Quantcast
Channel: Rogers Linky - Sports Home
Viewing all articles
Browse latest Browse all 12768

The Last Breath (Pumzi ya Mwisho) - 9

$
0
0
ILIPOISHIA...
JOHNSON na mke wake Loveness, wako porini huko Congo wakiwa miongoni mwa wapiganaji wa jeshi la Congo linalopambana na waasi wa Congolese Patriotic Front, nao ni kama wapiganaji, lengo lao ni kumtafuta mtoto wao Melania ambaye wanaamini alitekwa na waasi hao.
Kwa miaka mingi wamefanya jambo hili, wakiyatia maisha yao katika hatari mara kadhaa lakini bado hawakufanikiwa kumpata Melania! Wanahisi kukata tamaa lakini bado wanatiana moyo,  wakiamini ipo siku wangekutana na mtoto wao pekee.
Wazazi wakiwa katika hali hiyo, Melania yuko katikati ya pori kwenye kambi ya waasi, ameshazoea maisha ya kiuaji, akili yake imeshabadilika kabisa! Ni mjuzi wa kutumia bunduki na mtalaam wa kulenga shabaha.
Kijana aliyekuwa akimlinda asifanyiwe unyama (Paul) aliuawa kikatili na baada ya kifo chake ndiyo Melania akageuzwa mtumwa wa ngono na kamanda mkuu wa waasi ambaye baadaye alimgeuza kuwa mke wake, jambo ambalo hakika lilimuudhi sana Melania ambaye hivi sasa ana umri wa miaka kumi na sita.
Je, nini kitaendelea? Wazazi hawa watakuja kukutana na mtoto wao?
Songa nayo...

PAMOJA na kuwa mke wa kamanda mkuu wa waasi, asilimia kubwa ya maisha ya Melania ilikuwa ni mapigano msituni! Hakubaki kambini kama wake wengine duniani, yeye kila siku ilikuwa bunduki begani akizunguka msituni kupambana na majeshi ya serikali, kamanda mkuu alishamjaza matumaini ya kwamba, ipo siku wangeichukua Kinshasa kisha yeye kamanda kuwa Rais na Melania kuwa mke wa Rais.

“Maisha yatabadilika kabisa, utakuwa unatembea na ving’ora kila unakokwenda!”
“Nitafurahi sana.”
“Hivyo ni lazima upigane, lazima uue bila huruma.”
“Hakuna shida.”

Melania alishamweka Mungu kando, akili yake ilishaharibika, kutoa uhai wa mtu halikuwa jambo gumu tena kwake. Kila siku alikuwa mstari wa mbele, wakisogea kuelekea Kinshasa. Mara nyingi walikutana na mapigano makali, wakashinda ama kushindwa, lakini yeye na kamanda mkuu pamoja na baadhi ya waasi walinusurika.
Pale wao walipowashinda nguvu wapiganaji wa serikali, waliwaua bila huruma na wakati mwingine kuwateka hadi kambini ambako waliwapiga risasi wakiwa wamewafunga kwenye miti baada ya kuwa wamewahoji na kupata siri zote za  jeshi la serikali.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha ya Melania, mke wa kamanda mkuu, hakuwa na kumbukumbu kabisa na maisha ya uraiani. Pamoja na hayo yote taswira za wazazi wake hazikumwondoka kichwani, bado aliwakumbuka baba na mama  yake lakini alijua hapakuwa na namna ya kukutana nao tena, hata upendo kwao ulishapungua, akakubali kwamba maisha yake yalikuwa ni ya msituni na hakuwa na uhakika wa kuishi miaka mingi.
“Nimesikia majeshi ya serikali yako kwenye Mlima wa Mukunguzi, tena wanajiandaa kuja kuvamia kambi yetu, lazima tunyanyuke sasa hivi kwenda kupambana nao,  mmesikia?”
“Tumesikia kamandaaa!” kundi kubwa la waasi wasiopungua elfu mbili, wenye silaha nzito waliitikia.

Mwanzoni wakati Melania anaanza kuishi na kamanda mkuu, hakuwa akimpenda lakini miaka ilivyozidi kusonga, upendo ulianza kuingia hasa baada ya kugundua kwamba wakifanikiwa kuingia Ikulu yeye ndiye angekuwa mama wa taifa. Hakutaka apatwe na tatizo, hakutaka afe, hivyo alimlinda kila walikokwenda.
Siku hiyo waliondoka jeshi la watu elfu moja na mia tano kwenda kupambana na  jeshi la serikali, tofauti na siku nyingine zote, mapambano yalikuwa makali mno siku hiyo, jeshi la waasi likasambaratishwa, watu wengi wakafa, Melania na mume wake wakafanikiwa kutoroka, lakini wakiwa njiani kurejea kambini,  walimiminiwa risasi, Melania akakwepa lakini mume wake hakuweza,  akaanguka chini na kufa.
Alichokifanya Melania ni kuamua kujiokoa mwenyewe, huku akiwaua wapiganaji wote aliokutana nao njiani mpaka akafika karibu kabisa na kambi ambako alikutana na waasi wengine walionusurika, wote wakarejea kambini ambako walitangaza kwamba kamanda wao alikuwa ameuawa!
Melania hakuruhusiwa kumlilia mume wake,  kilichofanyika na kukubaliwa na waasi wote ni kumsimika yeye kuwa kiongozi  mpya wa waasi. Kila mtu akashangilia, lilikuwa jukumu kubwa kwa mwanamke mwenye umri wa miaka kumi na tisa kama ilivyokuwa kwa Melania wakati huo. Hata hivyo baada ya kushawishiwa sana na kuahidiwa kila aina ya ushirikiano kutoka kwa waasi wenzake, hatimaye alikubali.
Akiwa kamanda mkuu wa waasi, Melania aliongoza waasi katika mapambano mengi makali na kupata ushindi, jeshi la serikali likazidi kurudishwa nyuma kuelekea Kinshasa! Sehemu kubwa ya wapiganaji wa serikali waliotekwa, walikubali kujiunga na jeshi la waasi wakiwa wameahidiwa madaraka baada ya mapinduzi.

“Kamanda!”
“Ndiyo.”
“Tumeteka wengine kumi, tena walikuwa na hili begi!”
“Wako wapi?”
“Wako kule kwenye uwanja wa mauaji.”
“Mmewahoji?”
“Ndiyo.”
“Wanasemaje?”
“Kuna wawili wanaonekana kuwa ni mtu na mke wake, wao wanasema si wanajeshi!”
“Sasa wanafanya nini na Jeshi la Congo?”
“Hata sijui, hao ndiyo wenye hilo begi.”
“Mmewahoji wametoa siri?”
“Wengine wote wametoa lakini hao wawili wamekataa, wanadai wao wanamtafuta mtoto wao.”
“Ujinga mtupu, nendeni mkawafunge kwenye miti tumalize kazi.”
“Sawa kamanda.”
Waasi waliondoka haraka na kwenda kuwachukua mateka kumi na kuwafunga kwenye miti maalum ya kupigia risasi, Johnson na Loveness walikuwa miongoni mwao, kwa sababu ya kipigo wakiwa wamepoteza fahamu. Wakafungwa kwenye miti na kusubiri kufyatuliwa risasi.
Kazi ilipokamilika, Kamanda Mkuu Melania ambaye kwa wakati huo aliitwa Janette, alifuatwa na kuja kwenye uwanja wa mauaji ya mateka. Watu kumi walikuwa mbele yake, wakiwa wamefungwa vizuri kwenye miti na muasi mmoja mwenye bunduki iliyojazwa risasi alikuwa amesimama mbele yao akisubiri amri ya kamanda mkuu.
“Fyatuaa!” aliongea Melania.
Risasi zikaanza kumiminika, Melania akiwa hajui kabisa kwamba miongoni mwa watu aliokuwa ameamuru wauawe ni wazazi wake wapendwa ambao kwa miaka mingi waliteseka porini wakimtafuta yeye.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

Tuendelee ku-Like page hii www.facebook.com/2jiachie upate habari zote za mjini muda wote. 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 12768

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>