Quantcast
Channel: Rogers Linky - Sports Home
Viewing all articles
Browse latest Browse all 12768

MASSACRE (MAUAJI YA HALAIKI) SEHEMU 01 MPAKA 04

$
0
0
Kila aliyekuwa akizisoma taarifa ambazo zilikuwa zimeandikwa katika magazeti mbalimbali yaliyokuwa yakitoka katika siku hiyo alibaki akishangaa tu. Watu wakashtuka kupita kawaida, habari ile ilionekana kuwasisimua kupita kawaida. Imani juu ya wachungaji ikaanza kuondoka katika mioyo ya watu, hasa waumini wa dini ya Kikristo.
   Kanisa likaonekana kupotea njia, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea hasa katika makanisa mbalimbali kilionekana kuwa kama maigizo juu ya jukwaa au ndani ya luninga. Shetani akaonekana kuliteka kanisa na kulifanya alivyotaka kulifanya. Dhambi ambayo ilionekana kufanyika kwa kiongozi mmoja wa kanisa moja ikaonekana kama imetokea katika makanisa yote nchini Tanzania. Watu wengine wakataka kujitoa kutoka katika imani ya Kikristo kwa kudai kwamba shetani alikuwa amemzidi nguvu kila mtu.


   Wokovu wote ambao ulikuwa ukiendelea katika makanisa yote ukaanza kuyumba. Watu wengine wakaahidi kutokuhudhuria tena makanisani mwao kutokana na imani juu ya viongozi wao kuanza kupotea. Idadi kubwa ya watu wakaanza kupoteza uaminifu wao juu ya wachungaji wa makanisa yao.
   ‘MCHUNGAJI ATAKA KUMBAKA BINTI OFISINI’. Hicho kilikuwa ni kichwa cha habari ambacho kilikuwa kikisomekana katika magazeti mbalimbali jijini Dar es Salaam. Bado watu walikuwa wakiendelea kushangaa, hawakuamini kama mchungaji Matimya wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge angeweza kufanya kitu kama kile ambacho kilikuwa kimeonekana kuandikwa katika magazeti mengi.
   Habari ile ilionekana kuwa habari iliyokuwa na furaha kwa watu wote ambao walikuwa hawawapendi Watumishi wa Mungu. Watu wakaanza kupeana taarifa majumbani mwao huku kila aliyepewa taarifa ile akaanza kuelekea barabani kulinunua gazeti moja ambalo lilikuwa na habari ile.
   Katika mwaka mzima, habari ile ndio ambayo ilifanikiwa kuuza nakala nyingi kuliko habari yoyote iliyowahi kuandikwa katika mwaka huo. Mpaka inafika saa saba mchana, hakukuwa na gazeti lolote lililokuwa na habari ile ambalo lilikuwa katika meza ya wauza magazeti.
   Kila mtu ambaye alikuwa akiyaona magazeti yale, aliyanunua. Siku ya mwisho ikaonekana kukaribia kutokana na shetani kuonekana kulivamia kanisa hasa kwa viongozi mbalimbali wa makanisa. Aibu kubwa ikaanza kulikumba kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge.
   “Haiwezekani hata kidogo. Mbona huyu Mchungaji ni Mtumishi mzuri wa Mungu! Tena kwa sasa anataka kuwa Askofu Mkuu. Hawezi kufanya hivi” Sauti ya msichana mmoja ilisikika ikiwaambia wenzake huku mkononi akiwa ameshika Biblia katika kipindi ambacho walikuwa wakitoka kanisani siku hiyo ya Jumapili.
   “Kwa nini isiwezekane kwa mtu kama huyu kufanya hivi? Tumemkaribisha shetani sisi wenyewe. Acha awatumie watumishi wa Mungu anavyotaka” Mwanamke mmoja alisikika akisema huku akishika vizuri Biblia yake.
   Habari hiyo ndio ambayo ilikuwa imeshika hatamu katika kipindi hicho. Kila mtu ambaye alikuwa akiiona habari ile na kuisoma, alishtushwa kupita kiasi. Picha kubwa ya rangi ya mchungaji Matimya ilikuwa ikionekana vizuri katika kila gazeti ambalo lilikuwa na habari ile.
                                                       ****
   Mchungaji Matimya alikuwa amekaa katika kiti cha nyuma kabisa ndani ya kanisa lake. Uso wake alikuwa ameuinamisha chini huku machozi yakimtoka. Mbele yake aliiona aibu kubwa ikiwa imemkuta, hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya ili Watanzania waelewe kwamba hakuwa amekifanya kile kitu ambacho kilikuwa kikitangazwa sana na vyombo vya habari.
   Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kumuamini Mchungaji Matimya, kila mtu kanisani humo alimuona kuwa kama Mwakilishi wa shetani ambaye aliletwa kanisani humo kwa ajili ya kulitia aibu kanisa. Ingawa ibada ilikuwa ikiendelea kanisani humo, macho ya washirika wengi walikuwa yalikuwa yakimwangalia Mchungaji Matimya.
   Machozi yale ambayo yalikuwa yakimtoka, yalionekana kuwa kama ya kinafiki machoni mwa washirika wa kanisa lile. Mchungaji Matimya hakuwa peke yake, familia yake ilikuwa pembeni yake. Mkewe, Bi Meriana alikuwa upande wake wa kushoto huku watoto wake wawili, Benedict na Angelina wakiwa katika upande wa kulia.
   Kilio cha chini chini kilikuwa kikisikika kutoka kwa Bi Meriana. Kila alipokuwa akikumbuka aibu ile ambayo ilikuwa imemkuta mumewe, alizidi kuumia. Hawakuonekana kufuatilia kitu chochote kilichokuwa kinaendelea kanisani mule. Vichwa vyao vilikuwa vikifikiria mbali.
   Ibada iliendelea kama kawaida. Mara baada ya muda wa matangazo kuingia, Askofu wa dhehebu hilo la Praise And Worship, Askofu Lugakingira akasimama na moja kwa moja kuelekea katika madhabau ya kanisa hilo na kuchukua kipaza sauti. Kabla hajaongea kitu chochote kile, alitulia kwa muda huku akiliangalia kanisa.
   Kila mtu alikuwa kimya tayari kwa kusikiliza kile ambacho Askofu alitaka kukizungumza mahali hapo. Askofu alianzia mbali sana lakini huku lengo lake kubwa likiwa ni kufika katika kitu ambacho kilimfanya kuja katika kanisa lile katika siku hiyo ya Jumapili. Mara baada ya kutumia dakika kumi kuongea mambo tofauti tofauti, hapo hapo akamtaka Mchungaji Matimya kwenda mbele ya kanisa lile.
   Huku akionekana kuwa katika lindi la mawazo, Mchungaji Matimya akainuka kutoka katika kiti alichokuwa amekaa kule nyuma ya kanisa na moja kwa moja kuanza kuelekea mbele ya kanisa. Minong’ono ikaanza kusikika kutoka kwa washirika ndani ya kanisa lile, Mchungaji Matimya hakuonekana kujali, aliendelea kupiga hatua hadi mbele ya kanisa lile.
   “Nadhani hakuna mtu asiyejua kitu ambacho kimenifanya kuja ndani ya kanisa hili kwa siku ya leo. Lilikuwa ni suala ambalo lilihitaji kumuita Mchungaji Matimya. Niliongea nae kwa kirefu sana na kukiri kila kitu pasipo kuficha kitu chochote kile” Askofu Lugakingira aliliambia kanisa na kuendelea.
   “Ningependa kumpa nafasi ya kulieleza kanisa kama hiki kitu ambacho kimetawala kila sehemu ni kweli au kuna uongo wowote” Askofu Lugakingira alisema na kisha kumpa kipaza sauti mchungaji Matimya.
   Mchungaji Matimya hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku macho yake yakiangalia chini. Kila alipotaka kuongea kitu, aliuona mdomo wake kuwa mzito kufunguka, hakujua aseme kitu gani mbele ya kanisa na mbele ya familia yake. Kumbukumbu ya maisha yake ya nyuma ikaanza kujirudia kichwani mwake, katika hatua nyingine, alijuta kwa nini aliitwa kuwa Mchungaji.
   “Nalihitaji kanisa msamaha. Ni kweli nilitaka kumbaka Judith ndani ya of….” Mchungaji Matimya alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, akaanza kulia. Sauti ya kilio chake kilisikika kanisa zima kutokana na kipaza sauti alichokuwa amekishika. Wanawake wakashindwa kuvumilia, nao wakaanza kulia.
   Mtoto wake, Benedict hakuweza kuvumilia kubaki kanisani hapo akasimama na moja kwa moja kuanza kuelekea nje ya kanisa lile. Moyo wake uliumia kupita kiasi, maneno ambayo aliongea baba yake mbele ya kanisa yalionekana kumuumiza kupita kawaida.
   Mara baada ya kufika nje ya kanisa, moja kwa moja akalifuata gari lao na kuingia ndani na kisha kuliwasha. Kila mtu ambaye alikuwa nje ya kanisa alikuwa akimwangalia Benedict ambaye akaliwasha gari lile na kuondoka katika eneo lile la kanisa.
   Mchungaji Matimya akashindwa kuendelea, akakikabidhi kipaza sauti kwa Askofu Lugakingira ambaye alikuwa akimbembeleza kwa kumpiga piga mgongoni. Mchungaji Matimya akazidi kulia zaidi na zaidi, akapiga magoti chini huku uso wake akiwa ameuinamisha chini kwa aibu huku machozi yaliyokuwa yakimtoka kuloanisha sakafu ya pale madhabahuni.
   “Kila kitu kina sheria zake. Na hili kama dhehebu la Praise And Worship, mchungaji Matimya hatokuwa mchungaji wa kanisa hili tena. Tunamfungia kufanya huduma yoyote kwa muda wa mwaka mmoja na nusu” Askofu Lugakingira aliliambia kanisa.
   Idadi kubwa ya washirika ikaonekana kufurahia. Thamani ya mchungaji Matimya ikaonekana kushuka. Pepo la uzinzi likaonekana kumvaa mchungaji Matimya ambaye bado alikuwa pale mbele ya kanisa akiendelea kulia kwa uchungu. Kila kitu ambacho kiliendelea katika maisha yake kilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.
****
   Uchaguzi wa Askofu mkuu ndio ambao ulikuwa ukikaribia, siku tano tu ndizo ambazo zilikuwa zimebaki kabla ya uchaguzi huo. Wachungaji wawili, mchungaji Matimya wa kanisa la Praise And Worship la Mwenge lililoko jijini Dar es Salaam pamoja na mchungaji Mwakipesile wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Morogoro ndio ambao walikuwa wakiwania nafasi ya kuwa Askofu mkuu nchini Tanzania.
   Kila mtu alionekana kuwa na nafasi nzuri ya kuchukua nafasi hiyo lakini mchungaji Matimya ndiye ambaye alionekana kuwa na nafasi kubwa zaidi. Kila kanisa la dhehebu la Praise And Worship lililokuwa nchini Tanzania, jina la mchungaji Matimya ndilo ambalo lilikuwa likitajwa mara kwa mara.
   Wachungaji wengi walikuwa wakitamani Mchungaji Matimya achukue nafasi hiyo kutokana na huduma nzuri ambayo alikuwa akiitoa katika kanisa lake na makanisa mengine mbalimbali nchini. Hakuwa na roho ya majivuno kama aliyokuwa nayo mchungaji Mwakipesile.
   Kila mtu alivutiwa nae, kila mtu akatamani mchungaji Matimya achukue nafasi ile na kuwa Askofu mkuu. Asilimia zaidi ya themanini ya wachungaji wote wa dhehebu hilo walitamani mchungaji Matimya achukue nafasi hiyo ambayo ilitarajiwa kuachwa na Askofu Lugakingira siku chache zijazo.
   “Ni lazima nifanye kitu” Mchungaji Mwakipesile alijisemea huku akionekana kukasirika.
   Mbele yake hakuona dalili zozote za ushindi katika nafasi ya Uaskofu. Baadhi ya wachungaji ambao walikuwa katika upande wake, katika kipindi hicho walikuwa wamemsaliti. Kila kitu katika kipindi hicho kilionekana kwenda tofauti na matarajio yake ya nyuma.
   “Nitamtumia hata mshirika wake mwenyewe” Mchungaji Mwakipesile aliendelea kujisemea.
   Hakutaka kuendelea kubaki Morogoro, kitu alichokifanya siku iliyofuata ni kuchukua ndege na moja kwa moja kuanza kuelekea jijini Dar es Salaam. Hakutaka mtu yeyote afahamu juu ya safari yake hiyo ya ghafla, hakumpa taarifa hizo mtu yeyote zaidi ya msichana mmoja tu, Judith Simon ambaye alikuwa akiishi ndani ya jiji la Dar es Salaam.
*****
   Jina la Judith Simon wala halikuwa geni masikioni mwa washirika wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge. Binti huyu alikuwa na sifa zote ambazo msichana wa kisasa na mrembo alitakiwa kuwa nazo. Alikuwa na wembamba kama waliokuwa nao wasichana ambao walikuwa wakigombania nafasi ya kuwa mrembo wa Tanzania.
   Uso wake ulikuwa mwembamba, alikuwa akitembea kwa mwendo wa mapozi kana kwamba alikuwa hakanyag ardhi. Kila aliyekuwa akiuangalia mwendo wa Judith alikiri kwamba binti huyo alikuwa akitembea mwendo uliokuwa na mvuto kanisani hapo.
   Mashavu yake yaipendezeshwa na vishimo viliwili vilivyokuwa mashavuni mwake ambavyo vilikuwa vikionekana vizuri katika kila wakati alipokuwa akicheka au kutabasamu. Kila wakati Judith alionekana kuvutia.
   Uzuri wake ulikuwa ukionekana wakati wote. Haijalishi alikuwa amekarika, amenuna au ametabasamu, muda wote huo uzuri wake wa asili ndio ulikuwa ukionekana machoni mwa watu wengi.
   Judith alionekana kuwa mcha Mungu. Karama ya Uimbaji ambayo alikuwa nayo ndio ambayo ilimfanya kuzidi kukubalika katika kanisa hilo lililokuwa likiongozwa na mchungaji Matimya. Judith akaamua kujiunga na kwaya mojawapo iliyokuwa kanisani hapo. Kila mtu alionekana kubarikiwa katika vipindi vyote ambavyo Judith alikuwa akimsifu Mungu. Judith alikubalika na kila mtu kanisani hapo.
   Vijana hawakutaka kubaki nyuma kanisani hapo, harakati za kumtaka Judith zilikuwa zikiendelea kimya kimya kanisani hapo. Judith hakutaka kujirahisisha kwa wavulana kitu ambacho kiliwapelekea vijana wengi kusimamishwa huduma kanisani humo.
   “Watu wakijua?” Judith alimuuliza mchungaji Mwakipesile huku akionekana kuwa na hofu. Mchungaji Mwakipesile hakuongea kitu chochote, alibaki akimwangalia Judith na kisha kutoa tabasamu.
   “Utawaambia au?” Mchungaji Mwakipesile alimuuliza.
   Swali lile likaonekana kuwa gumu kwa Judith, alibaki kimya huku akimwangalia mchungaji Mwakipesile ambaye alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea kwa wakati huo. Alipoona Judith amekaa kimya, akachukua glasi iliyokuwa na juisi ya maembe na kisha kupiga fundo moja.
   “Kama hautowaambia nina uhakika hawatojua” Mchungaji Mwakipesile alimwambia Judith ambaye kwa kiasi fulani woga wake ukaonekana kupungua.
   “Na vipi kuhusu malipo?” Judith aliuliza.
   “Milioni tano baada ya kukamilisha kazi hii” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
   “Sawa” Judith aiitikia na moja kwa moja kuondoka huku akijiandaa na kazi ambayo alitakiwa kuifanya.
****
   Alipomaliza kuongea na viongozi mbalimbali wa kanisa lake, mchungaji Matimya akaanza kuelekea katika ofisi yake iliyokuwa pembeni ya kanisa hilo. Alipoingia ofisini mwake, akaanza kuifuata kiti chake na kukalia, akaichukua Biblia ambayo ilikuwa mezani na kuanza kusoma baadhi ya maandiko.
   Alitulia kimya huku akiendelea kupitia baadhi ya maandiko. Mara kwa mara uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu kila alipokuwa akisoma andiko ambalo lilionekana kumvutia. Alitumia muda wa dakika thelathini kuyasoma baadhi ya maandiko ambayo alikuwa ameyadhamiria kuyasoma katika kipindi hicho. Alipomaliza kuyasoma maandiko hayo, akaifunika Biblia yake na kuanza kusali.
   Huku akiwa katikati ya sala, mara mlango ukasikika ukianza kugongwa kitu ambacho kilimpelekea kukatisha sala yake na kumkaribisha mgongaji. Mlango ukafunguiwa na msichana Judith kuingia. Mchungaji Matimya akaonekana kushtuka kwani halikuwa jambo la kwaida kwa mgeni kuingia ndani ya ofisi yake katika kipindi hicho ambacho alijiandaa kufunga ofisi yake.
   Judith akaanza kupiga hatua kukifuata kiti cha wageni na kisha kutulia huku kikiwa mbele ya meza ile pale ofisini. Judith hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia mchungaji kwa kutumia macho ambayo yalionyesha mshtuo mkubwa kwa mchungaji Matimya. Mchungaji Matimya akasimama na kuanza kumsogelea Judith ambaye alibaki kimya akijifikiria namna ya kufanya kile ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati ule.
   “Kuna nini tena judith?” Mchungaji Matimya alimuuliza Judith.
   “Nina kiu mchungaji” Judith alijibu.
   “Kiu ya Neno la Mungu au?”
   “Hapana. Nina kiu ya penzi lako”  Judith alijibu huku akionekana kutokujiamini.
   Mchungaji Matimya akapigwa na mshtuko, jibu ambalo lilitoka mdomoni mwa Judith lilionekana kumshtua kupita kawaida. Hakujua kama masikio yake yalikuwa yamesikia vibaya au yalikuwa yamesikia kitu halisi ambacho kilikuwa kimetoka mdomoni mwa Judith.
   Akaanza kumwangalia Judith mara mbili mbili kana kwamba hakuwa amekielewa kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka mdomoni mwa Judith. Uso wa Judith haukuonekana kutania hata kidogo, alionekana kumaanisha kile ambacho alikuwa akikiongea kwa wakati ule.
   Huku akionekana kutokujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya kwa wakati ule, akashtuka mara baada ya kumuona Judith akianza kuvua nguo zake katika kasi ambayo ilionekana kumshangaza.
    Mikono ya Judith ikapata nguvu ya ziada, akamvuta mchungaji Matimya na kisha kuanza kulivua shati lake ambapo likafunguka huku baadhi ya vifungo viking’oka. Mchungaji Matimya alijaribu kuleta purukushani za kutaka kujiondoa mikononi mwa Judith lakini hakufanikiwa.
   “Niachie…niach…..” Mchungaji Matimya alimwambia Judith lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, akasukumwa na Judith ambaye alianza kupiga kelele za kuomba msaada huku akiifungua blauzi yake na kuyaacha matiti yake nje. Judith hakuona kuridhika, akaanza kuipandisha sketi yake juu ya kuyaacha mapaja yake wazi.
   “Ananibakaaaaaa…..ananibakaaaaa…..” Judith alipiga kelele huku akimsogelea mchungaji ambaye alionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Kwa kasi kubwa Judith akamvuta mchungaji na kisha kumuweka katikati ya mapaja yake na kisha kuibana miguu yake huku kelele za kubakwa zikiendelea kusikika.
   Ghafla mlango wa ofisi ile ukafunguliwa na wazee wa kanisa kuingia. Picha ambayo ilionekana ndani ya ofisi ile ilionekana kumshtua kila mtu. Judith alikuwa amelala juu ya meza huku mchungaji Matimya akiwa katikati ya mapaja yake yaliyokuwa wazi.
   “Yesu wangu!” Mzee kiongozi wa kanisa hilo, Bwana Onesmo alijikuta akisema huku akiiweka mikono yake kichwani. Mara baada ya Judith kuona kwamba wazee wa kanisa walikuwa wamefika ndani ya ofisi ile na kuliona tukio lile, hapo hapo akajitoa na kuelekea pembeni huku akijitahidi kuyafunika matiti yake.
   “Mchungaji! Umefanya nini?” Mzee Sule aliuliza kwa mshtuko.
   Mchungaji Matimya hakutoa jibu lolote lile, alibaki kimya huku akimwangalia Judith usoni. Judith alikuwa akilia huku mashavu yake yakiwa yameloanishwa na machozi ambayo yalikuwa yakimtoka. Mchungaji Matimya hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea ili aeleweke kwa wazee wa kanisa kwamba hakuwa amefanya kile kitu ambacho Judith alikuwa akikisema kwa wakati ule.
   Muonekano wa Judith ambao alikuwa nao ndio ambao ulikuwa ukiwahakikishia wazee wa kanisa kwamba mchungaji Matimya alikuwa amefanya kile ambacho Judith alikuwa akikisema kwa wakati huo.
   Sketi yake ilikuwa imechanika na kuyafanya mapaja yake kuwa nje. Blauzi yake ambayo alikuwa ameivaa ilikuwa imeng’olewa vifungo na kuyafanya matiti yake kuwa nje. Kila mtu alimwamini Judith juu ya kile ambacho alikuwa akikisema kwa wakati ule.
   Muda wote huo mchungaji Matimya alibaki kimya huku akiwa hafahamu ni kitu gani ambacho alitakiwa kufanya. Alionekana kuchanganyikiwa.
****
   Katika kipindi chote mchungaji Matimya hakuonekana kuwa na furaha, kila wakati alikuwa mtu wa majonzi tu. Skendo ya kutaka kubaka ambayo ilikuwa imemkuta ndio ambayo ilichangia kuwa katika hali hiyo ya majonzi. Katika vipindi vyote ambavyo alipitia katika maisha yake, kipindi hicho ndicho kilionekana kuwa kuwa kipindi kigumu kuliko vipindi vyote maishani mwake.
   Mara kwa mara alikuwa akijifungua chumbani akisali, alijiona kuwa kama mtu mwenye dhambi mbele za Mungu. Shetani alionekana kupewa nafasi ya kumjaribu.  Kila wakati alikuwa akisali huku machozi yakimtiririka, alilia kupita kiasi, hakuona msaada wowote mbele yake, alijiona kuwa kama mtu aliyetengwa pasipo msaada wowote ule.
   Marafiki zake wote aliokuwa nao walionekana kuwa kama kumtenga. Familia yake ndio ambayo ilionekana kuwa kila kitu katika maisha yake, hiyo ndio ilikuwa furaha yake, upendo wake na faraja yake kuu. Mchungaji Matimya hakupewa nafasi yoyote ya kujitetea, kila mtu alimuona kuwa mtu maalum ambaye aliitwa kanisani kwa ajili ya kuliharibu kanisa.
   Kanisani akawa akikaa katika viti vya nyuma pamoja na familia yake. Washirika wa kanisa hilo hawakuwaonyeshea upendo tena, kila mtu alionekana kuichukia familia hiyo. Tukio ambalo lilikuwa limetokea katika maisha yake lilionekana kutaka kuiyumbisha imani yake siku za usoni.
   Kila ibada ilipokuwa ikiisha, hakutaka kubaki kanisani hapo zaidi ya kuingia ndani ya gari na kuondoka pamoja na familia yake.
   Kila siku moyo wake ulikuwa na majonzi, furaha kwake ikapotea, majonzi yakautawala moyo wake. Mara kwa mara alikuwa akifikiria sababu zilizompelekea Judith kufanya kitendo kama kle ndani ya ofisi yake. Hakufikiria hata mara moja kama mchungaji Mwakipesile alikuwa nyuma ya tukio zima.
   Ndani ya gari kila mtu alikuwa kimya huku wote wakionekana kuwa na mawazo vichwani mwao. Vitendo ambavyo vilikuwa vikifanywa na washirika wa kanisa lile ndivyo ambavyo vilikuwa vikiwaumiza. Ukaribu ambao ulikuwepo kati yao na washirika wa kanisa lile ukaonekana kupotea. Familia nzima ilionekana kutenda dhambi isiyoweza kusameheka mbele za Mungu.
   “Siamini kama kanisa linaweza kufanya kitu kama hiki, yaani upendo wao wote umepotea, upendo ambao walikuwa nao kabla umepotea kabisa” Mzee Matimya alisema huku akionekana kuwa na majonzi.
   “Nafikiri Mungu anataka kuipima imani y….” Bi Meriana alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, Benedict akaingilia.
   “Silifikirii hilo mama. Hapa kuna kitu, ni lazima kutakuwa na mtu aliyefanya mpango huu” Benedict alisema huku mikono yake ikiwa imeshikiria usukani.
   “Hakuna mpango wowote Bened…..”
   “Usiseme hivyo baba. Sisi kama binadamu tuna udhaifu. Unaweza kukuta hata wachungaji wengine wamehusika katika hili” Benedict alisema huku akionekana kukasirika.
   “Usiseme maneno hayo juu ya watumishi wa Mungu, Benedict”
   Benedict hakutaka kuendelea kuongea kitu chochote kile kwani kila alipokuwa akiongea na ndivyo ambavyo hasira zilivyozidi kumpanda. Hakutaka kuwa na mapenzi yoyote na washirika wa kanisa la Praise And Worship. Alimchukia kila mtu kanisani. Akili yake haikukubaliana na kanisa kama kweli baba yake aliweza kufanya kitu kama kile. Alijua fika kwamba Judith alikuwa amefanya kitu kile kwa sababu ya kitu fulani.
   “Kuna mtu nyuma ya Judith” Benedict alisema mara baada ya ukimya kutawala kwa muda mrefu garini mule.
   Kila mtu akabaki akimwangalia Benedict ambaye alikuwa akitingisha kichwa chake juu na chini kuashiria kwamba alikuwa na uhakika juu ya kile ambacho alikuwa akikiongea katika kipindi kile.
   “Kuna mtu? Mtu gani?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kushangaa.
   “Simfahamu ni mtu gani lakini nafikiri mtu huyo atakuwa miongoni mwa wachun…”
   “Benedict…..” Mzee Matimya aliita kwa sauti iliyojaa hasira ambayo ilimfanya Benedict kunyamaza.
*****
   Mzee Matimya alibaki katika chumba chake cha kusalia. Macho yake yalikuwa yakiiangalia Biblia yake iliyokuwa juu ya meza. Aliiangalia kwa kipindi kirefu bila kufanya kitu chochote kile. Alitamani kuanza sala yake kama siku nyingine ambavyo alivyokuwa akifanya lakini kila alipojaribu kupiga magoti chini, aliiona miguu yake ikiishiwa nguvu.
   Aliendelea kutulia juu ya kiti ndani ya chumba kile. Alijikuta akipata nguvu mpya, akaipeleka mikono juu ya meza ile, akaichukua Biblia ile na kuifungua. Akaanza kusoma baadhi ya maandiko ambayo aliyaona yakimfariji. Ghafla macho yake yakaanza kujaa machozi ambayo baada ya muda fulani yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
   Nguvu za kuendelea kusoma Biblia zikatoweka. Akaifunika Biblia na kuyaelekeza macho yake darini. Alijiona kuwa peke yake, tumaini lote likatoweka, hasira zikaanza kumpanda kila kila alipokuwa akimfikiria Judith.
   Aliendelea kubaki katika hali ile kwa dakika kadhaa, mara akashtuka baada ya simu yake kuanza kuita. Akaupeleka mkono wake mfukoni na kuitoa simu ile na kuanza kukiangalia kioo cha simu ile. Namba ambazo zilionekana katika kioo cha simu ile zilikuwa ngeni machoni mwake. Hakutaka kujali sana, alichoifanya ni kuipeleka simu ile sikioni na kuanza kuongea.
   “Bwana Yesu Asifiwe mchungaji” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
   Mzee Matimya hakuitikia chochote kile. Kichwa chake kikaanza kujaza maswali juu ya mpigaji wa simu ile. Taarifa zilijulikana  Tanzania nzima kama katika kipindi hicho hakuwa mchungaji tena mara baada ya kuvuliwa uongozi huo. Ni nani alikuwa akiongea upande wa pili? Je alikuwa ni rafiki yake ambaye walipotezana kipindi kirefu kilichopita au alikwa mtu mwingine?
   “Mchungaji……” Sauti ya upande wa pili iliita mara baada ya kuona ukimya umetawala kwa kipindi kirefu.
   “Amen….Amen…Nani anaongea?” Mchungaji aliitikia na kuuliza swali huku akionekana dhahiri kutokumjua mpigaji wa simu ile.
   “Ni mimi Patrick. Patrick Chonya. Umenisahau mchungaji?”Sauti ya upande wa pili ilisikika
   Mzee Matimya akaonekana kupatwa na mshtuko, ghafla tabasamu likaanza kuonekana usoni mwake. Kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yak kilionekana kusahaulika kwa muda. Alimfahamu sana Patrick, kijana ambaye alikuwa mshirika wake kabla ya kuhamia jijini Mwanza. Alisafiri miaka miwili iliyopita kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kusomea udaktari wa mifupa.
   “Mungu wangu! Umerudi lini kutoka Marekani?” Mzee Matimya aliuliza huku akionekana tabasamu likiendelea kuwepo usoni mwake.
   “Leo hii ndio nimekanyaga ardhi ya Tanzania. Njoo hapa uwanja wa ndege mchungaji. Nataka kukuachia mizigo yako kutoka kwa mchungaji Macbeth Lewis. Nataka kuchukua ndege kuelekea Mwanza” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
   Tabasamu likaongezeka zaidi na zaidi usoni mwa mzee Matimya. Hakuamini kama mchungaji Macbeth kutoka nchini Marekani ndani ya jiji la Atlanta angeweza kumkumbuka kwa kumletea zawadi kwani kilipita kipindi kirefu sana tangu mchungaji Macbeth aje nchini Tanzania na kuhubiri ndani ya kanisa lake.
   Kwa haraka haraka akakata simu na kuanza kujiandaa. Moyo wake ulirejewa na furaha, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea katika maisha yake alikiona kuwa kama mpango wa Mungu katika kudhihirisha kwamba bado alikuwa pamoja nae. Mara baada ya kumaliza kujiandaa, akatoka na kuanza kuelekea uwanja wa ndege huku tayari ikiwa imetimia saa kumi na mbili jioni.
*****
   Muda ulizidi kwenda mbele lakini wala mchungaji Matimya hakurudi nyumbani. Kila mtu alionekana kuwa na wasiwasi kwani hali ile haikuonekana kuwa ya kawaida kutokea. Mara kwa mara Bi Meriana alijaribu kumpigia simu mchungaji Matimya lakini simu haikupatikana.
   Bi Meriana hakukata tamaa, bado aliendelea kumpigia simu mume wake lakini majibu yalikuwa yale yale, simu haikupatikana. Amani ikatoweka moyoni mwake, mashaka yakaanza kumjaa, mara kwa mara Bi Meriana alikuwa akiikodolea macho saa yake, masaa yalikuwa yakiendelea kusonga mbele lakini wala mzee Matimya hakurudi nyumbani.
   Bi Meriana akashindwa kuvumilia, akasimama na kuanza kuelekea sebuleni, alipofika, akatulia kochini huku macho yake yakiangalia darini hali iliyoonyesha kwamba alikuwa na mawazo katika kipindi hicho. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kuwa na wasiwasi zaidi.
   “Mungu wangu! Saa sita!” Bi Meriana aliasema hali iliyofanya Benedict ambaye alikuwa sebuleni pale kushtuka.
   “Mbona umeshtuka hivyo?” Benedict alimuuliza.
   “Baba yako”
   “Amefanya nini?”
   “Hajarudi”
   “Toka aliyoondoka saa kumi na mbili?”
   “Ndio”
   Benedict akaacha kufanya kazi ambayo alikuwa akiifanya na kisha kuanza kumsogelea mama yake. Alipomfikia, akajiweka karibu nae na kuchomoa simu yake na kisha kuanza kumpigia baba yake, mzee Matimya. Simu ilikuwa vile vile, mawasiliano hayakupatikana kabisa hali ambayo ikaanza kuibua wasiwasi moyoni mwa Benedict.
   Simu mbalimbali zikaanza kupigwa kwenda kwa ndugu, jamaa na marafiki ili kujua kama mzee Matimya alikuwa huko lakini hawakufanikiwa kumpata. Wasiwasi ukaongezeka maradufu mioyoni mwao, kitu cha hatari kilionekana kumtokea mzee Matimya kwani halikuwa jambo la kawaida kitu kama hicho kutokea.
   “Kwa hiyo tufanye nini?” Benedict alimuuliza mama yake.
   “Labda tupige simu pol….” Bi Meriana alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Kwa haraka haraka akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile. Mara ya kwanza alifikiri kwamba mpigaji wa simu ile alikuwa mumewe, lakini mara baada ya kuangalia kioo cha simu yake, namba ilikuwa ngeni.
   “Hallooo…! Wewe ni mke wa mchungaji?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza swali kwa sauti ya juu hata kabla ya salamu. Bi Meriana hakujibu chochote kile, alibaki kimya kwa muda kama mtu ambaye alikuwa akijifikiria namna ya kulijibu swali lile.
   “Haloo..! Upo hewani?”
   “Ndio”
   “Basi njoo hapa kituo cha polisi haraka iwezekanavyo”
   “Kituo gani?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
   “Mbezi kwa Yusufu” Sauti ya upande wa pili ilijibu na simu kukatwa.
   Bi Meriana akabaki kimya huku simu ikiendelea kuwa masikioni mwake japokuwa simu ile ilikuwa imekatwa. Mwili wake ukaanza kumtetemeka huku miguu yake akiiona ikifa ganzi. Hakuendelea kubaki katika hali hiyo zaidi, machozi yakaanza kumtoka.
   “Mama. Nini tena?” Benedict aliuliza mara baada ya kumuona mama yake akiwa kimya muda mrefu.
   “Kituo cha polisi Mbezi kwa Yusufu”
   “Kimefanya nini?” Benedict aliuliza huku akionekana kushangaa.
   “Twende” Bi Meriana alisema.
   Hakukuwa na sababu yoote kubaki mahali hapo, kwa haraka haraka wakachomoka kutoka ndani na moja kwa moja kuelekea nje ambako wakaingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea katika kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusufu. Machozi yakaanza kumtoka Bi Meriana huku sauti ya kilio cha chini chini kikianza kusikikika.
   Simu ile ambayo aliipokea muda mchache uliopita ilionekana kumchanganya, tayari alikwishajua kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Maswali mfululizo yakaanza kumiminika kichwani mwake. Katika kipindi cha nyuma mzee Matimya aliaga kwamba alikuwa akielekea uwanja wa ndege ambako alikuwa akihitajika, kwa nini simu ilipigwa kutoka Mbezi? Tena mbaya zaidi katika kituo cha polisi.
   Kutokana na kutokuwa na foleni ya magari, walitumia dakika thelathini mpaka kufika Mbezi kwa Yusufu. Moja kwa moja wasimamisha gari lao nje ya kituo kile cha polisi na kisha kuelekea katika kituo hicho.
   “Karibuni” Polisi mmoja ambaye alikuwa zamu aliwakaribisha mara baada ya kuwaona.
   “Kuna nini afande?” Mume wangu yuko wapi?” Bi Meriana aliuliza maswali mawili mfululizo hata kabla ya salamu. Sauti ya kilio cha chini ikaanza kusikika kutoka kwa Bi Meriana. Kitendo cha swali lake kutokujibiwa ndicho ambacho kilionekana kumtia wasiwasi.
   “Nini kinaendelea?” Benedict alivunja ukimya kwa kuuliza swali.
   “Ni taarifa za masikitiko sana. Kitu ambacho kimetokea kimeonekana kumshangaza kila mtu” Polisi alisema mara baada ya kuchukua maelezo ya Benedict na Bi Meriana na kisha kuendelea.
   “Mlisema aliondoka toka saa kumi na mbili kuelekea uwanja wa ndege?” Polisi aliuliza.
   “Ndio”
   “Alirudi baada ya kuondoka?”
   “Hapana”
   Polisi hakutaka kuendelea kuuliza maswali, akainuka kutoka pale kaunta na kuanza kuelekea katika chumba kimojawapo kati ya vyumba ambavyo vilikuwa ndani ya kituo kile ambapo baada ya sekunde kadhaa, polisi mwingine ambaye alikuwa mahali pale nae kuingia ndani ya kile chumba.
   “Nini kinaendelea afande?” Benedict aliuliza mara baada ya polisi wale kurudi kaunta.
   “Jambo hili bado linafanyiwa uchunguzi”
   “Uchunguzi? Uchunguzi gani?”
   “Uchunguzi juu ya kifo chake” Polisi alijibu huku akionekana kuwa na wasiwasi.
   Jibu lile likaonekana kumchanganya kila mmoja, Bi Meriana akaanza kulia kwa uchungu. Neno ‘kifo’ ambalo lilitamkwa na polisi yule ndilo ambalo lilionekana kumuumiza. Wala hakuchukua hata dakika moja kuwa katika hali ile, macho yake yakaanza kuona giza ambapo baada ya sekunde chache akaanguka na kupoteza fahamu.
****
   Maturubai zaidi ya matano yalikuwa yamefungwa katika eneo la nyumba ya mzee Matimya. Idadi ya watu ambao walikuwa wamehudhuria msibani hapo wala haikuwa kubwa kama jinsi ambavyo ilitarajiwa. Ingawa wachungaji mbalimbali kutoka katika makanisa tofauti tofauti walikuwa wamehudhuria msiba huo lakini wala hakukuwa na zaidi ya washirika watano kutoka katika kanisa la Praise And Worship la Mwenge.
   Watu wengi ambao walikuwa wamehudhuria msibani pale walikuwa watu ambao wala hawakutoka mbali na eneo lile pamoja na waandishi wa habari. Kanisa likaonekana kupunguza ukaribu, kitendo cha waumini watano kuhudhuria katika msiba ule kilidhihirisha wazi kwamba mapenzi makubwa juu ya mzee Matimya hayakuwepo tena katika mioyo ya waumini wa kanisa lile.
   Vilio vya ndugu wa marehemu vilikuwa vikisikika kutoka kila kona msibani hapo. Sehemu kubwa ya mikeka iliyokuwa mahali hapo ilikuwa wazi jambo ambalo lilionekana kumshangaza kila mtu.
   “Mbona washirika wa kanisa la Praise and Worship hawaonekani hapa msibani?” Mchungaji Melek aliuliza kwa mshangao huku akiangalia katika kila kona msibani hapo kana kwamba alikuwa akimtafuta mtu fulani.
   “Wote walikasirishwa na kitendo kilichotokea. Mapenzi yao yakapotea. Mbaya zaidi, mzee Matimya alijinyonga” Kijana mmoja alimjibu mchungaji Melek.
   “Mungu wangu! Kumbe alijinyonga?”
   “Ndio. Nafikiri alijiona kuwa mkosaji mbele za Mungu wake” kijana yule alijibu.
   Benedict alikuwa ametulia pembeni kidogo mwa mchungaji Melek. Maneno yote aliyoyaongea mchungaji Melek na yule kijana yalionekana kumuumiza kupita kiasi. Hapo hapo akanyanyuka na kuanza kuelekea ndani ya nyumba yao.
   Idadi kubwa ya wanawake ilikuwa ndani ya nyumba hiyo. Benedict hakutaka kuongea chochote kile, kitu alichokifanya ni kupiga hatua kuelekea chumbani kwake.
   Akajilaza kitandani huku macho yake yakiangalia juu, machozi yakaanza kumtoka. Benedict akazidi kushikwa na hasira juu ya washirika wa kanisa la Praise and Worship lililokuwa Mwenge. Kadri ambavyo alivyokuwa akilikumbuka kanisa hilo na ndivyo ambavyo hasira zake zilivyozidi kuongezeka zaidi.
   Huku Benedict akiwa katika hali hiyo chumbani, mara mlango ukafunguliwa na Angelina kuingia. Macho ya Angelina yalikuwa mekundu huku mashavuni akiwa na alama za michirizi ya machozi hali iliyoonyesha kwamba kipindi fulani kilichopita alikuwa akilia. Angelina akaanza kupiga hatua mpaka pale kitandani alipokuwa amejilaza Benedict.
   “Najiona kama tumetengwa” Angelina alimwambia Benedict kwa sauti ya chini iliyojaa majonzi.
   “Mapenzi yao yamepotea kabisa. Ukaribu wao hauonekani, ni lazima nifanye kitu juu ya kanisa hili” Benedict alimwambia Angelina huku akionekana kuwa na hasira.
   “Kitu gani?”
   “Niwaue. Ni lazima niwaue washirika wote wa kanisa lile. Hasa Judith” Benedict alisema.
   “Usifanye hivyo Benedict”
   “Haina jinsi, nataka kurudisha furaha yangu iiyopotea” Benedict alisema huku akichukua kitambaa chake cha mkononi na kujifuta machozi yaliyokuwa yakimtoka.
   Ukimya mrefu ukatawala mahali hapo huku kila mtu akionekana kufikiria lake. Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira za Benedict zilivyozidi kumkamata. Hakulipenda kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge, hakumpenda mshirika yeyote ndani ya kanisa lile, kila mtu alionekana kuwa adui namba moja katika maisha yake.
   Huku kila mmoja akifikiria lake, mara simu ya mkononi ya Benedict ikaanza kuita, akaitoa kutoka mfukoni. Kabla hajapokea, akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile, macho yake yakatua katika namba ambayo ilikuwa ngeni machoni mwake. Akabonyeza kitufe cha kijani na kisha kuipeleka sikioni.
   “Upo wapi Benedict? Mbona sikuoni hapa nje?” Sauti ya upande wa pili ilisikika ikiuliza.
   “Wewe nani?” Benedict aliuliza.
   “Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi”
   Benedict hakutaka kuongea kitu chochote kile, akakata simu, akainuka kitandani na kuanza kuelekea nje. Alipofika nje, akaanza kuangalia katika kila upande. Macho yake yakatua katika uso wa mwanaume mmoja aliyekuwa na ndevu nyingi ambaye alimuonyeshea ishara ya kumuita. Benedict akaanza kupiga hatua kumfuata mwaname yule.
   “Hebu tusogee pembeni kidogo” Mwanaume yule alimwambia Benedict na kuanza kusogea pembeni. Hata kabla mzee yule hakuongea chochote, akatoa kitambulisho chake na kumuonyeshea Benedict.
   “Uchunguzi wenu umeishia wapi?” Benedict aliuliza.
   “Kwamba baba yako hakujinyonga”
   “Unasemaje?”
   “Huo ndio ukweli. Hakujinyonga bali alinyongwa”
   “Umejuaje?”
   “Tulipima alama za vidole katika kamba ile, na vile vile tulikuta alama za kiganja katika shavu lake hali iliyoonyesha kwamba alipigwa kibao kabla ya kunyongwa”
   “Sawa. Kwa hiyo mmeamua nini?”
   “Kumtafuta muuaji. Jambo hilo libaki kuwa lako tu, usimpe taarifa dada yako wala mama yako katika kipindi hiki. Wape taarifa baada ya mwezi mzima kupita” Mkuu yule wa polisi alimwambia.
   Benedict akaonekana kuchanganyikiwa, maneno ambayo aliongea mzee yule ndio ambayo yalionekana kumchanganya zaidi. Alimwangalia mzee yule mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa ameambiwa. Hasira zikazidi kumpanda zaidi juu ya kanisa la Praise And Worship kwa kuona kwamba kanisa lile pia lilikuwa limehusika katika mauaji ya baba yake.
   Unyonge ukaongezeka zaidi moyoni mwake, kiu ya kumtafuta muuaji ikaonekana kumkamata. Maswali mengi juu ya muuaji huyo yakaanza kumiminika kichwani mwake, mbele yake akaona giza, tumaini ndani ya moyo wake likaonekana kupotea.
   “Ni kanisa. Kanisa linamjua muuaji” Benedict alijisemea kwa hasira.
****
   Mchungaji Mwakipesile hakuonekana kuridhika japokuwa mchungaji Matimya alikuwa amevuliwa cheo cha uchungaji na kusimamishwa kazi ya Utumishi wa Mungu. Hakutaka mzee Matimya abaki ndani ya dunia hii kwani kama angemuacha basi ni lazima ingetokea siku ambayo angekuja kufahamu njama zote alizozifanya na hivyo kumuingiza katika matatizo.
   Mchungaji Mwakipesile hakutaka kutulia, akaiweka pembeni kazi yake ya Utumishi wa Mungu aliyokuwa nayo na kujiingiza katika mambo ambayo yalikuwa kinyume na kazi yake. Akaamua kuwafuata vijana ambao akaamini kwamba wangeweza kumfanyia kazi yake kama alivyotaka kufanyiwa. Mchungaji Mwakipesile hakutaka kuendelea kubaki Morogoro, kitu alichokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia gari lake.
   “Unahitaji nini mzee?” Kijana mmoja aliyejazia mwili alimuuliza mchungaji Mwakipesile.
   “Nahitaji kuonana na kiongozi wenu”
   “Unamfahamu au?”
   “Hapana” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
   Hapo hapo akaambiwa ateremke kutoka ndani ya gari lake. Vijana watatu wakatokea mahali hapo kutoka katika sehemu ambayo hakuifahamu na kuanza kumpekua. Walitumia dakika tano kumpekua yeye pamoja na gari lake, walipomaliza wakaanza kumwangalia usoni.
   “Wewe ni polisi?” Kijana mmoja aliuliza.
   “Hapana”
   “Unahitaji nini?”
   “Nataka kuonana na mkuu wenu” Mchungaji Mwakipesile aliwaambia.
   Hapo hapo akafungwa kitambaa usoni na kisha kupakizwa ndani ya gari nyingine na safari ya kuelekea asipopafahamu kuanza. Muda wote mchungaji Mwakipesile alikuwa akitetemeka kwa woga. Imani aliyokuwa nayo juu ya vijana wale ikaanza kupotea, kitu alichokifanya katika kipindi hicho ni kutulia ili kuona ni mahali gani ambapo angefikishwa.
   Safari ilitumia dakika kumi huku kitamba kikiendelea kuwa usoni mwa Mchungaji Mwakipesile. Mara baada ya dakika chache gari likasimama nje ya jengo moja ambapo geti likafunguliwa na gari kuingizwa ndani. Mchungaji Mwakipesile akateremshwa na moja kwa moja kupelekwa ndani ya nyumba hiyo. Kitambaa kile alichokuwa amefungwa usoni kikafunguliwa na kuamrishwa kukaa kochini.
   Macho ya mchungaji Mwakipesile hayakutulia sehemu moja, yalikuwa yakiangalia kila kona sebuleni pale ambapo alikuwa ameachwa peke yake. Wala hazikupita dakika nyingi, mzee mmoja mnene akafika mahali hapo na kutulia katika kochi jingine huku mkoni akiwa na chupa ya kinywaji cha Heineken.
   “Nasikia unanihitaji” Mzee yule alimwambia mchungaji Mwakipesile.
   “Ndio”
   “Una shida gani?”
   Mchungaji Matimya akaanza kuelezea shida zake huku mzee yule akiwa kimya kumsikiliza. Mchungaji alitumia dakika tano kuelekezea kila kitu ambacho alitaka kifayike kwa wakati huo. Mara baada ya kumaliza maelezo yake, mzee yule akachukua kinywaji chake kile na kupiga funda moja.
   “Una kiasi gani?” Mzee yule alimuuliza.
   “Milioni mbili” Mchungaji alijibu lililomfanya mzee yule kuanza kucheka.
   “Unataka tumuue mtu au kuku?” Mzee yule aliuliza.
   Tayari muonekano wa mzee yule ukaonekana kuwa tofauti na jinsi alivyokuwa kabla, ndita zikaanza kuonekana usoni mwake hali ambayo ilimuongezea wasiwasi mchungaji. Mchungaji Mwakipesile akashindwa kutoa jibu, alibaki akimwangalia usoni mzee yule kana kwamba hakulisikia lile swali aliloulizwa.
   “Acha utani na kazi yetu” Mzee yule alimwambia.
   “Milioni tatu” Mchungaji Mwakipesile alimwambia.
   “Nimekwambia acha utani”
   “Milioni nne. Naomba unisaidie”
   “Utani wako umezidi”
   “Milioni tano. Please, naomba unisaidie”
   “Sawa. Nitafanya hivyo kwa kiasi hicho kwa sababu tu umeniomba” Mzee yule alimwambia Mchungaji Mwakipesile.
   Mchungaji akaanza kutoa maelekezo kama njia ambazo zingewezesha kupatikana kwa mzee Matimya. Akatoa picha yake na yule mzee kuanza kuiangalia kwa makini. Alieleza kila kitu ambacho kilionekana kuwa muhimu kuhitajika na watu hao.
   “Utafurahia kifo gani?” Mzee yule alimuuliza.
   “Chochote kile ili mladi aonekane amejiua” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
****
   Saa kumi na mbili, vijana watatu walikuwa wamelipaki gari lao dogo mita hamsini kutoka katika geti la nyumba ya mzee Matimya iliyokuwa Mwenge. Vijana wale hawakutoka nje ya gari lao, waliendelea kumsubiri mzee Matimya ambapo lengo lao lilikuwa moja tu, kumuua. Waliendelea kusubiri zaidi na zaidi lakini wala mzee Matimya hakutoka ndani.
   Mara baada ya kuona kwamba wamesubiri muda mrefu pasipo mzee Matimya kutoka ndani ya nyumba yake, kijana mmoja kati yao akachukua simu yake na kupiga namba ya mzee Matimya ambayo walikuwa wamepewa na mchungaji Mwakipesile. Simu ikaanza kuita, iliendelea kuita kwa sekunde chache, ikapokelewa.
   “Mungu wangu! Umerudi lini kutoka Marekani?” Sauti ya mzee Matimya ilisikika ikiuliza mara baada ya maongezi mengine.
   Maongezi kati ya mchungaji Matimya na kijana yule aliyejiita Zolaya yaliendelea zaidi na zaidi. Vijana wale wengine wala hawakuongea kitu chochote kile, walibaki kimya wakimsikiliza Zolaya. Maongezi hayo yalichukua dakika mbili nzima, simu ikakatwa, uso wa Zolaya ukajaa tabasamu hali ambayo iliwaonyeshea matumaini fulani.
   “Vipi?” The Killer aliuliza.
   “Anatoka. Jiandaeni, wekeni silaha zenu vizuri” Zolaya aliwaambia.
   Hawakutaka kusubiri chochote kile, silaha zikawekwa tayari. Kila mtu akabaki kimya huku macho yakiwa getini kwa mzee Matimya. Zilipita dakika tano, geti likafunguliwana gari aina ya Vitara kutoka. Wakayapeleka macho yao ndani ya gari lile, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya mzee Matimya. Walipoona kuwa mzee Matimya ameanza safari ya kuelekea uwanja wa ndege, hapo hapo Zolaya akawasha gari na kuanza kumfuatilia mzee Matimya.
   Hawakutaka kuwa karibu na gari la mzee Matimya, waliacha umbali wa hatua thelathini kati yao. Mara baada ya gari la mzee Matimya kuchukua barabara ya Sam Nujoma, nao wakachukua barabara hiyo na kuanza kuelekea Mwenge kituoni.
   “Unafikiri atatumia njia gani kwenda uwanja wa ndege?” The Killer aliuliza.
   “Labda atakwenda kuingilia pale Sayansi. Njia ya kule Ubungo hakutaka kuitumia kwa sababu ya foleni” Zolaya alijibu.
   “Kwa hiyo tufanye nini?”
   “Kama kutakuwa na foleni kidogo pale Sayansi itakayomfanya kusimama. Shukeni na mkamuingilie. Hakikisheni mnampa amri ya kuelekea Mbezi, hasa katika msitu wa Pande” Zolaya aliwaambia.
   “Sawa”
   Bado waliendelea kumfuatilia zaidi na zaidi huku wakiwa wametenganishwa na magari mawili kati yao. Mzee Matimya akakata kona na kuchukua barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Kila mmoja garini alikuwa na shauku ya kutaka kufanya kile ambacho walikuwa wameagizwa. Kama walivyotaka ndivyo ilivyokuwa, walipofika Sayansi, magari yakasimama kutokana na foleni iliyokuwa mahali hapo.
   “Fanyeni haraka. Mfuateni, mtekeni na kuanza kuelekea Mbezi” Zolaya aliwaambia.
   Kwa haraka sana bila kupoteza muda, The Killer na Zinja wakateremka na kuanza kulifuata gari alilokuwa mzee Matimya.Walipolifikia, wakaingiza mikono yao katika madirisha yale ambayo hayakuwa yamefungwa vioo na kisha kutoa loki za milango ile. Mzee Matimya akapigwa na mshtuko mara baada ya kuona vijana wawili wakiingia ndani ya gari lake.
   “Mbona mnaingia nd….?” Mzee Matimya aliuliza lakini hata kabla hajamalizia swali lake, The Killer akatoa bunduki yake iliyokuwa kiunoni.
   Mara baada ya mzee Matimya kuiona bunduki ile, hapo hapo akatulia, mapigo yake ya moyo yakaanza kumdunda kwa kasi kubwa huku woga ukianza kumuingia. Hakutakiwa kuongea kitu chochote kile katika kipindi hicho. Kitu walichokifanya ni kumuamuru mzee Matimya kutoka katika usukani na kuelekea katika kiti cha nyuma huku Zinja akishikilia usukani na safari ya kuelekea Mbezi kuanza.
   Walitumia dakika sabini kutoka Kijitonyama mpaka Mbezi Mwisho huku Zolaya akiwafuatilia kwa nyuma. Hawakutaka kuishia Mbezi Mwisho, kitu kilichowapelekea kuendelea mbele. Kutokana na kasi ambayo walikuwa wakiitumia, walichukua dakika tano mpaka kufika katika msitu wa Pande.
   “Hapa hapa panatosha” The Killer alimwambia Zinja.
   Wote wakateremka kutoka ndani ya gari, wakamshusha mzee Matimya na kuanza kusogea nae katika sehemu iliyokuwa na miti mingi zaidi. Zolaya akafika mahali hapo, akateremka huku mkononi akiwa na kamba ngumu na kisha kuanza kuwasogelea.
   Kutokana na giza nene lilikuwa mahali hapo, wakawasha tochi zao na kuanza kuelekea mbele zaidi. Mzee Matimya bado alikuwa akitetemeka, moyoni alikuwa akiendelea kusali kwa kumtaka Mungu amnusuru na kumlinda na chochote ambacho kilitakiwa kufanyika. Hali haikuonekana kuwa na usalama wa hali yoyote ile kwa mzee Matimya, kadri walivyozidi kusonga mbela na ndivyo ambavyo woga ulivyozidi kumshika zaidi.
   “Panatosha” Zolaya aliwaambia huku akiwa amemaliza kufunga kamba katika mtindo wa kitanzi.
   “Jamani vipi tena?” Mzee Matimya aliuliza mara baada ya kuona akivalishwa shingoni kamba ile ambayo Zolaya alikuwa amekwishaifunga mtini. Hakukuwa na mtu aliyejibu chochote zaidi ya Zolaya kumpiga kofi moja shavuni ambalo lilimfanya kulewa.
   Kutokana na ubishi ambao alikuwa akiuleta mzee Matimya, iliwachukua nusu saa mpaka kukiingiza kichwa chake katika tundu la kamba na kumnyonga huko porini. Hakukuwa na mtu aliyeonyesha roho yoyote ya huzuni, kila mtu alikiona kitendo kile kuwa cha maana kwake. Huo ndio ukawa mwisho wa maisha ya mzee Matimya.
   Kazi yake kubwa ya kumtumikia Mungu katika kipindi kilichopita ikabaki kuwa kama historia. Alinyongwa porini siku hiyo baada ya wiki mbili ndani ya skendo yake ya kutaka kubaka ambayo ilikuwa imevuma sana nchini Tanzania. Zolaya alipohakikisha kwamba mzee Matimya amefariki, akaondoka pamoja na wenzake huku wakiuacha mwili ule mtini.
*****
   Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira za Benedict juu ya kanisa la Praise and Worship lililoko Mwenge zilivyozidi kuongezeka. Hakuonekana kumpenda mtu yeyote ndani ya kanisa lile, kila mtu kwake alionekana kuwa adui wake. Kila alipokuwa akielekea kanisani pamoja na mama yake, Bi Meriana na Angelina, Benedict hakutaka kuongea na mtu yeyote kanisani hapo.
   Moyo wake aliuona kuwa kanisa lilihusika na kifo cha baba yake, mzee Matimya. Kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika kanisani kama mahubiri ya Neno la Mungu kilionekana kuwa kama unafiki. Mauaji ndicho kitu ambacho kilikuwa kimeutawala moyo wake katika kipindi hicho, hakutaka kuliacha kanisa hivi hivi, alitamani kuliangamiza kanisa.
   Ibada ya mwisho ya Jumapili ya mwisho katika mwaka huo ndio ambayo ilikuwa ikiendelea ndani ya kanisa hilo. Kila mtu alionekana kuwa uso ulioonyesha furaha. Wanakwaya walikuwa wakiimba kwa furaha, yaani kila kitu katika kipindi hicho kilikuwa kikifanyika katika hali ya furaha. Watu wote walikuwa wakiimba kwa furaha kwani zilikuwa zimebakia siku mbili kabla ya kumaliza kwa mwaka huo wa 2007.
   “Funguo ziko wapi?” Sauti ya shemasi ilisikika ikiuliza.
   Kila mtu aliyekuwa amekaa katika viti vya nyuma kanisani pale aligeuka na kuwaangalia mashemasi ambao walikuwa wakizitafuta funguo ambazo zilikuwa mlangoni katika kipindi kichache kilichopita. Ingawa ibada ilikuwa ikiendelea huku mchungaji mpya wa kanisa hilo, Munisi akiendelea kuhubiri, mashemasi hawakuwa wakisikiliza mahubiri hayo zaidi ya kuendelea kuzitafuta funguo za milango ya kanisa.
   “Kwani zilikuwa wapi?” Shemasi mwingine aliuliza.
   ”Zilikuwa hapa. Tena muda mchache uliopita”
   “Hebu angalia chini ya viti, labda kuna mtoto alizichukua”
   Hapo hapo Shemasi mmoja akaanza kuangalia angalia chini ya viti lakini funguo wala hazikuonekana. Tayari wasiwasi ukaanza kuwaingia, akili zao zikaanza kuchanganyikiwa. Hawakujua ni nani ambaye alizichukua funguo zile kutoka katika msumali uliochomekwa ukutani, wakazidi kuangalia katika kila sehemu huku mchungaji Munisi akiendelea kuhubiri.
   “Zile kule”
   “Ziko wapi?”
   “Kazishika yule mtoto” Shemasi alijibu.
   Kwa haraka haraka akaanza kupiga hatua kumfuata mtoto yule aliyezishika funguo zile ambazo alikuwa nazo, mtoto yule ambaye alikuwa pembeni mwa Benedict. Mara baada ya kumfikia mtoto yule, shemasi akazichukua funguo zile.
   “Mmechelewa sana” Benedict alijisemea moyoni huku akionekana kuwa katika utulivu mkubwa kumsikiliza mchungaji.
   Mara baada ya ibada kumalizika, moja kwa moja Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya kanisa lile huku furaha ikiongezeka maradufu moyoni mwake. Kitendo cha kuzipata funguo za milango ya kanisa lile kilionekana kumfurahisha kupita kiasi. Hakutaka kuliona kanisa likiendelea kumtumikia Mungu kwani kitendo kile kilionekana kuwa kama unafiki mbele ya macho yake.
   Mara baada ya kufika Kariakoo, akateremka na kuanza kuelekea katika kibanda ambacho kilikuwa na tangazo la kuchongesha funguo. Alipokifikia, akamuita mchonga funguo ambaye mara moja akafika mahali hapo. Akachukua kipande cha sabuni ambacho kilikuwa na alama tatu za funguo na kisha kumgawia.
   “Elfu moja kila moja”
   “Sawa” Benedict alisema na kisha kumgawia noti ya shilingi elfu kumi mchongaji yule.
   “Rudi saa kumi, kila kitu kitakuwa tayari”
   “Hakuna tatizo” Benedict alisema na kisha kuondoka mahali hapo.
****
   Masaa manne yalikuwa yamebaki kabla ya kuuingia mwaka ambao ulikuwa ukiitwa ‘Mwaka wa Baraka’, mwaka wa 2008. Kila mtu alionekana kuwa na furaha, waumini mbalimbali wa dini ya kikristo wakaanza kujiandaa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea makanisani mwao. Vijana mitaani wakaziweka ngoma zao vizuri huku mafataki ya aina mbalimbali yakiwa yamewekwa vizuri.
   Japokuwa waumini wa Kikristo walikuwa wakitaka mwaka uingie na kuwakuta wakifanya maombi ya kumshukuru Mungu kanisani lakini hali ilionekana kuwa tofauti kwa watu wengine. Walevi walitamani mwaka uingie huku wakiwa na vinywaji midomoni mwao, kwa wale ambao walikuwa wazinzi, walitamani mwaka uingie na kuwakuta wakifanya ngono na watu wawapendao.
   Benedict hakutulia, muda wote alikuwa akifikiria kufanya mauaji. Huruma ilitoweka moyoni mwake, hasira kali na roho ya kulipa kisasi ndio ambayo ilikuwa imeutawala moyo wake kwa wakati huo. Mara kwa mara macho yake yalikuwa yakiiangalia saa yake, dakika zilionekana kwenda taratibu tofauti na siku nyingine.
   “Jiandae twende kwenye mkesha kanisani” Bi Meriana alimwambia Benedict.
   Mishipa ya fahamu ya Benedict ikawa kama imezibuka, kitendo cha mama yake na dada yake, Angelina kwenda kanisani kingeweza kumzuia katika kufanya kile ambacho alitaka kukianya. Akili yake ikafanya kazi ya haraka haraka, akainuka na kuanza kuelekea chumbani kwake. Akaiangalia saa yake ya ukutani, masaa mawili ndio ambayo yalikuwa yamebaki kabla ya kuingia mwaka mpya wa 2008.
   Hakutaka kuendelea kukaa chumbani, hapo hapo akainuka na kuanza kuelekea sebuleni. Alichokifanya ni kuchomoa funguo za kuingilia mlango wa sebuleni na mlango wa nyuma. Akatoka nje na kisha kuifunga milango yote kwa nje. Hakutaka kubaki mahali hapo, akaingia garini na kisha kuanza kuelekea kanisani huku akiwa na funguo za kanisa lile ambazo alikuwa amezichonga Kariakoo.
   Hakutaka kuelekea kanisani moja kwa moja, akaanza kuelekea Sinza huku lengo lake likiwa ni kutaka kupata madumu ambayo angefanya nayo kazi. Mara baada ya kuliona duka la jumla maeneo ya Sinza Makaburini, hapo hapo akasimamisha gari, akateremka na kuanza kupiga hatua kulifuata duka lile.
   “Nahitaji madumu matatu ya lita ishirini” Benedict alimwambia muuzaji mara baada ya salamu.
   “Yenye mafuta?”
   “Hapana. Matupu”
   “Elfu tatu moja”
   Benedict akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kinatosha kwa madumu yote hayo matatu. Mara baada ya kumgawia muuzaji kiasi kile cha fedha, akapewa madumu ambayo akayapakiza ndani ya gari na kuondoka katika eneo hilo.
   Safari ya kuelekea katika kituo cha mafuta ikaanza. Akili yake ilikuwa ikicheza na muda tu, dakika tisini ambazo zilikuwa zimebaki kabla ya mwaka mpya kuingia zikaonekana kumtosha kabisa kwa kufanya kile ambacho alipanga kukifanya. Mara baada ya kufika katika eneo la kituo cha mafuta, akayatoa madumu yale na kuanza kujaziwa mafuta aina ya petroli. Yalipojaa yote, akalipa fedha na kisha kuyapakiza garini na kuondoka eneo hilo kuelekea kanisani.
   Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hasira zake juu ya kanisa lile zilivyozidi kukaba kiasi ambacho kiliyafanya machozi kutiririka mashavuni mwake. Kila wakati ambao picha ya marehemu baba yake ilivyokuwa ikimjia kichwani na ndivyo ambavyo hasira juu ya kanisa lile ilivyozidi kumpanda. Hakulipenda kanisa, alilichukia kanisa hilo, mbaya zaidi alimchukia kila mtu kaisani mule.
   Ibada ilikuwa ikiendelea kanisani, idadi kubwa ya washirika zaidi ya mia mbili hamsini ilikuwa ndani ya kanisa hilo. Nyimbo mbalimbali za dini zilikuwa zikiendelea huku watu wakiimba kwa furaha. Benedict akayapeleka macho yake katika saa yake ya mkononi, dakika arobaini na tano ndizo ambazo zilikuwa zimebaki kabla ya mwaka mpya kuingia. Benedict hakutaka kuteremka kutoka garini, aliendelea kubaki mule mule huku macho yake yakiendelea kuangalia mishale ya saa yake.
   “Mnahitajika kanisani” Shemasi Mjuni alimwambia Benedict huku akigongagonga katika kioo cha mlango wa mbele wa gari lile. Benedict akashtuka kutoka katika lindi la mawazo, akayapeleka macho yake katika kioo cha saa yake ya mkononi, dakika tano ndizo ambazo zilikuwa zimebakia kabla ya kuingia kwa mwaka mpya.
   Benedict hakutaka kuteremka japokuwa alikuwa amesikia kwamba washirika wote walikuwa wakihitajika kaisani, washirika ambao walikuwa nje ya kanisa wakaanza kuingia kanisani. Ndani ya dakika mbili tu, hakukuwa na mtu yeyote nje ya kanisa zaidi ya Benedict ambaye alikuwa ndani ya gari.
   “Tunataka kuukaribisha mwaka kwa maombi ya shukrani” Sauti ya mchungaji Munisi ilisikika na mashemasi kuanza kufunga milango. Kitendo kile kilionekana kuwa kama kosa, kwani kwa haraka haraka, Benedict akateremka kutoka garini na kuanza kuufuata mlango mkuu wa kuingilia kanisani mule. Akaanza kuchungulia ndani kwa kupitia katika vitundu vya ufunguo kitasani, hakukuonekana kuwa na ufunguo wowote kwa ndani. Benedict akauchukua ufunguo wake ambao aliuchongesha kwa fundi na kisha kuuingiza katika tundu lile na kisha kuufunga mlango ule.
   Akaanza kupiga hatua kuelekea katika milango mingine midogo, napo huko akafunga milango ile kwa funguo alizokuwa nazo. Hakutaka kuzitoa funguo zile katika vitasa, aliziacha pale pale ili kama watu waliokuwa kanisani watakapojaribu kuziingiza funguo zao basi zisiweze kuingia.
   Kwa wakati huo Benedict alionekana kuwa na haraka kupita kawaida. Akaanza kurudi garini ambapo akachukua dumu moja lililokuwa na mafuta ya petroli na kisha kuanza kuyamwaga mafuta yale kupitia katika nafasi ndogo chini ya mlango.
   Alipomaliza, akachukua madumu mengine mawili kutoka garini na kwenda kumwaga mafuta katika milango ile iliyobakia. Katika kila kitu ambacho alikuwa akikifanya katika wakati huo alikuwa akikifanya kwa haraka haraka kabla maombi ambayo yalikuwa yakiendelea kanisani hayajamalizika.
   Alipoona kuwa ameridhika, akachukua kiberiti na kisha kukiwasha na kuweka njiti katika mafuta yale. Mlipuko mkubwa ukasikika na moto kuanza kuwaka. Benedict akaanza kukimbilia katika milango ile mingine ambapo napo akawasha kama kawaida. Moto ambao ulikuwa umewaka ukaanza kuyafuata mafuta yale na kuingia kanisani.
   Sauti za maombi ambazo zilikuwa zikisikika katika kipindi kilichopita zikabadilika na kuwa kelele za kuomba msaada. Alipoona kwamba alikuwa amewasha moto katika kila mlango, akaanza kulifuata gari lake, akaingia, akaliwasha na kuondoka katika eneo hilo huku moyo wake ukiwa umefarijika kupita kawaida.
   Moto mkubwa ambao ulikuwa ukizidi kuongezeka ulikuwa ukiendelea kuliteketeza kanisa. Sauti za wakinamama pamoja na watoto zilikuwa zikisikika zikiomba msaada kanisani mule. Muungurumo wa moto ulikuwa ukisikika kwa sauti ya juu. Wala hazikuchukua dakika nyingi, kelele zote zilizokuwa zikisikika kanisani hazikusikika tena zaidi ya muungurumo wa moto ambao ulikuwa ukiendelea kuliteketeza kanisa.
*****
   Mchungaji Munisi alikuwa na shauku ya kuingia mwaka wa 2008. Mara kwa mara alikuwa akiagalia kioo cha saa yake huku nyimbo za kumsifu Mungu zikiendelea kuimbwa kanisani hapo. Washirika walicheza kupita kiasi hali ambayo ilisababisha miili yao kuloanishwa na jasho.
   Mara baada ya dakika kadhaa, akaomba kipaza sauti kutoka kwa kijana ambaye alikuwa akiongoza pambio kanisani hapo, alipokabidhiwa kipaza sauti kile, akawataka washirika wote wakae katika viti vyao. Kila moja alikuwa akionekana kuwa na furaha, tabasamu pana yalikuwa yakionekana katika nyuso zao muda wote.
   Mchungaji Munisi akaanza kuongea maneno malimbali yaliyomaanisha kumpa Mungu Utukufu. Alitumia dakika kumi kuongea, akayapeleka tena macho yake katika kioo cha saa yake, dakika tano tu ndio ambazo zilikuwa zimebakia kabla ya mwaka mpya kuingia. Mchungaji akawataka washirika waliokuwa nje ya kanisa kuingia kanisani.
   Washirika wote walipoingia ndani na mashemasi walipohakikisha kwamba hakukuwa na mshirika yeyote aliyekuwa nje, wakafunga milango. Mchungaji akaanza kuongea mambo mengi ambayo yalitokea katika mwaka huo huku dakika tatu tu ndizo ambazo zilikuwa zimebaki. Mchungaji alitumia dakika moja tu, akamaliza kuongea mambo hayo huku akiwa ameyaongea kwa kifupi sana.
   Akamuita muimbaji ambaye akaanza kuimba nyimbo mbalimbali za kuabudu. Huku sekunde thelathini zikiwa zimebakia, sala ya kumshukuru Mungu ikaanza kusikika kanisani hapo, sekunde zilikatika na hatimae saa sita kamili kuingia.
   Kelele za shangwe zikaanza kusikika kwa kila mshirika ndani ya kanisa lile. Watu wakaanza kukumbatiana, furaha ambayo walikuwa nayo katika kipindi hicho ilionekana kuwa kubwa zaidi ya kipindi kilichopita. Watu wengine wakashindwa kuamini kama kweli walikuwa wameingia mwaka mwingine, machozi ya furaha yakaanza kutiririka mashavuni mwao.
   “Ni jambo la kumshukuru Mungu sana. Hebu ruka ruka juu na upaze sauti yako mbele za Mungu Aliye Hai” Mchungaji Munisi aliliambia kanisa.
   Watu wakaanza kuruka ruka kwa furaha huku kelele za shangwe zikisikika zaidi na zaidi. Mashemasi ambao walisimama mlangoni walipigwa na mshangao mara baada ya kuona kimiminiko kilichofanana na maji kikiingia kanisani mule kwa kupitia katika nafasi ndogo iliyokuwa chini ya mlango.
   “Nini hii?” Shemasi Anania aliuliza.
   “Subiri kwanza” Shemasi John alimwambia Anania. Hapo hapo John akainama na kukigusa kile imiminiko kwa kutumia kidole chake na kisha kunusa.
   “Mungu wangu!”
   “Ni nini?”
   “Petroli” John alijibu.
   Kadri mda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo petroli ile ilivyozidi kusambaa kanisani mule.
   Kwa haraka haraka John akakishika kitasa na kuanza kukitekenya, mlango haukufunguka. Akaanza kuchukua funguo kutoka katika msumali na kisha kuuchomeka katika kitundu chake. Ufunguo wala haukuingia kitu kilichompelekea kuanza kuchungulia nje kupitia kitundu kile cha ufunguo, hakuona vizuri nje hali iliyoonyesha kwamba kulikuwa na ufunguo kwa nje.
   Hakukuwa na mtu aliyekuwa na taarifa juu ya mafuta ya petroli ambayo yalikuwa yameanza kuenea katika nusu ya sakafu kanisani mule. Kila mtu alikuwa akishangilia, hata kwa wale ambao waliyaona mafuta yale pale sakafuni walikuwa wakiyapuuzia.
   Tayari kijasho cha wasiwasi kikaanza kumtoka John, mshtuko ukampata zaidi mara baada ya kuufikia mlango wa upande mwingine. Petroli ile ilikuwa ikiendelea kuenea sakafuni kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Kwa haraka haraka John akauchukua ufunguo na kujaribu kuuingiza ufunguo ule katika kitundu kile pale mlangoni, ufungo ukagoma kuingia hali iliyoonyesha kwamba napo kulikuwa na ufunguo kwa nje.
   Hata kabla John hakujua afanye nini, ghafla moto mkubwa ukaanza kuonekana katika mlango mkuu wa kuingilia kanisani mule. Watu wote wakashtuka, moto ukaendelea kuwaka zaidi na zaidi. Kila mmoja akaanza kukimbilia katika mlango wa upande wa pili, bado John alikuwa akihangaika kuufungua.
   “Fungua haraka John” Mchungaji Munisi alimwambia John.
   “Siwezi mchugaji…”
   “Kwa nini?” Mchungaji aliuliza lakini hata kabla hajapewa jibu la swali lake, moto ukaanza kuwaka pale pale mlagoni walipokuwa wamejazana. Watu wakaanza kuteketea, wengine wakaanza kusogea katikati ya kanisa huku wakidhani kwamba moto ule usingefika mahali pale, baada ya muda nao wakajikuta wakiteketezwa kwa moto.
   Wakinamama pamoja na watoto wao ambao walikuwa wamewabeba wakaanza kuteketea kwa moto, kelele za shangwe ambazo zlikuwa zikisikika katika kipindi kichache kilichopita zikabadilika na kuwa kelele za kuomba msaada na maumivu makali. Wala hazikupita dakika nyingi, hakukuwa na sauti ya mtu yeyote ambayo ilisikika zaidi ya muungurumo wa moto ule ambao bado ulikuwa ukiendelea kuliteketeza kanisa lile.
****
   Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo idadi ya watu ilivyozidi kuongezeka karibu na eneo la kanisa lile.  Simu zikapigwa katika kitengo cha Zimamoto. Kadri ambavyo watu walivyokuwa wakiliona kanisa lile lilivyokuwa likiteketezwa na moto na ndivyo ambavyo machozi yalivyozidi kujaa machoni mwao.
   Tukio lile la kuteketezwa kwa moto lilikuwa likimhuzunisha kila mtu ambaye alikuwa akiliangalia. Furaha ambayo walikuwa nayo ya kuingia mwaka mpya ikatoweka kabisa mioyoni mwao. Hakukuwa na sauti ya mtu yeyote ambayo ilisikika kutoka kanisani, ni sauti ya muungurumo wa moto tu ndio ambao ulikuwa ukisikika.
   Zilipita dakika kumi na tano, magari mawili ya kitengo cha Zimamoto yakafika katika eneo hilo. Kazi kubwa ya kuuzima moto ule ikaanza huku idadi ya watu ikizidi kuongezeka mpaka kufikia watu elfu tatu. Hadi kufikia kipindi hicho, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu sababu zilizopelekea kuwaka kwa moto ule ambao ulikuwa umeliteketeza kanisa.
   “Au umeme ulilipuka kanisani?”
   “Hapana bwana. Nafikiri kuna mtu alilichoma moto”
   “Umejuaje?”
   “Hausikii harufu kali ya mafuta ya Petroli?”
   “Mhh! Inawezekana”
   Magari matatu ya polisi yakafika katika eneo hilo. Kwa haraka haraka, polisi ambao walikuwa na bunduki mikononi mwao wakateremka na kuanza kuelekea katika eneo lile la kanisa. Joto kali la mvuke wa moto ule bado lilikuwa likitawala mahali hapo. Walisubiri mpaka joto lile kuisha na ndipo wakaanza kwenda lilipokuwa gofu la kanisa lile. Wakaupiga teke mlango, ulipovunjika, wakaingia ndani.
   Picha ambayo ilionekana dani ya kanisa lile ilionekana kumuogopesha kila aliyeiangalia. Miili ya watu ambayo iliteketezwa na moto ule ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao, wakinamama ambao walikuwa wamewabeba watoto wao walikuwa wameteketezwa na moto pamoja na watoto wao. Mafuta ya binadamu yalikuwa yametapakaa sakafuni, hakukuwa na kitu ambacho kilikuwa kimesalia, kila kitu kilikuwa kimeteketezwa kwa moto.
   “Hali inatisha sana” Mkuu wa kituo cha polisi cha pale Mwenge, Bwana Marwa alisema huku akitoka nje ya kanisa.
   Bwana Marwa alionekana kuchanganyikiwa, akili yake bado ilikuwa ikijiuliza juu ya chanzo ambacho kilisababisha moto ule. Akaanza kuwaangalia wananchi ambao walikuwa wamesimama karibu na eneo lile, machozi yalikuwa yakijikusanya machoni mwake. Kwa mwendo wa taratibu akaanza kuwasogelea wananchi katika eneo ambao waliambiwa watulie kule hadi kila kitu kitakapokuwa sawa.
   “Kitu gani kilitokea?” Bwana Marwa aliuliza huku akionekana dhahiri kuchanganyikiwa.
   “Labda naweza kuhisi kitu” Mmoja wa wananchi alisema na hapo hapo kuitwa.
   “Unahisi nini?”
   “Kuna mtu amehusika”
   “Umejuaje?” Bwana Marwa aliuliza.
   “Nafikiri mnatakiwa mfanye kitu fulani ili hisia zangu ziwe na uhakika” Kijana yule alijibu.
   “Kitu gani?”
   “Mkamwangalie mtu fulani ambaye inawezekana amehusika na tukio hili”
   “Mtu gani?”
   “Benedict Matimya. Mtoto wa marehemu mchungaji Matimya” Kijana yue alisema.
   Hawakutaka kupoteza muda, kwa haraka haraka Bwana Marwa, polisi watano wenye bunduki pamoja na yule kijana wakaingia garini na kuanza kuelekea nyumbani kwa mzee Matimya. Kijana yule bado alikuwa akilia, moyoni alioekana kuumizwa kupita kawaida huku muda wote akisisitiza kwamba Benedict ndiye ambaye alikuwa akihusika katika mauaji yale.
   “Tukifika, hakuna kuuliza,tunamuweka chini ya ulinzi. Mmesikia?” Bwana Marwa alisema huku akionekana kukasirika.
   “Ndio mkuu” Polisi waliokuwa ndani ya gari lile waliitikia huku wakikoki bunduki zao.
   Safari ilichukua dakika tano, dereva akasimamisha gari nje ya geti la nyumba ya mzee Matimya. Honi zikaanza kupigwa na baada ya sekunde kadhaa, Angeline akafika mahali hapo na kufungua geti. Gari likaingizwa ndani na polisi wote kuteremka. Angelina hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea kwa wakati huo, alibaki akitetemeka tu.
   “Benedict Matimya yupo?” Sauti ya Bwana Marwa ilisikika ikimuuliza Angelina.
   “Ndio…”
   “Alitoka siku ya leo?”
   “Ndio. Alienda kanisani kwenye mkesha. Amerudi dakika tano zilizopita” Angelina alijibu.
   Bi Meriana akatokea mahali hapo, polisi hawakutaka kuongea kitu chochote kile, kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea katika chumba cha Benedict huku wakiongozwa na Angelina.
   “Jamani! Kuna nini tena?” Bi Meriana aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
   “Usihofu mama”
   “Lazima nihofu. Bunduki zinanikosesha amani”
   “Usijali mama” Bwana Marwa alisema huku wakiwa wamekwishafika katika mlango wa kuingilia chumbani kwa Benedict.
****
   Mara baada ya Benedict kulifikia gari lake akaufungua mlango na kuingia. Hakutaka kubaki mahali hapo, hivyo akaliwasha gari lake na kuondoka huku akiliacha kanisa likizidi kuteketezwa kwa moto ambao aliuwasha.
   Njia nzima Benedict alikuwa na furaha, kitendo alichokifanya cha kulichoma moto kanisa alikiona kuwa kitendo sahihi ambacho kilikuwa kimemletea furaha kwa wakati huo. Hakuonekana kuwaonea huruma watoto wadogo ambao walikuwa wakiteketezwa kwa moto kanisani mule, kila mtu ambaye aliteketezwa kwa moto ndani ya kanisa lile, kwake alimuona kuhusika katika mauaji ya baba yake.
   “Ni Biblia tu ndizo hazikustahili kuchomwa moto” Benedict alijisemea.
   Mara baada ya kufika katika geti la nyumbani kwao, akateremka, akalifuata akafungua na kuingiza gari katika eneo la nyumba yao. Alipoliegesha, akateremka, akaufuata mlango akaufungua na kuingia ndani.
   “Kwa nini ulitufungia mlango?” Bi Meriana alimuuliza Benedict huku akionekana dhahiri kukasirika.
   “Sikutaka muangamie. Bado ninawapenda na kuwahitaji” Benedict alijibu.
   Bi Meriana na Angelina wakabaki wakishangaa, jibu ambalo alilitoa Benedict lilionekana kumshtua kila mtu. Wakabaki wakimwangalia Benedict mara mbili mbili kana kwamba hawakukisikia kile ambacho kiliongelewa mdomoni mwake. Bi Meriana alitamani kuuliza swali jingine lakini Benedict akaelekea chumbani kwake.
   Moyo wa Benedict ulikuwa umetawaliwa na furaha, akajitupa kitandani huku macho yake yakiangalia darini. Moyo wake uliridhika na kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Kitendo cha kulichoma kanisa na kuua zaidi ya watu mia mbili hamsini kilikuwa ni kitendo ambacho kilimfurahisha kuliko kitu chochote katika maisha yake katika mwaka uliopita.
   Kwa kasi ya ajabu Benedict akainuka kutoka kitandani. Muungurumo wa gari kutoka nje ulionekana kumtia wasiwasi kupita kawaida. Kwa haraka haraka akaelekea dirishani, akalifungua kidogo pazia na kuanza kuchungulia nje. Macho yake yakatua katika gari aina ya Defender ambalo ubavuni liliandikwa ‘Polisi’ huku mbele kukiwa na polisi waliokuwa na bunduki mikononi.
   “Benedict Matimya yupo?” Sauti ya mwanaume mmoja ilisikika.

 Unataka niwe nakutumia CHOMEZO watu 200 wa kwanza kulike PAGE YA 2JIACHIE Mtatumiwa imbox chomezo LIKE PAGE YETU HAPA ==>www.facebook.com/2jiachie

ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA



Viewing all articles
Browse latest Browse all 12768

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>