumba zao. Kila mtu ambaye aliiona nyumba ile ilivyokuwa ikiteketea alishindwa kuelewa ni kitu gani ambacho kilisababisha nyumba ile kuteketea.
“Pigeni simu kitengo cha Zimamoto” Mwanamke mmoja aliwaambia wenzake.
“Nimekwishapiga kitambo” Mwanaume mmoja alimwambia.
Mpaka gari la kitengo cha Zimamoto linaingia mahali pale, tayari nyumba yote ilikuwa imeteketezwa wa moto. Hakukuwa na dalili za kupatikana na kitu chochote kile kilichokuwa kizima, kila kitu kilikuwa kimeteketezwa kwa moto.
**********
Dominick alionekana kuchanganyikiwa, tukio la kuchomwa moto kwa nyumba yake lilionekana kumchanganya kupita kiasi. Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, moyoni aliumia kupita kiasi. Picha ya mkewe mpendwa, Christina pamoja na mtoto wake, Ibrahim bado zilibaki kichwani mwake.
Mbele yake akaona giza, hakujua afanye nini ili atoke katika hali ambayo alikuwa nayo. Akili yake tayari ilimwambia kuwa kuna mtu ambaye alikuwa nyuma ya tukio lile, lakini hakuwa akifahamu ni nani hasa alihusika moja kwa moja na tukio la kuumiza moyo wake kupita kiasi.
Maisha yake katika kipindi hicho yalitawaliwa na majonzi, hakujua ni sehemu gani ambako angeweza kupata faraja ambayo ilionekana kupotea moyoni mwake. Kila siku alikuwa akielekea katika kaburi la mke wake na mtoto wake kama ishara kubwa ya kuwakumbuka.
Mara kwa mara alikuwa akiitwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa baadhi ya maelezo huku upelelezi ukiendelea kufanyika. Kila Mtanzania ambaye alilisikia tukio lile alijua moja kwa moja kwamba kuna mtu ambaye alikuwa amehusika katika kuiteketeza familia ya Dominick.
Maneno ya BoT ndio ambayo yalionekana kumchanganya kila mtu. Kila mmoja alijua fika kuwa kiongozi wa kitengo hicho ambaye aliandikwa sana na magazeti kuhusu wizi aliokuwa ameufanya ndiye ambaye alikuwa amefanya tukio lile.
“Sidhani kama atakuwa ni yeye” Dominick alimwambia kamanda mkuu wa polisi, Bwana Idrisa.
“Kwa nini unadhania hivyo?”
“Hebu jifikirie, kwanza habari kuhusu yeye niliiandika miaka miwili iliyopita, halafu kingine, tayari alikwishafariki. Unalikumbuka hilo mkuu?” Dominick alimwambia na kumalizia na swali.
“Mhhhh... Lakini hapa kuna ukweli”
“Sasa swali linalonijia kichwani juu ya mtu aliyehusika na tukio hili” Dominick alimwambia Bwana Idrisa.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo afya ya Dominick ilivyozidi kushuka. Mwili wake ukapungua kupita kiasi, mawazo juu ya familia yake bado yalikuwa yakimsumbua kila siku. Dominick alijiapia kutaka kulipiza kisasi kwa mtu yeyote mbaye alikuwa amehusika kwa namna moja au nyingine katika kumuumiza.
2
Katika kipindi hicho hakuwa na nyumba, alikuwa akiishi kwa rafiki yake, Edmund ambaye alikuwa akifanya kazi ya Uandishi pamoja nae. Maisha yake aliyaona yakianza nyuma kabisa katika pointi ya kwanza ambayo alikuwa akiishi kabla ya kuoa.
Kila siku Dominick alikuwa akiuliza kuhusu upelelezi ambao ulikuwa bado ukiendelea kufanyika. Aliona kila kitu kikikwenda taratibu sana. Katika kipindi hicho alihitaji hata tetesi ya nani alikuwa amehusika katika kufanya mauaji yale.
Hakukuwa na tetesi zozote zile alizozisikia kutoka katika kitengo cha polisi cha upelelezi, kila kitu kilionekana kuwa kigumu. Kwa wakati huo, kila gazeti lilikuwa na taarifa zake, waandishi wa habari wakaanza kuingiwa na hofu ya kuandika mambo mengi kuhusiana na wizi ambao ulikuwa ukifanyika katika sekta mbalimbali Serikalini.
Maisha yaliendelea kama kawaida. Baada ya miezi mitatu ya kujipanga upya, Dominick akajiona kuanza kusahau. Akaanza kufanya kazi kama kawaida japokuwa mara kwa mara alikuwa akiikumbuka familia yake hasa kila alipokuwa akiziangalia picha ambazo walipiga pamoja.
“Kuna habari kuhusu nini?” Dominick alimuuliza mwanamke ambaye alimpigia simu.
“Ufisadi. Kuna ufisadi umefanyika katika hili shirika la serikali la nyumba za taifa, NHC. Kuna kamchezo kamefanyika hapa” Sauti ya mwanamke yule ilisikika.
“Kuna ushahidi wowote juu ya habari hiyo?”
“Ushahidi upo. Tuna mikanda baadhi ambayo itakudhihirishia hilo” Sauti ya mwanamke yule ilisikika.
“Sawa. Uko wapi ili nije kuichukua habari hiyo?”
“Njoo hapa New Africa Hoteli”
“Nitakuwa hapo baada ya dakika ishirini” Dominick alisema na kukata simu.
Hakuwa na cha kufanya kwa wakati huo zaidi ya kujiandaa na kisha kuanza safari ya kuelekea katika hoteli ya New Afrika. Dominick alionekana kuwa na hamu kubwa ya kuandika habari ambazo zilikuwa zikihusu wizi ambao ulikuwa ukiendelea kufanyika japokuwa kwa wakati huo tayari ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa.
Ingawa saa yake ilikwa ikimwambia kuwa ni saa nne usiku lakini hilo hakuonekana kulijali,kitu ambacho alikuwa akikijali ni kufanya kazi yake tu.
Mara baada ya kufika Jangwani, akaongeza kasi ya gari lake mpaka alipofika maktaba ya Taifa ambapo akakata kona kulia na kuanza kuelekea Posta. Wala hakuchukua sekunde nyingi, akaaingia katika eneo la hoteli ya New Afrika.
Huku akiwa hajateremka, ghafla akashtuka baada ya kuwaona vijana watatu wakielekea kule alipokuwa garini. Hata kabla hajajiuliza juu ya watu wale, akashtukia wakiingia ndani ya gari lake.
“Mbona mnai.....” Dominick aliuliza lakini hata kabla hajaalizia swali lake, akajikuta akiwekwa chini ya ulinzi na mwanaume mmoja ambaye alishika bunduki.
“Fuata maelekezo yetu kuanzia sasa. Kama utakuwa mkaidi, utaifuata familia yako” Mwanaume yule alimwambia Dominick.
Hakuwa na la kufanya kwa wakati huo, mdomo wa bunduki ambao alikuwa ameelekezewa ulionekana kumuogopesha kupita kiasi. Akawasha gari lake na kuanza kuelekea kule ambako alitakiwa kwenda kwa wakati huo.
“Lakini nimefanya nini jamani?” Dominick aliuliza huku akionekana kuogopa.
“Kwani wewe umekuja hotelini kufanya nini?” Mwanaume mmoja kati ya wale watatu alimuuliza.
“Nilipigiwa simu ya kikazi. Kama mnataka kuchukua gari, tafadharini, lichukueni ila niachieni niendelee na kazi yangu” Dominick alijitetea.
“Hakuna. Hakuna kitu kama hicho. Kama magari, tunayo mengi na ya kutosha. Kwa sasa hatuhitaji gari, tunachohitaji ni roho yako tu” Mwanaume yule alisema maneno ambayo yalimshtua Dominick.
“Unasemaje?” Dominick aliuliza huku aisimamisha gari.
“Najua umenisikia. Topa, shikiria usukani” Mwanaume yule aliyejiita Kibra alimwambia mwenzake na Dominick kuchukuliwa na kuwekwa katika viti vya nyuma.
“Jamani. Nimefanya nini, nimefanya nini jamani. Mmeiua familia yangu, hamjalidhika tu mpaka mnataka kuniua na mimi?” Dominick aliuliza huku akianza kutokwa na machozi.
Hakuwa na tumaini lolote kwa wakati huo, tayari alijiona kuwa kama mfu ambaye alikuwa akitembea, aliuangalia mdomo wa bunduki ile, bado ulionekana kumtisha. Tayari akaanza kuhesabu dakika za yeye kuvuta pumzi ya dunia hii, hakuwa na uhakika kama angeweza kunusurika katika mikono ya watu hao.
“Lakini ni nani ananifanyia hivi? Kwa nini lakini” Dominick aliuliza.
“Hata sisi hatumfahamu na wala hatufahamu ni kwa nini anafanya hivi. Sisi tunachokitaka ni utekelezaji tu” Kibra alimwambia Dominic.
Njia nzima Dominick alikuwa akilia huku akiwaomba watu wale wamuachie. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kuelewa chochote kile, kitu ambacho walikuwa wakikitaka kukifanya kwa wakati huo kilikuwa ni utekelezaji wa kile walichotumwa tu.
Gari likafungwa breki katika msitu wa Nyakipande, Dominick akateremshwa. Giza lilikuwa kubwa wakati huo, moja kwa moja akaanza kuingizwa ndani ya msitu huku akiwa amefungwa kitambaa usoni. Muda wote Dominick alikuwa akilia tu huku akiomba msamaha japokuwa hakuwa amelifahamu kosa lake.
Dominick akapelekwa mpaka katika sehemu ambayo ilikuwa na nyasi ndefu na kulazwa chini. Kibra akachomoa bunduki yake na kuanza kuisafisha kwa mbwembwe zote. Bado Dominick alikuwa akilia ingawa hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kumjali.
“Tutakuua kifo kilichojaa maumivu, ili utakapokuwa ukiumia, basi ujute kwa nini ulikuwa ukipenda kuandika mambo ya watu gazetini” Kibra alimwambia Dominick huku akimwuelekezea bunduki.
“Paaaaaa....” Mlio wa risasi ulisikika, Dominick alikuwa akiugulia kwa maumivu huku akiushika mguu wake.
Damu zilikuwa zikimtoka mguuni, risasi ilikuwa imepenya katika mguu wake. Kilio kikubwa ndicho ambacho kilikuwa kikisikika kutoka kwa Dominick. Kibra na wenzake wakabaki wakicheka, walionekana kuyafurahia maumivu ya Dominick.
“Tutaendelea hivi hivi mpaka pale utakapoanza safari ya kuifuata familia yako” Kibra alimwambia Dominick huku akiwa amemuelekezea tena bunduki.
“Paaaaaaa.....” Mlio wa risasi ulisikika kwa mara ya pili.
“Paaaa... paaaa....paaaa...paaaaa...” Milio mingine ya risasi ikasikika katika eneo hilo, damu zikatapakaa katika eneo hilo, ukimya ukatawala, hakukuwa na sauti yoyote ambayo ilisikika katika kipindi hicho hata ile sauti ya kilio cha Dominick haikusikika tena.
************
Siku ziliendelea kukatika, wafanyakazi wa kampuni ya magazeti ya Hold on Publishers wakaonekana kuchanganyikiwa. Siku nyingi zilikuwa zimekatika pasipo Dominick kuonekana. Wasiwasi ukazidi kuogezeka zaidi hasa mara baada ya Edmund kusema kwamba hakuwa amelala kwake karibu siku tano.
Taarifa zikatolewa katika vituo mbalimbali vya polisi na kazi ya kumtafuta Dominick kuanza. Dominick alitafutwa katika sehemu nyingi lakini wala hakupatikana. Taarifa zikatolewa gazetini, kila mtu ambaye aliiona taarifa ile ya kupotea kwa mwandishi ambaye alikuwa akiandika mambo mengi kuhusiana na viongozi wezi alibaki na mshangao.
Maswali mengi yalikuwa yakimiminika vichwani mwa Watanzania, upotevu wa Dominick ukaonekana kumtia wasiwasi kila mmoja. Tetesi za Dominick kuuawa zikaanza kutapakaa katika kila kona ya jiji la Dar es Salaam. Kila mtu aliamini kuwa Dominick aliuawa na watu ambao walikuwa wameiteketeza familia yake.
Baada ya miezi mitatu, mazishi yakaanza kufanyika. Watu wengi walishiriki katika mazishi ya Dominick, picha yake kubwa ilikuwa mbele ya jeneza lake. Watu ambao walikuwa na upendo mkubwa kwa Dominick, walilia mpaka wengine kupoteza fahamu.
Nchi ya Tanzania ikaonekana kumpoteza mtu shujaa, mtu ambaye alikuwa akitaka Watanzania waishi katika maisha mazuri kupitia uandishi kwa kuwataja viongozi ambao walikuwa wakiiba fedha za wananchi. Jeneza likafukiwa katika makaburi ya Kinondoni, hakukuwa na mtu aliyeamini kama Dominick waliyekuwa wakimpenda alikuwa ameuawa.
“Acha akapumzike na familia yake” Kijana mmoja aliwaambia wenzake huku macho yake yakiwa mekundu.
Kampuni ya kutengeneza magazeti ya Hold On Publisher ikatoa siku thelethini za kuomboleza. Wafanyakazi wa kampuni hiyo walipunguziwa masaa mawili ya kufanya kazi ndani ya mwezi huo. Siku ziliendelea kukatika mpaka mwaka kuisha, Dominick akasahaulika vichwani mwa watu.
“Mwaka jana tulikuwa na mwandishi mzuri sana. Aliandika wizi ambao ulikuwa ukifanyika katika sekta mbalimbali, namkumbuka mtu huyu, familia yake iliuawa kabla ya yeye mwenyewe kuuawa na maiti yake kutoonekana mpaka leo” Mwandshi mmoja alimwambia mwenzake mara baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikubwa cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalism).
“Namkumbuka sana. Si yule Dominick aliyekuwa akiitwa shujaa. Namkumbuka sana, katika maisha yangu sitoweza kumsahau mtu kama yule” Mwandishi mwingine alisema.
“Mungu Amlaze Pahali Pema Peponi”
“Amen”
*************
Mzee Mrisho alikuwa mtu maarufu sana katika sehemu yote ya Mbezi. Kila mtu ambaye alikuwa akiishi Mbezi alikuwa akimfahamu mzee huyu kutokana na biashara yake aliyokuwa akiifanya ya kuuza nyama katika moja ya bucha lake lililokuwa Mbezi kwa Yusufu.
Nyama mbalimbali zilikuwa zikipatikana buchani kwake hali ambayo iliwafanya watu wengi kumiminika buchani hapo kununua nyama kwa ajili ya mboga. Nyama nyingi zilikuwa zikipatikana buchani hapo, swala, nyati, mbuzi na ng’ombe zilikuwa ni moja ya nyama ambazo zilikuwa zikipatikana kwa wingi.
Mzee Mrisho alizaliwa miaka hamsini iliyopita mkoani Shinyanga. Alizaliwa katika familia ya mwindaji, baada ya miaka kadhaa nae akaanza kuelekea kuwinda pamoja na baba yake. Mpaka anakuja kufikisha miaka kumi na nane, Mrisho alikuwa mwindaji mzuri.
Alipofikisha miaka ishirini, baba yake alifariki dunia, kazi ya uindaji ikabakia kwake, kila siku alikuwa akielekea porini kuwinda. Kila mtu aliyekuwa akiishi Shinyanga alikuwa akimfahamu Mrisho ambaye maisha yake yalikuwa yakiendeshwa na biashara hiyo.
Kila siku jina la Dar es Salaam lilikuwa kichwani mwake, jiji hilo ambalo alikuwa akilisikia masikioni mwake kutoka kwa watu mbalimbali lilionekana kumvutia. Mrisho akajikuta akitamani kufika jijini Dar es Salaam na kuanza maisha huko.
Alichokifanya Mrisho ni kuanza kuzihifadhi fedha alizokuwa nazo. Baada ya miaka miwili alikuwa na fedha za kutosha ambazo zilimfanya kusafiri kuelekea Dar es Salaam. Mrisho alionekana kuwa mshamba kwa kila kitu ambacho alikuwa akikiona, majengo mazuri pamoja na mpangilio wa nyumba vilikuwa vitu ambavyo vilimvutia kupita kiasi.
Mrisho hakutaka kukaa tu nyumbani, akaanza kutafuta kazi. Kazi hazikuwa rahisi kupatikana, alitembea umbali mrefu kutafuta kazi lakini hakukuwa na mafankio yoyote yale. Miaka ilizidi kukatika, Mrisho akaamua kuanza biashara ya kuuza genge.
Mara baada ya kusikia juu ya wanyama waliokuwa wakipatikana katika msitu wa Nyakipande, Mrisho akavutiwa, akaamua kuhamia Mbezi. Huko ndiko ambako akaanza kazi kama ile ambayo alikuwa akiifanya Shinyanga.
Kila siku alikuwa akitoka asubuhi kuelekea katika msitu wa Nyakipande ambako alikuwa akiwinda na kurudi jioni huku akiwa na vitoweo vya kutosha. Biashara ya kuuza nyama ikaonekana kuchanganya, akaamua kuanzisha bucha ambalo alikuwa akiuza nyama mbalimbali.
Watu walikuwa wakimiminika. Kila baada ya siku mbili alikuwa akiingia porini kuwinda. Mrisho akaonekana kuuzoea msitu wa Nyakipande, kila kona za msitu huo alikuwa akizifahamu vilivyo. Mrisho hakuwa akipata kazi kutokana na makazi mengi ya wanyama kuyafahamu.
Miaka iliendelea kwenda mbele hadi alipokuja kuoa na kupata watoto. Serikali ikakataza uwindaji ambao ulikuwa ukifanyika katika msitu wa Nyakipande, ulinzi mkali ukawekwa. Maisha yalionekana kuwa tofauti kwake lakini baada ya muda, maisha yakaanza kurudi katika hali ya kawaida kama zamani.
Akaanza kuwinda usiku na kurudi nyumbani asubuhi. Hayo ndio yalikuwa maisha yake, aliingia msituni usiku na kurudi asubuhi. Nyama ambazo alikuwa akizipata porini ndizo ambazo alikuwa akiziuza buchani ambako mtoto wake, Selemani ndiye alikuwa msimamizi wa bucha hilo.
“Twendeni kule” Sauti ilisikika msituni.
Mzee Mrisho aliisikia sauti ile vizuri, akachukua gobole lake na kujificha. Tayari akili yake ilikwishamwambia kuwa watu hao ambao walikuwa wakiongea walikuwa mapolisi ambao kazi yao ilikuwa ni kuhakikisha ulinzi msituni mule.
Sauti za watu wale ziliendelea kusikika. Mzee Mrisho alitaka kupiga hatua kurudi lakini akajikuta akishindwa kufanya hivyo. Alijikuta akivutiwa zaidi kuwafuatilia watu hao ambao alikuwa na uhakika kuwa hawakuwa walinzi.
“Hawa sio walinzi, ulinzi gani usiku namna hii?” Mzee Mrisho alijiuliza.
Akaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako watu hao walisikika wakielekea. Mgobole wake ulikuwa makini mkononi mwake, alionekana kutaka kujitetea na hatari yoyote ambao ingeweza kutokea mahali hapo.
Aliendelea kuwafuatilia watu hao huku akijifichajificha. Safari ya watu wale ikashia katika sehemu ambayo ilikuwa na uwazi mkubwa. Ingawa kulikuwa na giza lakini mzee Mrisho alikuwa akiona kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea.
Mtu mmoja aliwekwa chini, sauti ya mtu yule haikuwa ikisikika vizuri hali ambayo aliigundua kwamba alikuwa amezibwa mdomo kwa kutumia kitambaa. Mwanaume mmoja akaonekana akichomoa bunduki na kisha kumuelekezea mtu yule ambaye alikuwa chini.
“Tutakuua kifo kilichojaa maumivu, ili utakapokuwa ukiumia, basi ujute kwa nini ulikuwa ukipenda kuandika mambo ya watu gazetini” Sauti ya mwanaume mmoja ilisikika.
Mlio wa risasi ukasikika, mwanaume yule aliyekuwa chini alisikika akipiga kelele za maumivu. Tayari mzee Mrisho aliona hakukuwa na amani mahali pale, alijiona kuwa na nafasi ya kufanya chochote ili aokoe maisha ya mwanaume yule.
Wanaume wale watatu walibaki wakicheka hali iliyoonyesha kwamba walikuwa wakiyafurahia maumivu ya mwanaume yule aliyekuwa akilia. Mwanaume yule ambaye alimpiga risasi mwanaume yule aliyekuwa chini, akamuelekezea tena bunduki tayari kwa kumpiga risasi nyingine.
Mzee Mrisho akajikuta akichukua mgobole wake na kumwelekezea mwanaume yule aliyekuwa ameshika bunduki. Hakutaka kuchelewa, hapo hapo akamfyatulia risasi ya kichwa, mwanaume yule akaanguka chini kama mzigo wa viazi.
Hata kabla wale wenzake hawakujua wafanye nini, wakashtukia wakipigwa risasi za vifuani, damu zikatapakaa mahali pale. Wote wakaanguka chini ambako wakaanza kurusha mikono na miguu yao, baada ya muda, wakatulia hali iliyoonyesha tayari walikuwa wamekufa.
Mzee Mrisho akachomoka kutoka kichakani na kumfuata mwanaume yule aliyekuwa akilia kwa maumivu makali, akambeba na kuanza kuondoka nae pasipo kuongea nae kitu chochote kile. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza, ilikuwa safari ndefu huku mwanaume yule akiwa mgongoni mwake.
Alitumia masaa mawili, akawa amekwishafika nyumbani huku ikiwa saa tisa usiku. Mkewe akamfungulia mlango, mshangao mkubwa ukampata, hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mpaka mumewe kurudi na mtu ambaye alionekana kuwa kama maiti.
“Kuna nini tena mume wangu?” Bi Sikujua aliuliza.
“Bandika maji jikoni kwanza” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
Pasipo kuuliza kitu chochote kile, Bi Sikujua akaelekea jikoni ambako akabandika sufuria iliyokuwa na maji na kisha kurudi sebuleni ambako mzee Mrisho akaanza kumuelezea kila kitu kilichotokea.
“Kwa hiyo haumfahamu kabisa?”
“Ndio. Niliamua kumsaidia, niliona akiwa katika hali ya hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
Maji yalipochemka, yakaletwa na mzee Mrisho kuanza kufanya kazi ya kuiondoa risasi katika mguu wa mwanaume yule. Kilio kikubwa kilisikika lakini mzee Mrisho hakuonekana kujali, aliendelea na kazi ile mpaka risasi ilipotoka na kisha kumfunga bandeji.
“Asubuhi ikifika, tutaelekea hospitalini kumnunulia dawa” Mzee Mrisho alimwambia mkewe, Bi Sikujua.
“Kwa nini tusimpeleke hospitalini tu?”
“Hapana. Maisha yake bado nayaona kuwa katika hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
************
Maisha yaliendelea mbele, Dominick hakuruhusiwa kutoka nje, kila siku maisha yake yalikuwa ndani ya nyumba ya mzee Mrisho. Kila kitu alikuwa akikipata ndani ya nyumba ya mzee Mrisho, maisha yake hayauonekana kuwa na amani nje ya nyumba hiyo.
Kitu alichokuwa akikifahamu ni kwamba kila siku angekuwa akitafutwa kwa lengo moja tu la kuuawa. Hakuamini kama watu ambao waliwatuma vijana wale wangeridhika kama wangepeta taarifa kuwa mtu ambaye alitakiwa kuuawa hakuuawa kama ilivyotakiwa iwe.
Dominick akajiona kuingia katika vita, vita ambayo alitakiwa kuimaliza kwa mikono yake mwenyewe. Kila siku maombi yake yalikuwa juu ya kumfahamu mtu au watu ambao walikuwa nyuma ya mpango wa kuuawa kwake.
Kila siku Dominick alikuwa akiyafikiria maneno yale ya BoT ambayo yalikuwa yameandikwa nje ya geti lake katika siku ambayo nyumba yake ilichomwa moto na familia yake yote kuangamia. Maneno yale yalieleweka vizuri na hata makao makuu ya idara ile alipafahamu vilivyo.
Kitu alichokijua ni kwamba hakukuwa na mtu yeyote kutoka katika idara ile ambaye alihusika kutokana na yule mtu aliyefanya ufisadi kuuawa kwa kulegezewa breki ya gari lake alipokuwa akielekea Dodoma. Bado Dominick alionekana kuchanganyikiwa, hakuelewa kabisa mtu ambaye alikuwa nyuma ya tukio hilo.
Kila siku alitamani kuwasiliana na marafiki zake ili kuwapa taarifa juu ya uwepo wake katika nyumba ya mzee Mrisho lakini kila alipotaka kufanya hivyo, alisita kwa kuogopa kujulikana kuwa yuko hai.
Kila siku alikuwa mtu wa kulala ndani, hakutakiwa kutoka nje wala hakutakiwa mtu yeyote kufahamu kuwa yuko ndani ya nyumba ile.
Mpaka taarifa za kifo chake zilipokuwa zinatangazwa, yeye mwenyewe alikuwa akiangalia katika televisheni. Dominick alibaki akifurahia kwani alijua kuanzia kipindi hicho asingeweza kupata usumbufu wowote ule.
Siku ziliendelea kukatika mpaka mwezi mmoja kupita, bado Dominick alikuwa akishinda ndani. Hakutakiwa kutoka kabisa nje ya nyumba hiyo, na kama alitaka kutoka, basi kitendo hicho kilitakiwa kufanyika usiku, muda ambao hakukuwa na watu wengi mtaani.
Hayo ndio maisha ambayo Dominick alikuwa akiishi. Kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea, alikuwa akipata taarifa kupitia televisheni na magazeti ambayo mzee Mrisho alikuwa akiyaleta.
“Kila mtu anajua kuwa uliuawa, hakuna mtu ambaye anajua kama uko hai” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
“Kwa hiyo wanachofahamu kuwa kwa sasa nipo kaburini?”
“Ndio. Tena umeoza kabisa” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
Dominick hakutaka kuendelea kukaa sebuleni hapo, moja kwa moja akainuka na kuaelekea chumbani. Mzee Mrisho alibaki sebuleni pale akiangalia televisheni. Dakika ziliendelea kukatika, mzee Mrisho hakutaka kwenda chumbani mpaka muda wa taarifa ya habari utimie, aliendelea kusubiri zaidi na zaidi.
Huku akiendelea kuwa sebuleni hapo, mara umeme ukakatika na giza kutawala mahali hapo. Mzee Mrisho akaonekana kukasirika, akainuka kutoka pale alipokaa na kuelekea kule ilipokuwa soketi ya umeme na kuizima.
Hata kabla hajapiga hatua kuelekea chumbani, mara akasikia mlango ukigongwa. Mzee Mrisho hakuonekana kuwa na wasiwasi, akaanza kupiga hatua kuufuata mlango na kuufungua.
Mzee Mrisho akashtuka kupita kawaida, mdomo wa bunduki ulikuwa umeelekezewa usoni mwake na mtu ambaye hakuweza kumhamu kutokana na giza lililokuwa mahali pale. Hata kabla mzee Mrisho hajaamua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akaamriwa kuingia ndani.
“Jamani, kuna nini tena?” Mzee Mrisho aliuliza huku akionekana kuwa na hofu.
“Tutakachohitaji, tutataka kupatiwa. Na kama hatutopatiwa, milio ya risasi itakwenda kusikika mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho huku wenzake wawili wakiwa wamekwishaingia ndani ya nyumba ile.
“Mnataka nini? Mnataka nini jamani?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikizidi kuongezeka.
Hata kabla mwanaume yule hajajibu chochote juu ya kile walichokuwa wakikitaka, Bi Sikujua akatokea sebueni pale. Akaamriwa anyamaze kimya, sauti yoyote kutoka kwake isisikike. Mwanaume mmoja alimsogelea na kumvuta katika upande aliokuwa mzee Mrisho.
“Tunamuhitaji mtu wetu” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho
“Mtu gani jamani? Mbona mnanichanganya” Mzee Mrisho aliuliza.
“Unakumbuka nilichokuambia? Unakumbuka nilikwambia nini nilipoingia hapa?” Mwanaume yule aliuliza huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekasirika.
“Ndio. Ninakumbuka”
“Basi tunamuhitaji mtu wetu, hatuna muda mwingi wa kukaa mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
3
“Jamani, mtu gani ambaye mnataka mimi niwape?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikiongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele.
“Tunamuhitaji mwandishi wa habari. Mwandishi yule mbeya” Mwanaume yule alimwambia.
“Mwandishi gani jamani?”
Yule mwanaume hakuongea kitu, mpaka muda huo tayari aliona kama anafanyiwa mzaha, akaivuta bunduki yake kwake na kuikoki hali iliyoonyesha alikuwa tayari kumfyatulia risasi mzee Mrisho. Bi Sikujua alikuwa akilia tu, hakuamini kama muda huo walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi na watu ambao walionekana hatari, watu waliokuwa wameshika bunduki.
“Moja... niambie. Mbili.... niambie. Ta...”
“Subiri baba. Mimi nitakwambia ukweli” Bi Sikujua alimwambia.
“Ukweli gani?”
“Juu ya huyo mnayemtafuta”
“Tuambie yuko wapi?”
“Chumbani. Yuko chumbani. Naomba mmuache mume wangu” Bi Sikujua alimwambia.
“Chumba gani?”
“Chumba cha tatu koridoni upande wa kushoto” Bi Sikujua aliwaambia.
“Una bahati sana, mkeo ameokoa maisha yako” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
Hawakutaka kupoteza muda, wote wakaanza kuelekea katika korido ile na kisha kuanza kuufuata mlango wa chumba kila. Walipoufikia, wakajaribu kuufungua, mlango ulikuwa mgumu hali iliyoonyesha kuwa ulifungwa kwa ndani. Wakaanza kuugonga kifujo fujo lakini mlango wala haukufunguka.
“Tuuvunjeni” Mwanaume yule aliyeonekana kuwa kiongozi aliwaambia wenzake na hatua za kuuvunja mlango kuanza.
Ni ndani ya dakika moja tu, mlango ukavunjika. Wakawasha tochi ambazo walikuja nazo mahali hapo na kuanza kumulika ndani ya kile chumba alichokuwa Dominick.
“Yule pale kitandani” Mwanaume mwingine aliwaambia wenzake na wote kuanza kumfuata Domonick kitandani huku bunduki zao zikiwa tayari.
***********
Kikao cha dharura kilikuwa kinaendelea kufanyika ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa miongoni mwa vyumba vizuri vilivyokuwa katika nyumba ambayo ilikuwa ikiheshimiwa sana, nyumba ya kifahari iliyojengwa katika mtaa wa kifahari wa Osterbay.
Watu watatu ambao walikuwa wazee wa makamo ndio ambao walikuwa wamejikusanya ndani ya chumba hicho. Bado ajenda ambayo walikuwa wakiizungumzia katika kipindi hicho haikupatiwa muafaka kabisa. Kwa wakati huo, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa.
Dada waliyemtuma katika kufanya kazi ya kumuita Dominick katika hoteli ya New Africa alifanya kazi kama vile ilivyotakiwa kufanywa. Wasiwasi wao bado ulikuwa juu ya vijana wale ambao waliondoka na Dominick kuelekea katika msitu wa Nyakipande.
Bado hawakupata taarifa yoyote juu ya kilichoendelea msituni. Mara kwa mara walikuwa wakijaribu kuwapigia simu, simu hazikuwa zikipokelewa zaidi ya kuita mpaka kuzima. Mambo haya yote yakaonekana kuwatia wasiwasi.
Kikao kikaendelea zaidi na zaidi hadi kufikia muafaka wa kuwatafuta vijana wengine ambao wangeanza kufuatilia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea msituni. Kutokana na usiku kuwa umekwenda sana, wakaahirisha kikao ambacho kilitarajiwa kufanyika tena kesho.
Siku iliyofuata vijana watatu wakatafutwa na kupewa mavazi ya kipolisi pamoja na kuwa na mbwa mmoja ambaye angetumika katika kunusa nusa ndani ya msitu ule. Safari ya kuelekea katika msitu wa Nyakipande ikaanza mara moja.
Mara baada ya vijana wale kuingia msituni wakaanza kuwatafuta watu wale ambao walikuwa wametumwa kuifanya kazi waliyopewa jana usiku. Walitembea sana msituni huku wakiongozana na mbwa ambaye alikuwa makini kunusa katika kila njia.
Hakukuwa na dalili zozote za kuwapata vijana wale kitu ambacho kiliwapelekea kumfuata mbwa kila sehemu alipotaka waelekee. Mbwa aliendelea kunusa ardhini huku akipita katika kila njia ambazo aliziona kuwa sahihi kwake. Ni ndani ya dakika tano tu, wakafika katika eneo ambalo lilikuwa na nyasi fupifupi.
Wote wakaanza kuangalia katika eneo hilo, miili ya watu watatu iliyokuwa na michirizi ya damu ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao. Kwa haraka wakapiga simu kwa wazee wale ambao walikuwa wamewatuma na kuwapa taarifa juu ya kile walichokuwa wamekiona.
“Kama ni hivyo, basi rudini” Sauti ya mzee mmoja iliskika.
“Turudi pamoja nayo?”
“Nini?”
“Hii miili”
“Hapana. Iacheni, hatuna kazi nayo”
“Sawa mkuu”
“Kuna bunduki walizokuwa wanazitumia mahali hapo?”
“Ndio”
“Hizo njooni nazo”
“Sawa” Kijana yule alijibu na kisha kukata simu.
Wazee walionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha vijana wao kupigwa risasi na kisha Dominick kutoweka kilionekana kuwachanganya zaidi. Kila wakati walikuwa wakijiuliza ni kwa jinsi gani Dominick aliweza kupambana na vijana wao watatu waliokuwa na bunduki na kuwashinda nguvu.
Walichokifanya baada ya vijana wao kurudi ni kuwapa kazi ambayo vijana wale wengine walishindwa kuifanya. Dominick hakutakiwa kuwa hai tena, tayari alionekana kuwa hatari katika maisha yao kama tu wangemwacha aendelee kuvuta pumzi ya dunia hii.
Wakawatuma mitaani kuhakikisha Dominick anapatikana na kuuawa. Miezi miwili ilipita na ndipo taarifa za Dominick kufa zikaanza kutapakaa. Wazee wa hawakutaka kukubali kabisa. Ukweli waliujua kwamba Dominick hakuwa amekufa kama ilivyotangazwa, alikuwa hai akiwa amejificha sehemu fulani.
“Mtafuteni katika kila sehemu, ila Mbezi ndio muitolee macho sana” Mzee mmoja aliwaambia vijana wale.
“Sawa mkuu”
Dominick akaanza kutafutwa katika maeneo mengi ya Mbezi. Kazi haikuwa nyepesi hata kidogo, katika kila kona ambayo walikuwa wakifika, Dominick hakuwa akionekana kabisa. Siku ziliendelea kukatika lakini bado Dominick alionekana kuwa adimu kupatikana.
“Kuna tetesi zinasikika kuwa kuna nyumba ina mgeni ambaye hutoka nje usiku sana” Mmoja wa vijana wale waliotumwa na wazee wale, Pius aliwaambia wenzake.
“Nyumba gani?”
“Bado sijaifahamu, ila inatubidi tuendelee kuchunguza”
Uchunguzi wa kuigundua nyumba hiyo ukaanza mara moja, mara kwa mara walikuwa wakiwaaita vijana mbalimbali na kuwauliza swali juu ya nyumba hiyo.
“Hata mimi nimesikia. Ila si unajua umbea, kwanza mtu atakaaje na mtu pasipo kumtoa nje. Huo uzushi” Kijana mmoja alimwambia Pius.
“Kwani nyumba yenyewe ipi?”
“Kwani wewe mgeni maeneo haya? Hata nyumbani kwa mzee Mrisho haupafahamu?” Kijana yule alimuuliza Pius huku akionekana kumshangaa.
“Simjui yeyote huku. Bado mimi ni mgeni, nakaa hapo mtaa wa nyuma. Unamjua mzee Ally Mangushi?” Pius alisema na kuuliza swali.
“Yule mzee mfupi mwenye upara?”
“Ndio. Nyumbani kwake ndipo nilipopanga” Pius alimwambia kijana yule.
Pius hakutaka kuacha kuzungumza na kijana yule, muda wote alikuwa akiongea nae kama njia mojawapo ya kutafuta mazoea. Kijana yule akaonekana kumzoea Pius kana kwamba alikuwa rafiki yake wa muda mrefu.
“Ulisema nyumba ipi?”
“Kwa mzee Mrisho. Mzee mwindaji. Subiri akipita nitakuonyeshea”
“Hapana. Usifanye hivyo, kwani nyumba yenyewe iko wapi?”
“Kule mbele, nyumba yenye bucha kwa nje”
“Nimekwishaikumbuka. Kumbe pale ndipo anapokaa?”
“Ndio hapo hapo”
Pius hakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, tayari alikwishaonekana kupata kile ambacho alikuwa akitaka ukipata kwa wakati huo. Moja kwa moja akaanza kuwasiliana na wazee ambao walikuwa wamemtuma na kuwapa taarifa juu ya kile kinachoendelea kwa wakati huo.
“Msimcheleweshe. Mkimpata muueni”
“Sawa. Ila hamtaki hata kiungo kimoja kutoka mwilini mwake?”
“Kama itawezekan, tuleteeni kichwa”
Mipango ikaanza kufanyika usiku huo. Pius akawaita wenzake na kuwaambia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea. Hawakutaka kupoteza muda, walitaka kumtia mikononi Dominick hata kabla siku nyingine haijafika.
Wakapanga mpango mzima na hatimae wazo la kuzima umeme wa nyumba ile kupewa kipaumbele. Walitaka kuzima kwanza umeme wa nyumba ile kutoka katika chuma la umeme la nyumba ile kwa kutoruhusu umeme kuingia ndani na kisha ndipo wavamie.
“Hilo wazo zuri sana. Tufanyeni hivyo hivyo” Kimbetu alimwambia Pius.
Usiku ulipoingia, kazi ikaanza mara moja Wakaelekea katika duka la vifaa mbalimbali na kununua plaizi kwa ajili ya kukata waya wa umeme ambao ulikuwa ukipitisha umeme katika nyumba ya mzee Mrisho. Mara walipopata kila kitu walichokuwa wakikihitaji, wakajiandaa na kazi.
Usiku ulipoingia, wakasubiri mpaka ifike saa mbili. Muda ulipotimia, moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea katika eneo ilipokuwa nyumba ile.
“Kwa hiyo tunaanza kukata waya?”
“Ndio”
“Basi msitake kupoteza muda, mtakapoona umeme umezimika, pigeni hodi” Jonas aliwaambia.
“Poa” Pius aliitikia na kisha yeye na Kimbetu kuanza kuelekea mlangoni.
Jonas akaanza kupanda katika ukuta wa nyumba ile mpaka pale alipolifikia chuma la umeme na kisha kuchukua plaizi na kuukata waya uliokuwa ukipitisha umeme ndani ya nyumba ile. Umeme ndani ya nyumba ile ukakatika.Pius na Kimbetu hawakutaka kupoteza muda, wakaanza kugonga mlango.
*********
Dominick alikuwa amechoka kukaa sebuleni, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea katika vituo mbalimbali vya televisheni aliviona kuwa kama vikimpotezea muda. Akainuka katika kochi alilokuwa amekalia na moja kwa moja kuelekea chumbani huku akimwacha mzee Mrisho sebuleni pale.
Dominick akapanda kitadani, hata kabla hajachukua muda mrefu kitandani pale, akaanza kusikia minong’ono kutoka nje ya nyumba ile karibu kabisa na dirisha la chumba kile. Kwa kasi ya ajabu, Dominick akainukana kufungua pazia kuchungulia nje.
Vijana watatu walikuwa wamesimama nje karibu kabisa na dirisha la chumba chake. Dominick hakutaka kujiuliza watu wale walikuwa ni wakina nani, moja kwa moja akatoka nje ya chumba kile na kuelekea koridoni ambako akaanza kupiga hatua kuelekea jikoni.
Alipofika jikoni akaufungua mlango na kisha kutoka nje. Dominick akaanza kukimbia kuelekea mbali kidogo na nyumba ile, alipofika umbali fulani, akasimama kwa kujificha katika ukuta wa nyumba moja na kuanza kuchungulia kuona ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea.
Kwa mbali akamuona mwanaume mmoja akipanda katika ukuta ambao ulikuwa karibu na chuma lililokuwa limeshikiria nyaya iliyokuwa ikiingia ndani ya nyumba ile. Wala hazikupita hata sekunde ishirini, umeme ndani ya nyumba ile ukakatika.
Vijana wawili wakaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni ambako baada ya kuufikia, wakaanza kugonga. Wala haukupita muda mrefu, mzee Mrisho akaufungua mlango ule.
Kila kitu ambacho kiliendelea baada ya vijana wale kuingia ndani ya nyumba ile wala Dominick hakuwa akikifahamu. Alibaki pale katika kiambaza cha ukuta huku akiendelea kuangalia kule ilipokuwa nyumba ya mzee Mrisho.
Wala hazikupita dakika nyingi, akawaona wanaume wale wakitoka nje ambako mmoja wao akatoa amri wajitawanye mahali hapo.
“Atakuwa yupo karibu na hapa. Mtafuteni” Sauti ya Pius iliskika na vijana wale wawili kutawanyika kumtafuta Dominick ambaye waliamini kwamba hakuwa mbali na mahali hapo.
Dominick hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, tayari alikwishaona kuwa wanaume wale hawakuwa na amani hata kidogo. Kwa kasi ya ajabu nae akaanza kukimbia kuelekea mbele zaidi ya mtaa ule.
Dominick alipofika katika barabara ya lami, akasimamisha taksi moja ya kukodi na kuingia ndani. Kutokana na mwanga hafifu uliokuwepo ndani ya gari lile, dereva hakuweza kumjua kama mteja ambaye alimpakiza alikuwa Dominick, mwandishi ambaye alisemekana kufa miezi mitatu iliyopita.
Taksi ilisimama nje ya nyumba moja ambayo ilikuwa imezungushiwa ukuta pamoja na kuwa na geti kubwa la rangi nyeupe. Dominick akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi ambacho kilihitajika na dereva yule kisha kuteremka na kuanza kuugonga mlango.
Mlinzi alisikika akielekea getini pale ambako akafungua geti na moja kwa moja kuingia ndani. Mlinzi akamsimamisha Dominick huku akionekana kukasirika na kitendo kile cha kuingia moja kwa moja katika eneo la nyumba ile pasipo hata ruhusa.
“Mbona unaingia moja kwa moja hata bila kuuliza?” Mlinzi alimuuliza Dominik aliyeonekana kuchanganyikiwa.
“Samahani sana. Akili yangu haiko sawa kabisa. Edmund yupo?” Dominick alimuuliza mlinzi.
“Mbona usiku sana. Wewe nani?”
“Rafiki yake, ninafanya kazi pamoja nae”
“Namba yake ya simu si unayo hapo, kwa nini usimpigie?”
“Hapana. Simu yangu haina chaji. Naomba ukaniitie mara moja” Dominick alimwambia mlinzi ambaye pasipo kuuliza swali jingine akaanza kuufuata mlango na kubonyeza kengele.
Wala haikupita hata dakika moja, mlango ukafunguliwa na mfanyakazi wa ndani. Mlinzi akaanza kumuelezea mfanyakazi yule juu ya Dominick. Msichana yule wa kazi akaondoka na kuelekea ndani ambako baada ya muda, Edmund akatokea.
“Kuna mgeni gani?” Edmund alimuuliza mlinzi.
“Mimi hapa”
“Wewe nani?”
“Sogea karibu”
Edmund akaanza kupiga hatua kumfuta Dominick. Edmund hakuamini macho yake mara baada ya kumfikia Dominick. Hofu ilimjaa moyoni huku mapigo yake ya moyo yakiongeza kasi ya udundaji. Mtu ambaye alikuwa akionekana mbele yake, walikwishamzika miezi mitatu iliyopita, kwake, Dominick alionekana kuwa kama mzimu.
“Dominick!” Edmnd aliita huku akionekana dhahiri kutaka kukimbia.
“Ndio mimi, Edmund”
Edmund akapiga hatua zaidi, alipomfikia Dominick, akamkumbatia kwa furaha. Macho yake hayakuamini kabisa, alijiona kuwa kama ndotoni ambako muda mchache ujao angeamka na kujikuta yuko kitandani.
Wote wakaanza kuelekea ndani ambako wakakaa kochini na kisha Dominick kuanza kumuelezea Edmund kila kitu ambacho kilitokea baada ya kupotea kwake. Edmund alibaki akishangaa, hakuamini kama duniani kulikuwa na mtu aliyekuwa na bahati kama aliyokuwa nayo Dominick.
“Kwa hiyo unamaanisha hauwafahamu kabisa watu wanaokutafuta?”
“Hadi sasa sijafahamu. Ila kuna kitu nataka kukifanya na ningependa msaada wako” Dominick alimwambia Edmund.
“Kitu gani?”
“Subiri”
Dominick akaingiza mkono mfukoni na kisha kuitoa simu yake. Akaiwasha na moja kwa moja kwenda katika sehemu ambayo ilikuwa na kumbukumbu juu ya simu zote zilizoingia.
“Kuna namba hii nataka uende ukaiulizie” Dominick alimwambia Edmund huku akimpa simu.
“Namba ya nani hii?”
“Ya mwanamke yule aliyenipigia siku ile”
“Sasa nitamjua vipi?”
“Nenda katika kampuni hii ya simu, ukifika waambie uongo wowote hadi wakwambie namba hii ni ya nani na anakaa wapi. Tukimpata huyu mwanamke, kila kitu kitakuwa rahisi” Dominick alimwambia Edmund.
“Sawa”
**********
Pius akakifuata kitanda kile na kulifunua shuka. Kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amejifunika kitandani pale. Pius akalifunua shuka, ni mito tu ndio ambayo ilikuwa kitandani pale, ilikuwa imepangwa vizuri.
4
Kila mmoja alionekana kukasirika, hawakuamini kama Dominick angeweza kuwafanyia ujanja ule ambao kwao ulionekana kuwa wa kitoto sana. Walichokifanya baada a hapo ni kuanza kumtafuta katika kila kona ya chumba hicho.
Walifungua kabati na kutoa nguo zote lakini wala Dominick hakuonekana. Hawakuonekana kuridhika hali iliyowapelekea kutoa kila kitu uvunguni mwa kitanda lakini napo Dominick hakuonekana kabisa.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, kumkosa Dominick ndani ya chumba kile ilionekena kuwashangaza kupita kiasi. Kitu walichokifanya mahali pale ni wote kujitawanya na kuanza kumtafuta Dominick. Amri moja tu ndio ambao ilitolewa mahali hapo, kumuua popote pale watakapomuona.
*******
Siku iliyofuata, Edmund akaanza safari ya kuelekea katika jengo la kampuni ya simu za mkononi ya Etisalat lililokuwa Posta mpya. Tayari Edmund alikwishajua ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea mara tu atakapofika ndani ya jengo lile.
Mara baada ya kufika katika sehemu ya maulizo, akaulizia sehemu ambayo ilikuwa ikipatikana huduma ile ambayo alikuwa akiihitaji kwa wakati ule. Alipoelekezwa, moja kwa moja akaanza kuelekea kule kulipokuwa na chumba maalum.
“Nikusaidie nini?” Sauti nyembamba ya msichana ilimuuliza mara baada ya salamu.
“Kuna namba ya mtu ambaye ananitisha kila siku, ni namba ngeni kwangu, sifahamu anataka nini” Edmund alimwabia dada yule ambaye alikaa kimya kumsikiliza.
“Nafikiri ametumwa, kila siku sina amani moyoni. Natamani kumfahamu mtu huyu ili nijue ni kwa jinsi gani nitaweza kujilinda” Edmund alimwambia dada yule.
“Unafikiri anaishi hapa hapa Dar es Salaam?”
“Sifahamu. Kwa kweli sifahamu”
“Unafanya kazi wapi?”
“Mimi ni mfanyabiashara, mara kwa mara huwa ninasafiri kwenda nchi mbalimbali” Edmund alidanganya.
“Namba yenyewe iko wapi ya huyo mtu?”
Hapo hapo Edmund akaichukua simu yake na kuiangalia namba ile ambapo baada ya kuipata, akamgawia msichana yule. Kazi ya kuanza kuitafuta katika kompyuta yake iliyokuwa mezani ikaanza. Dakika mbili zikakatika, mtumiaji wa namba ile akapatikana.
“Mwenye namba hiyo anaitwa Saida Hamisi. Anaishi Sinza Makaburini” Msichana yule alimwambia Edmund.
“Kumbe Saida! Ni rafiki yangu ambaye mara kwa mara huwa tunataniana sana. Nafikiri amebadilisha namba. Nikitoka hapa, nitanunua laini nyingine na mimi nianze kumzingua” Edmund alimwambia dada yule huku akijifanya kumfahamu Saida.
“Kumbe unamfahamu?”
“Sanaaa. Nimesoma nae kuanzia msingi mpaka chuoni”
“Chuo gani?”
“I.F.M” Edmund alijibu na kisha kuondoka.
Tayari kazi ambayo alipewa alikuwa amekwishaimaliza. Ujanja alioufanya wa kujifanya kumfahamu Saida ulionekana kuwa ujanja ambao haukushtukiwa na msichana yule. Akaingia ndani ya gari lake na safari ya kuelekea nyumbani kuanza huku moyoni akiwa na shauku ya kumpa Dominick taarifa.
“Vipi?” Dominick aliuliza mara baada ya Edmund kuingia ndani.
“Poa. Nimefanikiwa”
“Kweli?”
“Ndio”
“Ni nani?”
“Msichana mmoja anakaa Sinza Makaburini, anaitwa Saida Hamisi” Edmund alimwambia Dominick.
“Safi sana. Huyu ndiye atakuwa mwanzo wa safari yangu ya kuwagundua wabaya wangu” Dominick alimwambia Edmund.
Kazi ya kumtafuta Saida ikaanza. Wakaanza kujiandaa tayari kwa safari ya kuelekea Sinza. Dakika kumi baadae walikuwa ndani ya gari wakielekea Sinza Makaburini. Ndani ya dakika kumi na tano, gari lao likasimama katika eneo lililo karibu na makaburi ya hapo Sinza.
“Samahani” Edmund alimwambia mwanaume mmoja ambaye alikuwa amekaa nje ya saluni moja.
“Bila samahni”
“Kuna dada yangu namtafuta, anaitwa Saida Hamisi”
“Umeelekezwa anakaa wapi?”
“Hapa Sinza Makaburini. Unamfahamu?”
“Mhhhh! Jina lake si geni masikioni mwangu”
“Ulikwishawahi kulisikia wapi?”
“Hapa hapa. Hebu subiri” Mwanaume yule alimwambia na kisha kuingia ndani ya saluni, alipotoka, alitoka na mwanaume mwingine.
“Kuna Saida Hamisi mmoja tu ndiye ninamfahamu”
“Yupi?”
“Anakaa hapo mbele, nyumba yenye rangi nyeupe isiyokuwa na geti” Mwanaume yule alimwambia Edmund.
Edmund akaridhika na kwa jinsi alivyoelekezwa, akarudi garini na kisha kumfahamisha Dominick kile ambacho kiliendelea mahali pale. Gari likawashwa na kisha safari ya kuelekea katika nyumba ile kuanza.
Huku wakiwa wamebakiza umbali mdogo kuifikia nyumba ile, wakashangaa watu wawili kutoka katika gari jingine lililopaki katika eneo la nyumba ile wakiteremka na kuanza kuingia ndani ya nyumba ile kifujofujo.
Tayari Dominick na Edmund walikwishaanza kuhisi kitu, wakatulia garini na kusubiria kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea mahali hapo. Wala hazikupita dakika nyingi, wanaume wale waliokuwa wameingia ndani ya nyumba ile wakaanza kutoka huku wakiwa na Saida ambaye alionekana kuwa chini ya ulinzi wao.
“Mh! Kuna usalama kweli hapa?”
“Wala hakuna, kuna kitu nafikiri kinaendelea”
Gari lile likaendeshwa mpaka barabarani na kisha safari ya kuelekea kusipojulikana kuanza. Dominick na Edmund hawakutaka kubaki mahali pale, tayari waliona kuna kitu ambacho kilikuwa kinaendelea mahali pale, wakaanza kulifuatilia gari lile.
“Hapa kuna kitu, tuendelee kufuatilia hivi hivi” Dominick alimwambia Edmund huku wakiendelea kulifuatilia gari lile ambalo likaanza kuingia katika barabara ya Nyerere kuelekea Bagamoyo.
********
Kila kitu kilionekana kwenda tofauti na mipango waliyokuwa wameipanga kabla. Kutokufanikiwa kuuawa kwa Dominick kulionekana kuwachanganya kupita kiasi. Kila siku walikuwa wakikutana na kufanya vikao vya dharura, hawakujua ni wapi walitakiwa kuanzia.
Hawakuelewa ni kwa nini vijana ambao walikuwa wakiwatuma walishindwa kabisa kufanya kazi ile ambayo walitaka ifanyike. Dominick alionekana kuwazidi ujanja vijana wao. Walipewa taarifa juu ya uwepo wa Dominick ndani ya nyumba moja iliyokuwa Mbezi, waliwatuma vijana wao kwenda kumuulia huko huko ndani ya nyumba hiyo, lakini cha ajabu, walishindwa kumuua.
Kila kitu kilionekana kwenda shaghalabaghala. Walijiona kuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha Dominick anauawa ndani ya miezi hiyo miwili. Mipango ilikuwa ikiendelea kama kawaida lakini walijiona kutakiwa kufanya kitu ambacho kingewafanya kutokujulikana na mtu yeyote juu ya uovu ambao waliufanya.
“Yule msichana” Mzee mmoja aliwaambia wenzake.
“Msichana gani?”
“Tuliyemwambia ampigie simu Dominick amuite pale New Africa Hotel”
“Amefanya nini sasa? Au anahusika na nini kwa sasa?”
“Anaweza akatoa siri ya kila kitu kinachoendelea, si unajua wasichana walivyo”
“Hiyo kweli. Kwa hiyo mnataka tufanye nini ili kujilinda”
“Tumuueni tu, hiyo ndio salama yetu ya kutokujulikana”
Hayo ndio maamuzi ambayo yaliafikiwa katika chumba ambacho walikuwa wamefanya mkutano wa siri. Benard, mvulana ambaye aliwaunganisha wazee hao watatu na Saida akaitwa na kuelezwa kwamba Saida alikuwa akihitajika kwa kazi nyingine mahali hapo.
Benard akaanza kuwaelekeza mahali msichana huyo alipokuwa anakaa. Hakukuwa na muda wa kupoteza tena, kila kitu kilitakiwa kufanyika kwa haraka haraka. Simu ikapigwa na baada ya dakika kumi na tano, vijana watatu wakaingia ndani ya nyumba hiyo.
“Kuna kazi moja mnatakiwa kufanya”
“Kazi gani bosi?”
“Kuna msichana tunataka apotee haraka iwezekanavyo”
“Msichana gani”
“Saida”
“Yule ambaye mlimshirikisha kipindi cha nyuma?”
“Ndiye huyo huyo” Mzee huyo aliyeonekana kiongozi kati ya wazee wale aliwaambia.
Akaanza kuwapa maelekezo juu ya mahali ambapo Saida alipokuwa akiishi kwa wakati huo. Maelekezo yalichukua dakika tano, vijana wote wakaonekana kuelewa mahali ambapo Saida alipokuwa akikaa.
“Kwa hiyo tumuue humo humo ndani?”
“Hapana, mchukueni na mumpeleke sahemu yoyote ile. Mtakapomuua, tuwasiliane basi”
“Sawa bosi”
Vijana wale wakaanza safari ya kuelekea Sinza huku akili yao ikiwa na lengo moja tu la kufanya mauaji. Wakaziangalia bunduki zao ambazo zilikuwa na risasi za kutosha. Walichukua dakika kumi na tano mpaka kufika Sinza Makaburini ambapo wakateremka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba ile iliyokuwa imepakwa rangi nyeupe. Hawakupiga hodi, wakaingia ndani.
Saida alikuwa amekaa kochini huku akiangalia filamu ya Kitanzania iliyoigizwa na msanii Steven Kanumba. Ghafla akashtuka kuona watu watatu waliokuwa na bunduki wakiingia ndani. Hata kabla hajafanya kitu chochote kile, akashtuka akivamiwa na kuwekwa chini ya ulinzi.
“Ukipiga kelele, ukionyesha mgomo wowote au ukiuliza swali, roho yako itakuwa halali yetu” Pius alimwambia Saida ambaye alikuwa akitetemeka tu.
Wote wakaanza kuelekea nje huku Saida akiendelea kuwa chini ya ulinzi wao. Walipotoka nje, wakaingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Bagamoyo kuanza. Saida hakuongea ktu chochote kile, alitamani kuulza juu ya kile kilichokuwa kinaendelea mahali hapo lakini kila alipokuwa akikumbuka maneno ambayo aliambiwa, alishindwa kuuliza.
“Mungu nisaidie... Mungu niokoe...” Saida alijikuta akiomba moyoni.
************
Dominick na Edmund bado walikuwa wakilifuatilia gari lile ambalo lilikuwa likeonyesha kwamba lilikuwa safarini kuelekea Bagamoyo. Hawakutaka kuliacha zadi ya mita ishirini, walikuwa wakiliangalia katika kila kona.
Bado walikuwa wakimhitaji Saida kuliko mtu yeyote katika kipindi hicho. Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika katika sehemu ambayo kulikuwa na pori la Mapinga. Gari likakata kona, likaacha barabara ya lami na kuingia katika barabara ya vumbi.
Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika katika sehemu ambayo haikuwa na dalili ya uwepo wa nyumba yoyote ile. Pius na wenzake wote wakateremka huku wakiwa na Saida na kisha kuanza kuelekea ndani ya msitu huo.
Dominick na Edmund wakalipita gari lile na kwenda kulisimamisha gari lao mbali na sehemu gari lile lilipokuwa. Wote wakateremka na kuanza kuelekea kule gari la Puis na wenzake liliposimama, walipofika karibu na eneo lile, nao wakaingia ndani ya pori lile kwa mwendo wa kunyata.
Sauti ya Sauda ilikuwa ikisikika ikipiga kelele, Dominick na Edmund wakajificha na kuanza kuchungulia kule kelele zilipokuwa zikisikika. Saida alikuwa amekaa chini huku akilia, Pius na wenzake walikuwa wameshika bunduki, walionekana kujiandaa kummiminia risasi Saida.
“Sali sala yako ya mwisho” Pius alimwambia Saida.
“Nitasali...nitasali ila kuna siri nataka kuwaambia” Saida aliwaambia.
“Unasemaje? Siri? Siri gani?” Pius alimuuliza Saida.
“Mtakaponiua mimi, na ninyi lazima mtauawa” Saida aliwaambia maneno ambayo yalionekana kuwashtua.
“Tutauawa? Kivipi?”
“Wanaona kwamba kama wakiniacha mimi nitatoa siri, lakini kwa upande mwingine, wamepanga kuwamaliza hadi ninyi, kwani watapowaacha siri itavuja juu ya uovu waliomfanyia Dominick. Kwa hiyo na ninyi lazima mtauawa” Saida aliwaambia.
Pius akashusha bunduki yake. Maneno aliyoyaongea Saida yalionekana kuwa na ukweli kabisa. Kila kitu ambacho walikuwa wakikifanya wazee wale kilikuwa siri kubwa ambayo hawakutaka ijulikane na mtu yeyote yule, hiyo ndio sababu ambayo iliwapelekea kuwatuma wao kumuua Saida.
Hawakujua ni nani angeuawa baada ya Saida. Hawakuwa na uhakika kama wazee wale wangewaacha hai kama wangekamilisha kila kitu, walijiona nao wao kuuawa kama alivyosema Saida.
“Ila kweli. Na sisi tunaweza kuuawa” Pius aliwaambia wenzake.
“Kwa hiyo tufanye nini sasa?”
“Tuondokeni”
“Tuondoke pasipo kumuua?”
“Ndio. Hauoni kama ameyaokoa maisha yetu!”
“Na wazee wakituuliza tuseme nini?”
“Kwamba tumeishafanya kazi waliyotutuma”
“Poa”
Pius na wanzake hawaktaka kuendelea kukaa mahali pale, walichokifanya ni kuanza kuondoka kurudi Dar es Salaam. Hawakutaka kuondoka na Saida, walitaka kuondoka peke yao.
“Wewe utarudi Dar peke yako” Pius aliwmwambia Saida na kisha wao kuondoka.
Saida akaanza kusali sala ya shukrani, hakuamini kama alikuwa amenusurika kuuawa katika tukio lile. Mara baada ya kumaliza kusali, akainuka kwa lengo la kuondoka, lakini hata kabala hajaondka, akashtukia akiwekwa chini ya ulinzi.
“Dominick.....!” Saida aliita kwa mshangao.
“Ndio mimi Saida. Sali sala yako ya mwisho. Ni lazima nikuue na ndio niende kuwaua watu waliokutuma” Dominick alimwambia Saida huku akionekana kukasirika.
“Naomba unisamehe Dominick. Naomba usiniue” Saida alimwambia Dominick huku akianza kulia.
“Ni lazima nikuue. Wewe si ulifanya mipango ya mimi kuuawa! Kuna sababu gani ya kukucha hai?” Dominick alimwambia Saida huku akiikoki bunduki yake.
“Naomba unisamehe” Saida alimwambia Dominick huku akipiga magoti mbele yake.
Dominick hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya akimwangalia Saida ambaye alikuwa akilia kama mtoto. Kila akikumbuka shida ambazo alizipata porini pamoja na mambo mengi yaliyotokea maishani mwake, alijiona kuwa na sababu ya kumuua Saida.
“Nisamehe Dominick....naomba unisamehe” Saida aliendelea kuomba msamaha.
“Kama utataka nikusamehe, nijibu juu ya kila swali nitakalokuuliza” Dominick alimwambia Saida huku akitetemeka kwa hasira.
“Nitakwambia. Niulize nitakwambia.....”
“Ni nani yuko nyuma ya haya yote? Ni nani ambaye aliiangamiza familia yangu? Ni nani ambaye anataka kuniua? Niambie maana ya maneno BoT kama kirefu chake si Bank Of Tanzania. Ninaitaka maana yake iliyomaanishwa na wauaji hawa” Dominick aliuliza maswali matatu mfululizo.
“Nitakwambia…nitakwambia Dominick” Saida alimwambia Dominick na kuendelea
“BoT ni kifupi cha majina matatu ya watu watatu wanayoyafaya haya” Saida alimwambia Dominick huku akiwa amepiga magoti karibu na miguu ya Dominick.
“Watu gani hao? Niambie ni watu gani hao” Dominick aliuliza kwa kukalipia huku akionekana kuwa na hasira.
“Mawaziri, mawaziri. Waziri Bonifasi wa Mali asili na Utalii, waziri Ombeni wa Miundombinu na waziri Tumaini wa Mambo ya Ndani” Saida alimwambia Dominick.
Dominick akaonekana kuchoka, hakuamini kile ambacho alikisikia masikioni mwake. Watu ambao walitajwa mahali hapo aliandika wizi wao wa mamilioni miaka miwili iliyopita, hakujua kama watu hao bado walikuwa na kisasi juu ya maisha yake.
“Yaani bado walikuwa na kisasi na maisha yangu mpaka wakaiangamiza familia yangu?” Dominick aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Edmund...Edmund...yaani watu hawa ndio waliiangaliza familia yangu? Ni lazima niwaue, ni lazima niangamize familia zao pia kama walivyoiangamiza yangu. Tena nitaziangamiza kwa kuzichoma moto na kisha kuwaua wao wenyewe. Ni lazima Edmund. NI LAZIMA……!!!” Dominick alimwambia Edmind huku akilia kama mtoto. Mwili wake ukabaki ukitetemeka kwa hasira, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kutetemeka kwa hasira.
“NI LAZIMA NIWAUE….” Dominick alisema kwa hasira huku akiondoka mahali hapo kwa mwendo wa kasi kuelekea kule walipolipaki gari.
**********
5
Dominick hakuonekana kuwa na raha kabisa, huzuni ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma ilikuwa imeongezeka zaidi. Kitendo cha kuwafahamu wabaya wake kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Hakuamini kama wale mawaziri ndio ambao wangeweza kumfanyia kitu kama kile.
Kila siku mawaziri wale walikuwa wakijifanya kuwa karibu na waandishi wa habari lakini kumbe walikuwa ni watu hatari ambao wala hawakutakiwa kusogelewa. Kila siku ambazo Dominick alikuwa akiwaona wakiongea katika vipindi mbalimbali vya televisheni, alibaki akiumia tu.
Akaamua kujipanga, alitaka kutekeleza kila kitu pasipo wasiwasi wowote wala kujulikana na mtu yeyote. Hakuona sababu ya watu wale kuendelea kuishi na wakati walikuwa wamemuumiza kwa kuiteketeza familia yake kwa kuichoma moto.
Alipanga kuwaua wote, tena si wao tu, angeanza na familia zao na kisha kuwaua wao wenyewe. Alitaka sana nao kwanza waanze kuumia kabla ya kuwamaliza. Alitamani wayaonje maumivu ambayo alikuwa ameyasikia hata kabla hawajaonja mauti.
“Nitaanza na nani sasa” Dominick alibaki akijiuliza.
“Walijiita BoT, nami nitaanza na majina yao kama jinsi yalivyo, ni lazima niwaue” Dominick alisema kwa hasira huku akijifunika shuka na kulala.
Siku iliyofuata Dominick akaanza kufanya maandalizi ya kazi yake ambayo alikuwa ameipanga kuifanya, alitamani kuifanya haraka sana hata kabla hakijaharibika kitu chochote kile. Hakuonekana kuwa na pupa, alitaka kuifanya taratibu lakini kwa umakini mkubwa sana.
Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuchukua kitabu kikubwa cha simu za mezani na kuanza kuziangalia namba za simu za ofisini mwao, alipozipata, akaziandika sehemu. Dominick hakuridhika, akaangalia na namba za simu za mezani za nyumbani kwao, nazo akaziandika pembeni pia.
“Nitahitaji unisaidie kitu kimoja” Dominick alimwambia Edmund.
“Kitu gani tena? Kukusaidia kazi yako?”
“Hapana. Kazi hii wala haihitaji msaada wa mtu yeyote, nataka kuifanya mimi mwenyewe”
“Sasa unataka nikusaidie nini?”
“Nahitaji mafuta ya petroli ya lita ishirini”
“Hilo si tatizo. Kuna jingine?”
“Labda na kiberiti pamoja na gari lako. Ile bunduki yako si unayo?” Dominick alimuuliza.
“Ninayo. Nayo pia unaitaka?”
“Ndo maana nikaiulizia”
Edmund akainuka na kwenda chumbani kwake ambako akamletea bunduki pamoja na kiberiti. Akachukua pochi yake na kutoa kiasi kilichotosha cha kununua petroli ya lita ishirini na kisha kuondoka kuelekea katika kituo cha kuuzia petroli.
Wala hakuchukua muda mrefu, akarudi, akamgawia Dominick mafuta yale na kisha kumkabidhi ufunguo wa gari lake. Dominick hakutaka kupoteza muda kubaki mahali hapo, moja kwa moja akatoka nje mpaka katika sehemu ya maegesho ya magari na kuchukua gari la Edmund.
“Nitachukua miezi mingi mpaka kurudi hapa. Nitahakikisha kazi inaanza kwa mmoja baada ya mwingine” Dominick alimwambia Edmund.
“Usijali. Kazi njema” Edmund alimwambia Dominick.
Dominick akaondoka na kuelekea katika hoteli ya La Vista Inn na kuchukua chumba. Hakutaka kuendelea kuishi nyumbani kwa Edmund katika wakati ambao atakuwa akiendelea na kazi yake ya kuuridhisha moyo wake. Huko hotelini ndipo sehemu ambayo alipanga kila kitu, namna ya kuanza kazi mpaka kuimaliza.
“Nitaanza na huyu waziri wa wa Utalii na Mali asili, Boniface Akwaiziwe. Nitaanza kuiangamiza familia yake kwanza, ili achanganyikiwe na aje Dar es Salaam kutokea Bungeni” Dominick alijisemea.
Tayari muda ulikuwa umekwenda sana. Saa ya ukutani wala haikuonekana kwenda tofauti na saa yake ya mkononi, zote zilikuwa zikimuonyesha kuwa tayari saa moja na nusu usiku. Akatoka chumbani na moja kwa moja kuanza kushusha ngazi mpaka chini ambako akaingia katika mghahawa wa chakula hapo hotelini na kuagizia chakula.
Kofia kubwa ya Malboro pamoja na miwani ambayo alikuwa ameivaa wala haikumfanya kujulikana. Alionekana kuwa mgeni kwa kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Alipomaliza kula chakula pale mghahawani, akarudi chumbani kwake kuendelea na kazi ya kupanga mbinu mbalimbali za mauaji.
“Nitaanza rasmi kesho. Ila dereva ndiye mtu wa muhimu sana kupatikana” Dominick alijisemea.
Siku iliyofuata ndio ilikuwa siku ambayo alitaka kuanza kazi. Alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika nyumba ya waziri Boniface ambako akakaa mbali kidogo na geti lile huku macho yake yakiangalia getini. Wala hazikupita dakika nyingi, akamuona mtu mmoja akipiga hodi katika geti lile.
Dominick akayapeleka macho yake katika saa yake, ilikuwa ikimuonyeshea kwamba tayari ilikuwa saa kumi na mbili na robo asubuhi. Hakuwa na shaka kwamba yule aliyekuwa akigonga hodi alikuwa dereva, mtu ambaye alikuwa akimtaka kwa udi na uvumba.
Dominick akaliwahsa gari lake na kuanza kusogea kule geti lilipokuwa, alipomfikia, akateremka na kuanza kumsogelea huku kofia na miwani vikiwa vimemkaa vizuri.
Dereva yule bado alikuwa akisubiri geti lifunguliwe ili aingie ndani, achukue gari na kumpeleka mtoto wa Waziri shuleni. Mara akashtukia kitu kikiwa kimemgusa kisogoni, alipogeuka, akakutana na mdomo wa bunduki.
Dereva akaonekana kushtuka kupita kiasi, mdomo wa bunduki ulimfanya kumuogopesha. Akayapeleka macho yake usoni mwa mtu aliyemnyooshea bunduki, hakumfahamu kabisa kutokana na kofia pamoja na miwani ambayo alikuwa ameivaa.
“Ingia ndani ya gari langu haraka” Dominick alimwambia dereva ambaye bila kubisha, na kwa nidhamu zote, akaingia huku akitetemeka.
“Shikilia usukani. Nataka uendeshe gari wewe mwenyewe” Dominick alimwambia dereva ambaye kwa haraka sana, akashikilia usukani.
“Endesha moja kwa moja kuelekea nyumbani kwako” Dominick alimwambia dereva yule.
“Kwa nini kwangu lakini? Nimekufanya nini mkuu?” Dereva aliuliza huku akitetemeka.
“Nisikilize. Sihitaji maswali, fanya kile ambacho ninakuamuru kukifanya. La sivyo, nitatawanyisha ubongo wako sasa hivi” Dominick alimwambia dereva maneno ambayo yalizidi kumtetemesha zaidi
Hakuwa na jinsi zaidi ya kuwasha gari na safari ya kuelekea nyumbani kwake kuanza. Njia nzima alikuwa akitetemeka kwa hofu, kila alipokuwa akiuangalia mdomo wa bunduki, alizidi kutetemeka. Tayari nguo zake zilikuwa zimekwishaloana kwa sababu ya jasho ambalo lilikuwa likimtoka, amani yote ilikuwa imemtoka.
Aliendesha kwa makini sana huku akitii kila kitu ambacho alikuwa akiambiwa. Gari likasimama nje ya nyumba moja ambayo ilikuwa katika ujenzi wa kuuzungushia ukuta. Dereva akasimamisha gari na kumwangalia Dominick kwa wasiwasi.
“Tu..mekw..ish..afik..a” Dereva alimwambia Dominick huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Liingize gari katika eneo la nyumba yako” Dominick alimwambia dereva yule ambaye akatii amri.
“Hautakiwi kuonyesha wasiwasi wowote. Japokuwa haunifahamu, jifanye mimi ni rafiki yako wa muda mrefu. Ukifanya vingine, nitakuua wewe pamoja na familia yako. Umenielewa?” Dominick alimalizia kwa kwa kuuliza swali.
“Nimekuelewa mkuu”
Dominick akaiweka bunduki yake kiunoni na kuifunika na fulana yake. Hakutaka mtu yeyote ajue kama alikuwa na bunduki. Dereva akatulia kama alivyoamrishwa, akaufungua mlango na kuingia ndani. Akaanza kumuita mkewe, ambaye baada ya muda, akafika sebuleni hapo.
“Mbona umerudi tena?” Mkewe, Bi Amina alimuuliza huku akionekana kushangaa.
“Nimekutana na rafiki yangu, nimeamua kuja nae hapa” Dereva, Omari alimwambia mkewe.
“Sawa. Karibu mgeni”
“Asante”
Omari akakaa kochini na kuanza kuangaliana na Dominick ambaye muda wote uso wake ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana. Bi Amina akaondoka mahali hapo na kwenda jikoni kuandaa chai. Omari hakujua ni kitu gani ambacho kilitakiwa kuendelea, akazidi kumuangalia Dominick katika hali ya kutaka kuuliza swali.
“Tumekwishafika. Kuna kingine?”
“Ndio. Nataka uende kwa bosi wako. Ninawataka watoto wake wawili pamoja na mkewe uje nao hapa. Hakikisha unakuja nao” Dominick alimwambia Mrisho.
“Sasa nitawezaje kuja nao wote?. Kwa watoto sawa. Ila kwa mkewe sijui kama itawezekana” Omari alimwambia Dominick.
“Itawezekana tu. Wewe nenda, kama haitowezekana, basi acha nimuue mkeo” Dominick alimwambia Omari ambaye akaonekana kushtuka.
“Umuue mke wangu?”
“Ndio. Sasa si utakuwa umeshindwa kazi. Ni lazima nimuue kama hautoweza kuniletea wote ambao ninataka kuwaona mahali hapa” Dominick alimwambia Omari huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea.
Omari hakuwa na jinsi, akamuita mkewe na kumuaga. Akaondoka mahali hapo huku akimuacha Dominick nyumbani hapo. Njia nzima Omari alionekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama Dominick angeweza kumuacha mkewe kama tu asingekifanya kile ambacho alitaka kifanyike. Akajiapiza ni lazima awachukue wote ambao walihitajika. Hakuonekana kuwa tayari kumpoteza mkewe.
Dominick hakutaka kuendelea kubaki mahali pale, alichokifanya ni kumuaga mkewe Omari kwa kumwambia kuwa alikuwa akielelekea sehemu fulani na baada ya muda angerudi. Dominick akatoka nje ambako akachukua gari lake na kuondoka mpaka hotelini, akaliacha na kurudi nyumbani kwa Omari kwa miguu huku kidumu cha petroli cha lita tano kikiwa mkononi mwake.
Dominick akafika na kukaribishwa tena na Amina, akatulia kochini na kuanza kunywa chai. Hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule hali ambayo Amina hakumtilia shaka hata kidogo. Kila wakati Dominick alikuwa akiiangalia saa yake, muda ulizidi kwenda lakini wala Omari hakurudi.
“Au atakuwa amekwenda polisi? Hapana hawezi kufanya hivyo” Dominick alijiuliza na kujijibu.
Wala haukuchukua muda mrefu sana, muungurumo wa gari ukaanza kusikikanje ya nyumba. Dominick akachungulia na alipoona ni gari la waziri Boniface, akatoka nje. Kwa haraka sana akaanza kulifuata, alipolifikia, Omari akateremka na Dominick kuingia ndani.
“Kazi nzuri sana. Mkeo yuko salama” Dominick alimwambia Omari huku akiingia garini na Omari akiteremka.
Kitu cha kwanza Dominick akayapeleka macho yake katika kiti cha nyuma, watoto wawili wa kike waliokuwa na sare za shule walikuwa nyuma pamoja na mama yao walikuwa wametulia. Mke wa waziri Boniface, Bi Upendo akaonekana kushtuka, tayari wasiwasi ukaanza kumuingia.
Hakujua sababu iliyompelekea Omari kuteremka na kumwachia gari mtu mwingie ambaye wala hakuwa akimfahamu. Akataka kuufungua mlango na kutoka nje, tayari milango yote ilikuwa imepigwa roki. Akateremsha kioo na kumwangalia Omari kwa uso uliojaa hasira.
“Ndio unafanya nini Omari?. Huyu ni nani na kwa nini unamuachia gari? Haujui kama hili gari ni la mtu mkubwa?” Bi Upendo aliuliza maswali manne mfululizo.
“Nimefanya hivi kwa ajili ya mke wangu mama. Kama nisingefanya hivi basi ni lazima ningempoteza mke wangu” Omari alimwambia Bi Upendo ambaye alionekana kushangaa.
Hata kabla hajauliza swali jingine, gari likaondolewa mahali hapo kwa mwendo wa kasi. Dominick hakutaka kuulizwa swali lolote lile, akaanza kuendesha gari kwa mwendo wa kasi. Lengo lake lilikuwa ni kufika katika ufukwe wa Coco kwani aliamini kwa asubuhi hiyo ya saa moja, kusingekuwa na watu wengi.
Bi Upendo alikuwa akiuliza maswali mengi huku akionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa lakini Dominick hakujibu lolote, alikuwa kimya huku akionekana kuwa na hasira. Picha ya familia yake ikaanza kuonekana kichwani mwake, nyumba ambayo ilikuwa ikiteketea ikaanza kujirudia kichwani kama mkanda wa filamu.
Taswira ya miili ya familia yake ambayo ilikuwa imeteketezwa kwa moto ikaanza kuonekana kichwani mwake. Machozi yakaanza kumtoka, hasira ikazidi kumpanda, akaanza kupaona ufukweni mbali, alitamani gari liwe na mabawa, lipae na kutua ufukweni.
“Nyamazaaaaa….!” Dominick alimwambia Bi Upendo kwa sauti ya kelele iliyojaa hasira.
“Ni lazima niwaue. NI LAZIMA” Dominick alijisemea huku akiyauma meno yake kwa hasira
********
Kundi la BoT likaonekana kujipongeza. Kila siku ilionekana kuwa ya furaha kwao. Walipongezana kwa kazi nzito ambayo walikuwa wameifanya. Taarifa za uongo walizoletewa juu ya kifo cha Dominick na kifo cha Saida zilionekana kuwafurahisha kupita kiasi.
Waliambiwa na vijana wale kuwa walimfuata Saida nyumbani kwake ambako wakakutana na Dominick ambaye wakaamua kuondoka nae mpaka porini, na huko ndipo walipoamua kuwaua wote wawili. Taarifa ile ya uongo ilionekana kuwa ya faraja kwao, hakukuwa na mtu ambaye alionekana kubisha na wakati mpaka picha za kutengenezwa walikuwa wamekabidhiwa.
Kila siku kwao ilionekana kuwa kama sikukuu. Walikunywa na kufurahia pamoja. Kila siku muda wa Bunge ulipokuwa ukimalizika, walikuwa wakikutana katika mghahawa ulioitwa Matimya ambao ulikuwa katikakati ya mkoa wa Dodoma na kufurahia pamoja.
Walionekana kukamilisha kazi ndefu ambayo ilikuwa ikiwasumbua vichwa vyao, walijiona kuwa na amani sasa. Glasi zao zilikuwa hewani, wakazigonganisha na kisha kuanza kunywa huku wakiongea maneno mbalimbali yaliyojaa dhihaka juu ya Dominick.
“Kiko wapi sasa? Alijifanya anajua sana” Mzee Boniface aliwaambia wenzake.
“Tusimlaumu jamani. Hakujua kama analeta mzaha kwa watu walio na mikono mirefu” Waziri Ombeni aliwaambia na wote kuanza kucheka.
“Cheeeeerrs! Kwa ajili ya marehemu Dominick na Saida” Waziri Tumaini alisema huku akinyanyua glasi juu.
“Cheeeeerss….! Bwana Ombeni na Boniface waliitikia.
********
Dominick akaingia katika eneo la ufukwe na kulipaki gari lile. Kutokana na wakati kuwa asubuhi sana, hakukuwa na watu ufukweni. Kwa haraka haraka huku akionekana kuwa na hasira akateremka huku mkoni akiwa na kidumu cha mafuta ya petroli.
Bi Upendo akabaki akipiga kelele za kuomba msaada, hali tayari ikaonekana kuwa ya hatari. Alipiga kelele sana lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alizisikia kelele zile. Dominick akaanza kulimwagia petroli gari lile. Kila kitu ambacho alikifanywa kwa wakati huo alikifanya kwa haraka haraka.
Alipomaliza kulimwagia petroli kwa nje, akafungua mlango na kuanza kuwamwagia petroli Bi Upendo pamoja na watoto wake. Wote walikuwa wakilia ndani ya gari lakini wala Dominick hakuonekana kujali. Machozi yalikuwa yakimtoka kwa hasira.
Taswira ya nyumba ambayo ilikuwa ikiteketea ikaanza kumjia kichwani, hasira zaidi zikampanda kiasi cha kujuta kwa kuja na lita tano, aliziona ndogo sana. Alipomaliza, akachukua kiberiti na kuliwasha moto gari lile. Kelele za Bi Upendo na watoto wake zikazidi kusikika zaidi.
Kila Bi Upendo alipojaribu kuufungua mlango kwa ajili ya kutoka nje, milango ilikuwa imepigwa roki. Harufu za nguo zlizokuwa zikiungua kwa moto ikaanza kusikika kunuka na hatimae harufu ya miili iliyokuwa ikiteketea ikaanza kunuka pia.
Kutokana na upepo kuwa mkubwa ufukweni pale, moto ule ukaonekana kuchochewa. Mara milio ya vitu vitatu vilivyoonekana kupasuka vikasikika kutoka garini, hivyo vilikuwa vichwa ambavyo vilikuwa vimepasuka kutokana na kuteketezwa sana na moto.
Kuteketea kwa gari lile kukawafanya watu waliokuwa mbali kabisa kuanza kuuona moto mkubwa, wakaanza kukimbilia kule ambako moto ule ulipokuwa. Dominick hakuwepo mahali pale, tayari alikuwa amekishaondoka huku moyo wake ukionekana kuridhika kiasi.
Kila mtu aliyefika mahali pale alibaki akishangaa, watu wote walibaki wakiwa wameduwaa tu, hawakujua wafanye nini na wakati gari lilikuwa likizidi kuteketea kwa moto. Baada ya muda watu wakaonekana kurudiwa na akili zao, wakaanza kuchukua maji baharini na kuanza kuuzima moto ule. Moto ukazimika, wakasubiri bodi lipoe ili kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote garini.
Mlango wa gari ukavutwa, kijana mmoja akachungulia garini, kile ambacho alikiona alishindwa kuvumilia, akatoka huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Kila alipokuwa akiulizwa aliona nini, hakuongea kitu chochote kile, alikwenda pembeni na kuanza kutapika.
“Kuna nini? Umeona nini?” Kijana mwingine alimuuliza.
“Nendeni mkaangalie wenyewe. Inatisha”
“Inatisha? Inatisha nini?”
“Nyie kaangalieni tu”
Vijana wengine wakaelekea katika gari lile na kuchungulia ndani. Miili mitatu ilikuwa ikionekana vizuri huku ikiwa imeteketea kwa moto na huku ikitoa moshi. Simu zikaanza kupigwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay ili kuwaomba mapolisi kufika mahali hapo haraka iwezekanavyo.
6
Watu ambao walikusanyika mahali pale walikuwa watano lakini kadri dakika zilivyozidi kwenda na ndivyo watu walivyozidi kuongezeka mpaka kufikia watu zaidi ya mia mbili. Kila aliyefika mahali pale na kuangalia miili ya watu wale, alishikw kichwa kwa huzuni.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo watu walivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi. Watu ambao walikuwa wakipita katika barabara ya lami wakasimamisha magari yao na kuanza kuelekea pale ambapo gari lile lilipokuwa limeteketezwa kwa moto.
Zilipita dakika thelathini na ndipo waandishi wa habari wakafika katika eneo la tukio hata kabla ya mapolisi. Wakaanza kupiga picha kila kitu kilichokuwa kinaendelea mahali pale huku wakichukua muda wao kuwahoji watu ambao walikuwa katika eneo hilo. Kila aliyekuwa akihojiwa, alikuwa akiongea kwa uchungu, wakinamama walishindwa kujizuia, muda wote walikuwa wakilia.
Mapolisi wakafika mahali hapo na kuwaomba watu kusogea mbali na gari lile, wakaingia ndani na kuanza kuitoa miili ile ya Bi Upendo na watoto wake na kisha kuiweka katika gari lao aina ya Defender. Hawakutaka kubaki mahali hapo, safari ya kuelekea hospitalini ikaanza.
“Hivi ilikuwaje?” Mwandishi mmoja wa habari alimuuliza kijana mmoja ambaye alikuwa mtu wa kwanza kufika mahali hapo.
“Yaani toka gari hili lilipokuwa linafika mahali hapa nilikuwa naliona japo nilikuwa mbali sana” Kijana yule alisema hali iliyowafanya watu wengine kumzunguka kutaka kujua ni kitu gani kilitokea.
“Sikulitilia shaka yoyote ile, nikamuona jamaa mmoja ambaye alikuwa amevaa kofia kubwa ya Malboro akiteremka huku akiwa na chombo kidogo, sijui kilikuwa kidumu kile…wala sikukiona vizuri. Nikamuona akianza kulimwagia gari hili. Nafikiri ilikuwa petroli japokuwa mimi nilifikiri maji huku nikidhani alikuwa akiliosha gari lake.” Kijana yule aliwaambia.
“Eheee..!! Ikawaje sasa?”
“Baaada ya muda nikaamua kwenda kuogelea kama kawaida yangu. Ile napiga mbizi mbili tatu, nikashangaa kuuona moto mkubwa ukiwaka. Unajua nilishtuka sana, nikajikuta nikitoka baharini na kuanza kuja huku” Kijana yule alielezea huku kila mtu akibaki kimya akimsikiliza.
“Kwa hiyo mtu mwenyewe hukumuona tena? Au alisimama pembeni?”
Sikumuona. Yaani sijui alikimbilia wapi”
*******
Wabunge wengi walikuwa Bungeni wakisiliza kwa makini sana namna ambavyo Bajeti ya taifa ilivyokuwa ikisomwa. Muda wote ambao bajeti ilikuwa ikisomwa, mawaziri ambao walijiita BoT walikuwa wakikenua kila wakati, vifo vya watu wawili vilionekana kuwafurahisha sana.
Mzee Boniface akahisi simu yake ikitetemeka mfukoni, akaitoa na kuanza kuangalia namba ya mpigaji. Namba ilikuwa ngeni kabisa machoni mwake. Akatamani kuipuuzia lakini akaamua kuanza kupiga hatua kuelekea nje ili kujua ni nani ambaye alikuwa akimpigia simu.
“Haloooo…!” Mzee Boniface aliita.
“Haloooo…Naongea na mheshimiwa waziri hapo?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza.
“Ndio. Wewe ni nani na sijui nikusaidie nini?”
“Kuna tatizo mzee. Nakuomba uje Dar es Salaam mara moja”
“Tatizo? Tatizo gani ambalo mpaka mnataka mimi nije huko?” Mzee Bonifasi aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Wewe njoo mzee. Tena ikiwezekana, njoo sasa hivi” Sauti ya upande wa pili ilisema.
“Hilo si tatizo. Nikija hapo Dar es Salaam nielekee wapi sasa?” Mzee Boniface aliuliza.
“Njoo katika hospitali ya Taifa”
“Hospitali ya Taifa?”
“Ndio. Fanya haraka sana” Sauti ya upande wa pili ilisikika na kisha simu kukatwa.
Mzee Boniface akaonekana kuchanganyikiwa, neno hospitali ya Taifa ndio ambalo lilionekana kumtisha zaidi. Tayari akaona kuna tatizo lilikuwa limetokea, hivyo alichokifanya ni kumpigia simu mkewe, simu haikuwa ikipatikana.
Mzee Bonifasi akaonekana kuchanganyikiwa. Akapiga katika simu ya mezani, simu ikaanza kuita na baada ya muda ikapokelewa na mfanyakazi wake wa ndani. Tayari kijasho chembamba kilikuwa kinamtoka, akajihisi kuchanganyikiwa kupita kawaida.
“Hallooo…! Mage, mama yako yupo hapo?” Mzee Bniface aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Hayupo. Ametoka”
“Ametoka? Ameelekea wapi asubuhi yote hii?”
“Amewapeleka watoto shule pamoja na dereva”
“Inakuwaje leo amewapeleka shule? Si huwa anawapeleka dereva peke yake?” Mzee Boniface aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Hata mimi sifahamu”
“Hakuna tatizo lolote lililotokea hapo nyumbani?” Mzee Boniface aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa zaidi.
“Mmmmm…!! Wala hakuna” Mage alisikika akijibu.
“Sawa. Nakuja huko huko”
“Sawa”
Mzee Boniface akaonekana kuchanganyikiwa zaidi. Hakuwa na sababu ya kuaga, moja kwa moja akampigia simu dereva wake ambaye alikuja na kumtaka kumpeleka uwanja wa ndege. Mwili wote ulikuwa ukimtetemeka, jasho ambalo lilikuwa likimtoka lilimfanya shati lake lote kulowana kana kwamba alimwagiwa ndoo ya maji.
“Mbona unaonekana tofauti leo?” Dereva alimuuliza.
“Wewe twende kwanza” Mzee Boniface alimwambia dereva.
Wala hazikupita dakika nyingi, wakafika uwanja wa ndege. Tiketi ya ndege ikakatwa kwa haraka sana. Akaichukua tiketi ile ya ndege na kuanza kuiangalia. Akaamua kumrudia dereva ambaye alikuwa nje ya jengo la uwanja wa ndege.
“Hivi hauwezi kuendesha gari kwa mwendo wa kasi. Yaani baada ya saa moja tuwe tumefika Dar es Salaam?” Mzee Boniface alimuuliza dereva wake.
“Ndani ya saa moja?” Dereva aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Sasa unaniuliza ina maana haujanisikia au?”
“Mheshimiwa haiwezekani. Labda kama hapa ingekuwa Morogoro sawa. Ila kumbuka hapa ni Dodoma” Dereva alimwambia mzee Boniface
“Lakini bado haujanijibu swali langu”
“Nimekwishakujibu mzee kwamba haiwezekani. Kutoka hapa Dodoma hadi Dar es Salaam ni mbali sana” Dereva alimwambia mzee Boniface.
Mzee Boniface akabaki kimya. Wasiwasi ukazidi kuongezeka moyoni mwake. Simu ambayo alipigiwa katika kipindi kichache kilichopita tayari ilikuwa imemchanganya. Furaha yote aliyokuwa nayo juu ya kifo cha Dominick na Saida ikapotea moyoni mwake.
Kadri muda ulivyozidi kusonga mbele na ndivyo wasiwasi ulivyozidi kumpanda zaidi. Alibaki katika kiti cha gari lake huku akiwa kimya, mawazo yake yalikuwa yakifikiria mbali sana kwa wakati huo. Kwa haraka sana, akaichukua simu yake na kuanza kubonyeza namba za simu yake ya mezani iliyokuwa nyumbani kwake, simu ikaanza kuita, baada ya muda, Mage akaipokea.
“Kuna kitu chochote kilichoendelea huko? Mzee Boniface alianza kuuliza swali.
“Kitu gani?” Sauti ya Mage ilisikika ikiuliza.
“Chochote kile”
“Hapana. Hakuna chochote kile?”
“Hakuna”
“Yaani hata mtu kuja kuniulizia?”
“Aaaah..! Nimekumbuka. Walikuja mapolisi hapa” Mage alimwambia mzee Boniface.
“Wamesemaje?”
“Hawakuniambia kitu chochote kile zaidi ya kukuulizia wewe”
“Sawa” Mzee Boniface alisema na kukata simu.
Akili yake ikachanganyikiwa zaidi. Dereva hakutaka kuuliza kitu chochote kile, alibaki kimya akimwangalia mzee Boniface alivyochanganyikiwa.
Dakika zilizidi kwenda mbele huku sekunde zikienda katika kasi yak kama kawaida. Saa la kwanza likakatika, na hatimae saa la pili kutimia. Abiria wote wakaitwa katika ndege ambayo walikuwa wakihitajika tayari kwa safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa kupitia Morogoro.
Kadri ndege livyokuwa ikisafiri angani kuelekea Dar es Salaam na ndivyo ambavyo wasiwasi wake ulivyozidi kuongezeka zaidi. Amani ikazidi kupotea moyoni mwake. Hakuwa na hamu ya kula kitu chochote kile, kila alipopitishiwa vyakula mbalimbali, alikataa kula, mbaya zaidi, hata maji hakutaka kunywa.
Ndege aliiona ikiendelea na safari kwa mwendo wa taratibu sana, alitamani afike haraka Dar es Salaam na kuelekea katika hositali ya taifa. Safari iliendelea zaidi na zaidi na hatimae kuingia katika uwanja wa ndege saa nne sita asubuhi.
Hakutaka kuchelewa kubaki uwanjani hapo, kwa haraka haraka huku akionekana kuchanganyikiwa, akachomoka na kuelekea nje ya jengo la uwanja ule ambako akachukua taksi.
“Twende Muhimbili” Alimwambia dereva taksi ambaye alikuwa akimshangaa.
“Elfu kumi na t….”
“Wewe twende bwana. Mbona unataka kunichelewesha” Mzee Boniface alimwambia dereva taksi ambaye kwa haraka sana, akaliwasha gari na kuondoka uwanjani hapo.
Mzee Boniface alimuona dereva taksi akiendesha kwa mwendo wa taratibu sana kiasi ambacho akatamani kushikilia usukani yeye mwenyewe. Kila wakati alikuwa akimuhamasisha dereva kuongeza kasi.
Mpaka wanafika katika hospitali ya Muhimbili, walitumia dakika arobaini na saba njiani. Akamlipa dereva kiasi chake cha fedha alichokihitaji na kwa haraka haraka akateremka na kuanza kuelekea katika eneo la hospitali ile.
Ingawa watu wengi walikuwa wamezuiliwa kutokana na wakati ule kutokuwa muda wa kuwaona wagonjwa, lakini kutokana na kuwa na nyadhifa kubwa serikalini, mzee Boniface akaruhusiwa kupita. Watu wote ambao walikuwa mahali hapo walikuwa wakimshangaa kwa jinsi alivyokuwa akitokwa jasho.
Kila mmoja aliyemuona mzee Boniface alikuwa akijiuliza juu ya hali ambayo alikuwa nayo. Kila mtu alifahamu kuwa kwa wakati huo alihitajika kuwa Bungeni kuwawakilisha wananchi wake, lakini kwa nini wakati ule alikuwa hospitalini, tena akionekana kuwa na haraka huu uso wake ukiwa umejaa wasiwasi?
“Mheshimiwa…!” Alisikia akiitwa. Kwa haraka haraka akageuka, macho yake yakagongana na umati wa mapolisi pamoja na baadhi ya manesi ambao walikuwa wamesimama nje ya chumba kimoja kilichoandikwa Monchwari kwa nje. Mzee Boniface akazidi kushikwa na wasiwasi zaidi, nyuso za watu wale zilikuwa zimejawa na huzuni kupita kawaida.
“Kuna nini? Niambieni kuna nini?” Mzee Boniface aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Twende kwanza ofisini” Daktari alimwambia na wote kuanza kwenda katika ofisi ya daktari huku baadhi ya mapolisi wakiwafuata.
Mzunguko wa damu mwilini mwake ulikuwa mkubwa, mapigo ya moyo yalikuwa yakimdunda kupita kiasi. Walipoifikia ofisi ile moja kwa moja wakaingia ndani na kutakiwa kukaa kitini. Macho yake yalikuwa yakimwangalia daktari kwa wasiwasi kupita kawaida.
“Kuna nini daktari? Mbona hamtaki kuniambia?” Mzee Boniface aliuliza huku akionekana kukasirika.
“Kuna habari mbaya. Ila kwa sababu wewe ni mwanaume, ningependa ujipe moyo wa ushujaa kuisikia habari hii” Daktari alimwambia mzee Boniface.
“Mbona unazunguka zunguka? Niambie kwanza” Mzee Boniface alimwambia daktari huku akionekana kuwa na hasira zaidi.
“Kuhusu familia yako”
“Familia yangu? Imefanya nini?”
“Imeteketezwa kwa moto. Mkeo na watoto wako wamefariki kwa kuunguzwa na moto vibaya” Daktari alimwambia mzee Boniface.
Mzee Boniface akaiona presha ikipanda kwa kasi. Akabaki ameganda kna kwamba alikuwa akijitayarisha kupigwa picha. Akailalia meza ya daktari, ghafla akaanguka chini kama mzigo. Hakujua kitu chochote kilichoendelea baada ya hapo. Alionekana kuwa katika hali ya nusu kifo.
*******
Miili ilikuwa imeteketea vibaya kupita kawaida. Kila polisi ambaye alikuwa akiiangalia alibaki kushika tama kwa huzuni. Haikuwa rahisi hata kidogo kuwatambua watu wale ni wakina nani. Walikuwa wakitisha kupita kawaida. Picha ambayo ilikuwa ikionekana mbele yao, ilikuwa ni picha mbaya ambayo ilikuwa ikiwasisimua kupita kawaida.
“Hali inatisha” Polisi mmoja alijikuta akisema.
Gari lile likaenda moja kwa moja hadi katika hospitalini ambacko machela zikaletwa na miili kupakizwa huku ikifunnikwa shuka. Machela zikasukumwa moja kwa moja mpaka katika chumba kikubwa cha kuhifadhia maiti. Mapolisi walibaki nje wakisubiri kuona ni kitu gani kingeendelea mahali hapo.
Mara mzee mmoja ambaye alikuwa na vazi refu jeupe akaanza kuelekea kule waliposimama na kisha kuingia ndani ya chumba kile. Wala hazikupita dakika hata tano, akatoka huku uso wake ukiwa umejawa na huzuni kupita kawaida.
“Kuna ndugu zao wowote mmekuja nao?” Dokta aliwauliza mapolisi.
“Hapana”
“Sasa hata majirani zao mmeshindwa kuja nao? Au walikuwa wanaishi porini?” Dokta aliuliza huku mawazo yake yakimpelekea kuwa ni ajali ya nyumba kuungua ndio ambayo ilikuwa imetokea.
“Bora ingekuwa hivyo daktari. Hawa watu wamechomwa moto wakiwa ndani ya gari, gari lenyewe lilikuwa limetelekezwa ufukweni” Polisi mmoja alimwambia daktari ambaye akaonekana kushtuka.
“Wamechomwa moto ndani ya gari?” Daktari aliuliza kwa mshtuko huku akionekana kutokuamini.
“Ndio”
Mapolisi hawakutaka kuendelea kubaki hospitalini hapo, bado walijiona kuwa na kazi ambayo ilibakia kwa ajili ya kumjua mmiliki wa gari lile. Moja kwa moja wakaenda katika kituo chao cha Oysterbay na kisha kuagiza gari lile lililoteketezwa kwa moto kuletwa kituoni pale.
Dakika arobaini na tano gari lile likaletwa kituoni pale. Rangi halisi ya gari lile haikuwa ikijulikana, lilikuwa limeteketezwa vibaya na moto. Walichokifanya ni kwenda mbele ya gari lile kwa ajili ya kuangalia namba za gari, namba hazikuwa zikionekana.
Wakajaribu kufungua milango ya gari lile na kuanza kuangalia kwa ndani, kila kitu kilikuwa kimeteketezwa kwa moto, hali ikaonekana kuwa ngumu kumjua mmiliki halisi wa gari lile. Milango ikafungwa na kwenda nyuma ya gari, namba zilikuwa zikionekana japokuwa hazikuwa zikionekana vizuri.
“Mhhhh!” Polisi mmoja alisikika akiguna.
“Vipi tena? Mbona umeguna?”
“Hizi namba. Naona si za kawaida”
“Kwa nini umesema hivyo?”
“Namba hizi ni za serikali. Nafikiri gari hili litakuwa linamilikiwa na mtu mkubwa serikalini”
Uchunguzi zaidi ukaendelea na zaidi. Namba zile zikaandikwa katika faili na kisha kuanza kuwasiliana na vitengo mbalimbali vya serikali ili kugundua ni nani hasa alikuwa mmiliki wa gari lile. Ndani ya dakika arobaini, simu ikapigwa kituoni na pale na kuambiwa mmiliki halisi wa gari lile.
Kila polisi akaonekana kushtuka, hawakuamini kama waziri Boniface ndiye alikuwa mmiliki wa gari lile. Bado maswali yakaendelea zaidi na zaidi juu ya watu ambao walikuwa ndani ya gari lile. Kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea katika nyumba ya mzee Boniface kumuulizia japokuwa walikuwa na uhakika kuwa wasingemkuta kutokana na kikao cha pili cha Bunge kuendelea mkoani Dodoma.
Wakafika nyumbani pale na kumuulizia, hawakumkuta mtu yeyote zaidi ya mfanyakazi wa ndani pamoja na mlinzi ambaye muda wote alikuwa getini akiendelea na ulinzi. Kitu walichokifanya ni kuchukua namba ya mzee Boniface na kisha kurudi ofisini na kumpigia.
******
Dominick akaonekana kuwa na amani japokuwa aliiona kutokukamilika. Alijilaza kitadani huku macho yake yakiangalia televisheni. Shauku yake kubwa ilikuwa ni kutaka kuiona taarifa ile ambayo aliamini ingempa furaha kwa wakati huo.
Muda wa taarifa ya habari ukawadia na habari ya kwanza kutangazwa ilikuwa ile ya gari la waziri kuchomwa moto na watoto wake pamoja na mkewe kuteketezwa kwa moto mpaka kifo. Habari ile ilikuwa inasikitisha na ilisomwa kwa majonzi makubwa lakini kwa Dominick hali ilionekana kuwa tofauti kabisa.
Uso wake ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana, muda wote alikuwa akikenua meno yake kwa furaha huku akishushia juisi nzito ya maembe. Moyo wake haukusikia hukumu kabisa, furaha ndio ambayo ilikwa imemtawala kuliko kitu chochote kile kwa wakati huo.
“Hivi ndivyo ninavyotaka. Nilivyoumia mimi basi nao waumie hivyo hivyo” Dominick alijisemea huku akibadilisha stesheni kuangalia taaarifa nyingine ya habari huku akitaka kuiona kwa mara nyingine habari ile ambayo ilikuwa ikimpa furaha kuiona.
“Ombeni ndiye anayefuata. Nitakwenda hivi hivi, zamu kwa zamu mpaka wote wamalizike” Dominick alisema huku tabasamu likiendelea kuwapo usoni mwake.
*******
Wabunge wote wakaonekana kuchanganyikiwa. Taarifa ya kuchomwa moto kwa gari la mbunge mwenzao ilipotangazwa, kila mtu akabaki kuwa na maswali kichwani. Hawakuamini kama Tanzania kungekuwa na mtu ambaye angekuwa na roho ya kufanya kitendo cha kikatili namna ile.
Kulichoma gari moto kwa makusudi huku watu wakiwa garini kilionekana kuwa kitendo cha kinyama ambacho hakikutakiwa kutokea katika nchi kama Tanzania. Mambo kama hayo yalitakiwa kusikika katka nchi nyingine, hasa katika nchi ambazo walipigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuuana kinyama.
Shughuli za Bunge zikaahirishwa, bunge likafungwa na kutolewa siku saba kwa ajili ya kuomboleza pamoja na mbunge mwenzao ambaye pia alikuwa waziri wa Mambo ya Utalii na Maliasili, mzee Boniface. Kila mbunge alikuwa na maoni tofauti juu mauaji yale ya kinyama. Kila walipokuwa wakiongea, maoni yao yalikuwa ni kuwataka mapolisi hasa katika kitengo cha upelelezi kufanya kazi mara moja ya kumtafuta na kumleta kwenye chombo cha dola mtu ambaye alihusika na mauaji yale.
Wazairi wa Miundo Mbinu, Bwana Ombeni akaonekana kuwa na wasiwasi zaidi, hakuonekana kuwa na amani, muda wote alikuwa mnyonge huku akionekana kuwa namawazo. Hakutaka kuendelea kubaki katika hali hiyo, moja kwa moja akampigia simu waziri mwenzake, Bwana Tumaini na kutaka kuonana nae katika hoteli ya Cat iliyokuwa Kariakoo.
Ndani ya dakika arobaini wakawa katika chumba kimoja ndani ya hoteli ile. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa, wasiwasi ukaonekana kuanza kuwashika. Mashaka makubwa yalikuwepo juu ya Dominick ambaye akaonekana kuwa nyuma ya mambo yote yale.
“Lakini si wale vijana walimuua?”
“Ndio. Kama aliuawa sasa ni nani ambaye anahusika na mauaji haya?”
Kila wakati walikuwa wakijiuliza juu ya muuaji ambaye aliiteketeza familia ya rafiki wao mkubwa. Akili zao zikaonekana kuchanganyikiwa, hawakuwa na uhakika kama mauaji yale alikuwa ameyafanya Dominick au mtu mwingine. Swali lao halikujibika vichwani mwao zaidi ya kupeana angalizo la kuzilinda familia zao.
“Unajua nae rafiki yetu alikua mtu wa matukio sana, unaweza kukuta kumbe kuna mtu aligombana nae na ndio maana aliamua kufanya kitu hiki” Bwana Tumaini alisema
“Ila inawezekana. Hata mimi nakuunga mkono”
Wakaachana siku hiyo na kila mtu kurudi nyumbani kwake ambako akajiandaa na kuelekea msibani nyumbani kwa mzee Boniface.
******************
Idadi ya watu zaidi ya elfu moja ilikuwa imekusanyika katika eneo la nyumba kubwa ya mzee Boniface. Vilio vilikuwa vimetawala katika kila sehemu nyumbani hapo. Wakina mama walikuwa wakilia kupita kawaida, ndugu ambao walikuwa wametoka mkoani nao pia walishiriki vilivyo msiba huo.
Kila mtu alionekana kuwa na huzuni, hakukuwa na utulivu msibani pale, wakina mama wengine walikuwa wakikimbia huku na kule huku wakiendelea kulia. Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya majonzi makubwa maishani mwao, kuwapoteza watu watatu kwa mpigo lilionekana kuwa tukio kubwa ambalo halikuwahi kutokea katika ukoo wao.
Waandishi wa habari hawakuwa mbali, walikuwa wamekusanyika katika msiba huo huku kamera zao zikiwa mikononi wakijaribu kupiga picha na kuandika kila kitu ambacho walikiona kikifaa kuandikwa na kupigwa picha tayari kwa kuitoa habari ile katika magazet yao siku itakayofuata.
Mzee Boniface alikuwa amekaa pamoja na wazee wenzake, muda wote uso wake ulionyesha kuwa na huzuni japokuwa alikuwa akiongea kama hakupatwa na kitu chochote cha kuhuzunisha. Moyo wake ulikuwa ukimuuma zaidi kutokana na watoto wake kuuawa.
Kila siku alikuwa akiwalea katika maisha bora, hakutaka wapate matatizo yoyote yle kiasi ambacho alikuwa akiwalinda sana. Kwa sasa maisha yake yalikuwa kama katika kipindi ambacho hakuoa, mkewe hakuwa pamoja nae, mbaya zaidi, hata watoto wake hawakuwa pamoja nae pia.
Ving’ora vikaanza kusikika kwa mbali, watu wakaanza kuambiwa wakae vizuri mahali hapo. Zikaanza pikipiki mbili kuingia mahali hapo zikiongozana na magari manne. Polisi mmoja akaufungua mlango na kuelekea katika garijingine na kuufungua mlango, rais Emmanuel Moses akaanza kuteremka na moja kwa moja kuelekea kule wafiwa walipokuwa huku akiongozana na mkewe, Jaqueline Mlolo.
Walipomaliza kuwapa pole, mke wa rais, Jaqueline akaenda kukaa na wanawake wenzake huku rais, Emamanuel akienda kukaa pamoja na wanaume.
Wala haukupita muda mrefu, majeneza matatu yakaanza kuletwa mahali hapo. Vilio vikaanza kusikika zaidi na zaidi. Wakina mama na ndugu mbalimbali wa kike wakaanza kulia kwa uchungu huku wakigalagala chini. Mzee Boniface alikuwa akiongea kama kawaida, mara akanyamaza baada ya kuyaona majeneza ya familia yake. Machozi yakaanza kumlenga na hatimae kutiririka mashavuni mwake.
Moyo wake ulikuwa na maumivu makubwa kupita kiasi zaidi ya kuchomwa kwa msumari wa moto moyoni. Mchungaji akasimama na kuanza kuongea maneno machache. Miili ile haikutakiwa kuagwa kutokana na kuharibika vibaya, na kama ingeagwa kwa kuangaliwa sura ya mwisho, wanandugu wangeumia zaidi na zaidi.
Harakati nyingine zikaendelea na maiti kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni huku idadi ya watu ikiwa imeongezeka zaidi.
“Nitatumia gharama zangu zote kumpata muuaji huyu. Ni lazima nimpate na kumuua kwa mkono wangu mwenyewe” Mzee Boniface alijisemea katika kipindi ambacho maiti za familia yake zilipokuwa zikifukiwa kwa mchanga.
*******
Mapolisi walionekana kuchanganyikiwa kupita kawaida. Taarifa ya gari la waziri kuchomwa moto na mtu hasiyejulikana na kusababisha kuipoteza familia yake ilionekana kuwachanganya. Kamanda mkuu akawaita watu wote ambao walikuwa katika kitengo cha upelelezi na kuanza kuongea nao.
Kamanda mkuu wa polisi, Bwana Innocent Ngomale alionekana kuchanganyikiwa, muda wote alikuwa akikipiga kichwa chake. Tukio lile likaonekana kulitia doa jeshi la polisi kuliko tukio lolote ambalo liliwahi kutokea. Kuchomwa moto kwa nyumba ya Dominick na familia yake wala halikuangaliwa kama tukio kubwa, tukio la kuteketezwa familia ya Waziri wa wa Mali Asili na Utalii, Bwana Boniface ndilo lilionekana tukio kubwa kwa mapolisi.
Kila polisi alibaki akiwa na wasiwasi, siku hiyo kamanda Ngomale alionekana kukasirika kuliko siku zote. Akasimama kutoka kitini kwake na kuanza kuangalia darini, akakaa na kuanza kutapitisha macho yake usoni mwa kila polisi aliyekuwa mahali pale.
“Hii ina maana gani?” Kamanda Ngomale alianza kwa kuuliza swali. Hakukuwa na polisi yeyote ambaye alilijibu swali lile, kila mtu alibaki kimya.
“Ina maana hamfahamu hali hii ina maana gani?” Kamanda Ngomale aliuliza huku akionekana kuwa na hasira. Bado ukimya ukatawala mahali pale, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alijibu kitu chochote kile.
“Hii ina maanisha kwamba tumeshindwa kazi. Ulinzi umekuwa mdogo sana siku hizi. Zaidi ya yote, hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyojisahau na kazi zetu” Kamanda Ngomale aliwaambia mapolisi.
Akachukua glasi ya maji ambayo ilikuwa mezani na kupiga fundo moja. Jasho tayari likuwa likimtoka, feni ambayo ilikuwa ikiendelea kupepea ndani ya chumba kile ilionekana kutokufanya kazi yake katika mwili wake. Akayarudisha macho yake katika uso wa kila mmoja na kuanza kuwaangalia tena kwa zamu.
“Muuaji anahitajika haraka sana. Nendeni mkajipange ninyi kama mapolisi wa kitengo cha upelelezi. Tunataka ndani ya mwezi huu muuaji apatikane hata kabla mambo mengine hayajatokea” Kamanda Ngomale aliwaambia.
Kikao kilipokwisha wala hakukuwa na muda wa kupoteza zaidi ya mipango kabambe kuanza kupangwa. Mpelelezi mashughuli ambaye alisomea shughuli za Upelelezi nchini Urusi, Emmanuel Bugabu ndiye ambaye akateuliwa kuanza kushughulikia suala la kumtafuta muuaji.
Mpelelezi Emmanuel Bugabu alizaliwa miaka ishirini na tano iliyopita. Mara baada ya kujiunga na jeshi la polisi, akafanikiwa kuwa miongoni mwa vijana ambao walifuzu mafunzo ya kwenda kufundishwa upelelezi nchini Urusi.
Maisha nchi Urusi yalionekana kuwa magumu kwake, hali ya hewa ambayo alikuwatana nayo ilikuwa tofauti kabisa. Kila siku alikuwa akishinda na jaketi kubwa ambalo lilikuwa juu ya sweta lililokuwa juu ya fulana nzito ambayo ilikuwa juu ya ngozi yake.
Ingawa alikuwa akipata tabu kila siku, Bugabu akavulimilia mpaka pale alipomaliza elimu yake ambayo ilichukua miaka mitatu mpaka kumalizika. Aliporudi nchini Tanzania, Bugabu akaanza kufanya kazi ya upelelezi. Mauaji pamoja na uvamizi mbalimbali ulikuwa ukitokea, Bugabu ndiye ambaye alikuwa akipewa kazi ya kupeleleza. Wala hakuchukua muda mrefu, kila kitu kilikuwa kinakamilika na wahusika kukamatwa.
Sifa hizi ndizo alizokuwa nazo mpelelezi Bugabu, hakushindwa kazi hata moja, kila kazi ya upelelezi aliyopewa ilionekana kuwa ngumu kwa watu wengine lakini kwake yeye aliifanya kwa haraka sana. Kujituma kwake kazini pamoja na umakini mkubwa aliokuwa nao ndio ukapelekea shirika la upelelezi nchini Marekani, F.B.I (Fideral Bureau of Investigation) kutaka kuwa pamoja nao.
Serikali ya Tanzania ikakataa, haikutaka kumuachia Bugabu aende nchini Marekani, alihitajika kubaki nchini Tanzania kuendelea na kazi ya upelelezi. Bugabu alikuwa akiaminika na kila mtu, neno kushindwa kazi kwake wala halikuwepo, kila siku alikuwa akifanikiwa kwa kuwatia watu mikononi mwa vyombo vya dola.
Kila siku kazi yake ilikuwa ni ya mafanikio makubwa, Umakini wake mkubwa ndio ambao ulikuwa ukimletea sifa za kukubalika katika kila idara za kipolisi kiasi ambacho mara kwa mara alikuwa akiitwa Ikulu kula chakula pamoja na rais. Emmanuel Bugabu huyu huyu ndiye ambaye alikuwa amepewa jukumu kubwa la kuhakikisha muuaji wa familia ya Waziri Boniface anakamatwa na kuletwa katika vyombo vya sheria.
“Nimefanya kazi kubwa tena kubwa mara mia ya hii, zote nikafanikiwa. Hii kazi niliyopewa ni ndogo sana, nitaifanikisha ndani ya mwezi mmoja tu” Bugabu alijisemea huku akionekana kutoa tabasamu la dhihaka.
*********
Kila siku Dominick alikuwa mtu wa furaha, mauaji ambayo alikuwa ameyafanya wala hakuyasikitikia, kila siku kwake ilikuwa siku ya furaha. Alifuatilia kila kitu kwa karibu sana, kuonekana kwa mzee Boniface kuwa na hzuni hadi makaburini, kwa Dominick ndio ilikuwa furaha kubwa.
Kamwe moyo wake wala haukujuta, kila siku alikuwa akifurahia. Kila siku magazeti yalikuwa yakimfikia chumbani, picha mbalimbali za watu ambao walikuwa wakionekana kuhuzunika zlimfurahisha. Akaamua kumpigia simu Edmund na kumueleza juu ya kazi ambayo alikuwa ameifanya.
Muda wote Dominick alikuwa akizielezea waziwazi hasira ambazo alikuwa nazo moyoni, hakuona sababu ya watu wale watatu kuendelea kuwa na maisha ya furaha na wakati wao ndio walikuwa wameyarudisha nyuma maisha yake.
Mwezi mmoja ukapita, bado watanzania walikuwa na kumbukumbu vichwani mwao juu ya mauaji yaliokuwa yametokea. Walimhuzunikia sana waziri Boniface ambaye kila siku alikuwa akionekana kuwa na huzuni. Muuaji wa familia yake alikuwa akipokea lawama kila siku pasipo watu kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Dominick bado alijiona kuwa na kazi kubwa ya kufanya, alitaka kukamilisha kila kitu ambacho kilitakiwa kukamilishwa kwa mikono yake. Jina la waziri Ombeni ndilo ambalo lilikuwa likitawala kichwani mwake kwa wakati huo.
Alijiona kuwa na uwezo mkubwa wa kumuua lakini kabla hata hajafanya hivyo alihitaji mzee huyo aumie kwanza, alitamani ayapate maumivu kama ambayo alikuwa ameyapata katika kipindi cha nyuma kwa kuiteketeza familia yake.
Akachukua karatasi na kupanga mipango mbalimbali juu ya namna kazi yake ambavyo angeifanya. Kila hatua ambayo alikuwa ameipanga kwa ajili ya kufanya mauaji, aliiona kutokuwa nzuri. Aliziandika mbinu zaidi ya kumi katika karatasi yake na kisha kuichagua mbinu moja ambayo aliiona kufaa sana.
“Nitaiteka familia yake halafu nitaichoma moto” Dominck alisema.
Akachukua karatasi ambayo alikuwa ameandika namba kadhaa za simu na kuiangalia namba ya simu ya nyumbani kwa waziri Ombeni. Dominick akaichukua ile namba na kuiandika katika simu yake.
“Nitaanza na familia yake” Dominick alisema huku akitabasamu.
*********
Kila siku baadhi ya watanzania walikuwa wakikasirika juu ya tabia ya Bi Magdalena ambaye mara nyingi sana alikuwa akitumia fedha nyingi kwa ajili ya kusafiri sehemu mbalimbali kwa ajili ya kufanya starehe. Bi Magdalena hakuonekana kuridhika na mumewe, hali ambayo ikamfany kuanza kutembea na vijana wadogo ambao damu zao zilikuwa zikichemka.
Hakuonekana kujitambua alikuwa nani na alikuwa na heshima gani, kitu ambcho alikuwa akikitaka ni kuifurahisha nafsi yake. Ngono na vijana ndio ikawa sehemu ya maisha yake. Mara kwa mara alikuwa akishinda klabu pamoja na vijana wadogo huku wakila na kunywa.
Jina lake lilikuwa kubwa katika kila klabu kubwa jijini Dar es Salaam. Umri wake ulikuwa ni miaka arobaini na mbili lakini kila siku maombi yake yalikuwa ni kutaka kurudishiwa miaka nyuma na kuwa kijana. Hakuutaka uzee, alijiona kuwa na nafasi kubwa ya kustarehe kwani fedha kwake haikuwa na tatizo lolote lile.
Ni mara chache sana alikuwa akilala nyumbani mpaka asubuhi, mara nyingi alikuwa akitoroka na kuelekea katika klabu za usiku. Bi Magdalena alikwenda sambamba na binti yake, Sara. Mara kwa mara walikuwa katika kumbi za starehe, mwanaume ambaye alikuwa akitembea na binti yake, Sara basi nae ilikuwa ni lazima atembee nae.
Pepo la ngono likaonekana kuikumba familia hiyo. Ukimuachilia mumewe, basi wao wawili ndio walikuwa wakiunda familia hiyo. Kila siku pombe na ngono ndio yalikuwa sehemu ya maisha yao. Walichukuana na kujirusha sehemu mbalimbali za starehe.
Kila starehe walitamani kufanya, pepo la ngono likaonekana kuwatawala zaidi hasa pale ambapo wakaamua kusafiri kwenda nchini Marekani ili tu kutafuta kampuni mbalimbali ambazo zilikuwa zikijihusisha na urekodiji wa filamu za ngono, nao walitaka kuigiza.
Kila kitu ambacho walitaka kukifanya kikajulikana, hai ambayo walitakiwa kurudi nchini Tanzania haraka iwezekanavyo. Hawakuonekana kukumbuka maisha ya tabu ambayo walikuwa wamepitia katika kipindi cha nyuma, wao walichokuwa wakikikumbuka ni kipindi ambacho walikuwa wameanza kupata fedha tu.
Familia hii ilionekana kuwa ya hatari hasa katika mchezo wa ngono, kila siku waliwaza ngono kiasi ambacho wakati wmwingine pasipo kufanya ngono, walijisikia wagonjwa. Hii ndio ilikuwa familia ya waziri wa Miundo Mbinu, Bwana Ombeni.
Kila siku Bwana Ombeni alionekana kuwa mtu wa matatizo, alijua kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea juu ya mke wake na mtoto wake lakini wala hakuwa akisema kitu chochote kile. Moyo wake ulikuwa katika mapenzi mazito juu ya mke wake. Alimpenda Bi Magdalena kuliko kitu chochote maishani mwake.
Kila siku Bi Magdalena alikuwa akilalamika juu ya uwezo wa mumewe kitandani, na hiyo ndio sababu iliyompelekea kuanza kutembea na vijana wadogo. Shughuli ambazo alikutana nazo kwa vijana wadogo ambao muda mwingi walikuwa wakitumia kuangalia picha za ngono zilimfanya kumsahau mumewe.
Bwana Ombeni alionekana kuchoka sana kitandani, hakuwa na nguvu zozote za kutosha kiasi ambacho muda mwingi Bi Magdalena alijiona kulala pamoja na mwanamke mwenzake. Fedha ambazo alikuwa nazo ndizo ambazo zilikuwa zikiwavutia vijana wengi kutembea nae.
Hakukuwa na kijana yeyote ambaye asingelala nae kwa usiku mmoja kwa malipo ya shilingi laki mbili. Kwa kila kijana ambaye alikuwa akitembelea klabu za usiku sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam basi ni lazima atakuwa akimfahamu mwanamke huyu.
Ingawa alikuwa akifanya mambo mengi pamoja na binti yake lakini wala hakikuandikwa kitu chochote magazetini. Kwanza waandishi wengi wa habari walikuwa wakiogopa, lakini wakati mwingine walikuwa wakipewa fedha nyingi kwa ajili ya kukaa kimya.
Picha zake na binti yake zilikuwa katika simu nyingi za vijana, tena zilikuwa picha ambazo walikuwa watupu au wakifanya ngono na watu mbalimbali. Kila siku kazi yake ilikuwa ni kuzikana picha zile ambazo zilikuwa zimesambaa katika kila kona jijini Dar es Salaam.
Yeye ndiye alliyemshauri mumewe kufanya ufisadi wa shilingi bilioni kumi ambazo zilikuwa zikielea elea katika idara yake. Kila siku fedha zile zilikua zikitumika katika kuwahonga vijana ambao alikuwa akitembea nao. Hakuonekana kuwa na wasiwasi na fedha ambazo wala hakuwa amezitolea jasho, kila siku fedha kwake aliziona kustahlli kutumiwa kwa kuwa tu zilikuwa zimetengezwa kwa kazi hiyo.
“Utamuweza lakini?” Mwanaume mmoja aliyekuwa na misuli alimuuliza Dominick ambaye alikuwa amevaa miwani mikubwa iliyokuwa na rangi nyeusi.
“Kwa nini nisiweze. Ebu niangalie, unanionaje?” Dominick alimuuliza kijana yule.
Muziki bado ulikuwa ukiendelea katika klabu hiyo ya Raspinho, taa hafifu ndizo ambazo zilikuwa zikiwaka. Wanawake mbalimbali wazuri ambao kazi yao ilikuwa ni kujiuza walikuwa wamesimama pembeni huku wakijaribu kufanya matangazo kwa kila mvulana ambaye alikuwa akiwaangalia katika klabu ile.
“Nakuuliza tena..utaweza?” Mwanaume yule bado alikuwa akimuuliza Dominick.
“Nitaweza bwana. Mimi ndiye Maliki Mtanga. Nimezaliwa kwa ajili ya kufanya ngono tu” Dominick aliongea huku akijisifia.
“Kumbe umetokea Tanga”
“Ndio. Kule Handeni”
7
“Basi wewe utakuwa unaweza. Manake mwanamke mwenyewe hataki niwaletee vijana legelege. Kama ndio hivyo basi poa” Mwanaume yule alimwambia Dominick pasipo kumfahamu kutokana na uhafifu wa taa pamoja na miwani ambayo alikuwa ameivaa.
Dominick hakuwa kabisa mtu wa klabu, ila alifika mahali hapo kwa ajili ya kazi kubwa ambayo alikuwa nayo mbele yake. Alizifahamu vilivyo tetesi alizokuwa nazo Bi Magdalena, alifahamu vilivyo kwamba mwanamke huyo alikuwa na pepo la ngono.
Hakuwa akimpenda, lakini alitakiwa kufanya hivyo kwa kuwa alihitaji sana kukamilisha kile ambacho alikuwa amekipanga. Kamwe Dominick hakuwa mtu wa pombe lakini siku hiyo pombe aina ya Kilimanjaro ilikuwa katika kaunta huku akijfanya anainywa.
“Huyo hapo. Ngoja nikaongee nae” Mwanaume yule alimwambia Dominick katika kipindi ambacho Bi Magdalena alikuwa akiingia pamoja na binti yake, Sara.
Dominick akaonekana kutabasamu. Yule mwanaume ambaye alionekana kuwa mlinzi wa klabu ile mule ndani akaanza kumfuata Bi Magdalena na kisha kuanza kuongea nae. Walitumia dakika kumi kuongea, mwanaume yule akaanza kumrudia Dominick huku akionekana kutabasamu.
“Vipi?” Dominick alimuuliza huku akiwa na shauku ya kutaka kufahamu.
“Tayari. Kila kitu kipo fresh ingawa alikuwa akikaza. Si unajua hataki skendo” Mwanaume yule alimwambia Dominick
“Kwa hiyo fresh kabisa?” Dominick aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Fresh. Nilipomwambia kwamba umetoka Tanga, alipagawa kinoma”
“Kweli?”
“Ndio hivyo”
“Kwa hiyo nini kinafuata?”
“Ngoja kwanza. Kila kitu kitakuwa fresh”
Dominick akaamua kutulia, akaangalia saa yake, saa ilikuwa ikionyesha kuwa tayari ilikuwa saa saba na nusu usiku. Aliendelea kuzuga kunywa pombe ile mpaka saa nane ilipotimia na Bi Magdalena kumtuma mwanaume yule kumuita Dominick ambaye alikuwa amejitambulisha kwa jina la Maliki.
Kwa haraka haraka Dominick akainuka na kuanza kuelekea kule alipokuwa Bi Magdalena. Akamsalimia kwa salamu kama ambavyo mara kwa mara alikuwa akiwasalimia vijana wenzake. Akakaribishwa kiti na kutulia. Hapo ndipo maongezi yalipoanza.
Waliongea kwa muda mrefu huku wakitafuta muda wa kuzoeana. Dominick akaamua kuitumia nafasi hiyo kumuonyeshea Bi Magdalena ni kwa kiasi gani alikuwa na uwezo wa kumfanya chochote alichotaka kufanyiwa usiku huo.
“Unajua kuchuma mboga?” Dominick alimuuliza Bi Magdalena.
“Aaaaah! Mbona kila mtu anaijua. Hata binti yangu Sara anaifahamu” Bi Magdalena alisema huku akionekana kuanza kulewa.
“Usijali. Nitakupa nyingine kama kumi hivi. Najua kifo cha mende unaifahamu sana…mimi nitakuwa mwalimu wako leo, nitataka tuandike herufi moja baada ya nyingine” Dominick alimwambia
“Tuandike herufi? Herufi gani?”
“Nimejua tu, bado u mdogo kimapenzi. Nitataka tuchore L kitandani, tukitoka hapo, tunachora C huku tukimalizia na T” Dominick alimwambia Bi Magdalena.
Bi Magdalena akaonekana kuchanganyikiwa, maneno ya kimahaba ambayo aliyaongea Dominick yalionekana kumchanganya. Moyo wake ukawa na shauku kubwa ya kutaka kuondoka nae ili aende akachorwe herufi hizo kitandani.
Akanywa pombe haraka haraka, tayari pepo la ngono lilikuwa limekwishampanda, akachanganyikiwa kabisa. Kila wakati akabaki akimwangalia Dominik kwa macho yaliyojaa mahaba. Akaanza kuupeleka mkono wake katika mapaja ya Dominick na kuanza kuupandisha juu hadi katika sehemu ya zipu.
“Mbona una haraka hivyo? Subiri, malizia pombe kwanza. Leo nataka kukuonyesha kwamba mimi ni mtoto wa Tanga. Tukianza tu…tunasitisha baada ya masaa mawili” Dominick alimwambia Bi Magdalena ambaye akaonekana kushtuka.
“Masaa mawili?”
“Ndio. Tena hapo kama utataka tufanye haraka haraka. Awamu ya pili sitokwambia tutachukua masaa mangapi, manake unaweza ukakataa” Dominick alimwambia Bi Magdalena
Bi Magdalena akaonekana kupagawa zaidi, akili yake ilikuwa ikijiuliza ni kwa jinsi gani kijana aliyekuwa akiongea nae alikuwa na uwezo mkubwa kitandani. Akamuita binti yake, Sara na kuanza kuongea nae kwamba alikuwa akitaka kuondoka mahali hapo.
“Utanipgia simu basi” Sara alimwambia mama yake.
“Sawa” Bi Magdalena alimwambia na kisha kuondoka pamoja na Dominick.
Safari ikaanza huku Dominick ndiye akiwa dereva wa gari la kifahari ambalo alikuja nalo Bi Magdalena na binti yake Sara. Ndani ya gari Bi Magdalena alikuwa akiongea maneno ya mahaba tu, alimuona Dominick akiendesha kwa mwendo mdogo.
Alitamani kufika haraka katika sehemu ambayo angechorwa herufi ambazo Dominick alikuwa amemulezea pasipo kujua mwanaume huyo alikuwa nani. Kila alipokuwa akijaribu kuvuta picha ya mambo ambayo yangefanyika kitandani, Bi Magdalena alibaki kuwa na mshawasha wa kufika haraka.
“Paki gari pembeni” Bi Magdalena alimwambia Dominick ambaye akatii amri kwa kulipaki gari lile pembeni.
“Kuna nini tena?”
“Tunachelewa bwana. Njoo huku nyuma” Bi Magdalna alimwambia Dominick huk akimvuta katiks viti vya nyuma.
“Subir tufike hotelini”
“Hapana. Nimezidiwa. Njoo japo unifanyie herufi moja, halafu nyingine tutazimalizia hotelini” Bi Magdalena alimwambia Dominick ambaye alibaki amechanganyikiwa.
********
“Unasemaje?” Sara aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndio hivyo. Jamaa ametoka Tanga, halafu inaonekana nuksi” Mwanaume yule mlinzi alimwamba Sara ambaye alionekana kuchanganyikiwa.
“Mbona haukuniambia? Au unataka raha azipate peke yake? Yaani leo unanigeuka Dickson” Sara alimwambia Dickson huku akilalamika.
“Mbona unakuwa mkali sana leo. Unanilalamikia sana na wakati muda mwingine nakuitia wewe peke yako” Dickson alimwambia Sara
“Lakini sio kwa mtu wa leo. Mtu ametoka Tanga halafu unampa yule bibi. Haiwezekani, kama mambo bora tupewe wote” Sara alisema huku akitoka ndani ya klabu ile. Akakodi bajaji na kuanza kuelekea katika hoteli ya Supernova ambayo mara zote mama yake alikuwa akiitumia kufanya ngono na vijana.
Njiani Sara alikuwa na mawazo, alitaka kufika haraka hotelini. Kijana ambaye aliondoka nae mama yake tayari alionekana kumchanganya. Pepo la ngo lilikuwa limekwishaanza kmpanda. Muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia nje huku upepo ambao ulikuwa ukimpiga ukionekana kumchanganya kabisa.
“Hebu subiri” Sara alimwambia dereva Bajaji mara baada ya kuiona gari aina ya VX likiwa limepakiwa pembeni mwa barabara. Sara akateremka na kuanza kupiga hatua kuifuata gari ile. Alijua fika kwamba gari lile lilikuwa lile walilokuja nalo, alimjua vilivyo mama yake ambaye mara nyingine alikuwa akifanya ngono garini.
Kadri alivyokuwa akilisogelea na ndivyo ambavyo mwili wake ulivyokuwa ukimsisimka. Nywele zilikuwa zikimsimama huku mshawasha wa kufanya mapenzi ukimshika. Alipolifikia gari lile, akajaribu kuchungulia garini, hakuona kitu chochote kutokana na giza kubwa. Akachukua simu yake ambayo ilikuwa na tochi na kumulika ndani.
“Mungu wangu……….!”
************
“Mbona unalia Ombeni. Yaani niliyefiwa wala silii namna hiyo, wewe ndiye ambaye unalia, kwa nini?” Bwana Boniface alimuuliza mzee Ombeni.
“Haujui kama nami familia yangu imeteketezwa kwa moto? Haujui kama nami pia nimempoteza mke wangu na mtoto wangu?” Mzee Ombeni alimwambia Bwana Boniface.
“Kumbe na wewe pia umeipoteza familia yako? Mungu wangu…….” Bwana Boniface alisema.
Mzee Ombeni akashtuka kutoka kitandani, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, ndoto ambayo alikuwa ameiota ilionekana kumtisha kupita kawaida. Cha kwanza akaangalia kitandani pale, alikuwa peke yake. Akainuka na kuelekea sebuleni, mkewe pia hakuwepo mahali pale. Wasiwasi ukaanza kumshika, akarudi tena chumbani na kuanza kumpigia simu mkewe lakini simu wala haikupatikana.
Mwili wake ukaanza kumsisi mka, kijasho chembamba kikaaanza kumtoka. Akaamua kutoka na kuelekea katika chumba cha binti yake, akanza kuugonga mlango lakini wala hakukuwa na mtu yeyote aliyemjibu hali iliyoonyesha kuwa hata nae hakuwepo.
Mzee Ombeni akarudi tena chumbani kwake na kutulia. Akaonekana kuwa na wasiwasi mwingi kupita kiasi. Ingawa mara kwa mara mkewe alikuwa akimtoroka usiku na kwenda katika nyumba za starehe wala hakujali kabisa lakini siku hiyo akaonekana kuwa na wasiwasi mwingi kupita kiasi.
Ndoto ya kutisha ambayo alikuwa ameiota ndio ambayo ilionekana kumtisha zaidi. Akatoka na moja kwa moja kuelekea nje, gari yake ya VX wala haikuwepo hali iliyoonyesha kwamba kulikuwa na mtu ambaye aliichukua. Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, moja kwa moja akalifuata gari jingine aina ya Range Rover na kuanza kuondoka mahali hapo.
Kazi yake ilikuwa moja tu, kulitafuta gari lak katika kila klabu ya usiku ambayo alikuwa akiifahamu. Breki ya kwanza ilikuwa San Siro, hakukuwa na gari lake katika sehemu ya kuegeshea magari.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, safari yake ikaendelea zaidi kwenda katika klabu nyingine zaidi. Katika kila klabu ambayo alikwenda, wala gari lake hakuliona. Akajihisi kuchanganyikiwa kupita kiasi. Alitembea katika klabu zaidi ya kumi na tano Dar es Salaam lakini wala hakuliona gari lake.
Akaliegesha gari lile pembeni na kuanza kufikiria kama kulikuwa na klabu yoyote ambayo hakuwa ameitembelea usiku huo. Jina la klabu ambalo lilikuwa limeingia kichwani mwake ilikuwa klabu ya Raspinho. Mzee Ombeni hakutaka kukubaliana na hilo, allijihisi kuchoka sana.
“Haiwezekani wawe kule bwana. Ngoja nirudi nyumbani” Mzee Ombeni alijisemea.
Akageuza gari na kuanza kuelekea nyumbani kwake. Ghafla akalisimamisha gari lake, akakata kona na kuanza kurudi kule alipotoka. Tayari akaonekana kushikwa na machale, hakuwa tayari kurudi nyumbani pasipo kwenda Raspinho Club kuhakikisha kama familia yake haikuwa kule.
Alipofika katika eneo la klabu ile, hakukuwa na gari lake hali iliyomfanya kukata tamaa zaidi. Akaanza kuligeuza, lakini alipoangalia vizuri, idadi ya watu ilikuwa kubwa sana nje hali iliyomfanya kuteremka na kuanza kupiga hatua kuelekea kule watu walipokuwa akikusanyika huku tayari ikiwani saa tisa usiku.
Watu walikuwa wakiongea kwa sauti kubwa sana lakni mara baada ya kumuona mzee Ombeni akiwasogelea, wote wakanyamaza na kuanza kumwangalia mzee huyo ambaye alionekana kutaka kusikia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
“Kuna nini jamani?” Mzee Ombeni aliuliza lakini hakukuwa na mtu aliyejibu chochote kile, umati wote wa watu themanini waliokusanyika mahali pale ulibaki kimya hali iliyoanza kumtia wasiwasi mzee Ombeni.
**********
Dominick hakutaka kabisa kufanya kufanya mchezo wowte wa ngono hasa na mwanamke yule ambaye alikuwa akionekana kuwa kama mama yake. Alimwangalia Bi Madgalena mara mbili mbili, tayari pepo la ngono lilikuwa limekwishampanda kwa asilimia mia moja.
Mwili wake ulikuwa umemlegea kupita kiasi, akaanza kuchojoa kila nguo ambayo alikuwa ameivaa. Alipomuona Dominick hafanyi kitu chochote kile, akaanza kumvua shati lake. Domonick alikuwa akipapaswa kila seheu ya mwili wake huku Bi Magdalena akitoa milio mbalimbali ya mahaba.
“Mbona una bunduki?” Bi Magdalena alimuuliza Dominick mara alipokuwa akimvua suruali.
“Si unajua mimi mlinzi wa Benki Kuu Tanzania. Nimetoroka kule kwa ajili yako, yaani kuja kukuonyesha ni kwa jinsi gani mapenzi yanavyofanywa, sio kama vijana wengine ambao wanakuvua nguo halafu mambo yao yanakuwa ya kitoto” Dominick alidanganya.
Udanganyifu ule ulimfanya Bi Magdalena kuchanganyikiwa, bado alitamanisana kuuona umakini wa Dominick wa kufanya mchezo wa ngono kitandani. Akamvua suruali haraka haraka na kisha kumvutia kifuani mwake.
Dominick hakuwa akijisikia kabisa kufanya mchezo wa ngono na mwanamke yule ambaye alikuwa taabani. Dominick akachukua bunduki yake na kuiweka vizuri. Akachungulia nje, hakukuwa na gari lolote lililokuwa likipita barabarani kutokana na usiku kuwa mkubwa.
“Bado sijaridhika. Nikimuua huyu, bado na binti yake. Halafu sitaki afe kwa risasi, huyu ni kuchomwa moto tu” Dominick aliwaza.
“Ngoja nimpige risasi hata ya mbavu, sitaki kumuua. Baada ya hapo nitamfuata binti yake kumleta huku” Dominick alijisemea.
Akaikoki bunduki yake vilivyo, Bi Magdalena bado alionekana kuwa katika mahaba mazito. Alichokifanya Dominick ni kuanza kumpapasa Bi Magdalena ili aweze kumvuruga zaidi. Bi Magdalena akachanganyikiwa kupita kawaida, akaanza kukunja kunja vidole vyake vya mguuni kuonyesha ni kwa jinsi gani kwa wakati huo alikwa amechanganyikiwa.
Dominck hakutaka kupoteza muda, hapo hapo akakibonyeza kitufe cha kuruhusu risasi, ukelele mkubwa ukaanza kusikika kutoka kwa Bi Magdalena. Damu nyingi zilikuwa zikimtoka mbavuni. Dominick akaonekana kushtuka, mara baada ya kuchungulia nje na macho yake kuiona Bajaji ikiwa imesimama kwa mbali, mtu msichana mmoja akateremka a kisha Bajaji ile kuondoka.
Kwa haraka haraka huku akiogopa kuonekana, akaufungua mlango wa upande mwingine na kuteremka huku akimvizia kuona msichana yule alikuwa nani. Dominick akashtuka kwa furaha, taa za gari lile ambazo zilikuwa zikiendelea kuwaka zilimuwezesha kumjua msichana ambae alikuwa akisogea mahali kule alipokuwa.
“Mungu wangu! Kweli Mungu yuko pamoja nami” Dominick alijisemea huku akisogea kule nyuma ya gari.
Sara akasogea mpaka katika mlango mmoja wa gari lile na kuanza kuchungulia. Alikuwa na uhakika kuwa mama yake alikuwa amezidiwa na hivyo alihitaji kufanya ngono hata garini kwani mara kwa mara alikuwa akifanya mchezo huo garini.
Hakuona vizuri garini kitu ambacho kilimfanya kuchukua simu yake iliyokuwa na tochi na kisha kuchungulia. Sara akashtuka, alimuona mama yake akiugulia kwa maumivu. Damu nyingi zilikuwa zikimtoka kupita kawaida. Alichokifanya ni kuanza kuufungua mlango ule, mlango ulikuwa umefungwa.
Kwa mwendo wa kasi akaanza kuzunguka nyuma ya gari ili kuufungua mlango mwingine, akashtukia akipigwa ngumi nzito usoni nzito ya kushtukiza ambayo ilimfanya hapo hapo kuanguka chini na kupoteza fahamu.
Kwa haraka haraka Dominick akambeba Sara na kumingiza garini. Akalwasha gari na moja kwa moja kuondoka mahali hapo. Breki ya kwanza ilikuwa katika kituo cha mafuta ya Petroli ambako akateremka na kumfuata muuzaji mmoja.
“Nahitaji mafuta ya petroli lita kumi” Dominick alimwambia muuza mafuta wa kituo cha kuuzia mafuta.
“Sogeza gari basi karibu”
“Hauwezi kuniwekea kwenye dumu? Si unajua nakwenda kuyamiminika katika gari jingine” Dominick alimwambia muuza mafuta
“Daaa! Kazi itakuwa kutafuta dumu”
“Kwa hiyo hakuna madumu kabisa mahali hapa?”
“Yapo ila mwenyewe akijua kwamba nimeyatoa na kumpa mtu mwingine anaweza akanianzishia utata” Muuzaji yule alimwambia Dominick ambaye alibaki kimya kwa muda.
“Huwa anayauza?” Dominick aliuliza
“Ndio. Moja elfu nne”
Dominick hakutaka kupoteza muda, akatoa kiasi cha shilingi elfu tano na kumgawia muuzaji mafuta ambaye akaenda kuchukua hilo dumu na kurudi nalo. Mafuta yakawekwa ndani ya dumu lile na kisha kulipa fedha zote ambazo zilikuwa zikihitajika.
Dominick akalichukua dumu lile na kulipandisha garini. Sauti ya Bi Magdalena ilikuwa ikisikika kwa chini sana, bado damu zilikuwa zikiendelea kumtoka. Sara ambaye alikua pembeni hakuonekana kurudiwa na fahamu, ngumi nzito na ya kushtukiza ilionekana kumuingia vilivyo.
Dominick akaangalia saa yake ambayo ilikuwa ikimuonyesha kuwa tayari saa tisa na nusu usiku. Alichokifanya ni kuendesha kwa kasi kuelekea katika ufukwe wa Coco ambako aliamini kwa muda ule, hakukuwa na mtu yeyote ambaye angekuwepo mahali pale.
Hakukuwa na magari barabarani hali ambayo ilimfanya Dominick kuendesha kwa kasi ambayo alitaka kuendesha. Alipoanza kuingia katika eneo la ufukwe ule, akazima taa zote na kuanza kuelekea katika eneo lile lile ambalo alilichomea gari la Bwana Boniface.
Akalisimamisha gari lile, akaanza kulimwagia mafuta kwa kasi ya ajabu kuanzia nje hadi ndani. Akawamwagia mafuta Bi Magdalena pamoja na binti yake, Sara. Bado sauti ya chini iliyojaa maumivu ilikuwa ikisikika kutoka kwa Bi Magdalena
Dominick hakuonekana kujali, bado aliendelea kuwamwagia petroli. Alipomaliza akaingiza mkono mfukoni na kuchukua kiberiti, akaliwasha gari lile. Moto mkubwa ukaanza kuwaka, Dominick akabaki pembeni akicheka tu. Gari liliendelea kuteketea zaidi na zaidi, uso wake bado ulikuwa umetawaliwa na tabasamu.
Mwanga wa tochi ukammulika usoni, Dominick akaonkana kushtuka kupita kiasi. Alijua kwamba mahali hapo alikuwa peke yake kutokana na usiku kuwa mwingi sana. Tochi ambayo ilimmulika usoni ndio ambayo ikamfanya kuanza kukimbia.
Milio ya mbwa waliokuwa wakija kwa kasi ikaanza kusikika. Dominick akaongeza kasi zaidi na zaidi. Mchanga mwingi wa ufukweni ndio ambao ulimfanya kutokukimbia kwa kasi. Mbwa watano walizidi kumsogelea zaidi na zaidi, ni umbali wa hatua kumi tu ndizo ambazo walikuwa wamebakiza kabla ya kumkamata Dominik ambaye alionekana kuchoka kutokana na mchanga mwingi uliokuwa pale ufukweni ambao ulimfanya kutokumbia kwa kasi.
“Kama kunikamata…acha tu wanikamate…sina ujanja” Dominick alijisemea huku kasi yake ikianza kupungua Tayari alikuwa amekwishakata tamaa kabisa. Aikuwa tayari kukamatwa na mbwa wale, kuumwa na hatimae mtu yule aliyemmulika tochi kumfikia.
*******
Walinzi wanne walikuwa wakiendelea na ulinzi katika nyumba ya balozi wa Marekani Bwana Brown Poll. Mbwa wakali ambao walikuwa wamepewa mafunzo ya kutoshwa walikuwa mikononi mwao, tochi pamoja na bunduki zilikuwa mikonon mwao.
8
Wawili walikuwa wakizunguka zunguka katika eneo la nyumba lile huku wengine wakiwa getini wakipiga stori lakini huku wakiwa makini kwa kila kitu ambacho kingeweza kutokea mahali hapo. Huku wakiwa katika maongezi yao, gari moja aina ya VX likapita kwa kasi mahali hapo kiasi ambacho kila mtu akabaki akishangaa.
Mbwa wakaanza kubweka kuashiria kitu cha hatari kilikuwa kinakwenda kutoke. Walinzi wote wakaonekana kupuuzia, wakabaki wakiendelea na stori zao. Wala hazikupita dakika nyingi, moto mkali ukaanza kuonekana kwa mbali.
Wote wakaonekana kushtuka. Moto ule ukaonekana kuwashtua kupita kiasi. Kwanza ilikuwa usiku sana kukutana na kitu kama kile. Kule baharini hakukuwa na mtu yeyote katika kipindi kile, sasa kwa nini kulikuwa na mwanga mkali wa moto.
Wakaandaa tochi zao na kuanza kusogea kule huku wakikimbia. Tayari walikwishaona kulikuwa na hatari ambayo ilisababisha moto ule kuwaka, walitaka kutoa msaada wa haraka katika kuuzima kutokana na maji kuwa karibu.
Kwa mbali wakaanza kumuona mtu akiwa amesimama pembeni, mlinzi mmoja akammulika kwa tochi aliyokuwa nayo, mara Dominick akaanza kukimbia hali ambayo iliwafanya kuwaachia mbwa wote watano waliokuwa nao mikononi kumkimbiza Dominick.
“Shiiiikaaaaa…shiiiiikaaaaa……” Mlinzi mmoja alisikika na kisha mbwa wale kuanza kumkimbiza Dominick ambaye akaanza kukimbia.
“Kumbe ni gari. Mungu wangu…!” Mlinzi mmoja alisema huku akishangaa.
Hawakutaka kuliona gari lile likizidi kuteketea, wakaanza kuchukua maji kutoka baharini kwa kutumia madumu mawili ambayo yalikuwepo mahali pale na kujaribu kulizima gari lile. Kazi haikuwa rahisi kabisa, kadri upepo ulivyozidi kuvuma na ndivyo ambavyo mot ule ulivyozidi kuchochewa.
8
Mpaka moto unazimika, tayari gari lile lilikuwa limeteketea kwa ailimia kubwa. Wakasubiri kwanza mpaka bati lipoe na ndipo wakaingia ndani. Miili miwili ndio ambayo ilikuwa imepatikana huku ikiwa imeteketezwa vibaya na moto ule ambao ulikuwa umeteketeza gari lile.
“Wewe si unajua kidogo kizungu..nenda kule waamshe watoto wa bosi waje huku kutoa msaada” Mlinzi mmoja alimwambia mwenzake ambaye akaanza kuondoka mahali hapo na kuelekea katika nyumba ile ya balozi wa Marekani.
Mara baada ya kufika kule, mlinzi akaanza kuugonga mlango ambako baada ya muda mtoto mmoja wa balozi akatokea na kisha kuanza kumuelezea kile ambacho kilikuwa kimetokea ufukweni. Kwa haraka sana kijana yule akachukua gari pamoja na yule mlanzi na kuanza kuelekea kule katika ufukwe.
Mara baada ya kuitoa miili ile, wakaipakiza katika gari lile na safari ya kuelekea hospitalini kuanza. Miili ilikuwa imeteketea vibaya kiasi ambacho ilikuwa ni vigumu kumjua huyu ni nani na yule ni nani.
“Mbwa wako wapi?” Mlinzi mmoja kati ya wale waliobaki aliuliza.
“Kumbe bado hawajarudi? Ebu twende tukaangalie, watakuwa wamemkamata na kuanza kumshambulia kiasi ambacho wamejisahau kurudi” Mlinzi mwingine alimwambia mwenzake huku wakianza kuelekea kule Dominick alipokimbizwa na mbwa.
********
Kijasho kilikuwa kikimtoka, alikuwa akikimbia kwa mwendo wa kasi kuifuata taksi moja ambayo ilikuwa katika eneo la hospitali ya taifa. Mara baada ya kuchukua taksi na kulipia gharama zote, safari ya kuelekea huko alipookuwa akitaka kuelekea kuanza.
Mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda mbio kutokana na kitu ambacho alikuwa amekiona. Aliliona gari likiendeshwa taratibu sana kiasi ambacho alimwambia dereva aendeshe kwa mwendo wa kasi. Bado moyo wake ulikuwa na hamu moja ya kufikisha taarifa juu ya kile ambacho alikuwa amekiona.
Taksi ikapaki katika eneo la kupakia magari ya klabu ya usiku ya Rapinho. Kwa haraka haraka kijana yule akateremka na kuanza kuelekea ndani ya klabu ile. Akaanza kumtafuta baunsa ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kulinda usalama katika klabu ile.
“Vipi tena Steve?” Dickson aliuliza huku akimwangalia Steve ambaye alikuwa akionekana kuwa na kiu ambacho alitaka kumwambia.
“Nimetokea Muhimbili” Steve alimwambia Dickson.
“Kwa hiyo?”
“Nimekutana na kitu ambacho kimenishtua sana” Steve alimwambia Dickson ambaye nae akaonekana kushtuka.
“Kitu gani tena?”
Steve hakujibu kitu, akabaki kimya kwa muda, akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule hali ambayo ilionyesha kama alikuwa akimtafuta mtu fulani mahali pale. Alipoona hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimtafuta, akayarudisha macho yake usoni mwa Dickson.
“Mama yuko wapi?”
“Mama gani?”
“Mke wa Mheshimiwa”
“Kama kawaida yake, kuna kijana kutoka Tanga alikuja mahali hapa, wakatamaniana, akaondoka nae” Dickson alimwamba Steve ambaye akaonekana kushtuka.
“Na binti yake?”
“Nani? Sara? Nae amemfuata alipokwenda” Dickson alijibu.
Steve akaonekana kushtuka zaidi. Mwili wote ukamlegea, us wake ukaonekana kujawa na majonzi. Dickson akaonekana kuhisi kitu, hali aliyokuwa ameionyesha Steve mbele yake tayari ikaonekana kumpa wasiwasi na kuona kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
Steve akaanza kupiga hatua kuelekea katika kaunta na kutulia. Bado alionekana kuwa na huzuni usoni mwake. Dickson akaanza kumfuata, tayari nae akahisi kwamba kulikuwa na kitu kimetokea ambacho Steve hakutaka kukiongea.
“Kuna nini lakini?”
“Ajali. Ajali ya moto” Steve alimwambia Dickson.
“Nyumba imeungua?”
“Hapana. Nafikiri mke wa mheshimiwa alichomwa moto pamoja na binti yake” Steve alimwambia Dickson.
Dickson akahisi mwili wake ukianza kupoteza nguvu, magoti yake yakalainika kiasi ambacho kikamfanya kuchuchumaa. Hakuamini kutokana na maneno ambayo alikuwa ameyasikia kutoka kwa Steve, akamwangalia mara mbili mbili huku akionekana kutokumuamini kabisa.
“Umesemaje?” Dickson aliuliza huku akionekana kutokuamini kibisa.
“Ndio hivyo”
“Umejuaje kama ni wao?”Dickson aliuliza.
“Nilikuwa hospitalini pale kumpeleka mke wangu, si unajua anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo, wakati nimemfikisha na kuanza kuondoka, nikakuta gari moja likiingia, nafikiri ni la balozi fulani kwani hata namba zake zilikuwa si za raia wa kawaida” Steve alimwambia Dickson an kuendelea.
“Nikaonekana kuvutiwa kuangalia ni mtu gani ambaye angeteremka, mara mzungu mmoja na kijana mwingine mweusi wakateremka na machela kuletwa haraka haraka. Miili ya watu wawili iliyoonekana kuungua vibaya na moto ikateremshwa. Nikaiangalia vizuri. Nikamgundua Sara kwa kuwa sura yake haikuwa imeungua sana, lakini kwa Bi Magdalena, sijui kama utaweza kumjua kama ukionyeshewa” Steve alimwambia Dickson.
Dickson akachoka zaidi na zaidi. Steve akaanza kuwaambia na watu wengine juu ya tkio lile hali ambayo ikawafanya watu wengi kutoka nje ya ukumbi kuona kama gari lake lao lilikuwa mahali pale. Gari halikuwepo, kila mmoja akajua kwamba kile ambacho alikuwa amekiongea Steve kilikuwa na ukweli.
Kila mtu mahali pale akaanza kuongea lake, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo idadi ya watu ikazidi kuongezeka zaidi na zaidi. Kila mtu alikuwa akionyesha kuhuzunika, taarifa ile ilionekana kumshtua kila mtu, hakukuonekana kuwa na haja ya kurudi ndani ya klabu na kuburudika.
Wala hazikupita dakika nyingi, mzee akafika mahali hapo, akateremka kutoka garini na kuanza kuwafuata watu wale waliokusanyika huku uso wake ukionekana kuwa na mashaka.
“Kuna nini jamani” Mzee Ombeni aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
*********
Dominick alikuwa amechoka kupita kiasi, alibaki akiwa amesimama tu huku akiwasubiria mbwa ambao walikuwa wakimfuata kwa kasi huku wakibweka. Ghafla, akili ikamjia kichwani mwake. Akaanza kuiangalia bahari ambayo ilkuwa imetawaliwa na mawimbi mengi makubwa.
Akili ambayo ilimjia kwa wakati huo ni kukimbilia na kwenda kujiingiza katika bahari ile. Wala hakutaka kuchelewa, moja kwa moja akaanza kukimbia tena kuifuata bahari ile na kuingia. Kutokana na mawimbi makubwa ambayo yalikuwepo baharini, mbwa wale wakashindwa kuingia, wakabaki pembezoni mwa bahari huku wakiendelea kubweka.
Walinzi wa nyumba ya barozi wakafika mahali pale, wakawaona mbwa wao wakiendelea kubweka huku wakiangalia baharini hali iliyowafanya kujua kwamba mtu ambaye walikuwa wakimkimbiza alikuwa amekimbilia baharini. Wakajaribu kuangalia anglia baharini lakini hawakuona mtu yeyote.
Dominick alikuwa akiendelea kupiga mbizi kuelekea katika upande mwingine. Mawimbi makubwa ya bahari ile yalionekana kumchosha zaidi lakini hakutaka kuacha kupiga mbizi. Moyo wake ulikuwa na furaha kila alipofikiria kuwa tayari alikuwa ameiteketeza familia ya waziri Ombeni..
Alipiga mbizi na kutokea katika sehemu nyingine ya mbali. Akaanza kutoka na kuelekea katika barabara ambayo wala haikuwa na magari mengi katika muda huo. Akaangalia macho yake katika kila upande, akaziona bajaji kadhaa zikiwa zimepaki nje ya ukumbi wa sinema wa 3D Movie.
Akakodi bajaj moja na kuanza kurudi nayo hotelini, La Vista Inn. Muda wote Dominick alikuwa akionekana kuwa na furaha, alijiona kuwa shujaa kuliko hata mwanajeshi ambaye alikuwa ametoka kupigana vita na kushinda.
“Mmmmh! Mbona hela yenyewe imeloa broo?” Dereva wa bajaji aliuliza huku akiigeuza geuza noti ya shilingi elfu kumi aliyopewa.
“Si unajua nilitumbukia kwane bwawa la kuogelea. Ila usijali, chukua yote tu” Dominick aimwambia dereva ambaye alionekana kushukuru.
Dominick akaanza kupiga hatua kuelekea katika ngazi za hoteli ile ambako akapanda mpaka katika ghorofa aliyoitaka na kuanza kutembea hadi katika chumba chake. Akajilaza kitandani, uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu pana. Akachukua rimoti ya televisheni yake na kisha kuiwasha tv huku akiwa na hamu ya kutaka kuangalia kile ambacho kilikuwa kimeajili kwa wakati huo.
*************
Mpelelezi Bugabu alikuwa akijiandaa kuanza kufanya kazi ambayo alikuwa amekabidhiwa na serikali ya kumtafuta muuaji ambaye alikuwa ameiteketeza familia ya waziri Boniface. Kitu cha kwanza ambacho alikifanya ni kwenda katika kituo cha polisi cha Osterybay nawa lengo la kutaka kuonana na Mrisho, dereva aliyekuwa akiendesha gari la waziri Boniface.
Kutokana na umaarufu wake pamoja na cheo chake, hakukuwa na polisi yeyote ambaye alimzuia, kwa haraka sana akapelekwa katika chumba cha mahojiano ambapo baada ya muda wa dakika chache, Mrisho akaletwa mahali hapo.
Hali ya afya yake ilikuwa imeanza kubadilika, muda wote alikuwa akionekana mpweke, unyonge ulionekana kumjaa. Akakaa kitini na kuanza kumwangalia mpelelezi Bugabu. Akili yake ikaanza kurudi nyuma huku akianza kufikiria kama alikwishawahi kumuona mtu huyo katika maisha yake, jibu alilolipata, lilikuwa ‘hapana’
“Karibu” Bugabu alimkaribisha Mrisho mahali pale. Mrisho hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia mpelelezi Bugabu huku akionekana kuchoshwa na maisha ya pale.
“Unataka nikusaidie nini?” Mrisho aliuliza.
“Nataka kumfahamu huyu muuaji. Najua utakuwa umemuona tu. Nataka uniambie huyu muuaji ni nani” Mpelelezi Bugabu alimuuliza Mrisho ambaye bado alikuwa akimwangalia Bugabu kwa macho yaliyokuwa na hasira.
“Simfahamu mtu huyu”
“Haumfahamu? Acha utani. Kwenye maelezo yako ulipoingia katika kituo hiki ulisema alikuteka garini, ukaenda nae mpaka kwako, sasa kwa nini unasema haumfahamu? Yaani hata rangi ya ngozi yake?” Bugabu aliuliza huku akionekana kuanza kupata hasira.
“Ningemfahamu vipi kama mtu mwenyewe muda wote alikuwa amevaa kofia? Toka aliponiteka mpaka kuniacha, hakuitoa kofia yake kichwani” Mrisho alimwambia Bugabu.
“Kwa hiyo haufahamu kitu chochote kile?”
“Sifahamu”
“Ila si alikuja na gari lake?”
“Ndio”
“Nalo pia haulifahamu?”
“Nalifahamu. Ilikuwa chesser mayai nyeusi”
“Namba za gari?”
“Nilichanganyikiwa sana kiasi ambacho sikuweza hata kuangalia namba za gari” Mrisho alimwambia Bugabu.
“Nashukuru kwa ushirikiano wako” Bugabu alimwambia.
Buganu akainuka kutoka kitini, hakuona kama Mrisho angeweza kumsaidia katika kile ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo. Akaondoka na moja kwa moja kuelekea nje ya kituo kile abako akachukua gari lake na kuanza kuelekea nyumbani kwake.
Hakujua aanze wapi, kazi kwake ilikuwa ikionekana kuwa rahisi katika kipindi cha nyuma lakini kwa wakati huo tayari akaanza kuiona ngumu. Ila pamoja na mambo hayo yote, hakutaka kukata tamaa, dhamira ya kutaka kumkamata muuaji ilikuwa ikiendelea kubaki moyoni mwake.
***************
Mzee Ombeni hakuonekana kuamini kile ambacho alikuwa ameambiwa, hakuamini kabisa kama ndoto ile ambayo alikuwa ameiota kuhusiana nakuchomwa moto kwa familia yake ndicho ambacho kilikuwa kimetokea. Akanyong’onyea na kuchuchumaa chini.
Kila mtu akabaki akimwangalia mheshimiwa Ombeni kwa jinsi ambavyo alivyochanganyikiwa. Hakuamini kama kwa wakati huo alikuwa ameipoteza familia yake kama jinsi ambavyo Bwana Boniface alivyoipoteza familia yake. Mauaji ya kuteketezwa kwa moto ndio ambayo yalionekana kumchanganya zaidi.
Akainuka na kuanza kukimbia kulifuata gari lake ambalo alikuwa amelipaki katika maegesho ya magari mahali pale. Akapanda na moja kwa moja safari ya kuelekea katika hospitali ya Muhimbili kuanza. Muda wote alikuwa amechanganyikiwa, machozi yalikuwa yameanza kumtoka, hakuamini kama siku hiyo ndio ilikuwa siku ya kuipoteza familia yake.
Kutokana na namba za gari lake kuonyesha kwamba alikuwa mtu kubwa Serikalini, geti likafunguliwa na moja kwa moja kuliingiza gari ndani ya eneo la hospitali ile. Akatereka huku akionekana kuchanganyikiwa
“Mheshimiwa….” Aliisikia sauti ikimuita.
Akageuka nyuma, macho yake yakatua kwa daktari ambaye alikuwa amevaa koti refu jeupe huku akiwa na msichana ambaye alikuwa na gauni refu jeupe. Akaanza kupiga hatua kuwafuata watu hao.
“Niambie daktari” Bwana Ombeni alimwambia dokta hata kabla ya salamu.
“Nikuambie nini?”
“Kuhusu mke wangu na binti yangu”
“Njoo ofisini”
************
Muda wote Bwana Ombeni alikuwa akilia, hakuami kama kweli alikuwa ameipoteza familia yake. Maisha yake akayaona kuanza kubadilika, kuishi pasipo familia yake lilikuwa jambo ambalo hakuwahi kuliwaza katika maisha yake.
Kwenye msiba, muda wote alikuwa akilia tu kama mtoto, familia yake ilikuwa kila kitu maishani mwake. Akajiona kupoteza kitu cha maana sana katika maisha yake yaliybakia. Hakujua ni kitu gani ambacho angemfanya yule ambaye alikuwa amehusika katika kuiteketeza familia yake, moyo ulimuuma kupita kiasi.
Magazeti mitaani yalikuwa na habari juu ya mauaji hayo. Kila mtu aliyeisoma alibaki kuwa na mshangao. Wala haukupita hata muda mrefu tangu Bwana Boniface alipoondokewa na familia yake, tena kwa kuteketezwa na moto namna ile, tukio jingine lilikuwa limetokea.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akifahamu chanzo cha muuaji kuziteketeza familia hizo, tena kwa moto katika magari yao. Mapolisi walibaki wakiwa wamechaganyikiwa kupita kawaida. Mt ambaye alikuwa amevaa kofia kubwa aina ya Malboro ndiye ambaye alikuwa akihusishwa katika matukio yae.
Kila mtu alikuwa akijiuliza juu ya muuaji huyo ambaye alikuwa akipenda kuvaa kofia ya aina hiyo. Viongozi wengine wakaanza kupatwa na wasiwasi juu ya matukio hayo ambayo yalikuwa yametokea. Hakukuwa na kiongozi ambaye alikuwa akiishi kwa furaha, kila mmoja alikuwa akiishi kwa wasiwasi huku ulinzi wa familia yake ukizidi kuongezeka.
“Mmmmh! Au atakuwa Dominick?” Bwana Boniface alimuliza Bwana Tumaini.
“Hakuna. Yule kwa sasa ni maiti, amekwishazikwa muda mrefu uliopita” Bwana Tumaini alijibu.
Hakukuwa na mt ambaye alikuwa akimfikiria Dominick kuhusika katika mauaji yale, bado kitendawili kilikuwa mioyoni mwao juu ya muuaji ambaye alikuwa ameziteketeza familia zile. Kila siku waandishi wa habari walikuwa wakitoa taarifa kuhusu matukio hayo ambayo yalionekana kuitikisa Serikali.
“Au vyama pinzani wanataka kuchukua majimbo yetu?” Bwana Boniface aliuliza.
“Hilo linawezekana. Si unajua kwa jinsi tunavyochukiwa! Ni lazima watakuwa wapinzani, katika hili yatupasa kujiandaa” Bwana Tumaini alijibu.
**************
Katika maisha yake hakuwahi kupata mtoto. Kila siku haya ndio yalikuwa maombi yake kwa Mungu, alitamani kupata mtoto katika maisha yake kuliko kitu chochote. Aliiona ndoa yake kutokukamilika kabisa, ni kweli alimpenda sana mumewe lakini tatizo lilikuwa mtoto.
Aliangaika kwenda sehemu zote lakini hakupata suluhisho la tatizo lake. Alibaki nyumbani akilia, mumewe ndiye alikuwa mtu ambaye alikuwa akimbembeleza kila siku. Alimtumaini Mungu kwa kuamini kwake Yeye hakuna ambacho kilishindikana.
Kila siku alikuwa akimuomba Mungu pamoja na mumewe lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Kwa kuwa mumewe alikuwa na fedha nyingi, wakaamua kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta suluhisho lakini bado tatizo lilikuwa vilevile tu, mtoto hakupatikana.
Suala la kutokupata mtoto ndio likaonekana kuwa tatizo kubwa katika ndoa yao. Ingawa alikuwa ameridhiana na mumewe lakini tatizo kubwa lilikuwa kwa ndugu wa mume. Kila siku walikuwa wakiongea yao, kila siku malalamiko yalikuwa hayaishi nyumbani.
Maisha ya msichana Edith yakapoteza kitu muhimu sana katika maisha yake, furaha. Kila alipokuwa akiongea na mumewe, bado alikuwa akijiona kuumia kupita kiasi, alihitaji kuitwa mama, alihitaji kunyonyesha kama wanawake wengine walivyokuwa wakinyonyesha.
Kila alipokuwa akiondoka nyumbani asubuhi kuelekea kazini, basi alipokuwa amerudi, nyumba haikuwa na mabadiliko hata kidogo. Kama aliacha vitambaa vya makochi vikiwa makochini, alivikuta hivyo hivyo. Alitamani apate mtoto ambaye angeweza kuvirusharusha vitambaa vile na kuifanya nyumba kutokuwa na mvuto.
Kila siku ndoto zake zilikuwa ni kupata mtoto, hata mtoto mmoja kwake ilikuwa tosha kwani aliamini ni lazima angewanyamazisha ndugu ambao walikuwa wakiendelea kulalamika. Mumewe hakutaka kumuacha, kila siku alikuwa akiongea nae huku akimfariji, aliamini kila kitu kilichokuwa kinatokea, kilikuwa katika mipango ya Mungu.
Kilio kiliendelea kila siku, Mungu akakisikia kilio chake, Edith akapata ujauzito ambao ulionekana kuleta matumaini katika maisha yake. Furaha ilikuwa kubwa katika maisha yake. Mapenzi yakaongezeka katika familia hiyo, ndugu ambao kazi yao ilikuwa ni kulalamika kila siku wakawa wamefungwa midomo, hawakuwa na la kuongea.
Kila siku mumewe alikuwa akitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa kununua vitu mbalimbali na kuvileta nyumbani kwa mkewe, Edith. Ndoto zake zilioekana kutimia, hasa kila alipokuwa akiliona tumbo la mkewe likizid kuongezeka kila siku.
“Ni mwanaume” Edith alimwambia mumewe katika kipindi ambacho walikuwa sebuleni.
“Mwanaume! Mungu wangu! Ataitwa Brian…ataitwa Brian” Mumewe alimwambia huku akiishika shika tumbo lile.
Furaha ilikuwa ikiongezeka kila siku, ujauzito ule ukaonekana kuleta furaha kubwa na mabadiliko makubwa maishani mwao. Mumewe akawa akirudi mapema tofauti na zamani. Hakutaka kuwa mbali na mkewe kwani aliona kwamba alikuwa akihitajika kuliko mtu yeyote kwa mwanamke huyo.
Huyu ndiye alikuwa Bwana Tumaini, mlengwa ambaye familia yake ilikuwa ikihitajika kuliko kitu kingine na Dominick. Taarifa za ujauzito wa mke wa waziri kijana zilipokuwa zikitolewa gazetini, kila mtu alijisikia kuwa na furaha lakini kwa Dominick hali ilikuwa ni tofauti kabisa, moyo wake ulikuwa ukitaka kumuua Edith kama kulipa kisasi kwa kile ambacho alifanyiwa na mawaziri hao.
Mipango yake ilikuwa ikiendelea kila siku. Akaifuatilia ratiba nzima ya muda ambao Edith alikuwa akitoka nyumbani na kuelekea kliniki. Ratiba nzima alikuwa nayo, hakujali kuhusu ujauzito ambao alikuwa nao,kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kumuua Edith, msichana ambaye wala hakuwahi kumuona hata kwa sura zaidi ya kumsikia katika vyombo mbalimbali vya habari akitangazwa.
“Ni lazima nimuue. Mumewe si aliiangamiza familia yangu! Na yeye ni lazima afe kwa ajili ya mumewe, ni lazima nilipe kisasi” Dominick alijisemea.
**************
9
Miezi miwili ikakatika, mawaziri wale watatu wakakutana. Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakujua ni nani ambaye alikuwa nyuma ya matukio yale. Kila mmoja alikuwa akimfikiria Dominick lakini kila walipokuwa wakikumbuka kama Dominick walikuwa wamemuua, waliyapuuzia mawazo yao.
Swali lilikuja juu ya nani ambaye alikuwa akifanya mauaji yale, tena mbaya zaidi kwao, watu ambao walikuwa wamehusika na mauaji ya familia ya Dominick. Suala hili likaonekana kuwachanganya vichwa vyao. Bwana Boniface na Ombeni walikuwa wameumizwa na vifo vya familia yao, na sasa walikuwa wakimsikitikia Tumaini kwani waliamini kwamba nae ni lazima familia yake ingeangamizwa tu.
“Hapana…huyu ni Dominick tu” Bwana Bonifce aliwaambia.
“Dominick! Hapana bwana. Ninakataa hilo” Bwana Ombeni alimwambia.
“Kwa nini unakataa?’
“Tulikwishamuua”
“Una uhakika gani kama vijana wetu walimuua?”
“Na wewe una uhakika gani kama anayefanya mauaji ni Dominick?”
“Hebu sikiliza. Tuliiangamiza familia ya Dominick kwa kuichoma moto. Unakumbuka?” Bwana Boniface aliuliza.
“Nakumbuka sana”
“Na unakumbuka kama tuliichoma moto nyumba yake?”
“Ndio”
“Nafikiri nae anaziteketeza familia zetu kwa moto kama tulivyoiteketeza yake” Bwana Boniface aliuliza.
“Kama ni yeye, alijua vipi kama sisi ndio tulioiteketeza familia yake?” Bwana Tumaini aliuliza.
Hilo lilikuwa swali jingine ambalo lilionekana kumchanganya kila mtu. Sababu ambazo alizitoa Bwana Boniface zilionekana kuwa na ukweli kwamba mauaji yale yalikuwa yakifanywa na Dominick, lakini alijua vipi kama wao ndio walikuwa wameiteketeza familia yake?
Kila mmoja akabaki kimya huku akionekana kufikiria lake tu. Tayari akili zao zilikuwa zimetoka kabisa nje ya kikao kile. Walitumia dakika kadhaa, Bwana Boniface akanyanyua glasi ya maji na kupiga fundo moja na kisha kuirudisha glasi ile mezani.
“Nimekumbuka” Bwana Boniface aliwaambia.
“Umekumbuka nini” Tumaini aliuliza.
“Tulifanya makosa sana kuwaambia vijana wae waandike maneno yale yaliyoandikwa”
“Unamaanisha BoT?”
“Ndio”
“Lakini si tulikubaliana kwamba yaandikwe ili kumchanganya kila mtu?”
“Ndio. Ila hayo ndio yaliyotuharibia. Ila hapa kuna swali najaribu kujiuliza. Alijua vipi kama sisi ndio tumehusika? Katika Serikali kuna watu wengi ambao majna yao huanzia na herufi hizi. Amejua vipi kama ni sisi?” Bwana Boniface aliuliza
Hilo lilikuwa swali jingine ambalo liliwafanya kubaki kimya kwa muda, hawakujua ni kitu gani ambacho kilitakiwa kujibiwa ili kumridhisha kila mmoja. Ni kweli waliiteketeza familia ya Dominick kwa kuichoma moto na kuandika maneno ambayo waliamini yangeweza kumchanganya kila mtu ila Dominick aliipataje maana ya maneno yale?
“Hakuna haja ya kuumiza vichwa”
“Kwa nini?”
“Wote si tunaamini kwamba Dominick ndiye anayefanya haya?”
“Ndio”
“Kwa hiyo hii inamaanisha kwamba vijana wetu walitudanganya?”
“Ndio”
“Basi inatubidi tuamini kwamba wao ndio waliomwambia” Bwan Boniface aliwaambia.
Kila mmoja aliliona jambo hilo kuwezekana. Kama kulikuwa na uwezekano wa vijana wale waliowatuma kumuua Dominick waliwadanganya, basi ingekuwa jambo rahisi hata kwa wao kumwambia Domonick maana ya maneno yale.
Tumaini akaonekana kuwa na wasiwasi. Tayari alikwishaona kuwa familia yake ndio ambayo ilikuwa ikifuata baada ya wale wenzake kuzipoteza familia zao. Hakutaka kabisa mkewe auawe, kila wakati alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi kupita kawaida.
Moja kwa moja akaichukua simu yake na kuanza kumpigia mkewe. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo wasiwasi ulivyozidi kumpata. Simu ilikuwa ikiita, iliendela kuita zaidi na zaidi lakini wala haikupokelewa.
Wasiwasi ukazidi kuongezeka zaidi mara baada ya kujaribu tena kuipiga simu ile na kukuta ikiwa imezimwa. Akaitoa simu sikioni na kuanza kuiangalia, Bwana Boniface na Ombeni walibaki wakimwangalia, waliuona wasiwasi ambao alikuwa nao lakini hawakuelewa sababu ambayo ilimfanya kubadilika namna ile.
“Vipi?’
“Mke wangu”
“Amefanya nini?”
“Nafikiri kuna tatizo. Nampigia simu, inabaki inaita pasipo kupokelewa. Sasa hivi nimempigia, haipatikani hali inayoonyesha imezimwa” Tumaini aliwaambia.
“Kawaida tu. Si unajua wanawake watu wa kujisahau sana” Bwana Ombeni alimwambia.
“Hapana. Hii si kawaida. Ni lazima niende nyumbani Najua huyu anaweza kuwa Dominick” Tumaini alisema na kwa kasi kubwa akaondoka mahali hapo huku akiwaacha wenzake wakibaki na mshangao.
Njia nzima alikuwa akijaribu kuipiga simu ya mke wake akini hakukuwa na majibu, bado simu ilikuwa imezimwa. Akili yake ilichanganyikiwa kupita kiasi. Alitumia dakika kumi mpaka kufik nyumbani ambako akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika eneo lanyumba yake.
Hakukuwa na watu wengine zaidi ya wafanyakazi wake wa ndani ambao. Kila mfanyakazi ambaye alimuuliza, jibu lilikuwa ni kutokumuona toka alipokwenda kliniki. Maneno hayo ndio yaliyoonekana kumchanganya zaidi, masaa matatu yalikuwa yamepita tangu Edith aende kliniki.
Huku akionekana kuchanganyikiwa, akaingia garini na kisha kuanza safari ya kuelekea Kliniki. Bado akili yake haikuwa sawa kabisa, tayari wasiwasi ulikuwa umemshika moyoni.
Mara baada ya kufika kliniki, moja kwa moja akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi. Hakukuwa na wagonjwa wengi katika kliniki ile jambo ambalo lilioekana kumtia wasiwasi kwani alijua kama mkewe angekuwa amekwenda mahali pale angekuwa amekwisharudi nyumbani.
“Mke wangu alifika hapa?” Tumaini alimuuliza dada wa mapokezi hata kabla ya salamu
“Mmmmh! Hata salamu!”
“Samahani. Za sa hizi! Mke wangu alifika hapa?”
“Nani?”
“Ina maana mimi haunijui?” Timoth aliuliza swali lililomfanya dada yule kuanza kumwangalia katika hali ya kumchunguza.
“Aaaahh! Kumbe mheshimiwa! Samahani. Mkeo hajafika hapa” Yule dada alijibu.
“Hajafika? Mbona niliambiwa amekuja hapa Kliniki!”
“Mhh! Hapa ala sijamuona toka asubuhi” Yule dada alitoa jibu lililomchanganya sana Timoth.
**************
Dominick alikuwa akifuatilia kila kitu, ratiba ya Edith ya kwenda katika kliniki ilikuwa kichwani mwake. Kitu alichokifanya kwa wakati huo si kumfuatilia kuanzia nyumbani, alichokifanya yeye ni kwenda moja kwa moja katika kliniki ambayo Edith alikuwa akienda kila siku.
Kwa kuwa hakuja na gari lake, akaelekea katika sehemu ambayo wagonjwa walikuwa wakipumzikia. Dominick alitulia huku akiwa amevalia kofia kichwani mwake. Dominick hakuwa hivi hivi, mkononi alikuwa na kidumu cha njano ambacho ndani yake kulikuwa na petroli.
Alikaa katika sehemu ile kwa takribani dakika kumi, gari aina ya Harrier ikaanza kuingia mahali hapo. Tayari Dominick alijua kwamba lile gari lilikuwa likiendeshwa na Edith, mke wa waziri Timoth, Wala hakuonekana kuwa na haraka, aliendelea kusubiri kwa muda, Edith akateremka kutoka garini nakuanza kuelekea ndani ya jengo la kliniki ile.
Baada ya dakika arobaini na tano, Edith akatoka na kuanza kulifuata gari lake. Dominick akaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata Edith. Mara baada ya Edith kuufungua mlango wa upande wa dereva, Dominick akaufuata mlango wa upande mwingine na kuingia huku akiwa na kidumu chake.
Edith akaonekana kushtuka, hakuelewa ni mtu gani alikuwa ameingia garini mwake. Hata kabla hajaongea kitu chochote kile, akauona mdomo wa bunduki ukiwa umemlenga mahali pale alipokuwa. Edith akaanza kutetemeka kwa hofu, tayari alijiona kuwa nusu mfu.
“Ukipiga kelele…ukiongea chochote au hata kuuliza swali lolote…roho yako halali yangu” Dominick alimwambia Edith huku akiiweka vizuri kofia yake pamoja na miwani yake myeusi.
“Unachotakiwa ni kufuata maelekezo yangu. Washa gari na moja kwa moja endesha kuelekea katika pori la Nyakipande” Dominick alimwambia Edith ambaye alikuwa akitetemeka tu.
Hakukuwa na sababu ya kuuliza swali, tayari mkwara ambao alikuwa amepigwa ulikuwa umemuogopesha kupita kawaida. Akaliwasha gari na safari ya kuelekea katika pori la Nyakipande lililokuwa Mbezi kuanza. Garini Dominick hakutaka kuongea kitu chochote kile, alikuwa makini kuangalia mbele.
Alikishikiria vizuri kidumu chake kilichokuwa na petroli tayari kwa kumchoma moto Edith mara tu watakapofika Nyakipande. Dominick hakujali kama Edith alikuwa mjauzito au la, kitu ambacho alikuwa akikijali mahali hapo ni kulipiza kisasi kwa kuteketezwa kwa familia yake.
Muda wote Edith alikuwa akitetemeka, tayari alijiona kuelekea kuuawa. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka kupita kiasi. Hakuwa na amani kabisa moyoni mwake, tayari aliona muda wowote ule alikuwa akielekea kuuawa.
Kutokana na foleni za hapa na pale, walitumia saa moja mpaka kufika Mbezi na kuingia katika pori hilo. Gari likaegeshwa katikati ya pori, sehemu ambayo hakukuonekana kuwa na dalili yoyote ile. Dominick akaufungua mlango na kutoka nje, akaelekea katika mlango uliokuwa katika upande wa dereva na kumfungulia Edith mlango.
Dominick akamshika Edith na moja kwa moja kumpeleka katika mti mmoja mkubwa na mrefu. Edith alikuwa akilia, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa akielekea kuuawa. Tayari harufu ya petroli ilikuwa ikisikika vizuri puani mwake, hakuona kama angeweza kunusurika.
Dominick akaingiza mkono mfukoni na kutoa kamba ngumu, akamsogeza Edith mtini na kisha kumfunga. Muda wote Edith alikuwa akilia huku akipiga kelele lakini Dominick hakuonekana kuelewa kitu chochote kile. Edith alikuwa akiomba msamaha japokuwa hakujua kosa lake lilikuwa nini.
“Ni lazima nikuue kwa kukuchoma moto” Dominick alimwambia Edith na kuanza kummwagia petroli.
“Naomba unisamehe…naomba unisamehe..” Edith aliendelea kuomba msamaha
“Ni lazima nikuue. Mumeo aliiangamiza familia yangu. Na mimi ni lazima niiangamize familia yake pia” Dominick alimwambia.
“Naomba unisamehe…naomba unisamehe. Sijui chochote…” Edith alimwambia Dominick.
“Sitoweza. Mimi kama Dominick sitoweza. Nataka kuwaonyeshea kwamba sikufa, bado ninaendelea kulipiza kisasi kwa ajili ya mke wangu Christina pamoja na mtoto wangu Ibrahim” Dominick alisema huku akiungiza mkono mfukoni na kutoa kiberiti.
“Dominick….Dominick Hyera, naomba usiniue” Edith alimwambia Dominick.
Dominick akaonekana kushtuka, hakuelewa kama jina alilokuwa ameitwa aliitwa na Edith au mtu mwingine. Akayapeleka macho yake usoni mwa Edith na kuanza kumwangalia kwa makini. Dominick akazidi kusogea karibu zaidi huku macho yake yakimwangalia vizuri Edith katika hali ya kumchunguza.
“Naomba usiniue Dominick…Naomba usiniue” Edith alimwambia Dominick.
Dominick akaanza kupiga hatua kumsogelea Edith, alipomfikia na kumwangalia vizuri, Dominick akapiga magoti chini, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake, hakuamini kukutana na mtu huyo katika maisha yake. Mwili wote ulikuwa umenyong’onyea.
“Edith Philip….”
“Ni mimi Dominick…ni mimi” Edith alijibu.
*************
Kila alipokuwa akipita kwa mwanafunzi yeyote, alikuwa akichekwa kupita kiasi. Mavazi yake hayakuwa masafi hata kidogo, yalionekana kuchakaa kupita kawaida. Katika maisha yake shuleni hapo, Dominick hakuwahi kuvaa viatu, kila siku alikuwa akienda shuleni na kandambili miguuni.
Alionekana kuwa mwanafunzi wa tofauti kuliko wanafunzi wote shuleni pale. Wazazi wake hawakuwa na fedha hata kidogo, fedha ambazo walikuwa wamezipata katika biashara yao waliyoifanya ya kuuza shamba hazikuweza kumsaidia Dominick kutokana na asilimia kubwa ya fedha zile kuingizwa katika mahitaji mengine.
Shuleni alijisikia mpweke, hakuwahi kusifiwa kupendeza hata mara moja, kila siku alikuwa akionekana kituko machoni mwa wanafunzi wengine. Dominick hakuwa na marafiki shuleni, rafiki yake mkubwa alikuwa kitabu, kila alipokuwa akikaa peke yake, alikuwa akisoma jambo ambalo lilionekana kumpa faraja kubwa.
Katika mwaka wa kidato cha kwanza chote, Dominick hakuwa na marafiki wa kukaa nae na kuongea nae, wanafunzi wengi ambao walikuwa marafiki zake, walikuwa wakimsalimia mbali mbali tu. Jambo hili lilionekana kumuumiza sana Dominick ambaye hakuonekana kujali sana.
Alipoingia kidato cha pili, msichana Edith ndipo akaingia shuleni hapo. Kutokana na uzuri wake mkubwa aliokuwa nao, wavulana wengi walikuwa wakianza kumfuatilia Edith ambaye alionekana kuwa mgumu kumkubalia mvulana yeyote shuleni hapo.
Kit ambacho wanafunzi hawakuamini ni pale Edith alipoanza urafiki mkubwa na Dominick. Kila siku ilikuwa ni lazima kwa Edith kuelekea katika darasa la Dominick na kukaa nae huku wa kipiga stori hasa katika kipindi ambacho hakukuwa na walimu.
Edith akaonekana kuwa rafiki mkubwa wa Dominick, wakatokea kupendana kuliko wanafunzi wengine shuleni pale. Kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao wazazi wake, Edith akaanza kununua baadhi ya nguo kama mashati ya shule na kumpelekea Dominick ambaye alionekana kuwa na furaha kupita kiasi.
Ukaribu wao ulikuwa ukiongezeka kila siku kiasi ambacho mapenzi makubwa yakaanza kuibuka mioyon mwao. Wote walionekana kujaliana ingawa hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa radhi kumwambia mwenzake juu ya alivyojisikia moyoni
“Nakupenda Dominick” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara yalikuwa yakisikika kutoka mdomoni mwa Edith.
Dominick alikuwa akiogopa kumwambia Edith kitu chochote kuhusu mapenzi. Kila siku alikuwa akiyaangalia maisha yake na kisha kuyaangalia maisha ya Edith. Walionekana kuwa watu wawili tofauti hali ambayo ilimfanya Dominick kujiona kutokuwa na hadhi ya kuwa na msichana kama Edith.
Kama kulia, Edith alilia sana, na kama kubembeleza, Edith alibembeleza sana lakini Dominic hakuwa tayari kuwa na Edith. Alihitaji kuwa peke yake, maisha ya kutengwa ambayo alikuwa akiyaishi nyumbani, alijiona kutokustahili kupendwa na msichana yeyote yule.
Edith hakukoma, kila siku alikuwa akisisitiza juu ya upendo wake kwa Dominick ambaye bado aliendelea kukataa. Edith hakuonekana kuwa na raha, kila siku alionekana kuwa na maumivu moyoni, kuataliwa na Dominick kulionekana kuwa jambo kubwa na baya ambalo halikuwahi kutokea maishani mwake.
“Naomba unielewe Dominick” Edith alimwambia Dominick.
“Nafahamu Edith. Hebu jiangalie jinsi ulivyo, halafu niangalie na mimi. Hivi tunalingana kweli?” Dominick alimuuliza Edith.
“Mapenzi hayako namna hiyo Dominick. Mapenzi hayaagalii kuhusiana na mambo ya fedha. Mapenzi uangalia mioyo yetu. Nakuomba Dominick, nakuomba niwe pamoja nawe” Edith alimwambia Dominick.
Maneno hayo kila siku yalikuwa yakipita katika sikio la kushoto na kutokea sikio la kulia, Dominick hakuonekana kuelewa kitu chochote kile.
Siku ziliendelea kwenda mbele mpaka katika kipindi ambacho Dominick akaanza kuzielewa hisia za Edith juu yake. Dominick akagundua ni kwa jinsi gani Edith alikuwa amedhamiria kumpenda. Akaanglia jinsi ambvyo alijitolea kila kitu kwa ajili yake, hakuona sababu ya kumkataa.
Mapenzi yao yakaanza katika mwaka huo ambao walikuwa kidato cha pili. Kila siku walikuwa pamoja huku Edith akimtembelea Dominick nymbani kwao, Manzese Midizini.. Maisha ambayo alikuwa akiishi Dominick na wazazi wake yalimsononesha Edith ambaye kila wakati alikuwa akilia tu.
Alimpenda sana Dominick kiasi ambach hakutaka apate shida yoyote ile katika maisha yake, maisha ya dhiki ambayo alikuwa akiishi Dominick yalikuwa yakimuumiza kama alikuwa akiishi yeye. Pamoja na maisha hayo yote lakini Edith bado mapenzi yake makubwa yalikuwa juu ya Dominick.
Wakati wanaingia kidato cha tatu, baba yake Edith, mzee Philip akaamishiwa Kagera kikazi. Huo ndio ukawa mwisho wa wawili hawa kuwasiliana. Edith hakuwa na simu na wala Dominick hakuwa na simu. Kila siku waliendelea kukumbukana lakini hawakuwa na jinsi y kufanya zaidi ya kuendelea kukumbukana na kuotana ndotoni.
Baada ya mwaka mmoja, Dominick akamaliza kitato cha nne. Matokeo yake yalikuwa mazuri, akachaguliwa kujiunga na shule ya Azania. Moyo wake ambao ulikuwa ukimpenda sana Edith ukaanza kumpoteza kwa sababu akajiona kukata tamaa ya kumpata msichana huyo.
Pamoja na hayo yote Dominick hakutaka kumchukua msichana mwingine, alitamani maisha ya kuwa peke yake shuleni. Miaka miwili ikakatika shuleni na kufanya mtihani wa kidato cha sita. Matokeo yake hayakuwa mazuri sana hivyo akaamua kwenda kujiunga na chuo cha kuliia cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalism)
Katika kipindi ambacho alikuwa akisoma huko ndipo alipokutana na msichana Christina katika sherehe moja iliyoandaliwa na wanachuo wa chuo hicho. Christina hakuwa mwanachuo wa chuo hicho, yeye alikuwa akitokea katika chuo cha IFM ila alikuja mahali hapo kama sehmu ya kusherehekea pamoja na marafiki zake.
Wakaanza kupeana namba za simu ambzo ziliwafanya kila siku kuwasiliana. Urafiki huo ukaendelea zaidi na zaidi huku wakichukua nafasi za kutoana mtoko. Wala haikupita hata miezi miwili, wakajikuta wakiwa wapenzi na kupeana ahadi mbalimbali za kuoana.
Edith hakuwepo tena kichwani mwa Dominick, mapenzi ya Christina yalionekana kumchanganya kupita kiasi hali ambayo baada ya kumaliza chuo, wakafunga ndoa na kuwa mume na mke.
************
Bado Edith alikuwa akiendelea kusoma mkoano Kagera. Kichwani mwake bado Domininick aliendelea kuwapo. Hakuona kama ingetokea siku ambayo angemsahau Dominick. Maisha yaliendelea kusonga mbele kama kawaida, akamaliza kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga na shule ya wasichana ya Tabora.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele, Edith akaanza kusahau maisha ya nyuma kwani hakuwa na matmaini yoyote kama angerudi jijini Dar es Salaam na kuonana na Dominick. Maisha yake yalikuwa ni kama yakianza upya, akaaua kujipanga upya.
Alipomaliza kidato cha sita, Edith akajiunga na chuo cha SAUT mkoani Mwanza. Huko ndipo alipokutana na mtoto wa Mbunge wa Mwanza Mjini, Tumaini Silikawa. Wakaanza urafiki ambao uliwanya kila siku kuonana na kutoka mitoko mbalimbali kama kenda ufukweni na hotelini.
Ndani ya mwezi mmoja, kila mtu akaingia katika mapenzi makubwa na mwenzake. Edith na Dominic wakatokea kupendana kupita kiasi. Kila siku walikuwa pamoja wakila raha za kila aina, mapenzi yao yalizidi kuchangamka kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Mara baada ya kumaliza chuo, wakaamua kufunga ndoa ya kifahari ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi Kanda ya ziwa.
Mara baada ya Bwana Silikawa kufariki, mtoto wake, Tumaini akshinda uchaguzi mdogo na kuwa Mbunge wa Mwanza Mjini. Maisha yao yakaonekana kubadilika, fedha kwao hakikuonekana kuwa jambo kubwa, wao kama mume na mke wakanunua nyumba mbili za kifahari, moja ilikuwa hapo Mwanza na nyingine ilikuwa Dar es Salaam.
Kutokana na kukaa Mwanza kwa uda mrefu, wakaamua kwenda kuishi katika nyumba yao iliyokuwa jijini Dar es Salaam. Tumaini hakuwasahau wananchi wake ambao walimfanya kuwa hapo, mara kwa mara alikuwa akielekea Mwanza na kuongea nao.
Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika tena, Tumaini akshinda nafasi ya ubunge tena wa Mwanza Mjini. Maisha yalionekana kubadilika hasa mara baada ya rais kuchagua na kuwa waziri wa Mambo ya Ndani. Kwake ilionekana kuwa kama bahati, aliitumikia nafasi hiyo kadri ya uwezo wake.
Alimpenda sana mke wake lakini tatizo likawa moja, kupata mtoto. Kila siku maombi yake yalikuwa ni kupata mtoto. Hawakutaka kupima, kwani hawakutaka kujua ni nani alikuwa na tatizo katika mfumo wake wa uzazi. Waliendelea kubaki kama walivyokuwa kwani mapenzi ambayo walikuwa wakipeana, yalionekana kuwatosha.
Ujauzito ambao mke wake alikuwa nao ulionekana kumchanganya kupita kiasi, kila wakati alikuwa akiliangalia tumbo la mke wake, Edith uku akionekana kutokuamini kabisa kama katika miezi michache ijayo alikuwa akienda kuitwa baba.
Alizidi kumpenda mke wake kuliko kitu chochote kile huku akiitunza mimba ile kuliko kitu chochote kile. Alihakikisha mke wake anakula vizuri kutunza afya yake na ya mtoto wake wa tumboni.. Kila siku aliyaona masaa kwenda taratibu sana kwani kila siku alitamani kumuona mtoto wake akizaliwa, akijifunza kuongea na kutamka neno ‘Baba’ mbele yake.
***************
Dominick alibaki kimya huku akiwa amechuchumaa chini, machozi ambayo yalikuwa yakimtoka yaliloawanisha mashavu yake, Ni kweli allikuwa katika mipango yake kabambe ya kulipiza kisasi lakini kwa Edith ambaye alikuwa mbele yake ilionekana ngumu kufanya hivyo.
Alikumbuka mambo mengi ambayo alikuwa amefanya na Edith toka katika kipindi cha nyuma, aliyakumbuka mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo juu ya mwanamke huyu, kingine zaidi ambacho alikikumbuka zaidi ni wema ambao alikuwa amemfanyia.
Shule nzima ilikuwa imemtenga katika kipindi kile kutokana na kuwa katika hali ngumu na uchafu ambao alikuwa nao, Edith ndiye alikuwa mtu pekee ambaye alimsaidia kwa kila kitu katika kipindi kile kigumu, iweje leo hii amuue kwa ajili ya kulipiza kisasi? Hii ingemaanisha nini katika maisha yake? Ingemaanisha kuwa ameusahau wema wote ambao alikuwa amemfanyia katika kipindi cha nyuma au alikuwa ameyasahau mapenzi makubwa ambayo alikuwa nayo shuleni?.
Kila alipokuwa akiyakumbuka mambo hayo, Dominick alibaki akiwa amechanganyikiwa. Akabaki akiwa haelwi ni kitu gani kiilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Huku akiwa na mawazo juu ya nini cha kufanya, mara simu ya Edith ikaanza kuita, Dominick akaichukua, akapeleka macho yake katika kioo cha simu, jina ‘My lovely husband’ lilikuwa likionekana vizuri machoni mwake.
Dominick akasikia hasira kupita kiasi, wivu mkali wa mapenzi ukawa umemshika moyoni. Alimchukia sana Bwana Tumaini kuliko mawaziri wote, hii ilitokana na kushiriki katika mauaji ya kuiangamiza familia yake pamoja na kumchukua mwanamke ambaye alikuwa akimpenda.
“Nitamuua mumeo. Ni lazima nimuue” Dominick alimwambia Edith huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Usimuue. Nakuomba usimuue…” Edith alimwambia Dominick.
“Nitamuacha vipi mumeo? Ameiangamiza familia yangu kwa kuichoma na moto ndani ya nyumba yangu. Amebadilisha maisha yangu, nimekuwa mtu wa kutanga tanga. Ameuumiza moyo wangu kwa kunifanya kuwa mpweke katika kipindi chote hiki. Hakuna sababu ya kufanya afurahie maisha Ni lazima nimuue tu” Dominick alimwambia Edith huku akiendelea kulia.
Kadri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo maisha yake ya nyum yalivyokuwa yakijirudia kichwani mwake kama mkanda wa filamu. Alikumbuka kila kitu, hakuona sababu yoyote ya kumuacha waziri Tumaini hai, ni lazima amuue, tena kwa mkono wake mwenyewe.
“Naomba umsamehe….naomba umsamehe Dominick” Edith alimwambia Dominick.
“Nitaanzia wapi? Hivi familia yangu itanielewa? Haiwezekani kabisa, kama alivyoiangamiza familia yangu, na yeye nitamuangamiza pia” Dominick alimwambia Edith ambaye alikuwa akilia tu.
Dominick akazunguka nyuma ya Edith na kuanza kuzifungua kamba zile ambazo alikuwa amemfunga pale mtini. Edith bado alikuwa akilia huku akiwa haamini kama Dominick yule mpole ambaye alikuwa pamoja nae shuleni ndiye yule ambaye alikuwa nae mahali pale.
Hakuamini kama mumewe alikuwa amehusika katika mauaji yoyote, uovu wa mumewe ulionekana kumsikitisha kupita kawaida. Alimwangalia Dominick mara mbili mbili, Dominick alionekana kuwa na hasira kupita kiasi, matukio mengi ya nyuma ambayo yalitokea nyuma yake yalionekana kumsikitisha.
“Nitamuua. Nitamuua baada ya kupata msaada mkubwa kutoka kwako”Dominick alimwambia Edith.
“Kupata msaada mkubwa kutoka kwangu? Siwezi Dominick kukusaidia. Siwezi” Edith alimwambia Dominick.
Dominick alimwangalia Edith mara mbili mbili, akaonekana kubadilika zaidi, hasira ambazo alikuwa nazo katika kipindi cha nyuma zikaonekana kuongezeka maradufu. Edith akaonekana kuogopa, hakuwahi kumuona Dominick akiwa katika hali ile hata siku moja.
“Nitakuua. Sitojali chochote kile” Dominick alimwambia Edith ambaye akaanza kutetemeka.
“Naomba unisamehe”
“Nitahitaji msaada wako. Msaada wako ndio utakuwa uhai wako. Kama ukienda kinyume. Nitakuua” Dominick alimwambia Edith.
Dominick akaonekana kubadilika. Tayari hasira zilionekana kumkaba rohoni. Hakuonekana kujali tena kwamba yule aliyekuwa akiongea nae alikuwa Edith au nani, kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa kipindi hicho ni kusaidiwa tu.
“Nitakusaidia” Edith alisema.
“Sio kwa maneno. Nitahitaji kwa vitendo” Dominick alimwambia Edith.
“Ingia ndani ya gari” Dominick alimwambia Edith na kisha wote kuanza kuingia garini.
Dominick hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku macho yake yakiangaia mbele. Alama za machozi ambayo yalikuwa yakimtoka katika kipindi cha nyuma zilikuwa zikionekana mashavuni mwake. Edith nae alibaki kimya, hakuongea kitu chochte kile kwani aliogopa kumkwaza Dominick.
Safari ile iliishia katika jengo bovu bovu lililokuwa katika uwanja wa Tanganyika Pakers. Giza lilikuwa limeanza kuingia mahali hapo. Hakukuwa na watu wengi mahali pale kitu ambacho wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika jengo lile.
“Mpigie simu mumeo. Mwambie aje mahali hapa, tena akiwa peke yake” Dominick alimwambia Edith.
Edith akachukua simu yake, akawaiwasha na kisha kuanza kumpigia mumewe. Simu ilianza kuita, iliita kwa muda fulani, ikapokelewa. Sauti ya Bwana Tumaini ilisikika kwa wasiwasi, aliongea kama mtu ambaye alikuwa na kigugumizi. Ila baada ya kipindi fulani, ikakaa sawa.
“Umesema uko nae hapo?”
“Ndio. Alitaka kuniua kwa kunichoma moto”
“Mungu wangu! Nakuja sasa hivi” Bwana Tumaini alisema na kisha kukata simu.
Edith alibaki akimwangalia Dominick. Machozi yakaanza kumtoka, alijua fika kwamba kitendo cha mumewe kufika mahali pale basi kingeashiria kwamba angekwenda kuuawa. Alitamani kumuomba Dominick msamaha kwa ajili ya mumewe lakini akaona kuwa ngumu kufanya hivyo.
Dominick akaa kimya. Kadri muda ulivyozidi kwenda na ndivyo ambavyo hasira zake zilivyokuwa zikizidi kuongezeka. Muda aliuona ukienda taratibu sana kuliko siku nyingine, alitamani dakika ziende haraka haraka ili Tumaini afike mahali hapo na kumuua.
***********
Bwana Tumaini alikuwa akitetemeka kwa woga, kitendo cha mke wake kutekwa na mtu mbaye alisadikiwa kuua familia za mawaziri kilionekana kuwa kitendo ambacho kilimuogopesha. Hakutaka kabisa kwenda peke yake huko ambako aliiitwa, kitu alichokitaka ni kwenda pamoja na mapolisi.
Moja kwa moja akaanza kuondoka kuelekea kituo cha polisi. Mapolisi wote wakaonekana kutetemeka mara baada ya kumuona waziri akiingia ndani ya kituo hicho. Bwana Tumaini hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya kwa muda huku akiwaangalia mapolisi ambao walikuwa katika kituo kile.
“Karibu mkuu” polisi mmoja alimkaribisha Tumaini.
“Asante. Nina tatizo na ninahitaji msaada wenu”
“Msaada gani mkuu?”
“Mke wangu ametekwa na mtu ambaye aliua familia za mawaziri wengine” Bwana Tumaini aliwaambia mapolisi ambao walionekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Ameniambia kwamba ni lazima niende Tanganyika Parkers kuonana nae. La si hivyo, atamuua mke wangu” Bwana Tumaini aliwaambia.
Mapolisi wote wakaonekana kuogopa, taarifa ambayo walikuwa wamepewa ilionekana kuwaogopesha kupita kiasi. Walikumbuka baadhi ya mauaji ambayo yalikuwa yamepita katika miezi iliyopita, muuaji hakuonekana kuwa na hurma.
Mapolisi hawakutaka kubaki mahali hapo, moja wa moja wakaingia katika gari lao aina ya Defender na moja kwa moja kuanza safari ya kuelekea katika viwanja vya Tanganyika Parkers. Kila mmoja akaanza bunduki yake vizuri, hawakutakiwa kuuliza kitu chochote mara watakapofika, ni kumkamata muuaji huyo na kumfikisha katika vyombo vya dola.
***********
Muda ulizidi kwenda zaidi na zaidi mpaka giza kuingia. Hakukuwa na mtu yeyote uwanjani pale zaidi ya wao ambao walikuwa wamelipaki gari pembeni. Dakika ziliendelea kwenda mbele, Dominick hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kumwangalia Edith ambaye muda wote alikuwa akilia.
Mwanga wa taa ukaanza kuonekana kwa mbali jambo ambalo lilimfanya Dominick kuanza kutabasamu. Sauti ya muungurumo wa gari lile ukaonekana kumshtua. Ingawa muungurumo ule ulikuwa ukisikika kwa mbali lakini alijua vizuri kama gari lile halikuwa lile ambalo alikuwa akiliitaji kufika mahali pale.
Muungurumo ulikuwa mzito, wasiwasi ukaanza kumuingia, akamshika Edith mkono na kuanza kuondoka nae mahali pale. Edith alitamani kukataa lakini kutokana na kuvutwa kwa nguvu, Edith akajikuta akisonga kule ambapo Dominick alitaka waelekee.
Wakasimama katika ukuta karibu kabisa na kutoka nje ya uwanja ule. Macho yao yalikuwa yakielekea kule ambapo gari lao lilipokuwa. Mara wakawaona watu wanne wakiteremka kutoka katika gari lile na moja kwa moja kulifuata gari alilokuja nalo Dominick na Edith.
“Amekuja na mapolisi. Vizuri sana. Sidhani kama ataweza kumuona mkewe tena” Dominick alisema maneno ambayo yalisikika vizuri masikioni mwa Edith.
Akamshika mkono Edith na kuanza kuondoka nae mahali hapo. Tayari Edith akaona kwamba ni lazima Dominick angechukua hatua kali zaidi juu yake kwa ajili ya kumkomoa Tumaini. Kwa haraka haraka akaichukua simu yake na kuanza kumpigia mume wake ambaye alikuwa pamoja na mapolisi kule uwanjani.
“Anataka kuniua…..” Edith alimwambia mumewe kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
“Naomba niongee nae” Bwana Tumaini alisema huku akihofia.
Dominick akaichukua simu ile, hata kabla hajaongea kitu, akaanza kumwangalia Edith kwa macho ya chuki. Dominick alionekana kukasirika kupita kawaida. Mapenzi yote ambayo alikuwa nayo juu ya Edith yalionekana kupotea kwa wakati huo.
“Nakuombaaa…nakuomba usimuue mke wangu…” Bwana Tumaini alisema.
“Mjanja wewe. Mjanja wewe kwa kuja na mapolisi. Sasa ninataka kukuonyeshea kwamba mimi ni mjanja zaidi yako. Ni lazima nimuue” Dominick alimwambia Bwana Tumaini.
Bwana Tumaini hakuwa na la kuongea, tayari alitambua kwamba alifanya makosa kuja na mapolisi mahali pale. Akazidi kuomba msamaha zaidi lakini Dominick hakuonekana kuelewa zaidi. Kitu ambacho alikuwa akiking’angania kwa wakati huo ni kumuua Edith tu.
“Niambie nije wapi. Sitokuja na mapolisi” Bwana Tumaini alimwambia Dominick.
“Kama umeshidwa kuja peke yako, utaweza kuja peke yako baadae?” Dominick aliuliza.
“Nitawezaaaa..nitawezaaa…”
“Mimi sio mtoto. Hautoweza. Nakwenda kumchoma moto mkeo” Dominick alimwambia Bwana Tumaini ambaye alionekana kuchanganyikiwa zaidi.
“Nakuomba…nakuo…” Bwana Tumaini alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, simu ikakatika.
Dominick akamchukua Edith na kuanza kuondoka nae. Alipofika nje ya eneo la uwanja ule, akaifuata bajaji moja, akaingia ndani pamoja na Edith na kisha dereva kuwasha bajaji na kuondoka mahali hapo.
Bajaji ilisimama karibu na ufukwe wa Msasani. Wote wakateremka na kuanza kuingia ndani ya ukumbi huo. Hawakutaka kukaa ndani ya ukumbi huo, wakapitiliza nakwenda katika sehemu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya miti.
Dominick akachukua simu ile na kisha kuiwasha. Akampigia simu Bwana Tumaini. Simu ilianza kuita, iliita kwa muda mfupi, ikapokelewa.
“Niambie nije wapi….niambie nije wapiiiii…” Bwana Tumaini alisema.
“Njoo Msasani Club huku kulipokuwa na miti. Mara ya mwisho, kama utakuja pamoja na mapolisi, nitamchoma moto mkeo kama nilivyozichoma moto familia za marafiki zako” Dominick alimwambia Bwana Tumaini.
**********
Bwana Tumaini alikuwa amechanganyikiwa, kitendo cha kumkosa mkewe pamoja na muuaji ambaye wala hakuwa akimfahamu katika kipindi hicho kilionekana kumchanganya kupita kiasi. Simu ambayo alikuwa amepigiwa hakutaka kuidharau hata mara moja, akatoka nje ya kituo cha polisi kimya kimya na kuingia garini mwake.
Safari yake ikaanza ya kuelekea katika ufukwe wa Msasani Club. Moyo wake ulikuwa na wasiwasi kwa kuona kwamba angekuta muuaji amekwishamuua mke wake, Edith. Muda wote alikuwa akisali njiani huku akimtaka Mungu Amnusuru mke wake ambaye alikuwa akimpenda kupita kiasi.
Mara baada ya kuliegesha gari lake, moja kwa moja akaanza kuingia ndani ya eneo la ukumbi ule na moja kwa moja kuteremka na kuanza kupiga hatua kuingia ndani ya ukumbi ule. Macho yake hayakutulia sehemu moja, yalikuwa yakiangalia katika kila kona mahali pale.
Akatka kabisa nje ya ukumbi ule na kuelekea katika michanga mingi pembezoni mwa bahari ya Hindi. Akayapeleka macho yake huku na kule, kwa mbali akauona mwanga wa simu. Hakutaka kujiuliza zaidi, moja kwa moja akaanza kuufuata mwanga ule wa simu huku moyo wake ukia na shauku kubwa ya kutaka kumuona mkewe ambaye alikuwa mjauzito.
Bwana Tumaini akaanza kutabasamu, hakuamini kama angemkuta mkewe mzima mahali pale. Kwa furaha kubwa aliyokuwa nayo, akamfuata na kumkumbatia. Edith alikuwa akilia kwa furaha, tukio la kumuona mumewe mahali hapo, aliona ni jinsi gani alikuwa akimthamini.
“Uliiangamiza familia yangu” Dominick alimwambia Bwana Tumaini.
“Wewe ni nani?” Bwana Tumaini aliuliza huku akijaribu kumwangalia vizuri Dominick usoni.
“Najua unanifahamu. Ulisaidiana na wenzako kuiangamiza familia yangu kwa kuichoma moto ndani ya nyumba yangu. Umeuumiza moyo wangu kupita kawaida” Dominick alimwambia Bwana Tumaini.
“Dominick…Dominick..naomba unisamehe…”
“Nitaanza vipi kukusamehe. Nitaanzia wapi. Ni lazima nikuangamize wewe pamoja na familia yako” Dominick alimwambia Bwana Tumaini na kuanza kuikoki bunduki yake na kuwanyooshea.
“Naomba unisamehe”
“Haiwezekani. Ni lazima niwaue wote” Dominick aliwaambia.
Tayari alikuwa amekwishaiokoki bunduki yake. Moyo wake ulikuwa ukimuuma kupita kawaida. Tayari mapenzi kati yake na Edith yalikuwa yamekwisha kabisa. Hakuwana kitu kingine cha kufanya zaidi ya kutaka kuiangamiza familia hiyo. Walijitahidi kuomba msamaha lakini Dominick hakuonekana kuelewa.
“Ni lazima niwaue” Dominick alisema.
Ghafla milio ya risasi ikasikika mahali hapo, damu zikaonekana kutapakaa katika michanga ufukweni hapo na ukimya kutawala kwa muda.
********
Damu zilikuwa zimetapakaa chini. Bwana Tumaini pamoja na mkewe Edith walikuwa chini huku wakirusha rusha miguu yao. Risasi zaidi ya nane zilikuwa zimeingia katika miili yao. Vifua vyao vilikuwa vimetobolewa na risasi ambazo zilipigwa kwa haraka sana.
Dominick akawasogelea na kuwaangalia vizuri, alihitaji kufahamu kama watu hao walikuwa wamekufa kama alivyokusudia au la. Wote walikuwa wamekufa pale pale hasa mara baada ya kuacha kurusha rusha miguu yao. Dominick akaachia tabasamu pana, kitendo kile cha kishujaa kilionekana kumfurahisha kupita kiasi.
Moyoni hakuhuzunika hata mara moja mara baada ya kumuua Edith. Ni kweli alimpenda sana mwanamke yule, lakini kwa kipindi kile, alijiona kuwa na uhitaji wa kufaya jambo lile ili mladi tu kutunza siri na kutokujulikana na mtu yeyote.
Mara baada ya kuwaangalia kwa muda, akaanza kuondoka mahali hapo. Alipofika nje ya ukumbi ule wa Msasani Beach, akakodi bajaji nyingine na kisha kuondoka mahali hapo kuelekea katika hoteli ya La Vista Inn ambayo alikuwa amechukua chumba.
Dominick alikaa chumbani kwa muda, kichwa chake kikaanza kuifikiria familia yake ambayo iliteketezwa kwa moto katika kipindi kirefu kilichopita. Moyo ulimuuma sana lakini wakati mwingine alibaki akitabasamu kutokana na kuanza kulipa kisasi kwa wale wote ambao walikuwa wameiteketeza familia yake.
Bado kazi ya kuwaua watu wawili ndio ilikuwa imebaki mbele yake, alitamani kazi hiyo kuifanya haraka iwezekanavyo ili apumzike na kuishi maisha ya amani. Kila siku alikuwa akielekea katika makaburi ya familia yake na kusimama pembeni kama ishara ya kuwakumbuka kwa kuacha maua kadhaa ambayo yalionyesha kuwa tukio kubwa ambalo alikuwa akilifanya maishani mwake kama kuwaenzi.
Hakujua ni wapi pa kuanzia ingawa aliona kuwa ni lazima watu hao wauawe kwa mkono wake mwenyewe. Hakutaka kuwaacha kwani kama angfanya hivyo basi angeonekana kutowatendea haki. Mikono yake aliiona ikiwa imejaa damu lakini bado hakuonekana kuridhika.
Alihitaji kuwaua wote ili kuiridhisha nafsi yake, hakutaka kumuacha yeyote yule ambaye alikuwa amehusika katika mauaji ya familia yake. Kila siku alikuwa akifikiria namna ya kulipiza kisasi hicho kwa watu hao ambao kwake aliwaona kuwa kama wanyama.
Waliuumiza moyo wake na kuuwekea majeraha ambayo hakujua kama ipo siku majeraha hayo yangekuja kupata nafuu. Alihitaji kuyaponya maumivu ya moyo wake na hata kama angeshindwa kuyaponya basi hata kuyapunguzia maumivu.
Kila siku alikuwa akiuma meno yake kwa hasira katika kipindi ambacho alikuwa akiwaona viongozi wale ambao walikuwa wameiangamiza familia yake. Aliwachukia kuliko alivyomchukia shetani ambaye hakuwa akimuona, hakukuwa na kitu chochote ambacho alikuwa akikihitaji katika kipindi hicho zaidi ya kuwaua viongozi hao wawili ambao walikuwa wamebakia.
“Ni lazima niwaue….tena kwa mikono yangu mwenyewe” Dominick alijisemea huku akivuta shuka na kulala.
*************
Nchi ya Tanzania ikashtuka kupita kiasi. Mauaji ambayo yalikuwa yametokea katika ufukwe wa Msasani yalionekana kumshtua kila mtu. Viongozi wakakosa amani, kila mmoja akajiona kuwa yuko njiani kumfuata marehemu Tumaini na mkewe.
Mauaji yalitotokea ndani ya miezi michache yalionekana kuwasisimua wattanzania. Muuaji alikuwa hajajulikana mpaka katika kipindi hicho. Maswali kadhaa yalikuwa yakimiminika vichwani mwa Watanzania juu ya polisi ambao bado walionekana kuzembea katika kila kitu.
Miili iliyochukuliwa katika ufukwe ule ikapelekwa mpaka katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi ukiendelea kufanyika kila siku. Kamanda wa polisi alionekana kuchanganyikiwa, kila siku alikuwa akiongea peke yake kana kwamba pembeni yake kulikuwa na mtu.
Matukio ya mauaji ambayo yalitokea mfululizo tena yote yakiwa yakiwahusu viongozi yalionekana kumchanganya kila mtu. Viongozi walitakiwa kuwa makini katika maisha yao ya kila siku hali iliyowafanya kuwaajili walinzi kwa ajili ya kuwalinda katika maisha yao ya kila siku.
Upelelezi ambao bado ulikuwa ukifanyika haukusaidia kitu chochote kile. Mara kwa mara mpelelezi Bugabu alikuwa akiitwa na kuulizwa juu ya mahali ambapo alifikia katika upelelezi wake. Hakuwa na chochote cha kujibu zaidi ya kuomba muda zaidi kwa kuwa kazi ambayo alikuwa akiifanya ilikuwa ngumu tofauti na jinsi ambavyo aliitarajia kabla.
Kila siku waandishi wa habari walikuwa wakielekea katika ofisi ya kamanda mkuu wa jeshi la polisi, Bwana Ngomale huku lengo lao likiwa ni kutaka kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea kuhusu muuaji ambaye bado alikuwa akiendeea kuua viongozi wa Serikali.
Bwana Ngomale hakuwa na cha kuongea zaidi ya kuwataka Watanzania wawe wavumilivu kwa kuwaambia kwamba kila kitu kilikuwa kikiendelea kama kilivyopangwa na baada ya muda fulani basi muuaji angeweza kutiwa nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kila siku Watanzania walikuwa wakiendelea kulalamika katika vyombo vya habari kwa kudai kwamba mapolisi walikuwa wameshindwa kumtia nguvuni mtu huyo ambaye bado alikuwa akiendelea kufanya mauaji kuwaua viongozi.
Magazeti ya udaku hayakuishiwa na habari, kila siku yalikuwa yakiandika habari mbalimbali kuusiana na muuaji huyo, huku hata siku nyingine wakithubutu kusema kwamba muuaji alikuwa akikaribia kujulikana, hiyo yote ilikuwa ni njia mojawapo ambayo iliyafanya magazeti yao kununuliwa kila siku.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akimfahamu muuaji ambaye alikuwa amehusika na mauaji yale ya kutisha. Kila siku tetesi zilikuwa zikiendelea kusikika mitaani lakini kiukweli hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiufahamu ukweli.
Mpelelezi Bugabu bado alikuwa akiendelea na upelelezi wake kama kawaida, kila siku alikuwa akihakikisha anaandika kitu chochote kuhusiana na mambo yote ambayo yalikuwa yakiandikwa magazetini na kuongelewa na watu mbalimbali.
Listi yake ya mauaji ambayo yalikuwa yameitikisa nchi ilikuwa katika mikono yake. Hakutaka kuyawekea maanani mauaji megine ambayo alikuwa ameyaandika katika kitabu chake. Akaanza kuangalia mauaji ya familia ya Bwana Boniface, familia ile ilikuwa imeteketezwa kwa kuchomwa na moto katika ufukwe wa Coco.
Mpelelezi Bugabu hakuishia hapo, akazidi kufuatlia mauajia mengine zaidi, kwa sasa akafikia katika mauaji ya familia ya Bwana Ombeni, nayo kama kawaida ilikuwa imeteketezwa kwa moto. Mpelelezi Bugabu akatikisa kichwa chake juu na chini kwa kuona kwamba upelelezi wake ulikuwa ukienda kufanikiwa.
Akaanza kuyafikiria mauaji ya Bwana Tumaini na familia yake. Mauaji ambayo yalikuwa yamefanyika hayakuwa ya kuchomwa moto, bali yalikuwa ni mauaji ya kupigwa risasi za viafuani na kufa. Hakutaka kuyapuuzia mauaji haya japokuwa yalikuwa tofauti na mauaji mengine.
Akafunga kitabu chake kidogo ambacho kilikuwa na matukio mengi ya mauaji. Akabaki kimya kwa muda huku akionekana kujifikiria. Kuna mauaji mengine yakamjia kichwani, haya yalitokea katika kipindi kirefu cha mwaka mmoja uliopita, haya yalikuwa mauaji ya familia ya Mwandishi Dominick ambayo iliteketezwa kwa moto ndani ya nyumba yao.
Bugabu akakohoa kidogo, akaendelea kufikiria zaidi. Alionekana kuyatilia shaka mauaji yale. Alimfahamu vilivyo Dominick kama mwandishi bora ambaye alikuwa akiandika mambo mengi tofauti tofauti ambayo yalikuwa yakifichua maovu mengi.
Familia yake pia ikateketezwa kwa moto huku baadae nae akisadikiwa kuuawa baada ya kutekwa na wauaji. Kuna vitu ambavyo alitamani sana kuvifahamu kuhusiana na mauaji haya yote ambayo yalikuwa yametokea. Kwanza alitaka kufuatilia makaburi ambayo maiti za familia zote zile zilipozikwa hata kabla hajaamua ni hatua gani ambayo ingefuata baada ya hapo.
Bugabu akaanza kuelekea katika makaburia ambayo yalizikiwa miili ya familia za viongozi. Aliyaangalia kwa muda mrefu na kisha kuondoka zake. Akaanza kuelekea katika makaburi ya familia ya Dominick, kidogo Bugabu akapigwa na mshtuko mara baada ya kuona maua yakiwa juu ya makaburi mawili, kaburi la Christina na Ibrahim.
Bugabu hakuishia hapo, aliendelea na uchunguzi wake, moja kwa moja akaelekea katika kaburi la Dominick ambalo wala halikuwa mbali kutoka pale yalipokuwa makaburi yale mawili, alipolifikia, akaanza kuliangalia, hakukuwa na ua lolote jambo ambalo likaanza kumtia mashaka.
“Kuna kitu hapa. Kazi yangu itaanzia hapa” Bugabu alisema.
************
Mawaziri wakaonekana kuogopa, matukio ya mauaji ambayo yalikuwa yametokea kwa mawaziri wenzao yalionekana kuwatisha kupita kawaida. Kila waziri akahakikisha kuandaa ulinzi wa kutosha katika maisha yake ya kila siku.
Wasiwasi ukaanza kuwatawala hasa wale mawaziri kutoka katika chama tawala cha Republic. Kila mmoja alikuwa na hofu kubwa, mauaji yalionekana kuwatisha kupita kawaida.
Mawaziri wawili, Bwana Ombeni na Boniface ndio ambao walikuwa na wasiwasi zaidi. Tayari walikuwa na uhakika kuwa Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika katika mauaji yote ambayo yalikuwa yametokea. Kila siku walikuwa wakijiuliza njia ambazo alizitumia Dominick katika kuwatoroka vijana ambao walikuwa wamewatuma.
Tayari Dominick akaonekana kuwa mtu hatari katika maisha yao, hawakutaka kuongea na waandishi wa habari kuhusu habari yoyote ya Dominick kwa kuogopa maswali zaidi. Kila Mtanzania alijua kwamba Dominick alikuwa ameuawa na watu wasiojulikana, ingekuwaje kama wangesema kwamba Dominick aikuwa hai na ndiye ambaye alikuwa amehusika katika mauaji yote?
Jambo lile la kuwaeleza waandishi wa habari likaonekana kuwa gumu kwa upande wao, kitu ambacho walitakiwa kukifanya kwa wakati huo ni kuyalinda maisha yao kwa kuwaita vijana ambao wangekuwa wakiwalinda usiku na mchana.
Waliogopa maswali kutoka kwa Watanzania juu ya Dominick kama tu wangejaribu kuwaambia kwamba mambo yale yote ambayo yalikuwa yakifanyika yalikuwa yakifanywa na Dominick. Walijuaje kama Dominick ndiye ambaye alikuwa akifanya mauaji yale? Na kwa nini alikuwa akiwauwa mawaziri tu na familia zao na si watu wengine?. Kila walipokuwa wakiyafikiria maswali yale, wakaamua kubaki kimya huku wakijihakikishia ulinzi katika maisha yao.
*************
Ukimya ulikuwa umetawala katika nyumba hii kana kwamba ndani hakukuwa na mtu yeyote yule. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akizunguka zunguka katika eneo la nyumba ile zaidi ya mlinzi ambaye alikuwa na bunduki katika mkono wake wa kulia.
Giza lilikuwa kubwa huku saa zikisoma kwamba tayari ilikuwa imetimia saa saba usiku. Milio ya mbwa kutoka katika nyumba nyingine za jirani ndio ambayo ilikuwa ikisikika kwa wingi mahali hapo. Mara mwanga wa taa ukaanza kuonekana ukimulika, kwa haraka sana mlinzi akaanza kulisogelea geti na kisha kufungua kitundu kidogo kilichokuwa getini.
Gari aina ya Range ilikuwa imesimama nje. Honi mfululizo zikaanza kusikika kutoka katika gari lile. Bwana Boniface akatoka kutoka ndani ya nyumba yake. Mwili wake ulikuwa ukitetemeka kupita kiasi. Alionekana kuwa na shauku ya kutaka kufahamu kitu kimoja mahali hapo.
Akampa mlinzi ishara ya kufungua geti lile. Mlinzi akafanya hivyo, geti likafunguliwa na gari lile kupita. Mwanaume mmoja ambaye alikuwa na mwili uliokuwa umejazia akateremka kutoka garini na moja kwa moja kumfuata Bwana Boniface na kuongea nae kwa sekunde kadhaa.
Mwanaume yule akaufuata mlango wa nyuma wa gari lile na kisha kuufungua. Mwanaume mwingine akateremka kutoka garini. Kichwa chake hakikuwa na nywele kabisa. Ndevu nyingi zilikuwa kidevuni mwake huku akiwa amevaa miwani ya jua.
Alionekana kuwa kama daktari, hii ilitokana na koti refu jeupe ambalo alikuwa amelivaa pamoja na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo. Bwana Boniface akaanza kumwangalia daktari yule kwa macho yaliyokuwa na shauku ya kutaka kufahamu kile ambacho kilikuwa kinatarajiwa kuongea kutoka kwa mtu huyo.
Mara baada ya kusalimiana, akamkaribisha ndani. Mwanaume yule ambaye alijitambulisha kama dokta Pius akaingia ndani pamoja na Bwana Boniface na yule mwanaume ambaye alionekana kuwa mlinzi wa Bwana Boniface.
“Umenishangaza sana” Bwana Boniface alimwambia dokta Pius.
“Huo ndio ukweli. Ni ukweli kabisa ambao wala hautakiwi maswali yoyote yale” Dokta Pius alimwambia.
“Kwa hiyo una uhakika kwamba mtu anayefanya mauaji haya ni Dominick?” Bwana Boniface aliuliza.
“Asilimia mia moja”
“Umejua vipi?”
“Nilisoma nae shuleni. Ninafahamu mambo mengi sana. Alikuwa akiniamini sana mpaka alipoanza kazi. Alinieleza kila kitu kuhusiana na ninyi jinsi mlivyoiteketeza familia yake” Dokta Pius alimwambia.
Bwana Boniface akashusha pumzi ndefu. Hakuonekana kuamini kama kweli kulikuwa na mtu mwingine zaidi ya Dominick ambaye alikuwa akifahamu kila kitu kilichokuwa kimetokea. Tayari aliiona siri ambayo ilikuwa maishani mwao ikiwa imeanza kuvuja.
Alimwangalia dokta Pius mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini. Akasimama na kuanza kutembea tembea mahali pale huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa. Tayari hatari ikaonekana kuanza kumnyemelea, akaanza kuwakumbuka waandishi wa habari kwa kuona kwamba ni lazima habari ile ingeenea na hivyo kuitoa katika vyombo vya habari.
“Naomba msaada wako” Bwana Boniface alimwambia dokta Pius.
“Msaada gani?”
“Yaani haujanielewa? Sitaki siri hii ifichuke. Nahitaji iendelee kuwa siri” Bwana Boniface aimwambia dokta Pius.
“Kuna kitu labda unatakiwa kukifanya”
“Kitu gani?”
“Kumuua Dominick. Hilo ndilo suruhisho la mwisho”
“Sawa. Ila nitaweza vipi kumuua? Sipajui sehemu alipojificha. Yaani sifahamu chochote kile”
“Usijali. Nitakusaidia. Anaishi hotelini kwa sasa” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface.
“Unaijua hoteli yenyewe?”
“Naifahamu. Huwa ninawasiliana nae mara kwa mara. Na sasa anataka kukua wewe na kisha kumuua Bwana Ombeni” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface.
“Mungu wangu! Yupo hoteli gani?”
“La Vista Inn pale Magomeni”
“Sawa. Inatubidi twende. Naomba unisaidie kumuua. Ninakuahidi kukupa kiasi chochote ukitakacho” Bwana Boniface alimwambia dokta Pius.
“Sawa. Kajiandae. Nitakusaidia kila hatua” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface ambaye akanyanyuka na kuanza kuelekea chumbani kwake.
Dokta Pius akabaki sebuleni pale huku akionekana kuwa na mawazo. Mara baada ya kutulia kwa sekunde kadhaa, akainuka na kisha kuanza kuelekea ndani ya chumba cha Bwana Boniface ambako alikuwa amekwenda kujiandaa. Dokta Pius alionekana kuwa mtu mwema ambaye alidhamiria kumsaidia Bwana Boniface.
***************
10
Kila siku Dominick alikuwa akiwaza jinsi ya kufanikisha pango wake wa kuwaangamiza wabaya wake ambao walimpa majeraha moyoni mwake. Hakutaka kuwaacha wakiwa hai, alijiona kukosa amani kila alipokuwa akijifikiria kuwaacha.
Kitu alichokifanya Dominick kwa wakati huo ni kuanza kutafuta urafiki na dokta Silyvester wa zahanati ya St’ Maria iliyokuwa Magomeni. Kila siku alikuwa akifika hospitalini hapo huku akionekana kubadilika kupita kawaida. Kichwa chake hakikuwa na nywele kabisa, alivaa ndevu za bandia ambazo ilikuwa ni jambo gumu sana kumgundua.
Siku ziliendelea kwanda mbele huku ukaribu wake na dokta Silyvester ukizidi kukua kila siku. Ndani ya mwezi mmoja tu, wakawa wamezoeana kana kwamba walikuwa wamefahamiana kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Dominick akawa akitumia muda mwingi sana kuonana na dokta Silyvester ambaye alikuwa akimkaribisha sana katika zahanati yake. Hakuwa na hofu kabisa na Dominick na wala hakufahamu kwamba kulikuwa na kitu ambacho Dominick alikuwa akikihitaji kutoka kwake.
Kitu ambacho alikuwa akihitaji Dominick ni mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo tu. Hakuwa na shida ya kutafuta koti la daktari kwani aliamini kama angetumia koti lolote la muuza nyama buchani basi ilikuwa ni lazima mtu yeyote afahamu kwamba alikuwa daktari wa hospitali fulani.
“Nataka unifundishe mengi kuhusu udaktari” Dominick alimwambia dokta Silyvester.
“Kama kipi Pius?”
“Kwanza hii mashine. Unajua inaonekana kuwa mashine ya kawaida sana lakini kwa mtu kama mimi inaweza kuwa tofauti na ninavyodhani” Dominick alimwambia dokta Silyvester ambaye akaanza kumulekeza Dominick kuhusiana na mashine ile.
Dominick alijifanya kuwa msikivu wa hali ya juu. Dokta Silyvester aliendelea kumuelekeza kila kitu kuhusiana na mashine ile. Dokta Silyvester hakumfundisha kuhusiana na mashine ile tu bali aliendelea kumfundisha na mambo mengine pia.
“Hivi inauzwa?” Dominick aliuliza.
“Ndio. Hasa katika maduka makubwa ambayo yanauza vifaa mbalimbali vya hospitalini” Dokta Silyvester alimwambia.
Dominick hakuona ugumu wowote ule, tayari akawa na matumaini ya kuweza kuipata mashine ile. Akaulizia kuhusu gharama ya mashine ile na kisha kutaka kufahamu maduka ambayo yalikuwa yakiuza mashine zile. Alipopata maelekezo ya kutosha, kesho yake akapaelekea kununua.
Akarudi katika chumba ambacho alikuwa amepanga na kutulia. Akaanza kuangalia mashine ile pamoja na koti, vitu vyote hivyo alikuwa amevinunua kutoka katika maduka ya vifaa vya madaktari katika duka moja kubwa lililokuwa Mwenge.
Dominick akachukua simu yake ya mkononi na kuchukua line ya simu mpya, akaingiza salio na kisha kupiga namba za Bwana Boniface. Simu ikaanza kuita, iliita kwa zaidi ya dakika moja, wala haikupokelewa. Hakukata tamaa, aliendelea kupiga zaidi na zaidi, baada ya muda, simu ikapokelewa.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo mzee. Yaani nimeshtuka sana aliponiambia” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Habari zako zimenishtua sana, naomba tuonane ili tuweze kuliongea hili” Bwana Boniface alimwambia huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Haitowezekana kuonana na mimi. Nina majukumu mengi ya kazi. Nimejaribu kukwambia ili tu ujue jinsi gani utaweza kujilinda” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Nahitaji msaada wako. Najua kutakuwa na mambo mengi unayafahamu. Naomba tuonane. Nakuomba kukuona dokta Pius” bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Kila kitu fedha. Kila kitu fedha mzee wangu”
“Nalifahamu hilo. Naomba tuonane, kuhusu fedha si tatizo kwangu. Ninachotaka ni kuonana nawe tu” Bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Sawa. Kama kuonana, nitahitaji kuonana nawe usiku, kwa mchana haitowezekana kabisa kutokana na ubize wa kazi” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Unafanya kazi katika hospitali gani?”
“Amana”
“Sawasawa. Nitamtuma mtu akufuate hapo muda wowote ule”
“Sawa. Mwambie aje saa tatu usiku. Ila atakapofika, hatakiwi kuteremka kutoka garini. Sitohitaji wafanyakazi wanione nikiongozana na mtu kuelekea katika gari lake.Nitakachokifanya nitawasiliana nae, cha msingi nitumie namba yake ya simu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Usijali. Nitakutumia sasa hivi” Bwana Boniface alisema na simu kukatika.
Dominick akabaki katika hali ya mawazo. Kwa kiasi fulani akajiona kuanza kupata mafanikio juu ya kile ambacho alikuwa amepanga kukifanya. Akajilaza kitandani huku akianza kufikiria ni kwa jinsi gani angefanikiwa kufanya kile ambacho alikusudia kukifanya.
Kwanza akainuka kutoka kitandani na moja kwa moja kuanza kuelekea katika droo ya kabati na kisha kutoa bunduki yake, akaanza kuiangalia kwa muda fulani na kisha kuirudisha na kwenda kitandani.
*********
Simu ya Dominick ambaye alikuwa katika eneo a hospitali ya Amana ikaanza kuita. Akitoa simu ile na kuanza kukiangalia kioo cha simu ile, namba ilikuwa ngeni, hivyo akaonekana kumjua mtu ambaye alikuwa akimpigia muda huo.
Alichokifanya ni kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea nje ya eneo la hospitali ile huku akiwa na koti refu jeupe pamoja na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo ambayo alikuwa ameizungushia shingoni mwake. Mara baada ya sekunde kadhaa, akafika nje ya eneo la hospitali ile.
Akaanza kuangalia huku na kule, gari aina ya Range ilikuwa imepaki pembeni kabisa. Hakuwa na wasiwasi nalo kwani alikuwa na uhakika kwamba gari ile ndilo ambalo alihitajika kuingia kwa wakati huku. Akaanza kupiga hatua za haraka haraka kulifuata.
“Karibu dokta Pius” Mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa na mwili uliojazia alimwambia Dominick huku akimfungulia mlango.
“Asante” Dominick alijibu huku akiingia ndani ya gari lile na safari ya kuelekea katika nyumba ya Bwana Boniface kuanza.
**************
Dominick akakigusa kitasa cha mlango wa chumba cha Bwana Boniface na kuufungua mlango. Bwana Boniface alikuwa akijiandaa tayari kwa ajili ya kwenda kumuua Dominick ambaye alikuwa katika hoteli ya La vista Inn. Tegemeo lake kubwa kwa wakati huo lilikuwa kwa dokta Pius ambaye alikuwa amemuacha sebuleni.
Kichwa chake kikaguswa na mdomo wa bunduki. Akaonekana kushtuka kupita kiasi, akaanza kugeuka nyuma, macho yake yakatua katika uso wa dokta Pius. Bwana Boniface akabaki akishangaa pasipo kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
Alimwangalia dokta Pius usoni, macho yake yalikuwa mekundu huku machozi yakiwa yanamlenga. Bwana Boniface hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kinaendelea mpaka dokta Pius kumnyooshea bunduki. Bwana Boniface akabaki akitetemeka tu.
“Dokta! Vipi tena?” Bwana Boniface aliuliza huku akionekana kuhofia.
“Unachokiona ndicho kinachoonekana” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Kwa nini unataka kufanya hivi?”
“Kwa sababu ya kisasi. Hiki ndicho kitu nilichokuwa nikikihitaji kwa kipindi kirefu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Sijakuelewa. Nimekuita hapa kwa sababu ya kunisaidia…lakini kwa nini unataka kunigeuka? Au Dominick amekutuma?” Bwana Boniface aliuliza.
*********
Bado Dominick alikuwa akitokwa na machozi, kila alipokuwa akimwangalia Bwana Boniface ndivyo ambavyo mambo mengi ya nyuma yalivyokuwa yakimiminika kichwani mwake. Alikumbuka vilivyo siku ambayo nyumba yake ilikuwa ikiteketezwa kwa moto na mkewe mpendwa pamoja na mtoto wake kuuawa siku hiyo.
Alijiona kuwa na sababu zote za kumuua Bwana Boniface kama kisasi cha familia yake. Hakutaka kumuacha katika usiku huo, hiyo ilionekana kuwa nafasi kubwa katika maisha yake juu ya kuendelea na zoezi lake lile. Aliendelea kumwangalia Bwana Boniface kwa macho yaliyojaa hasira.
“Ninakuua…ninakuua kwa mkono wangu mwenyewe” Dominick alimwambia Bwana Boniface ambaye muda wote alikuwa akishangaa.
“Dokta Pius….mbona unanifanyia hivi?” Bwana Boniface aliuliza.
Dominick akabaki akimwangalia kwa muda, akaitoa miwani yake na kuiweka katika mfuko wa koti lake na kisha kuzitoa zile ndevu za bandia. Bwana Boniface akabaki akimwangalia Dominick, sura yake wala haikuwa ngeni machoni mwake.
“Najua umekwishawahi kuniona kabla ya hapa” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Hapana. Hii ndio mara ya kwanza kukuona. Sikuwahi kukuona kabla ya hapa” Bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Niangalie vizuri. Hauwezi kusema kwamba haunifahamu. Nitazame vizuri” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
Bwana Boniface akabaki akimwangalia Dominick. Ni kweli sura yake haikuwa ngeni machoni mwake lakini kila alipojaribu kukumbuka mahali ambapo alikuwa amekwishawahi kuiona sura ile, alikosa jibu.
“Wewe ni nani?” Bwana Bonifac aliuliza.
“Muuaji nisiyekuwa na huruma. Mimi ni mwandishi ambaye nimerudi tena kutoka kaburini” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Dominick! Mungu wangu! Dominick!”
“Ndio mimi. Nimekuwa nikiisubiri nafasi hii kwa muda mrefu sana. Nimekuwa nikiangaika maishani mwangu. Nilikuwa na furaha katika kipindi chote, mkataka kunipa huzuzni maishani mwangu, nawapongeza kwa kuwa mlifanikiwa kwa asilimia mia moja” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Dominick. Dominick……” Bwana Boniface alijikuta akiita jina la Dominick pasipo kuongea kitu chochote kile.
Alimwangalia Dominick mara mbili mbili, hakuamini kama Dominick angeweza kutumia njia ile kuingia ndani ya nyumba yake. Alitamani kuleta ubishi ili apate kujiokoa kutoka katika mikono ya Dominick lakini kila alipokuwa akiuangalia mdomo wa bunduki ile akabaki akiogopa kufanya hivyo.
Dominick akaanza upiga hatua mpaka kitandani ambako akauchukua mto wa kulalia na kuuweka mbele ya mdomo wa bunduki ile huku lengo lake kubwa likiwa ni kuuzia mlio wa risasi ile usisikike kwa sauti kubwa.
“Wote mtaelekea kule mlipoipeleka familia yangu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
Wala hazikupita hata sekunde kumi, milio kadhaa ya risasi ikasikika kwa mbali kabisa. Dmu zilikuwa zikimtoka Bwana Boniface. Akabaki chini huku akirusha miguu yake huku na kule. Kifua chake kilikuwa kimetobolewa na risasi kadhaa.
Dominick akaiangalia ile maisti ya Bwana Boniface. Hakuonekana kuridhika kabisa, akaifuata ale chini na kuanza kuiongezea risasi kadhaa. Kila alipokuwa akiiangalia maiti ile na ndivyo ambavyo hasira zilivyozidi kumpanda.
Mara baada ya kuridhika, akairudisha miwani yake pamoja na ndevu zake za bandia na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea nje ya chumba kile. Akayafuta macho yake ambayo yalikuwa yakitokwa na machozi na kujiweka katika hali ya kawaida, alipomaliza, akatoka nje ya nyumba ile na kuingia garini.
“Tayari dokta?” Mwanaume yule aliyekuwa na mwili wa kujazia alimuuliza Dominick.
“Tayari. Nirudishe hospitalini” Dominick alimwambia mwanaume yule na kisha kuanza kumudisha hospitalini ambako baada ya kufika Amana akateremka na kumzuga dereva kwamba alikuwa akielekea katika hospitali ile.
Alipoona gari lile limeondoka mahali pale, moja kwa moja akaanza kulifuata garil lake na kisha kuanza kuelekea katika hoteli ya La Vista Inn.
********
Hali ya hewa ikachafuka zaidi, viongozi wa Serikali wakachanganyikiwa zaidi, mauaji ambayo yalikuwa yametokea katika usiku uliopita yakaonekana kuwachanganya. Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama Bwana Boniface angeweza kuuawa ndani ya nyumba yake iliyokuwa na ulinzi wa kutosha.
Kitu walichokifanya mapolisi ni kumuita mwanaume yule ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kumuendesha Bwana Boniface katika gari lake la kifahari aina ya Range. Moja kwa moja mwanaume yule akaingizwa katika chumba zcha mahojiano.
“Unaitwa nani?” Polisi aliuliza.
“Bakari Omari” Mwanaume yule alijibu.
“Ulikuwa wapi katika kipindi ambacho Bwana Boniface alikuwa akiuawa?” Polisi aliuliza.
“Kama ni yule dokta ndiye aliyefanya mauaji hayo, basi naweza kusema kwamba nilikuwa nje ya nyumba yake ila kama si yeye basi sikuwapo katika eneo la nyumba yake” Bakari alijibu.
“Ninahitaji kufahamu mengi kuhusiana na huyo dokta” Polisi alimwambia Bakari.
“Mzee alinipigia simu nyumbani na kunieleza kwamba kuna daktari ambaye nilitakiwa kwenda kumchukua katika hospitali ya Amana ifikapo usiku. Nilichokifanya kwa wakati huo ni kwenda katika hospitali hiyo na kumchukua na kisha kuanza kwenda nae nyumbani kwa marehemu” Bakari alielezea na kukaa kimya.
“Anaitwa nani?”
“Dokta Pius”
“Sawa. Endelea”
“Kwa jinsi nilivyokuwa nikiwaangalia wote kwa pamoja, niliweza kugundua kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba walikuwa wakifahamiana, naweza kusema hivi kwa kuwa muda mwingi walikuwa wakionyesheana tabasamu katika nyuso zao. Mara baada ya muda fulani, wakaingia ndani” Bakari alisema.
“Inamaanisha ulibaki nje?”
“Ndio”
“Kwa nini?”
“Mzee hakutaka niingie kitu ambacho nilijua kwamba walikuwa na kitu cha siri walitaka kuongelea ambacho sikutakiwa kukifahamu” Bakari alielezea.
“Sawa. Endelea”
“Ilichukua muda kama wa dakika ishirini, dokta Pius akatoka ndani ya nyumba ile na kisha moja kwa moja kuingia garini. Alinitaka niondoke mahali hapo na kumrudisha kazini kwake, katika hospitali ya Amana. Nilipomfikisha huko, nikaondoka zangu” Bakari alielezea.
Maelezo yote ambayo alikuwa ameyatoa yalikuwa yameandikwa katika faili maalumu na kisha kuruhusiwa. Walichokifanya mapolisi kwa wakati huo ni kuondoka kituoni hapo na moja kwa moja kuelekea katika hospitali ya Amana.Kitu ambacho walikuwa wakitaka kukifahamu katika wakati huo ni juu ya uwepo wa dokta Pius ambaye hadi muda huo ndiye alikuwa akionekana kuwa muuaji. Mara baada ya dakika kadhaa, wakafika katika hospitali ile na moja kwa moja kuelekea ndani ya jengo lile.
Kitu ambacho walikuwa wakikitaka katika muda huo ni kuonana na dokta mkuu ambaye angewapa maelekezo kuhusiana na dokta Pius ambaye kila mmoja alikuwa na wasiwasi nae. Mara baada ya kuelekezwa mahali ilipokuwa ofisi ya dokta mkuu, wakaanza kuelekea huko.
“Inashangaza sana” Dokta mkuu, Bwana Samuel aliwaaambia mara baada ya kuongea kwa muda.
“Kwa nini?”
“Katika hospitali hii wala hakuna dokta mwenye jina hilo” Dokta Samuel aliwaambia huku akitoa faili ambalo lilikuwa na majina ya wafanyakazi wote wa hospitali ile na kuwagawia.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Ni kweli kutokana na maelezo ya Bakari, dokta Pius alitoka ndani ya jengo lile la hospitali na kisha kuelekea katika gari lile ambalo alikuja kumpokea, sasa kwa nini dokta yue hakuwa na mmoja wa wafanyakazi katika hospitali ile?
Kila walipokuwa wakifikiria, hawakupata jibu, hai ilionekana kuwashangaza kupita kawaida, hawakuelewa ni kitu gani ambacho kilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Kitu walichokifanya ni kuondoka katika hospitali ile na kuelekea ofisini huku wote wakionekana kukasirika kupita kawaida.
Bado hali haikutulia mitaani, magazeti ambayo yalikuwa yameandika taarifa ya kifo cha Bwana Boniface yalikuwa yakinunuliwa kuliko magazeti yote. Kila mtu kwa wakati huo alitaka kufahamu sababu halisi ambazo zilimfanya Bwana Boniface kuuawa.
Wananchi hawakuelewa juu ya matukio yale ya mauaji kutokea. Kila mtu mitaani alikuwa akisema lake, wengine walidiriki hata kusema kwamba vyama pinzani ndio ambavyo vilikuwa vikifanya mauaji yae.
Matukio haya yaliyofuatana yakatengeza historia kubwa nchini Tanzania ya kuwapoteza viongozi wawili ndani ya miezi kumi na moja tena huku wote wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi. Hakukuwa na amani tena katika maisha ya viongozi, wasiwasi mkubwa ukawa umeongezeka katika maisha yao.
Hawakutakiwa kumuamini mtu yeyote katika maisha yao ya kila siku. Walitakiwa kuishi maisha ya peke yao na familia zao. Mauaji yale yalionekana kuendelea kama mfululizo wa filamu za tamthilia.
Upelelezi bado ulikuwa ukiendelea kufanyika lakini hakuna kitu ambacho kilipatikana, muuaji hakupatikana japokuwa kila mtu alijua kwamba muuaji huyo alikuwa akiishi miongoni mwao.
*******
Bwana Tumaini alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika na mauaji yote ambayo yalikuwa yametokea. Hakutaka kujiuliza kitu chochote kile, jambo ambalo aikuwa amedhamiria ni kuwaeleza mapolisi kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika katika kila kitu.
11
Hakujali maswali ambayo angeulizwa baada ya kutoa maelezo yale, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kuwaeleza mapolisi tu kwani aliona kwamba ilikuwa bora kufanya hivyo kuliko zamu yake ya kuuawa itakapofika.
Alidhamiria kweli kwenda kuwaeleza mapolisi ukweli wote kwamba kila mauaji ambayo yalikuwa yakitokea yalikuwa kama kisasi kutoka kwa Dominick ambaye waliiteketeza familia yake. Muda wote alikuwa na presha, alitaka mazishi ya Bwana Boniface yamalizike haraka haraka ili aelekee katika kituo cha polisi na kueleza kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
Siku zikaanza kukatika huku mazishi yakiwa yamelizika. Bwana Ombeni akajipanga vilivyo kwenda kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea toka siku ile ambayo walikuwa wamewatuma vijana wao kwenda kuiteketeza familia ya Dominick.
Hakutaka kuuawa kama wengine walivyouawa, alitaka kuinusuru roho yake haraka iwezekanavyo. Moja kwa moja akatoka kutoka ndani ya chumba chake na kuingia garini huku lengo lake likiwa ni kuelekea katika kituo cha polisi cha Oysterbay kwa ajili ya kuelezea kila kitu.
Garini, akili yake wala haikutulia, muda wote alikuwa akimfikiria Dominick. Alitamani kufika katika kituo cha polisi haraka iwezekanavyo na kuelezea kile ambacho kilikuwa kikimsumbua moyoni mwake. Safari iliendelea kama kawaida mpaka akaanza kuingia katika eneo la kituo cha polisi cha Oysterbay. Kwa haraka haraka akateremka na kuanza kuelekea ndani ya kituo kile.
“Karibu mzee” Poisi ambaye alikuwa kaunta alimkaribisha.
“Asante” Bwana Ombeni aliitikia.
Mapolisi wote ambao walikuwa nje wakaingia ndani kwa ajili kumsikiliza Bwana Ombeni ambaye alikuwa ameingia ndani ya kito kile. Kila mmoja akajua kwamba Bwana Ombeni alikuwa na kitu kizito moyoni ambacho alikuwa akitaka kuielezea polisi.
*************
Bwana Ombeni alionekana kuchanganyikiwa. Tayari alikuwa katia kituo cha polisi kwa wakati huo. Hakuwa na nguvu za kuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku akiwaangalia mapolisi tu. Alikuja hapo akiwa na nguvu kabisa za kuwaeleza mapolisi kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake pamoja na njama zote ambazo alikuwa amezifanya katika kuiteketeza familia ya Dominick na kutaka kumuua Dominick mwenyewe.
Kwa wakati huo alikuwa akijutia uamuzi ambao alikuwa ameuchukua, alijuta kwa kushirikiana na wenzake katika kutekeleza kile kitu ambacho kwa wakati huo alikiona kuanza kukilipia. Hakutaka tena kujificha, alitamani aendelee kuishi kuliko kuendelea kuficha kitu kile ambacho alikiona ni lazima akilipie kwa yeye mwenyewe kuuawa.
“Nimekuja……” Bwana Ombeni aliwaambia mapolisi ambao walikuwa kimya wakimwangalia.
“Ndio mzee. Tumekuja hapa kukusikiliza” Mkuu wa kituo hicho, Hussein alimwambia.
“Nimekuja kueleza ukweli. Kila kitu na njama zote ambazo nilizifanya katika maisha yangu kushirikiana na wenzangu” Bwana Ombeni aliwaambia.
“Ndio mzee tunakusikiliza”
“Nimefanya mambo mabaya sana kwa kushirikiana na wenzangu. Sisi ndio tuliiangamiza familia yake” Bwana Ombeni aliwaambia na kunyamaza kwa muda.
“Mliiangamiza familia yake? Nani?”
Bwana Ombeni akabaki kimya kwa muda, akaanza kujifikiria kama ingekuwa vizuri kumtaja Dominick mahali pale. Alijua fika kwamba angewekwa chini ya ulinzi hapo hapo kabla ya mambo mengine kufuata.
“Nani mheshimiwa?” Hussein aliuliza.
“Familia ya……” Bwana Ombeni alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, simu yake ya mkononi ikaanza kuita.
Kwa haraka haraka akaichukua kutoka katika mfuko wake wa suruali na kisha kuangalia kioo cha simu, namba ambayo ilikuwa ikiingia katika muda huo ilikuwa ngeni simuni mwake. Kwa haraka haraka akaipeleka sikioni.
“Halloooo….” Bwana Ombeni aliita.
“Hallooo…!” Sauti ya upande wa pili iliitikia.
“Naongea na nani?” Bwana Ombeni aliuliza.
“Mwandishi wa habari wa gazeti la Mambo leo”
“Sawa. Nikusaidie nini?”
“Tumezipata taarifa zote kuhusu wewe na wenzako ambao mlifanya mauaji kwa kuiangamiza familia ya mwandishi mwenzetu, Dominick. Kila kitu tumeambiwa na ushahidi umekamilika. Hapa ninapoongea na wewe nipo ofisini mwangu nikiandaa gazeti kwa ajili ya kuitoa taarifa hiyo gazetini kesho” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
Bwana Ombeni akaonekana kushtuka kupita kiasi. Akaonekana kuanza kutetemeka huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Hakuamini kama mambo yale ambayo walikuwa wameyafanya na kuwa kama siri tayari yalikuwa yameanza kutapakaa.
Alijua kwamba kama taarifa ingetolewa gazetini basi ingekuwa hatari zaidi. Wananchi wote wangeshtuka na kuitaka serikali kumchukulia hatua kali kwa kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela au kunyongwa.
Kwa haraka haraka akatoka pale kaunta alipokuwa na moja kwa moja kuelekea garini mwake huku akionekana kutetemeka. Mapolisi wote wakabaki wakishangaa, hawakuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kikiendelea kwa mzee huyo kwa wakati huo.
“Umesemaje?” Bwana Ombeni aliuliza mara baada ya kuingia garini.
“Ndio hivyo mzee. Nilifanya uchunguzi wa muda mrefu. Nimeweza kugundua hayo, na sasa ndio ninaandaa gazeti. Kesho, kila Mtanzania ataweza kugundua uovu wako ulioufanya” Mwandishi yule ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake kiusalama alimwambia.
“Nimekusikia. Naomba unielewe kitu kimoja. Nikweli nimefanya uovu huo ila kwa sasa ninahitaji sana kitu hiki kutokujulikana. Nakuomba, nakuomba sana kama itawezekana tukutane na kuweza kuinunua habari hiyo kwa kiasi chochote cha fedha” Bwana Ombeni alimwambia mwandishi.
“Hauwezi kuinunua habari hii. Hivi unajua kuwa kama nikiiweka habari hii gazetini nitaweza kupata zaidi ya milioni ishirini? Hii ni habari yenye fedha sana” Mwandishi wa habari alimwambia Bwana Ombeni.
“Nakuomba sana. Nitainunua hata kwa milioni hamsini” Bwana Ombeni alimwambia.
“Haitowezekana kabisa. Ni lazima niiuze kama hautoongeza kiasi kikubwa zaidi” Mwandishi alimwambia.
“Nimekuelewa. Nitakupa milioni mia moja. Najua ni fedha nyingi sana, ila ninachokitaka ni kwamba kitu hicho kiwe siri kati yangu na wewe tu. Nakuomba unisaidie, nina milioni mia moja mwandishi” Bwana Ombeni alimwambia mwandishi huyo.
“Sawa. Njoo na fedha hizo hapa Caspian Hotel. Chumba namba 18. Kuwa mwangalifu asikugundue mtu yeyote yule” Mwandishi yule alimwambia.
“Usijali. Ninakuja na fedha hizo”
“Kama ukichelewa. Hautonikuta”
“Usijali, nitafanya haraka iwezekanavyo” Bwana Ombeni alisema na kisha simu kukatwa.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo tena, moja kwa moja akaliwasha gari lake na safari ya kuelekea benki kuanza. Alihitaji kufanya kila kitu kuhakikisha jambo lile linakuwa siri ambayo hatoweza kuitambua mtu yeyote yule.
Mara baada ya kufika benki, moja kwa moja akaelezea shida yake na kisha kupelekwa katika chumba maalumu ambako huko akakabidhiwa kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikihitaji kwa muda huo na safari ya kuelekea katika hoteli ya Caspian kuanza.
Garini, kichwa chake hakikutulia kabisa. Muda wote alikuwa akimfikiria mwandishi yule wa habari pamoja na habari ambayo alikuwa nayo juu yake. Ni kweli hakutaka Mtanzania yeyote afahamu juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake.
Hakujali kama alikuwa akilipa kiasi kikubwa cha fedha kwa wakati huo kwa ajili ya kuinunua habari ili, ila kitu ambacho alikuwa akikijali ni kuifanya habari ile kuendelea kuwa siri tu. Hakutaka kupata aibu yoyote ile na hiyo ndio maana alihakikisha kufanya kila kitu kuwa siri.
Mara baada ya kufika katika eneo la hoteli ya Caspian, moja kwa moja akateremka na kisha kuanza kuelekea sehemu ya mapokezi. Alipofika, akaelekezwa kwenda katika chumba ambacho alitakiwa kwenda na kuanza kwenda kule.
Mara baada ya kukifikia, akaanza kupiga hodi na kukaribishwa. Mwandishi alikuwa bafuni, hivyo moja kwa moja akatulia kitandani huku brifukesi yake akiiweka pembeni. Bwana Ombeni alibaki kuwa na mawazo mahali pale, alitaka mwandishi yule atoke bafuni na kumkabidhi habari ile haraka iwezekanavyo na yeye kuondoka mahali pale.
Mlango wa bafuni ukafunguliwa na mwandishi kutoka. Bwana Ombeni akaanza kumwangali mwandishi yule kuona kama alikuwa akimfahamu. Hakuweza kuuona vizuri uso wake kutokana na mwandishi yule kutumia taulo kuufuta uso wake.
“Mungu wangu! Dominick!” Bwana Ombeni aliita kwa mshtuko mara baada ya kuona uso wa mwandishi yule.
“Umeshtuka sana?” Dominick alimuuliza Bwana Ombeni huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Usishtuke. Wewe ni rafiki yangu mkubwa sana. Mara zote nilikuwa nikiandika habari zako gazetini. Au umesahau?” Dominick alimuuliza.
Bwana Ombeni hakujibu kitu chochote kile, alibaki akimwangalia Dominick kwa macho yaliyojaa mshtuko. Hakuamini kama yule mtu ambaye alikuwa akimwangalia mbele yake kwa wakati huo alikuwa Dominick, mwandishi ambaye walikuwa wameiangamiza familia yake.
“Nataka tuongee tu leo. Wewe ni rafiki yangu mkubwa. Au umesahau hilo?” Dominick aliuliza.
“Sijasahau” Bwana Ombeni alijibu huku akitetemeka, tayari kijasho kikaanza kumtoka.
“Kila siku nilikuwa nakufagilia katika magazeti na kukufanya kujulikana zaidi nchini hapa. Unakumbuka hilo?” Dominick aliuliza.
“Nakumbuka” Bwana Ombeni alijibu.
“Wewe ni rafiki yangu Ombeni, wala hautakiwi kuogopa lolote. Umekumbuka kuja na fedha zangu?” Dominick alimuuliza.
Bwana Ombeni akaanza kuliangalia brifukesi lake ambalo alikuja nalo mahali pale na kisha kulichukua na kumkabidhi Dominick ambaye tayari alikuwa ameufunga mlango kwa ufunguo. Dominick akaifungua brifukesi ile na kisha kuanza kuziangalia fedha zile, akatabasamu.
“Lakini kumbuka kwamba ulinisaliti. Yaani upendo wote ule niliokuonyeshea, malipo yake yakawa ni usaliti. Unakumbuka kama ulinisaliti?” Dominick aliuliza huku tabasamu pana likionekana usoni mwake. Bwana Ombeni hakujibu kitu chochote kile, alibaki kimya huku akimwangalia Dominick.
“Swali gumu hilo, inaelekea haukumbuki kitu chochote kile” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
“Nakumbuka” Bwana Ombeni alimwambia Dominick.
“Safi sana. Unakumbuka kwamba ulinisababishia kidonda kikubwa maishani mwangu?” Dominick aliuliza, tayari uso wake ukabadilika, tabasamu lote ambalo lilikuwa likionekana kabla likapotea.
12
Bwana Ombeni hakujibu chochote kile, alibaki akimwangalia Dominick usoni. Dominick akaifuata droo yaa kitanda na kutoa bastora yake ndogo na kisha kuanza kuiangalia. Bwana Ombeni akazidi kutetemeka zaidi.
“Unakumbuka?” Dominick aliuliza kwa sauti ya taratibu. Bwana Ombeni hakujibu chochote kile.
“Unakumbuka?” Dominick aliuliza kwa sauti iliyojaa ukali huku akimgusisha bunduki ile kichwani.
“Nakumbuka” Bwana Ombeni alijibu.
“Safi sana. Ulimuua mtoto wangu na mke wangu. Najua hao sitoweza kuwapata tena. Uliiteketeza nyumba yangu kwa moto, na fedha hizi ambazo umeniletea ndizo ambazo nitazitumia kununulia nyumba nyingine. Chagua nikufanye nini siku ya leo?” Dominick alimuuliza Bwana Ombeni.
“Naomba unisamehe”
“Ningekusamehe kama tu usingeiangamiza familia yangu” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
“Naomba unisamehe”
“Nitakupiga risasi nne za miguuni ili usitembee tena, nitakutoboa macho yako ili usione tena na kuukata ulimi wako ili usiongee tena. Utakapoulizwa chochoe juu yangu, hautoweza kujibu wala kuona. Na pia nitavikata vidole vyako ili usiweze kuandika chochote. Nitakufanya uishi katika maisha ya mateso kipindi chote cha maisha yako” Dominick alimwambia Bwana Ombeni na kuendelea.
“Ila nitafanya hivyo kama hautotaka nikuue” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
“Ni adhabu kali Dominick….naomba unisamehe” Bwana Ombeni alimwambia Dominick.
Dominick akachukua mto kutoka katika kitanda kile na kisha kuuweka mbele ya bunduki yake. Bwana Ombeni akabaki akiendelea kuomba msamaha huku akilia kama mtoto mdogo.
“Nililia hata zaidi ya unavyolia sasa, nikaumia sana” Dominic alimwambia Bwana Ombeni na kisha kubonyeza kitufe cha kuruhusu risasi.
Risasi tano zikatoka, mwili wa Bwana Ombeni ukatobolewa kwa risasi, damu zikatapaa kitandani pale alipokuwa amekaa. Akaangukia kitandani, miguu na mikono yake wala haikutulia, aliendelee kuirusha huku na kule, baada ya sekunde chache, akatulia.
Dominick hakutaa kuendele kubaki ndani ya cumba kile, alichokifanyani kuvaaa nguo zake pamoja na ndevu zake za bandia, akachukua brifukesi ile na kisha kuondoka chumbani mule.
Safari yake ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa rafiki yake Edmund na kumuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimeendelea baada ya kuondoka nyumbani kwake mwaka mmoja uliopita kwa ajili ya kutekeleza kile ambacho alikuwa amekipanga kukitekeleza.
“Nimefanikiwa. Najiona kuwa amani kwa sasa” Dominick alimwambia Edmund.
“Safi sana. Vipi kuhusu brifukesi hiyo?”
“Kuna kiasi cha shilingi milioni mia moja” Dominick alimwambia.
“Umezitoa wapi tena”
“Aliniletea yeye mwenyewe. Sikiliza Edmund, nitahitaji kuondoka kueleke nchini Congo” Dominick alimwambia Edmund.
“Congo! Kufanya nini tena?”
“Usijali. Nitataka kuonekana kama nilitekwa na kupelekwa nchini Congo. Nitarudi huku na kujifanya nimerudi nyumbani. Unauonaje mpango huo?” Dominick aliuliza.
“Uko safi. Utasema ulikuwa wapi uko Congo?”
“Katika msitu wa Bwambiro kwamba nilikaa mateka chini ya waasi. Kila kitu kitakuwa safi, ila ninachokihitaji ni msaada wako. Sitoweza kwenda Congo kwa ndege, nitata nisafiri kwa basi mpaka Kigoma ambako nitaonganisha mpaka Congo kwa kutumia meli pale ziwani Tanganyika” Dominick alimwambia.
“Sawa. Nitakwenda kukata tiketi kesho” Edmund alimwambia Dominick.
Kama jisi ilivyopanga ndivyo ilivyofanyika, moja kwa moja siku iliyofuata Dominick akaingia katika basi la Shibobo na kisha safari ya kuelekea mkoani Kigoma kuanza. Safari ilichukua siku moja na nusu na ndipo gari likaanza kuingia katika kitu cha mabasi cha Mwandiga ambako akateremka na kuanza kuelekea katika hoteli ya Mamboleo iliyokuwa katika mtaa wa Mwanga. Siku iliyofuata, akapanda meli ambayo ilikuwa ikielekea nchini Congo.
*************
Taarifa hii ilikuwa ni zaidi ya mshtuko mkubwa nchini Tanzania. Kila mtu ambaye alikuwa ameisikia alionekana kuogopa, amani ikaonekana kupotea muda wowote ule. Watu wakaanza kuhuzunika kupita kawaida, Waziri wao ambaye walikuwa wakimpenda hakuwa nao tena, alikuwa ameuawa ndani ya hoteli ya Caspian.
Mapolisi walikuwa wamekusanyika nje ya hoteli ile huku wengne wakiwa wameelekea katika chumba kile ambacho kilikuwa kimetokea mauaji. Bwana Ombeni alikuwa chini huku damu zikiwa zimetapakaa chumbani mule.
Wapelelezi wengine kutoka katika kitengo cha polisi walikuwa wakipiga picha za tukio lile kwa ajili ya kwenda kuzihifadhi katika ofisi zao. Kila mtu ambaye alikuwa akiiangalia maiti ile, alibaki akihuzunika.
Siku iliyofuata, asilimia tisini ya magazeti yalikuwa yameandika taarifa ile ambayo ilikuwa imeshika sana hisia za watu nchini. Kila mtu alitaka kuisoma habari ile kwa undani zaidi na kutaka kujua chanzo cha mauaji yale.
Mpaka inafika saa saba mchana, hakukuwa na gazeti lolote mtaani ambalo lilikuwa na habari ile, magazeti yote yalikuwa yamenunuliwa. Hiyo ndio ilikuwa habari ambayo ilishika sana katika masikio ya kila mtu ambaye aliisoma na kuisikia.
“Mapolisi walisema amepigwa risasi ngapi?” Jamaa mmoja aliwauliza wenzake
“Tano. Ila si unajua mapolisi wetu wanavyoficha, unaweza kukuta kapigwa hata risasi hamsini” Jamaa mwingine alijibu.
*******
Edmund alikuwa akionyesha uso uliojaa mshtuko, wafanyakazi wote ambao walikuwa ofisini pale walionekana kumshangaa, hawakujua sababu ambayo ilimfanya Edmund kuwa katika hali ile. Wafanyakazi wengine wakaanza kuendelea na kazi zao kama kawaida ila wengine wakaanza kumsogele karibu.
“Dominick…!” Edmund alisema kwa mshtuko.
Wafanyakazi wote wakashtuka, jina lile bado lilikuwa katika kumbukumbu zao. Wote wakajikuta wakianza kumsogelea, tayari wakaona kuna kitu ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo. Edmund alikuwa ameishika simu yake, kila mfanyakazi alitamani aiachie simu ile na kuwaelezea kitu ambacho kilikuwa kinaendelea juu ya jina lile ambalo alikuwa amelitaja.
“Kuna nini?” Mfanyakzi mmoja aliwauliza wenzake.
“Subiri kwanza”
Mara baada ya muda wa sekunde kadhaa, Edmund akaitoa simu yake sikioni na kuanza kuwaangalia wafanyakazi ambao walikuwa wamemzunguka katika meza ile. Kwa mbali tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake.
“Kuna nini?” Mfanyakazi mmoja alimuuliza.
“Dominick….Dominick yupo hai….!” Edmund aliwaambia wafanyakazi wenzake.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, hawakuyaamini maneno yale ambayo Edmund alikuwa ameyaongea, kila mmoja akaonyesha mshtuko wa wazi. Ilionekana kuwa ngumu sana kwa Dominick kuwa hai katika kipindi hicho na wakati Tanzania nzima ilikuwa inajua kwamba aliuawa na tayari alikuwa amezikwa.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo. Amesema anakuja, yuko njiani kutoka mkoani Kigoma” Edmund aliwaambia.
Siku iliyofuata, wafanyakazi hawakutaka kuwepo maofisini mwao, wote walikuwa katika kituo cha mabasi cha Ubungo kwa ajili ya kumpokea Dominick ambaye hawakuwa wamemuona kwa muda wa mwaka mzima.
Mara baada ya basi la Zainabu kupaki sehemu husika, Dominick akaanza kuteremka. Kila mmoja alionekana kutokuamini, mwili wake ulikuwa umepungua sana kuonyesha kwamba alikuwa katika kipindi kikubwa cha matatizo.
Ilionekana kuwa shangwe kwa kila mfanyakazi ambaye alikusanyika kituoni hapo. Moja kwa moja baada ya kumkumbatia, wakaanza kuelekea katika gari la kampuni ambal walikuwa wamekuja nalo na kisha kuanza kuelekea ofisini.
“Tuambie nini kilitokea?” Bosi wa kampuni hiyo alimuuliza Dominick mbele ya wafanyakazi wake.
“Ni habari ndefu sana. Kuna siku nilipigiwa simu niende kuchukua habari pale Africa Hotel. Nilipofika pale, nilitekwa na kupelekwa mkoani Kigoma ambako huko safari ilionganishwa mpaka nchini Congo katika msitu mmoja ambao ulikuwa ukitisha sana” Dominick aliwaambia.
“Mungu wangu! Ni watu gani hao ambao walikuwa wamekuvamia?” Bosi aliuliza.
“Siwafahamu, walikuwa wamevalia kofia kubwa za kihuni. Nilipata mateso sana nchini Congo, kwa kifupi ni kwamba walitaka kuniua kwa kifo kilichojaa maumivu makali” Dominick alisema.
“Pole sana. Ilikuwaje sasa mpaka wakakuachia?”
“Hawakuniachia, nilitoroka mara baada ya majeshi ya serikali kuvamia kambi ile ya waasi. Mateka wenzangu wengi waliuawa kwa kupigwa risasi ila mimi walikuwa wakiniacha kwa kusema kwamba mtu ambaye alikuwa amewapa maagizo alitaka kuniua kwa mkono wake mwenyewe” Dominick aliwaambia.
“Mtu gani huyo?”
“Mpaka naondoka, sijamjua ni mtu gani” Dominick alijibu.
“Karibu sana nyumbani”
“Asanteni sana. Vipi kuhusu upelelezi wa mauaji ya familia yangu?” Dominick aliuliza huku akionekana kutojua chochote kile. Wafanyakazi wote wakaanza kuangaliana.
“Bado hatujajua. Yaani kuna matukio kadhaa ya mauaji yalitokea, nafikiri mapolisi walikuwa bize wakiyashughulikia”
“Mauaji? Mauaji gani?”
Kila kitu ambacho kilielezewa mahali hapo kilionekana kuwa kama kipya kwa Dominick, muda wote alikuwa akitingisha kichwa chake kushoto kulia hali iliyoonyesha kuhuzunika. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu juu ya kila kilichoendelea zaidi ya Edmund ambaye nae alikuwa akijifanya kutokuelewa kitu chochote kile.
Siku iliyofuata, magazeti yalikuwa yakiandika taarifa juu ya ujio wa Dominick, taarifa ile ilionekana kuwa kama muujiza ambao ulikuwa umemtokea Dominick. Wananchi wakawa na furaha kwa kuwa mwandishi ambaye alikuwa akionekana kuwa shujaa alikuwa amerudi tena kazini baada ya kipindi cha mwaka mzima kupita.
Wiki nzima, sura ya Dominick ndiyo ambayo ilikuwa ikionekana katika magazeti mbalimbali. Magazeti hayo yote yalikuwa yakinunulika sana mitaani, ujio wa Dominick ukaonekana kuwa kitu kikubwa ambacho kila siku alitakiwa kumshukuru Mungu kwa kumuokoa kutoka katika mikono ya waasi.
“Kuna mwanaume anataka kukuona” Msichana mmoja alimwambia Dominick.
“Mwanaume gani?”
“Simfahamu, ila amesema ametoka kituoni” Mwanamke yule alimwambia Dominick.
Dominick akaonekana kushtuka, hakujua ni mwanaume gani huyo ambaye alikuwa amefika ofisini hapo na kumuulizia, alichokifanya ni kumwambia yule mwanamke kumruhusu mwanaume huyo.
Bugabu akaanza kuingia ndani ya ofisi ile. Shati lake jeupe pamoja na tai yake nyekundu vilimfanya kupendeza kupita kawaida. Moja kwa moja baada ya kuingia ndani ya ofisi ile, akakaa katika kiti kimoja kilichokuwa wazi.
“Karibu”
“Asante sana” Bugabu alijibu na kujitambulisha kwamba alikuwa mpelelezi kutoka katika kituo cha polisi.
Maongezi yalianzia hapo, walizidi kuongea mambo mengi sana na ya kawaida kabisa. Mpelelezi Bugabu akaonekana kutaka kujua kitu fulani kutoka kwa Dominick ambaye alikuwa akijibu kila swali ambalo alikuwa akiulizwa kiufasaha kabisa.
“Wewe ndiye muuaji Dominick. Wewe ndiye uliyewaua Mawaziri wote hawa” Bugabu alimwambia Dominick ambaye alionekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Usishtuke. Mimi ni mpelelezi na kila siku nilikuwa nikiendelea na upelelezi wangu. Wewe ndiye muuaji. Nimepeleleza kwa kipindi kirefu sana. Nimegundua kwamba Mawaziri hawa waliiteketeza familia yako. Usitake kuuliza nimejua vipi, kumbuka kwamba mimi ndiye mpelelezi na nimefanya kazi kwa muda mrefu sana. Nilikwenda makaburini, makaburi ya familia yako yalikuwa yakiwekwa maua mara kwa mara lakini kaburi lako halikuwa likiwekwa maua, hii ilinionyesha kwamba wewe ndiye ulikuwa akifanya yale. Nimegundua mengi, niliyaangalia maneno yale yaliyoandikwa ukutani siku ile familia yako ilipoangamizwa, nikafuatilia majina ya Mawaziri waliouawa, nikagundua kwa asilimia mia moja kwamba ni wewe, ninaamini kwamba ulifanya hivi kwa ajili ya kulipa kisasi” Mpelelezi Bugabu alimwambia Dominick ambaye alikuwa kimya huku akionekana kuwa na wasiwasi tele.
“Nakuunga mkono kwa vyote ulivyofanya, hata kama ningekuwa mimi, ningeziteketeza familia zao na kuwamaliza wao pia. Hongera kwa kazi kubwa. Hautakiwi kujali hata kidogo. Kila kitu kipo ofisini mwangu, nakuhakikishia kwamba hakuna atakayefahamu hili. Nimeamua kuja kukueleza kwa kuwa tu nilitaka ujue kwamba mimi ni mpelelezi wa kimataifa na huwa hakuna upelelezi unaonishinda. Nakutakia kazi njema na hongera Dominick” Mpelelezi Bugabu alimwambia Dominick.
Bugabu akainuka, Dominick akashusha pumzi ndefu na kuipeleka mikono yake mezani. Baada ya sekunde chache nae akainuka na kupeana mikono na Bugabu ambaye wala hakutaka kuendelea kukaa ofisini pale zaidi ya kuaga na kuondoka.
“Asante Mungu” Dominick alijikuta akijisemea na kuegemea kiti chake.
Maisha mapya ya Dominick yakaanza, kiasi cha fedha cha shilingi milioni mia moja alikuwa amekwishazitumia kwa kununua nyumba kubwa iliyomgharimu milioni sitini huku milioni arobaini akifanyia biashara nyingine.
Mara kwa mara alikuwa akielekea katika makaburi ya Kinondoni na kuyaangalia makaburi ya familia yake na kisha kuweka maua. Kila siku ambazo alikuwa akiendelea kuishi katika dunia hii ambayo ilionekana kujaa mambo mengi, alikuwa akiikumbuka familia yake.
Baada ya miaka miwili, Dominick akaamua kumuoa msichana mrembo Magreth. Magreth ndiye ambaye akaonekana kuanza kuyabadilisha maisha yake, hakuwa mtu wa mawazo tena kama ilivyokuwa siku za nyuma. Alimpenda mkewe Magreth na kumthamini katika maisha yake yote.
Baada ya mwaka mmoja, wakafanikiwa kupata mtoto wa kiume aliyempa jina la Ibrahim, jina ambalo alikuwa amempa marehemu mtoto wake. Alifanya hivi kuwa kama ishara maalumu ya kumkumbuka mtoto wake ambaye alikuwa akimthamini kuliko mtu yeyote.
MWISHO